by Admin | 1 August 2024 08:46 pm08
SWALI: Kwenye 2Wakorintho 8:18, Mtume Paulo anamtaja ndugu ambaye jina lake hajaliweka wazi. Ni kwanini afanye hivi tofauti na alivyozoea kufanya katika nyaraka zake nyingine, kuwataja aliowatuma?
2Wakorintho 8:18 Na pamoja naye tukamtuma ndugu yule ambaye sifa zake katika Injili zimeenea makanisani mwote.19 Wala si hivyo tu, bali alichaguliwa na makanisa asafiri pamoja nasi katika jambo la neema hii, tunayoitumikia, ili Bwana atukuzwe, ukadhihirike utayari wetu.
JIBU: Katika waraka huu, tunaona Paulo akiwaandikia kanisa la Korintho, suala la changizo kwa ajili ya watakatifu maskini waliokuwa Yerusalemu. Hivyo akawatuma pia na watatu ili kulifanikisha jambo hilo. Wa kwanza ni Tito, Ukisoma mstari wa 16-17, katika sura hiyo hiyo ya 8, anatajwa, wa pili ndio huyu ambaye sifa zake za injili zilivuma kwenye makanisa, na watatu ni ndugu mwingine ambaye pia hajatajwa jina, isipokuwa Paulo alimwita kama ‘ndugu yetu’ ambaye tunamsoma kwenye mstari wa 22
2Wakorintho 8:22 Nasi pamoja nao tumemtuma ndugu yetu tuliyemwona mara nyingi katika mambo mengi kuwa ana bidii, na sasa ana bidii zaidi sana kwa sababu ya tumaini kuu alilo nalo kwenu.
Watu hawa watatu ndio waliotumwa kwa ajili ya huduma hiyo ya changizo kwa wakorintho. Lakini swali huulizwa huyu ndugu wa pili ni nani hasaa?
Wengine husema ni Luka, wengine Barnaba, wengine Apolo, wengine Marko, Aristako. Kutokana na kwamba wengi wa hawa walisifika kwa usambazi injili, lakini pia walikuwa na Paulo mara nyingi kwenye huduma.
Lakini Hayo ni makisio tu, anaweza akawa miongoni mwa hawa, lakini pia asilimia kubwa anaonekana sio kabisa miongoni mwao, waliowahi kutajwa na Paulo.
Jambo la muhimu ambalo, linalengwa hapo, kufichwa kwa jina lake. Sio kwamba Mungu anataka tumchunguze ni nani? Hapana Lakini alipenda kutuonyesha kwamba SIFA, hujitambulisha zaidi kuliko jina.
Ukichunguza hapo, utaona Paulo anasema sifa zake zimeenea kwenye “makanisa yote”. Ikiwa na maana kuanzia huko Akaya mpaka Makedonia. Alijulikana kuwa mhubiri mwenye juhudi na mwenye kuthamini injili. Na si hivyo tu, walimchagua mwenyewe kusafiri pamoja na Paulo. Hivyo Paulo kuandika waraka huo, kwa kueleza sifa zake, aliona hilo latosha tu, kumtambulisha bila hata ya jina. Kwasababu hakuna mwingine zaidi yake. Yaani kwa namna nyingine Paulo anasema, “Mpaka hapo mmeshamtambua ni nani”.
Sikuzote wanaotambulishwa kwa majina huwa ni watu wasiojulikana, au wasio na sifa za kutosha kwenye jamii husika.
Ndivyo ilivyokuwa pia kwa Yule mtu wa tatu ambaye Paulo alimwita kama “NDUGU YETU”. Kulikuwa hakuna haja ya kumtambulisha kwa jina kwasababu walikuwa wanamwona wakati wote akiwa na akina Paulo katika ziara zake na huduma. Hivyo kumtafaja tu ndugu yetu ilitosha, alijua kila mmoja alielewa ni nani aliyekuwa anazungumziwa, kwasababu mitume hawakuwa na ndugu mwingine zaidi ya huyo, aliyekuwa karibu nao.
Hata leo, Bwana anapenda sisi tutambuliwe kwa SIFA zetu, zaidi ya MAJINA yetu. Kiasi kwamba kazi itakayoonekana kwa ajili ya Kristo, itutambulishe sisi, sio sisi tuyatambulishe majina yetu katikati ya watu.
Utaona baadhi ya wahubiri wanachokifanya, ni kutumia nguvu kubwa kutangaza majina yao, na sura zao, ili wajulikane, lakini kazi zao hazitambuliki. Hilo sio lengo la mhubiri, au Mtumishi wa Mungu. Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa duniani, haikuwa na muda wa kujitangaza, wakati mwingine hakutaka mambo yake yadhihirishwe kiwepesi, mpaka atakapomaliza kazi yake, Na sisi pia tupende aina hii ya utumishi.
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Epafrodito ni nani kwenye biblia?
Epafra ni nani katika biblia? (Wakolosai 1:7)
Je ni sawa kuukubali udhaifu kama mtume Paulo alivyojisifia kwa huo? (2Wakorintho 12:9-10)
Rudi Nyumbani
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/08/01/ndugu-yule-anayezungumziwa-kwenye-2wakorintho-818-ni-nani/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.