KWA KUWA NGUVU ZA MBINGUNI ZITATIKISIKA.

by Admin | 18 November 2019 08:46 am11

Kwanini nguvu za mbinguni zitikisike?.

Bwana Yesu alitabiri na kusema kipindi kifupi karibu na mwisho wa dunia kutaanza kuonekana baadhi ya ishara za kutisha kutoka mbinguni, na mambo ya ajabu sana, Na hiyo itawafanya watu wengi waingie katika hofu sana, wakijiuliza nini maana ya mambo haya na nini kitatokea baada ya hayo..

Luka 21:25 “ Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake;

26 watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika”.

Kama tunakumbuka  Octoba 1 mwaka 2016, kulitokea Ishara ya ajabu pale Yerusalemu Israeli, sauti kama za baragumu nyingi zilisikika zikipigwa angani (tarumbeta zikilia Israeli angani)kwa umbali mrefu sana.. Na pale ambapo sauti zilipokuwa zinatokea kulionekana mduara mkubwa sana wa wingu lililozunguka kama pete..Jambo ambalo liliwashtua wakazi wengi wa mji wa Yerusalemu sio tu Israeli peke yake, bali hata dunia nzima. Kama hujalifahamu hilo bofya link hii utazame baadhi ya video zilizo rekodi tukio hilo(youtube).

https://www.youtube.com/watch?v=AwCc45T38SU

Haikuishia hapo lakini Inaripotiwa miaka ya hivi karibuni mambo kama hayo ya ajabu yamekuwa yakitokea angani, karibu dunia nzima, mambo ambayo hayajawahi kusikika wala kuonekana siku za huko nyuma,..hata wanayansi wanakosa majibu ya maswali hayo, wengine wanadai dunia inatembelewa na viumbe kutoka sayari nyingine (Aliens), wengine wanasema hivi, wengine vile, lakini biblia imeweka wazi kabisa katika siku za mwisho nguvu za mbinguni zitatikisika, na ishara kama hizo zitaendelea kuwa nyingi, na hiyo yote tunapaswa tujiulize ni kwanini hayo yote yanatokea?..Ni kwasababu Mungu anatukumbusha kuwa ule mwisho upo karibu na hivyo tujiweke tayari kwasababu saa ya ukombozi wetu imekaribia..

Amosi 3: 6 ”Je! Tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope?…”

Kusikika kwa matarumbeta kama hayo, ni kutuonyesha kuwa Upo wakati parapanda halisi ya mwisho italia na wafu waliokufa katika Kristo watafufuliwa na kupewa ile miili ya utukufu pamoja na watakatifu waliokuwa hai kisha wote kwa pamoja watanyakuliwa na kwenda kumlaki Bwana Yesu mawinguni, kisha wataenda katika karamu ya mwana kondoo waliyoandaliwa mbinguni,

Lakini kumbuka kwa wakati huo ambao tutakuwa mbinguni, huku chini dhiki kuu itakuwa inaendelea,. Kumbuka hizi ni saa za majeruhi, Injili ya Kristo iliyotabiriwa ya siku hizi za mwisho sio ile ya kuwavuta tena waje kwa Kristo hapana bali ni injili ya kuhimiza, kumtia moyo yule ambaye tayari ni mtakatifu ili azidi kuwa mtakatifu na kumuhimiza yule ambaye ni mwovu na azidi kuwa mwovu (Soma Ufunuo 22:11), …

Kwasababu wakati wa mavuno umekaribia na magugu na ngano tayari yameshajitenga..Hivyo hakuna tena muda wa kuanza kutafuta magugu ni yapi na ngano ni zipi katika shamba la Mungu…

Hivyo ndugu kama bado unasuasua ni heri ukayajenga Maisha yako sasa upya, mkaribishe Kristo katika Maisha yako, ulimwengu huu usioisha masumbufu na mahangaiko, ukiendelea nao, utajikuta unaendelea hivyo hivyo mpaka unakufa au unyakuo unakukuta kwa ghafla..Hivyo kama upo tayari leo, hapo ulipo tafuta nafasi yako mwenyewe, upige magoti, umweleze Mungu dhambi zako zote, kisha mwombe akusamehe, unafanya hivyo huku ukiwa umemaanisha na umekusudia kuacha dhambi zako kabisa kwamba kuanzia leo unataka kuishi Maisha yale Kristo anayotaka..

Na kama utakuwa umefanya hivyo kwa Imani basi fahamu kuwa Umeshasamehewa,..Amani ya Bwana itaingia ndani ya moyo wako, (Huo ndio uthibitisho wa Msamaha wako), sasa unachopaswa kufanya baada ya hapo ni kwenda kubatizwa kama hujabatizwa, Hivyo tafuta kanisa linaloamini katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na uwe kwa jina la YESU KRISTO ubatizwe sawasawa na Matendo 2:38,..Ili kuukamilisha wokovu wako, Na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu. Kwasababu hiyo ni ahadi aliyoiahidi kwa wale wote wanatakao mpokea. Roho Mtakatifu atakusaidia kushinda dhambi na kukupa uelewa wa maandiko kwa namna isiyokuwa ya kawaida.

Bwana akubariki sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Maran Atha.

Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2019/11/18/kwa-kuwa-nguvu-za-mbinguni-zitatikisika/