by Admin | 17 November 2019 08:46 pm11
SWALI: Kwanini biblia sehemu moja inasema mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, na sehemu nyingine inasema tukisema hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe?. Je! Ni lipi hapo lipo sahihi kati ya hayo mawili?.
JIBU: Tukisoma 1Yohana 3:9 inasema..
“Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”.
Tukisoma pia 1Yohana 1:8-10 inasema..
“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu”.
Hivyo ukisoma kwa juu juu mistari hiyo utaona kama inajichanganya yenyewe lakini ukweli ni kwamba haijichanganyi na yote miwili ipo sawa, isipokuwa tunapaswa tuelewe Mtume Yohana alikuwa anaizungumzia hiyo mistari katika Nyanja ipi?, kwamfano kama ukiutazama vizuri huo mstari wa pili unaosema,“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.,” Utagundua kuwa Mtume Yohana alikuwa analenga katika eneo la mtu kujiona kuwa mkamilifu asilimia mia kama Mungu mwenyewe, suala ambalo halipo, hakuna mwanadamu ambaye ni mkamilifu kwa asilimia zote, anayesema hana chembe ya dhambi hata kidogo ndani yake, vinginevyo basi neema itakuwa ni bure…..yapo makosa madogo madogo ambayo mtu anayatenda pasipo hata yeye kujua kama ameyafanya sasa haya ndio yanayotufanya tusijigambe kuwa hatuna dhambi hata kidogo.
Na tukiwa na ufahamu huo kichwani mwetu basi, tutajinyenyekeza mbele zake, na kuungama makosa yetu kila siku kwa yale ambayo tunamkosea Mungu pasipo kujua na kwa yale tunayoyajua.
Lakini sasa tukirudi katika ule mstari wa kwanza unaosema.. “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”.
Ni kwamba hakuna mtu yeyote anayesema amezaliwa mara ya pili kwa akili zake na kwa ufahamu wake akaenda kutenda dhambi…Hicho kitu hakiwezekani kabisa, kutokuwa wakamilifu asilimia 100 kama Mungu hakumaanishi kuwa ndio tufanye dhambi kwa makusudi, wanaoweza kufanya hivyo ni watu ambao hawajazaliwa mara ya pili, wao ndio wanaweza kutamani na muda huo huo wakaenda kuzini au kufanya mustarbation, au kutazama pornography, wanaweza wakakasirika na muda huo huo wakaleta madhara na wakati mwingine hata kuua, wanaweza wakatamani mali ya mwingine na muda huo huo wakaiba, wanaweza kuudhiwa na muda huo huo wakaporomosha matusi, au kulipiza kisasi..
Lakini kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili jambo hilo haliwezekaniki kabisa, ni kwasababu gani?. Ni kwasababu biblia inasema,uzao wake wakaa ndani yake, (yaani Uzao wa Mungu) na kama uzao wake wakaa ndani yake, basi mtu huyo ataonyesha tabia za yule aliyemzaa, ataonyesha tabia za YESU ndani yake..Kwamfano haiwezekani, mtoto akazaliwa na mtu halafu siku hiyo hiyo akaanza kula majani kama ng’ombe,tutajiuliza ni nini kimetokea,.. lakini tukimwona ndama aliyezaliwa leo anakula majani hatushangai kwasababu uzao wa ng’ombe upo ndani yake..Vivyo hivyo na sisi tuliozaliwa mara ya pili, hatuwezi sisi wenyewe kutenda dhambi kwa makusudi halafu tukasema tumezaliwa na Mungu, huo ni uongo…
Ukiona mtu anakwenda kuzini halafu anasema nimepitiwa huyo bado hajazaliwa mara ya pili, ukiona mtu anafanya mustarbation halafu anasema ameokoka huyo bado hajazaliwa mara ya pili, ukiona anakwenda disko bado hajazaliwa mara ya pili..ukiona mtu ni mlevi, au mvutaji sigara au mvaaji vimini, mzinzi, mtukanaji, na bado anasema amezaliwa mara ya pili fahamu kuwa huyo bado yupo ulimwenguni. Uzao wa Mungu haupo ndani yake. Hivyo anahitaji kutubu na kuzaliwa mara ya pili.
Ubarikiwe.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
DHAMBI YA MAUTI
DHAMBI ISIYO NA MSAMAHA.
IELEWE SAUTI YA MUNGU.
Katika Yakobo 1:13 Biblia inasema Mungu hamjaribu mtu, lakini tukirudi kwenye kitabu cha Mwanzo 22:1 tunaona Mungu alimjaribu Ibrahimu. Hapo naomba mwanga zaidi.
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/11/17/biblia-inamaana-gani-kusemaaliyezaliwa-na-mungu-hatendi-dhambi/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.