by Admin | 13 December 2024 08:46 am12
Swali: Je kipindi Ibrahimu anatoka Uru ya Ukaldayo, hakuwa anajua anakokwenda kwamba ni Kaanani? au alikuwa anaongozwa na Roho Mtakatifu mpaka pale alipofika, ndipo Bwana akamwambia hapo hapo atulie?…na mbona tukisoma Mwanzo 12:5 tunaona kama Abramu alikuwa anajua kabisa anakoelekea, au je biblia inajichanganya?
Jibu: Biblia, Neno la Mungu halijichanganyi kamwe..
Turejee …
Waebrania 11:8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka ASIJUE AENDAKO”.
Hapa ni kweli panaonesha kuwa Ibrahimu alikuwa hajui aendako, lakini hebu tusome maandiko mengine ndipo tutapata kuelewa zaidi..
Mwanzo 12:1 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;
2 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka………………
5 Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani”
Hapa panaonyesha kuwa Abramu alikuwa anajua anakokwenda, kuwa ni Kaanani, Je lipi ni sahihi?
Jibu ni kwamba Abrahamu alikuwa anajua anakokwenda isipokuwa alikuwa hajui kama nchi hiyo aiendeayo (yaani ya Kaanani) kama ndio itakuwa ya ahadi..
Hivyo alienda mpaka alipofika na alipofika ndipo Mungu akamtokea na kumwambia kuwa nchi hiyo aliyopo ndiyo itakuwa milki yake (ya ahadi).
Mwanzo 12:5 “Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani.
6 Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo.
7 BWANA akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu BWANA aliyemtokea”
Sasa swali linakuja, je ni kitu gani kilichomwelekeza Abramu aende nchi ya Kanaani na si nchi nyingine?
Tulirejea ule mlango wa 11 wa kitabu cha Mwanzo, tunasoma kuwa wazo la kuhama Uru wa Wakaldayo na kuelekea Kanaani halikuanzia kwa Abramu, bali lilianzia kwa baba yake aliyeitwa Tera, huyo ndiye aliyefikiri kuhama Ukadayo na hata kuchukua hatua ya kuhama pamoja na watoto wake wote ikiwemo Abramu.
Mwanzo 11:31 “Tera akamtwaa Abramu mwanawe, na Lutu mwana wa Harani, mwana wa mwanawe, na Sarai mkwewe, mke wa Abramu mwanawe, wakatoka wote katika Uru wa Wakaldayo, waende nchi ya Kanaani, wakafika mpaka Harani wakakaa huko”.
Umeona hapo?..sio Abramu aliyekuwa na wazo la kuondoka Ukaldayo bali ni Tera, na sababu za kuwaondoa kule hazijulikani, kwani biblia haijaweka wazi, labda huenda ni maasi ya nchi hiyo, au sababu nyingine za kijamii au kibiashara.
Lakini katika wazo hilo la kuhama, lilikuwepo pia kusudi la Mungu ndani yake, kwamba Abramu afike Kanaani.
Hivyo kwa hitimisho ni kwamba Abramu alijua anakoenda, lakini hakujua nchi atakayopewa mpaka alipofika.
Nini tunajifunza hapo?
Wakati mwingine Bwana anaweza kutumia wazo la mtu mwingine kukupeleka wewe mahali Mungu anapotaka uwe.
Hivyo wakati mwingine usinung’unike unapoona unahamishwa mahali ulipo, kwani pengine Mungu anakupeleka mahali anapotaka wewe uwe, na ukishafika ndipo atakuonyesha.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/13/je-kweli-abramu-alikuwa-hajui-aendako-kulingana-na-waebrania-118/
Copyright ©2024 unless otherwise noted.