Kwanini wale askari walirudi nyuma, wakaanguka chini (Yohana 18:6)

by Admin | 14 June 2024 08:46 pm06

Kijeshi kushindwa kumtambua adui yako mpaka adui yako anajitambulisha kwako tena mbele ya macho yako ni ishara kubwa ya kushindwa mapambano.

Ndivyo ilivyokuwa kwa wale askari, walipofika na ujasiri wao mwingi, wakiwa na wazo la kumkamata mlengwa wao, tunaona mambo yalikuwa ni tofauti, kwasababu viashiria na matarajio yaliyokuwa kichwani mwao, hayakuweza kumfunua ni nani miongoni mwao ndiye mlengwa, huwenda wengine walidhani hayupo amekimbilia mapangoni kama Daudi. Lakini Yesu baada ya kuona wanahangaika sana ndipo akawauliza mnamtafuta nani.. Na wao kwa ujasiri wakajibu Yesu Mnazareti.. Yesu akasema ni mimi hapa! Tusome;

Yohana 18:3-8

[3]Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha.

[4]Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta? 

[5]Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. 

[6]Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini. 

[7]Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakasema, Yesu Mnazareti. 

[8]Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao. 

Hivyo kibinadamu kwa taarifa hizo za ghafla nguvu lazima zikuishie, na kunyong’onyea ujikutapo kwenye mazingira kama hayo. Ni mfano tu wa ile habari ya Elisha (2Wafalme 6:8-23), Mfalme wa Shamu alituma majeshi kwenda kumkamata kwasababu alikuwa anatoa siri za ufalme wake kwa mfalme wa Israeli. Na hiyo ikapelekea washindwe sana mbele ya wayahudi. Lakini tunaona walipomfuata Elisha, alimwomba Mungu jeshi zima lipigwe upofu wasimtambue. Ndipo Elisha akalipeleka hilo jeshi katikati ya mji. Na baadaye akaomba wafumbiliwe macho, wakafumbuliwa wakagundua kumbe adui yao ndiye aliyekuwa kiongozi wao wa mbele. 

Nguvu ziliwaishia kujikuta katikati ya maadui zao, wakifahamu kinachofuata ni kifo. Lakini Elisha hakuagiza wauliwe, bali aliwaombea kwa mfalme wapewe chakula wale wanywe kisha waondoke. Ndipo walipoondoka, hawakurudi tena kuwasumbua Israeli kwa kipindi kirefu. Kwasababu waliwapaliwa makaa ya moto kichwani.

Inamfunua Kristo kwa wakati ule, maadui zao walipofika pale bustanini, hakuwaua kwasababu alikuwa na uwezo huo, lakini alipokatwa sikio, mmojawapo wa wale askari alikuwa radhi kumponya, (kumfanyia huduma). 

Na zaidi sana alikuwa tayari kuondoka na wale askari kuuawa nao, jambo ambalo Elisha hakufanya. Ili tu yeye afe taifa zima lipone..ni upendo wa namna gani huu usioweza kuelezeka aliuonyesha!.

Na kwa kifo chake hawakupona wayahudi tu, bali mpaka ni sisi watu wa mataifa kwa vizazi vyote, tumepona. Utukufu na heshima ni zake milele na milele.

Kwa hitimisho ni kuwa wale askari waliorudi nyuma wakaanguka chini, haikuwa bure hure, yote hiyo ilikuwa ni kufuatana na mwitikio wa Yesu kwao ambao hawakuutazamia. 

Ni kutufundisha kuwa mawazo ya Mungu, sio mawazo yetu, rehema zake na fadhili zake na huruma zake ni nyingi kiasi ambacho kinaweza kumfanya mwanadamu aanguke na kutetemeka, kwa mwitikio wake mkuu wa upendo kwa wenye dhambi.

Je! Umempokea Kristo? Kumbuka lengo lake ni kukuvuta ili usiangukie hukumu. Okoka leo

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Swali: Je idadi ya askari waliohesabiwa katika 1Nyakati 21:5 na 2Samweli 24:9 inajichanganya?.

Nini maana ya “Uweza wa kifalme utakuwa begani mwake” (Isaya 9:6)?.

Nini maana ya Dirii, Chapeo na Utayari?(Opens in a new browser tab)

(Opens in a new browser tab)

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/06/14/kwanini-wale-askari-walirudi-nyuma-wakaanguka-chini-yohana-186/