1 Petro 3:3 “Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi”.
Sasa kuvaa mavazi si vibaya, hata hivyo tunapaswa tuvae mavazi, (hilo ni agizo la Bwana tangia Edeni, Bwana Mungu alipowafanyia mavazi ya ngozi wazazi wetu wa kwanza).
Lakini hapo katika 1Petro 3:3 hasemi “kuvaa mavazi”..bali na anasema “kuvalia mavazi”.
Kuna tofauti ya “kuvaa” na “kuvalia”.
Kuvalia maana yake “hayo mavazi yamelengwa kwa kusudi maalumu la kutazamwa na watu”
Kwamfano makahaba (wanawavalia mavazi ya kikahaba wateja wao ili miili yao iuzike vizuri). vile vile wahuni wanawavalia mavazi wahuni wenzao ili watazamwe na wao.
Kijana wa kiume anayevaa suruali ya kubana huyo hajavaa mavazi bali “amevalia mavazi”…. amewavalia mavazi aina fulani ya watu (wahuni wa kike), ili wamtazamapo wamtamani.
Dada anayevaa suruali ya aina yoyote ile, anakuwa hajavaa mavazi bali kavalia mavazi (kamvalia mtu),
Na lengo lake si lingine zaidi ya kutaka kutamaniwa, na Neno la Mungu linasema “yeyote amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye nafsini mwake”
Kwahiyo mwanamke anayetazamwa na kutamaniwa kwa uvaaji wake, naye pia kazini na yule aliyemtamani (hiyo ni kulingana na Neno la Mungu).
Kama unavyokuwa makini na kile kinachoingia ndani yako (yaani chakula)...vile vile ongeza umakini kwa kila unachojivika nje.
Usiwe mwepesi wa kwenda na kila fasheni inayoingia…kiasi kwamba kila mtindo unaoingia unaupokea, ni lazima uchague kama unavyochagua chakula.
Ni lazima uwe na uchaguzi unaokufaa kama vile ulivyo na uchaguzi wa baadhi ya vyakula vikufaavyo.
Jiulize je hilo vazi la mgongo wazi kama umevaa au umevalia,?…
Hilo vazi linaloonyesha kitovu na mapaja je umevaa au umevalia?
Hiyo kaptura kijana uliyoivaa na kutembea nayo barabarani umevaa kwa lengo gani?..je unamvalia nani?
Jisitiri, na pia jiheshimu.
Bwana akubariki.