Kwanini Mungu auweke Mti wa Mema na Mabaya katikati ya bustani?

by Admin | 13 December 2024 08:46 am12

Swali: Kulikuwa na sababu gani ya Bwana MUNGU kuuweka mti wa mema na mabaya katikati ya bustani ili hali anajua kuwa mti huo ndio utakaowakosesha Adamu na Hawa, kwanini Mungu asingeondoa, na kuubakisha tu ule mmoja wa uzima katikati ya bustani?


Jibu: Ni kweli inaweza kuonekana ni busara mti mmoja tu kuwepo pale bustanini lakini ukweli ni kwamba endapo Mti mmoja tu ungekuwepo pale bado MTI WA UZIMA, usingeeleweka na wala maana yake isingekuwepo..

Kwani ili kuuthibitisha wema lazima uwepo ubaya mahali fulani… kwasababu wema hauwezi kujilikana kama ubaya haujadhihirishwa, vinginevyo ule wema utaonekana ni kitu cha kawaida, lakini ukifunuliwa ubaya ndipo wema unapopata kujulikana na kueleweka.

Nuru haiwezi kujulikana kama ni njema na kitu kizuri, kama giza halipo.. lakini ili Nuru ipate sifa, na kuheshimika ni lazima giza liwepo mahali ili nuru ilishinde giza.

Vile vile Mungu aliuweka ule mti wa ujuzi wa mema na mabaya ambao matunda yake ni MAUTI, ili kuuthibitsha MTI WA UZIMA ambao matunda yake ni UZIMA.

Adamu na Hawa wasingeweza kuelewa nini maana ya UZIMA kama kisingekuwepo kingine kinachoelezea/kuhubiri MAUTI, vile vile hata sisi leo tusingejua Uzima ni nini kama MAUTI isingekuwepo, vile vile hatuwezi kujua Amani ni nini, kama hatujawahi kusikia kuhusu vita, au kupitia vita..

Hatuwezi kujua umaskini ni nini kama hatujawahi kuona utajiri, vile vile hatuwezi kujua utajiri ni nini kama hatuwahi kuona au kupitia umasikini,.. hatuwezi kujua kuwa tuna afya kama hatujawahi kuona wagonjwa, wala hatuwezi kujijua kuwa tuna ugonjwa kama hatujawahi kuona wenye afya, au sisi wenyewe kuwa na afya, huwezi kujua hiki ni kirefu kama kifupi hakipo, wala huwezi kujua hiki ni kirefu kama kifupi hakijawekwa mahali kama mfano.

Hivyo utaona kuwa uwepo wa vibaya au vyenye kasoro ni ili kuvithibithisha vile vilivyo vizuri na visivyo na kasoro.. Na lengo la Mungu kuuweka mti ule wa ujuzi wa mema na mabaya lilikuwa ni kuwapa kuelewa Adamu na Hawa Uzima ni nini, na thamani yake, na ili wauthamini na kuushika… na wala lengo lake si kuwatega!.

Hebu pia tengeneza picha miili yetu isingekuwa na maumivu, je unadhani ni nini kingetokea?…bila shaka hakuna mtu ambaye angehangaika kuutunza… hakuna mtu angeogopa kujikata na kisu, au kutembea peku kwenye miiba, au kunywa maji ya moto yale yanayotokota… lakini maumivu yamewekwa ili tujue na kutamani kuwa katika hali ya kutokuwa na maumivu na vile vile kuitunza miili yetu na kuushikilia uzima vizuri .

Hali kadhalika uwepo wa mti ule wa ujuzi wa mema na mabaya ni ili kuuthaminisha mti wa UZIMA. Ili mtu ajue umuhimu wa UZIMA, na RAHA ya Uzima, faida za uzima.

Je wewe umempokea YESU, na kuoshwa dhambi zako? Kumbuka YESU ndiye njia ya Mti wa UZIMA, na yeyote anayempokea humpa matunda hayo na kuishi milele, ndani yake.

Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”.

Ufunuo 2:7 “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu”

Bwana akubariki.

Kujua kwanini BWANA MUNGU awazuie wasile matunda ya Mti wa Uzima baada ya kula ya ujuzi wa mema na mabaya fungua hapa >>>

Kwanini Bwana MUNGU aliwazuia Adamu na Hawa wasile matunda ya Mti wa uzima waishi milele?

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Rudi Nyumbani

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/13/https-wingulamashahidi-org-2024-12-06-kwanini-mungu-auweke-mti-wa-mema-na-mabaya-katikati-ya-bustani/