AINA SABA (7), ZA SIFA KIBIBLIA.

by Admin | 1 July 2024 08:46 pm07

Katika biblia zipo aina mbalimbali za kumsifu Bwana, lakini kuna kuu saba ambazo zilitambuliwa na wayahudi kwa wakati wote. Hivyo ni vema kuzifahamu ili wigo wako uwe mpana zaidi katika eneo hili la sifa. Kwasababu ndio huduma kuu tuliyonayo duniani kwa Mungu wetu. Kumbuka chakula chetu ni Neno, lakini chakula cha Mungu wetu ni Sifa zetu. Hivyo ni lazima tujue tunamsifuje yeye kiufasaha kwa jinsi apendavyo.

Hizi ni aina saba za sifa.

1.) Kucheza: Kwa kiyahudi huitwa ‘Hallal’

Hii ni aina ya kumsifu Mungu ambayo, mwimbaji hujidai, hujigamba mbele za Mungu wake kwa kuuhusisha mwili wake, yaweza kuwa kuruka kuruka, au kucheza.

Agizo hilo lipo katika Zaburi 149:3 Na walisifu jina lake kwa kucheza, Kwa matari na kinubi wamwimbie.

Ndio lile Daudi na Israeli wote walilolifanya walipokuwa wanalileta sanduku la Bwana Yerusalemu,

 2Samweli 6:14 Daudi akacheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote; na Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani.

15 Basi Daudi na nyumba yote ya Israeli wakalileta sanduku la Bwana kwa shangwe, na kwa sauti ya tarumbeta.

16 Ikawa, sanduku la Bwana lilipoingia mji wa Daudi Mikali, binti Sauli, akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akiruka-ruka na kucheza mbele za Bwana; akamdharau moyoni mwake.

Hivyo na wewe kama mtu uliyeokolewa na Kristo, kujidai kwa ujasiri wote mbele ya Mungu wako usijizuie, angalizo tu ni kwamba usifanye kidunia, kana kwamba unacheza dansi, huku moyoni mwako hakuna ibada. Hiyo sio sawa, lakini kumwimbia Mungu kwa kucheza hakuna kosa lolote ikiwa ni jambo la kububujika  moja kwa moja kutoka moyoni mwako.

2) Kuinua mikono: Kwa kiyahudi huitwa ‘Yadah’.

Hii ni aina ya kumsifu Mungu kwa kuinua mikono juu, Kama ishara ya kutambua tegemeo lako kwako, kama mtoto mdogo kwa mzazi wako anapomlilia. Na kuonyesha upendo wako wa dhati kwa Mungu wako.

Zaburi 63: 3 Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai; Midomo yangu itakusifu.  4 Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai; Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.

Kama mtakatifu jizoeze mara nyingi, kunyanyua mikono yako juu wakati unamwabudu Mungu, au wakati mwingine unapoomba. Binafsi, nimeona tofauti kubwa sana, niinuapo mikono yangu, pindi niombapo au nisifupo, najikuta nazama rohoni kwa haraka sana, zaidi ya napoweka mikono yangu chini. Kumbuka ile habari ya Musa, alipoinua mikono juu, Israeli ilishinda, lakini alipoweka mikono chini, Waamaleki walishinda. (Kutoka 17:11) Hivyo jifunze sana, kuiinua mikono yako juu, katika ibada zako.

3) Kuinama, kujusudu, kupiga magoti: Kwa kiyahudi huitwa ‘Barak’.

Hii ni aina ya kumsifu Mungu kwa kumbariki Mungu, lakini kwa kuonyesha heshima kubwa kama mfalme, kujishusha chini, kusujudu au kupiga magoti, kuonyesha yeye ni mkuu sana wa kuogofya zaidi ya wafalme wote na wakuu wote ulimwenguni.

Zaburi 5:7 Bali mimi, kwa wingi wa fadhili zako, Nitaingia nyumbani mwako; Na kusujudu kwa kicho, Nikilielekea hekalu lako takatifu.

Kama mwamini, sifa zako zisiwe za mdomo tu wakati wote, jifunze kupiga magoti, au kusujudu ni ishara ya unyenyekevu  wa hali ya juu. Fanya hivyo nyakati za sifa, nyakati za maombi.

4) Kusifu kusiko na maandalizi: Kwa kiyahudi huitwa Tehillah:

Aina ya kusifu moyoni mwako, kwa namna isiyo na maandalizi Fulani maalumu, mfano wa kwaya, ni nyimbo ambazo zitainuka  katikati ya mapito yako fulani, wakati mwingine unapopitia kutendewa mema mengi na Mungu, na hapo ghafla tu moyoni mwako unasikia kumsifu Mungu, kumpa utukufu.

Kwamfano Daudi alipokuwa anapitia magumu,au anashindaniwa na Mungu, akimtafakari Mungu, mara anaachilia kinywa chake, Mungu anaanza kububujisha nyimbo mpya ulimini mwake.

Mfano mwingine wa sifa kama hizi, ni pale Mungu alipowavusha wana wa Israeli, bahari ya Shamu, na kuona maadui zao wamefunikwa na habari, ndipo Israeli wote, pamoja na Miriamu na wanawake wakasimama kumwimbia Mungu nyimbo za Furaha (Kutoka 15).

