by Admin | 2 September 2019 08:46 pm09
Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, maandiko yanasema,
Mhubiri 10:10 “Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi; Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi. Walakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa”.
Katika tafsiri nyingine hilo Neno Chuma limetafsiriwa kama shoka, ikiwa na maana kuwa kama shoka ni butu au halinolewi mara kwa mara basi itampasa mtu kutumia nguvu zaidi katika kukata vitu au kuchonga, au kuchanja kama anakata nyama itampasa atumie nguvu zaidi kuikata nyama ile, kama anakata mti basi itampasa atumie jitihada ya ziada yenye kuchosha kuudondosha mti kwasababu Shoka ni butu haliwezi kupenya kwa haraka ndani ya shina..Tofauti na kama kifaa hicho kingekuwa ni kikali, angetumia nguvu chache tu na matokeo kuwa makubwa ndani ya muda mfupi…
Ni kama tu kisu au kiwembe kikiwa ni kakali basi ukipitisha hata kwenye karatasi ni mara moja tu limegawanyika, lakini kama ni butu basi utakipeleka mbele na nyuma, na utachukua muda, na bado halitachanika vizuri kama lile lililochanwa na kiwembe kikali..
Lakini Mhubiri anaendelea kwa kusema, “walakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa”,.. Ikiwa na maana usipoweza kutumia hekima, kuamua maisha yako kwa kukifanya kisu chako kuwa kikali basi mambo yako, licha tu ya kuwa magumu lakini pia utatumia nguvu nyingi kuyafikia…
Duniani Vipo visu vingi tofauti tofauti na mashoka tofuati tofauti na kila mtu analo lake, ambalo kwa namna moja au nyingine linamsaidia kufanya mambo yake kuwa mepesi, wengine ni elimu, wengine ni ujuzi, wengine ni fedha n.k..Lakini hasara moja ya vifaa hivyo vyote sio vya kudumu, huwa vinakuwa butu kwa jinsi muda unavyokwenda na kwa jinsi vinavyotumika…. Mtu akiviacha vinachakaa na pia isitoshe havitumiki kila mahali…huwezi kutumia elimu kutibu kifo, vile vile huwezi tumia pesa kununua furaha, au upendo au amani..
Ni kifaa kimoja tu ambacho Mtu mwenye akili na Hekima anaweza kukitumia kwa matumizi yote na kukata kila kitu pasipo kutumia nguvu, na bado kutokupungua ubora wake na makali yake…Nacho ni Neno la Mungu..
Waebrania 4:12 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
13 Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.”
Mtu akiwa na Neno la Mungu peke yake, hiyo ni salaha tosha, ya kurahisisha mambo yako..hili haliwi butu kama vile mengine, linao uwezo sio tu wa kukata kwa ukali zaidi ya upanga wowote, bali pia linaweza kuchoma hata kuzigawanya nafsi na roho, yaani linaingia ndani ya moyo wa mwanadamu na kugawanyisha kila kitu na kutambua mawazo yake, kitu ambacho pesa haiwezi kufanyi, elimu ya dunia hii haiwezi kufanya, ujuzi wowote ule wa mwanadamu hauwezi kufanya..
Ndio maana mtu yeyote aliyejaa Neno la Mungu ndani yake, hakuna jambo lolote linaloweza kumlemea hata liwe gumu kiasi gani kwasababu anafahamu vizuri silaha aliyonayo inaubora kiasi gani..
Mhubiri anatushauri NI HERI KUTUMIA HEKIMA NA KUFANIKIWA, tunapaswa tujue ni kifaa gani kitakachotufaa katika maisha yetu, katika mapori yanayotuzunguza mbele yetu ambayo yanapaswa yafyekwe kweli kweli, kifaa ambacho tunaweza kukabiliana na adui yetu ibilisi na kummaliza haraka sana bila kutumia nguvu nyingi… silaha hiyo si nyingine zaidi ya Neno la Mungu.
Waefeso 6: 17 “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;”
Tunapoliishi Neno la Mungu, maisha yetu hatutayaona ni magumu, hatutasumbuka kama ulimwengu unavyosumbuka, Kwani ni Mungu mwenyewe ndiye atakayekuwa anatupigania,,Lakini tunapoliweka Neno la Mungu kando, tunapolidharau na kuchagua mambo mengine, au kuyaona mambo mengine ni ya muhimu zaidi ya Neno lake, tuwe na uhakika kuwa safari yetu itaishia ukingoni…Ni kutumia kifaa butu, kuufyeka msitu…Mambo yatakuwa magumu tu, huo ndio ukweli, Nira iliyo nyepesi ipo kwa Bwana Yesu tu, pengine kote ni Nzito na mateso yasiyoelezeka..(Mathayo 11:28)
Ndugu/Kaka Ikiwa hujayakabidhi maisha yako kwa BWANA Mlango wa Neema upo wazi, usisubiri baadaye au kesho, muda umekwenda sana kama unyakuo hautakukuta moja ya hizi siku, hujui baadaye yako itakuwa vipi, waliokufa leo asubuhi sio kwamba walikuwa waovu zaidi yako wewe, au walikuwa wameshajiandaa kwa safari ya kwenda huko ng’ambo, hapana lakini kifo kiliwakuta kwa ghafla tu, na ndivyo kitakavyotukuta wote walio haki na wasio haki…Hivyo fanya uamuzi wa busara wakati huu kwa kutubu dhambi zako kama hujatubu na kumgeukia Bwana sasa hivi.. kumgeukia Bwana Yesu sio kuwa vuguvugu, ni kitendo cha kumaanisha kabisa….Kisha utafute mahali wanapobatiza ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi kwa Jina la YESU KRISTO, kama pia bado hujafanya hivyo..Upate ondoleo la dhambi zako, kulingana na (Matendo 2:38) ili Bwana akupe kipawa cha Roho wake Mtakatifu ambaye ndio muhuri wetu, Mungu anaotutia mpaka ile siku wa ukombozi wetu (Waefeso 4:30).
Bwana azidi kukubariki.
Maran atha!
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/09/02/kifaa-bora-cha-matumizi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.