HATA NA BARNABA PIA AKACHUKULIWA NA UNAFIKI WAO!!

by Admin | 11 January 2020 08:46 am01

Tukisoma kitabu cha Matendo ya mitume tunaona kikizungumza habari za matendo ya kishujaa yaliyofanywa na mitume wa Bwana, jinsi walivyofanya bidii kuieneza injili ya Kristo ulimwenguni kote, lakini pamoja na hayo biblia inatueleza pia yapo makosa yaliyofanywa nao wao katika huduma zao, Na lengo la Mungu kuruhusu yaandikwe ni ili kutufunza sisi nasi tusije tukayarudia makosa yale yale yaliyofanywa na wao katika utumishi wetu.

Sasa kama wewe ni msomaji mzuri wa biblia utakumbuka kuna wakati Mtume Petro alianza kutoka kidogo na msingi wa Imani Kristo aliompa kwa kuwaagiza watu wa mataifa mambo ambayo si sahihi wao kuyafanya, na huku akijua kabisa ukweli kwamba anachokifanya sio sawa, lakini alifanya vile kwa unafki ili tu kuwapendezesha wayahudi, Na mtume Paulo alipoligundua hilo alimkemea mbele ya wote..Tusome.

Wagalatia 2:11 ‘Lakini Kefa alipokuja Antiokia, nalishindana naye uso kwa uso, kwa sababu alistahili hukumu.

12 Kwa maana kabla hawajaja watu kadha wa kadha waliotoka kwa Yakobo, alikuwa akila pamoja na watu wa Mataifa; lakini walipokuja wao, akarudi nyuma akajitenga, huku akiwaogopa waliotahiriwa.

13 Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao.

14 Walakini, nilipoona ya kuwa njia yao haiendi sawasawa na ile kweli ya Injili, nalimwambia Kefa mbele ya wote, Ikiwa wewe uliye Myahudi wafuata desturi za Mataifa, wala si za Wayahudi, kwa nini unawashurutisha Mataifa kufuata desturi za Wayahudi?

15 Sisi tulio Wayahudi kwa asili, wala si wakosaji wa Mataifa,

16 hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki.

17 Lakini ikiwa sisi wenyewe, kwa kutafuta kuhesabiwa haki katika Kristo, tulionekana kuwa wenye dhambi, je! Kristo amekuwa mtumishi wa dhambi? Hasha!’

Kumbuka Petro alijulikana kama nguzo katika kanisa, na hivyo ilikuwa ni rahisi kuaminiwa na kufuatwa kwa kila alichokuwa anakisema hata kama kwa namna Fulani kingeonekana kuwa sio sahihi, wengi bado wangemfuata tu, Na ndio maana tunasoma hapo biblia inasema, Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye…Lakini tendo Hilo halikumshutua sana Paulo, pengine mamia ya wayahudi waliobadilishwa kuwa wakristo walifuatana na unafki wa Petro, wakawa nao wanakula pamoja na mataifa, na wakiwaona tu wayahudi wenzao wanakuja wanajigeuza na kuwashurutisha mataifa nao washike sheria za kiyahudi kama vile kutahiriwa, kutokula vyakula najisi, kutawadha baada ya kula n.k. mambo ambayo walikuwa hawayafanyi wakiwa na watu wa mataifa peke yao..Ni kinyume na agizo la Bwana.

Lakini hayo yote hayakumshutua sana Paulo, wala hakuwataja myahudi mmoja mmoja aliyechukuliwa na unafiki wa Petro, lakini alikwenda moja kwa moja kumtaja Barnaba ..na kusema

“Na hao Wayahudi wengine wakajigeuza pamoja naye, hata na Barnaba pia akachukuliwa na unafiki wao”.

Hata na Barnaba pia??

Kwanini Paulo alimstaajabia Barnaba.

Tunasoma tena katika biblia Barnaba alikuwa ni mtume mwenye karama ya kitofuati sana na wengine katika kanisa, aliitwa mwana wa faraja (Matendo 4:36), hakuwa tu faraja kwa ndugu wa kikristo peke yake bali alikuwa pia faraja kwa kanisa la Kristo kwa ujumla, tunaona mwanzoni kabisa alikuwa tayari kuuza shamba lake ili tu kuhakikisha fedha inapatikana miguuni pa mitume kulihudumia kanisa Matendo 4:36-37).

Utaona tena wakati ambao Paulo ndio kwanza kaguezwa kuwa mkristo, na kanisa linamwogopa kushirikiana naye kutokana na historia yake ya nyuma kuwa mbaya ya mauaji, Barnaba ndiye aliyekwenda kumchukua Paulo na kumtambulisha kwa mitume, ndipo akakubaliwa kukaa nao. Biblia inasema alikuwa ni mtu aliyejaa Roho Mtakatifu, na kila alipokwenda alikuwa analithibitisha kanisa kwa karama ya faraja iliyokuwa ndani yake, Huyu ndiye baadaye alikwenda kumchuka tena Paulo kutoka Tarso na kumleta Antiokia ili kuhudumu naye..(Matendo 11:25)..