Mfano mwingine ni pale Mariamu alipomtembelea Elizabeti, na kutolewa unabii kuwa atamzaa Masihi, alishangalia na ghafla  akafungua  kinywa chake kwa wimbo, kumsifu Mungu kwa namna hii,  (Luka 1:46-56)

Hivyo kila mkristo, katika majira yote, vipindi vyote, viwe vyepesi, viwe vingine, hana budi kutafakari na kufungua kinywa chake kumsifu Mungu kwa aina hii ya sifa ya Tehillah. Ni muhimu sana, na inampendeza, Mungu, hii haina maandalizi, haina mpangilio maalumu, hutoka moyoni mwako, kwasababu Fulani Mungu alizokuonekania.

5) Kusifu kwa vyombo vya muziki: Kwa kiyahudi huitwa “Zamar”.

Mungu aliwaagiza pia watu wake, wamwimbie si kwa vinywa vyao tu na makofi, lakini pia pamoja na kuchanganya zana mbalimbali za muziki.

Zaburi 150:3 Msifuni kwa mvumo wa baragumu; Msifuni kwa kinanda na kinubi;

4 Msifuni kwa matari na kucheza; Msifuni kwa zeze na filimbi;  5 Msifuni kwa matoazi yaliayo; Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.

6 Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Haleluya.

Ni wazi kuwa kuchanganya ala mbalimbali,kama vile gitaa, vinanda, filipi, tarumbeta, ngoma, zeze, marumba, n.k. Katika kumwimbia Mungu, huongeza ladha na hisia njema katika kumsifu, na hivyo hupendeza sana machoni pake. Wapo watu hawaamini katika matumizi ya vyombo. Lakini maandiko yanatuagiza tumsifu Mungu kwa hivyo.

6) Kusifu kwa kupaza sauti kuu: Kwa kiyahudi huitwa “Shabach”.

Aina hii ya sifa, ni kwa kupaza sauti yako juu sana kwa Mungu. Hii Huonyesha ujasiri wa Mungu unayemwabudu, na kuutangazia umati na ulimwengu kuwa yupo Mungu mahali hapo anayeabudiwa.

Zaburi 47:1 Enyi watu wote, pigeni makofi, Mpigieni Mungu kelele kwa Sauti ya shangwe.

Sifa hizi zina nguvu sana, ndio zile ambazo ziliangusha kuta za Yeriko. Wana wa Israeli walipoambiwa wapaze sauti zao kwa Mungu. Zile sauti hayakuwa makelele tu, bali zilikuwa ni sauti za kumtukuza Mungu.(Yoshua 6:20).

Tumwimbiapo Mungu, hatupaswi tuwe kama mabubu, au tuimbe kinyonge, au kwa kutegea-tegea. Mungu anajivunia sana watu wale wanaomwabudu kwa ujasiri, kwa kufumbua vinywa vyao na kupaza sauti zao kwa nguvu  kumwadhimisha yeye.

7) Kusifu kwa ukiri, shukrani, kutoa: Kwa kiyahudi huitwa “Todah”.

Ni aina ya sifa inayofanana na ile ‘Yadah’,ya  kumwinulia Mungu mikono kumwimbia. Isipokuwa hii, ni kumwadhimisha Mungu, kwa matendo ambayo bado hujayaona kwa macho. Kutambua uweza wa Mungu, hata kama huoni matokeo yoyote, na kumshukuru katika hayo. Hata pale ambapo hujisikii.  .

Mfano ya sifa hizi, ni labda wewe ni mgonjwa, daktari amekuambia una siku chache za kuishi, ukiangalia umeombewa mara nyingi hakuna matokeo yoyote, lakini unakumbuka Neno la Bwana linalosema ‘kwa kupigwa kwake sisi tumepona’. Unaanza kufurahi, ukimwinulia mikono Mungu na kumshukuru ukisema asante, Bwana kwa kuniponya, huku ukimsifu katika hali yako hiyo hiyo ya udhaifu.

Sifa hizo ni muhimu sana kwetu, na zinaugusa moyo wa Mungu kwa namna ya kipekee, Kwasababu kamwe haziwezi kuwa na unafiki ndani yake.

Hizi zinapaswa ziwepo ndani yetu wakati wote. Unakumbuka ahadi za Mungu ambazo bado huoni zimetimia, unamsifu Mungu sana kwa furaha kana kwamba umekwisha vipata vyote sasa, umetafuta kazi umekosa, unamsifu Mungu kana kwamba umepokea ripoti ya kuajiriwa.

Hizi ndio aina saba za sifa, ambazo ukiziachilia katika maeneo yako yote ya kiibada. Utampendeza Mungu sana. Lakini pia zinapaswa ziwe katika Roho na Kweli, tafsiri yake, ni sharti mtu umsifuye Mungu uwe umeokoka, umeshatambua kazi ya Kristo ya ukombozi kwenye maisha yako ipoje. Tayari wewe ni  mfuasi wa Kristo. Ndipo sifa hizo zitakubalika. Vinginevyo haziwezi kumpendeza Mungu hata kama utazifanya zote kwa ufasaha.

Ikiwa bado hujaokoka, na upo tayari kufanya hivyo leo. Basi kwa msaada unaweza fungua hapa kwa msaada wa mwongozo huo wa kumkaribisha Yesu maishani mwako.>>>>  KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

SAFINA NI NINI?

Je kumwimbia Mungu kwa kucheza ni sahihi kibiblia?

(Opens in a new browser tab)

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/07/01/aina-saba-7-za-sifa-kibiblia/