by Admin | 31 July 2024 08:46 am07
SWALI: Nini maana ya vifungu tunavyovisoma katika Wakolosai 2:18,
‘Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili;
JIBU: Tukianzia mistari ya juu anasema..
16 Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;
17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. 18 Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili;
Katika vifungu hivyo, Mtume Paulo anaanza kwa kuwaambia ‘mtu asiwanyang’anye thawabu yenu’. Akiwafananisha na wana-michezo ambao wanashiriki katika mashindano Fulani, ambao hujitahidi kwa kila namna kujizuia, na kujichunga ili wafanye vema katika mashindano hayo wachukue tuzo.
Sasa Paulo, anatoa angalizo, akirejea mfano wa washindani hao, yawezekana mwingine akamfanyia hila mwenzake, ili asiwe na ufanisi, kwenye michezo hiyo akashindwa kushiriki vema na kuchukua tuzo, kwamfano anaweza kumpa kinywaji Fulani ambacho kitadhoofisha uchezaji wake, au atamdanganya afanya zoezi Fulani, ambalo anajua kabisa halina manufaa kwake, kwamfano labda mchezaji ni mwana-riadha, utaona Yule mwingine anamwambia akanyanyue vyuma vizito atakuwa mwepesi kukimbia. Kumbe kukimbia hakuhusiani na misuli mikubwa bali pumzi.
Vivyo hivyo Paulo aliona kuwa kuna waalimu wa uongo, viongozi wa uongo,watakaozuka, kuwadanganya watu waiache njia sahihi, ya kukubaliwa na Mungu. Na ndio hapo anataja mambo matatu ambayo watakuwa nayo;
Jambo la kwanza,
Watachukua thawabu yao kwa kunyenyekea kwa mapenzi yao wenyewe tu,
Kunyenyekea sio kubaya, ni tunda la Roho Mtakatifu ndani ya mtu, na wakristo wote, tunasukumwa katika unyenyekevu. Lakini angalia hapo anasema kunyenyekea KWA MAPENZI YAKE MWENYEWE. Maana yake, ni kuwa hanyenyekei kwa mapenzi ya Mungu, bali yake. Na hiyo ni mbaya, kwasababu watu wa kidini leo hii ndio kanuni yao, hubuni njia zao za kumwabudu Mungu, na hiyo huwavutia watu wengi, waone kama ni Mungu kweli anaabudiwa, kwa unyenyekevu na heshima, nao wanaingia kwenye mkondo huo. Wanasahau kuwa ibada lazima ifanyike kwanza katika Roho na Kweli.
Mambo kama kusujudia, kuvaa mavazi Fulani meupe, kutawadha mwili, kuvua viatu katika nyumba za ibada, kuomba kwa sauti ya kuvuta sana, ya upole, huku umeinamisha kichwa chini, unaibusu biblia. Hudhanikuwa kuwa ndio hicho Mungu anakitaka, Lakini ndani, kinywa chake kina matusi, akitoka hapo anakwenda kuishi maisha kishirikina, na ulevi. Huo ni udanganyifu mkubwa sana.
Ndicho Paulo alichokiona kwa kanisa la Kolosai, kulitokea watu wanawaambia usile kambale ni chukizo kwa Mungu, shika siku ya sabato, inatosha.. Yote hayo yakifanyika kimwili. Lakini wasifundishe kwamba unyenyekevu wa ki-Mungu hutoka rohoni, ukisukumwa na neema katika Roho Mtakatifu, Ambapo mtu kupaswa kukubali wokovu kwanza, na kutii kwa kumfuata Kristo anayeweza kumfanya mtu kiumbe kipya, na sio jambo la kufanya kimwili tu, akidhani atampendeza Mungu.
Jambo la pili
wanaweza kuwanyang’anya thawabu yao kwa mafundisho ya kuabudu malaika.
Tangu zamani, kulikuwa na watu waliowaweka malaika katika nafasi ya Mungu. Na kuvuka ile mipaka ya kutuhudumia tu sisi (Waebrania 1:14). Hivyo ikiwa mtu alikuwa na karama Fulani ya maono, ambapo mengine huletwa kwa mikono ya malaika, tunaliona hilo mara nyingi tangu Musa, na wana wa Israeli jangwani, pamoja na mitume mpaka Yohana kule Patmo. Mungu aliwatumia malaika kwa sehemu kubwa kutufikishia sisi jumbe zake, kwasababu waliwekwa kutuhudumia sisi.
Lakini dini na imani zikazuka kuanzia hapo, kwa baadhi ya watu wakaanza kuwafanyia ibada, jambo ambalo ni chukizo kwa Bwana. Hata leo utaona zipo sala za malaika na watakatifu kuwataka wawaombee. Au wawasaidie vitani. Ikiwa wewe ni mtoto wa Mungu umeokoka, kuwa makini na ibada hizo, taabu yako kwa Mungu yaweza kuwa bure, kwasababu unamudhi Mungu. Ibada za namna hiyo hazina tofauti na ibada za majini. Usiabudu mwanadamu, wala kiumbe chochote kilicho mbinguni wala duniani.
Jambo la tatu
Na mwisho anasema wakijivuna bure kwa akili zao za mwili.
Kujivuna, maana yake kusifia vitu vya mwilini mfano vipaji vyao, wengine ujuzi wa kuongea vizuri, na kupangalia maneno, werevu, elimu za falsafa, mambo ambayo Paulo aliyaona, yakiwavuta wengi, na kuacha njia kamilifu ya Kristo iliyo katika neema, upendo, Imani na nguvu za Mungu. (2Wakorintho 11:18-20).
Injili inabadilishwa inakuwa vichekesho, na kanuni za ki-ujasiriamali,
Hata leo mimi na wewe ni kuwa makini, bidii yako katika Kristo isichukuliwe na udini, bali Neno, isichukuliwe na maono na karama, na ibada za malaika bali Mungu, isichukuliwe na falsafa za kibinadamu, na mwonekano, bali, Roho Mtakatifu na kweli, katika neema.
mtu asichukue taji lako
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 1)
JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 2)
Rudi Nyumbani
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/07/31/wakolosai-218-mtu-asiwanyanganye-thawabu-yenu/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.