Na baadaye wakiwa katika ziara za kuhubiri injili mataifa mengine, wakiwa wote pamoja, waliondoka na kijana mmoja kwenda kuhubiri nao aliyeitwa Marko, lakini huyu Marko hakumaliza nao safari, hiyo ni baada ya kuona kuna ugumu mbeleni, hivyo alirudia katikati na kuwaacha Paulo na Barnaba wakiwa katika nguvu chache, suala lile halikumpendeza sana Paulo, hivyo katika awamu ya pili ya kwenda kuhubiri tena wakati Paulo na Barnaba wanataka sasa kwenda kuyahakiki makanisa, huyu kijana Marko akataka kufuatana nao lakini Mtume Paulo kwasababu hakuwa na karama ya faraja na uvumilivu ndani yake hakumruhusu aongozane naye, akamchukua Sila badala yake..Lakini Barnaba hakutaka amuache akaondoka na Marko.

Huyu Marko akiwa chini ya matengenezo ya Barnaba baadaye alikuja kujirekebisha na kuwa thabiti kweli kweli katika Imani, hadi mtume Paulo utakuja kusoma huko mbeleni anasema anamfaa sana kwa utumishi. (2Timotheo 4:11). Na ndio huyu huyu aliyekuja kuandika kitabu cha Marko. Lakini kama Barnaba angemuacha, leo hii tungepata wapi injili nzuri ya Kristo kama ile ya Marko?, vilevile angemwacha Paulo, kule Tarso, au angemwacha kule mwanzoni alipokuwa anakataliwa na makanisa yote injili ya Paulo ingeeneaje katikati ya mataifa na kwetu sisi pia?.

Barnaba alikuwa amejitoa, hata suala la mke kwake halikuwa la muhimu sana, alizunguka kuyathibitisha tu kanisa kwa karama yake ya faraja iliyokuwa ndani yake, hususani kwa wakristo waliokuwa wanasumbuliwa na sheria za wayahudi, na wapagani..yeye alipokuwa akienda mafundisho yake tu na uwepo wake tu, basi kanisa lilisimama tena na kupata nguvu mpya.

Hivyo Paulo alimchukulia kama mlevi wa karibu wa Huduma yake na Kanisa la Kristo kwa ujumla, alijua atakapokuwepo Barnaba mambo yote yatakuwa sawa..Lakini sasa hapa anaona amekutana na Mtume Petro, na kibaya Zaidi anachokifanya yeye, ni kinyume na kitu Mungu alichokiweka ndani yake.

Mpaka Paulo anasema..Mpaka na wewe Barnaba?..Ni nini kimekutokea? Wewe huduma yako ni msingi wa kuwajenga mataifa imekuwaje umechukuliwa tena na unafki wa hawa wengine??..Wewe ndio ungepaswa uwakemee hawa wayahudi waache kuwataabisha mataifa waliomwamini Kristo wasijisumbue na torati, lakini leo hii na wewe umekuwa huzuni kwao badala ya faraja?

JE! NA SISI LEO TUNAAMBIWAJE?

Biblia inasema..

Ufunuo 3:11 “Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako”.

Bidii zetu katika kumtumikia Mungu tusiruhusu kuzimishwa na mtu yeyote,kisa yeye anacheo Fulani au ni kiongozi Fulani, kumbuka anayeweza kuchukua taji lako, sio tu shetani, bali hata askofu wako, mchungaji wako, kiongozi wako wa kiroho anaweza kuchukua na kukimbia nalo ukabakia huna kitu..Pale anapotaka kuizimisha karama yako ili tu matakwa yake binafsi yafanikiwe..Na wote mnajua kabisa mnachokifanya sio sahihi lakini bado mnaendelea kukifanya!! Pale Mungu anapokupa karama ya uponyaji, ulikuwa unawaombea watu wengi wanaponywa, lakini kanisani kwako wanakuambia hatuamini kama kuna uponyaji wa ki-ungu na wewe umeacha kutumia karama hiyo? ..Mungu anakuuliza Je! Hata na wewe umechukuliwa na unafki wao?

Pale Mungu anapokupa karama ya kunena kwa lugha, lakini kanisani kwako hawaamini mambo kama hayo, na wewe unawatii tu ili kuwapendezesha, Bwana anakuambia Je! Na wewe umechukuliwa na unafki wao?, Pale unaposikia ndani kuhimizwa kusali masafa marefu, lakini nyie mmefundisha tu kusoma liturjia za kimapokeo, Na huku unajua kabisa moyoni mwako unachokifanya sio sahihi na unaendelea kubaki hapo, Bwana anakuambia JE! Na wewe umechukuliwa na unafki wao?

Unajua kabisa moyoni mwako unahitaji wokovu, unamuhitaji Yesu ayabadilishe Maisha yako, lakini kwasababu Padri wako amekuambia ukipata kipaimara na komunio inatosha unamsikiliza na huku rohoni unazidi kutetereka..Roho Mtakatifu anakuambia Je! Na wewe unataka kuchukuliwa na unafki wao?

Toka huko!! Umgeukie Kristo, uanze kuishi kulingana na Neno la Mungu, Ili Mungu akutumie kwa jinsi apendavyo, na taji lako halitatwaliwa na mwingine. Kumbuka tena anayetwaa taji lako ni mtu si malaika wala shetani…Biblia inasema… Ufunuo 3:11 “Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije MTU akaitwaa taji yako”.

Ubarikiwe sana

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/01/11/hata-na-barnaba-pia-akachukuliwa-na-unafiki-wao/