BARAKA ZA WAZAZI KWA WATOTO.

by Admin | 6 February 2024 08:46 am02

Masomo maalumu kwa wazazi/walezi.

Je unazijua kanuni za kuwabariki watoto wako?.. Wengi tunaijua kanuni moja tu ya kuwatamkia Baraka!..Hiyo ni sahihi kabisa na ipo kibiblia..(kwasababu maneno ya kinywa yana nguvu).

Lakini ni vizuri kufahamu jambo moja, kama Maneno yako hayataambatana na matendo yako, uwezekano wa hayo uliyoyasema kutokea bado utakuwa ni mdogo sana.

Kama unataka mtoto wako apate Baraka zote ulizozitamka juu yake, (na kwa njia ya maombi) ikiwemo Baraka katika kumjua Mungu, kuwa na afya na mafanikio, basi ongezea yafuatayo..

   1.MFUNDISHE SHERIA ZA MUNGU.

Wafundishe watoto wako sheria za Mungu, huku wewe mwenyewe ukiwa kielelezo cha kuzifanya, ili wasione kama ni sheria tu za MUNGU bali hata zako wewe mzazi!.. Mtoto wako anapaswa azione sheria za Mungu kama ni za kwako wewe. Lakini asipoona wewe mwenyewe ukizifanya hata yeye hataweza kukusikiliza wala kuzitenda, hata kama kwa mdomo atakuitikia.

Mithali 1:8 “Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako,

9 Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako, Na mikufu shingoni mwako”.

   2. USIMNYIME MAPIGO.

Yapo makosa yanayoweza kurekebishwa kwa maneno peke yake na mtoto akajengeka na kubadilika, lakini yapo yanayohitaji kurekebishwa kwa maneno pamoja na kiboko, hususani yale ya kujirudia rudia tena ya makusudi.

Biblia inasema ukimpiga hatakufa bali utakuwa umemwokoa roho yake na kuzimu.. (Hapo utakuwa umembariki pakubwa Zaidi ya kumtamkia tu baraka za maneno halafu hufanyi chochote).

Mithali 23:13 “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.

14 Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu”.

   3. MFUNDISHE KUSHIKA ELIMU

Badala ya kumtakia tu Baraka kwa kinywa (au kumwombea tu katika chumba chako cha ndani), tenga muda wa kumfundisha Umuhimu wa Elimu (kwanza ya Mungu) na pili ya dunia… Hapo utakuwa umembariki kwa vitendo na si mdomo tu.

Mithali 4:13 “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako”

    4. MFUNDISHE KUSHIKA SHERIA ZA NCHI na KUWAHESHIMU WENYE MAMLAKA (Wafalme).

Badala ya kumtamkia tu mafanikio, na kumwombea.. tenga muda kumfundisha umuhimu wa kuwatii wenye mamlaka na kuzingatia sheria ya nchi, hiyo itakuwa Baraka kwake katika siku zijazo za maisha yake.

Mithali 24:21 “Mwanangu, mche Bwana, NA MFALME; Wala usishirikiane na wenye kigeugeu;

    5. MFUNDISHE KATIKA NJIA INAYOMPASA

Ni njia gani inampasa katika umri wake na jinsia yake?.. Je! Katika umri wake huo anapaswa amiliki simu??..je katika umri wake anapaswa asemeshwe maneno hayo unayomsemesha?..je katika umri wake anapaswa atazame hayo anayoyatazama katika TV?.. je katika umri wake huo anapaswa awepo hapo alipo?..anapaswa afanye hicho anachokifanya?.Je! Kwa jinsia yake anapaswa kuvaa hayo mavazi unayomvika??..

Ni muhimu sana kujua mambo yampasayo mwanao/wanao kwa rika walilopo na jinsia zao…

Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”

Ukiyafanya hayo na mengine kama hayo pamoja na MAOMBI umwombeayo kila siku, basi utakuwa umembariki mwanao/wanao  kweli kweli.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

JE! UMEYABATILISHA MAMBO YA KITOTO?

FIMBO YA HARUNI!

MANENO YA MUNGU YANAPINDULIWAJE?

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?

MAOMBI YA KUOMBEA WATOTO.

Rudi nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/02/06/baraka-za-wazazi-kwa-watoto/