by Admin | 19 December 2024 08:46 am12
Silaha ya Mwisho mwisho kabisa ya adui kumshambulia Mtu ni “ULIMI WA UOVU”.. Ukiona Maneno ya uongo kuhusu wewe, au ya vitisho au ya uchonganishi yanatembea huku na huko basi fahamu kuwa adui ndio yupo katika hatua za mwisho mwisho, kukuacha!..(Ni wakati wa kumaliza jaribu).
Na kama ukiweza kusimama katika hiko kipindi bila hofu, wala kutetereka wala kurudi nyuma, basi shetani unaweza usimwone tena baada ya hapo, kwa kipindi kirefu sana.
Mfano katika biblia tunamwona Nabii Yeremia,
Adui alimtafuta mara nyingi kwa njia mbalimbali ili amnyamazishe asitoe unabii, lakini kila alichojaribu ili kumzuia Yeremia asitoe unabii, kilishindikana, na ndipo akatumia silaha yake ya mwisho ya NDIMI ZA UOVU, ili yamkini amtishe Yeremia, lakini pia haikusaidia,
Yeremia 18:18 “Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na TUMPIGE KWA NDIMI ZETU, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote.
19 Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami”.
Wakati huo kilitokea kikundi kiovu na kuanza kumtisha Yeremia kwa maneno mengi, na pia kumzushia mambo mengi na zaidi ya yote, ya uchonganishi na kumchafua mbele ya Mfalme, ili tu Yeremia akamatwe asiendelee kutoa unabii.
Yeremia 38: 4 “Ndipo wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari.
5 Naye mfalme Sedekia akasema, Tazama, yu mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lo lote kinyume chenu”.
Mtu mwingine aliyepigwa kwa NDIMI OVU ni nabii Danieli, soma Danieli 6..
Sasa kwanini Adui, aiweke hii silaha ya ulimi kama chaguo lake la mwisho?… Ni kwasababu anajua ulimi wa mtu unaweza kuwasha moto mkubwa, na kama mtu hatakuwa na Imani ya kutosha basi anaweza kuanguka kabisa…
Yakobo 3:6 “Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum”
Hivyo shetani anaweza kukuwashia tu moto kupitia ulimi wa mtu au ndimi za watu, na moto huo ukawa mkubwa sana, kiasi kwamba kama huna imani na ujasiri wa kutosha, unaweza kurudi nyuma kabisa.
Shedraka, Meshaki na Abednego walijikuta wapo katika tanuru la Moto, kwasababu tu ya baadhi ya watu waliotumia ndimi zao kupeleka mashitaka kwa mfalme kuwa hawataki kuisujudia ile sanamu.(Danieli 3:8-12).
Danieli naye alijikuta katika tundu la simba kwasababu tu ya vinywa vya watu, na Yeremia naye alijikuta katika lile shimo refu lenye giza lililojaa matope kwasababu ya maneno ya watu(Yeremia 38:6)..
Lakini wote hao walishinda, kwani moto ule uliokusudiwa juu yao uliwala maadui zao, na mashimo yale na matundu yale yaliyokusudiwa juu yao yaliwaharibu maadui zao, lakini kama wangetetemeka na kuogopa na kurudi nyuma bila shaka wangepotea kwa kuharibiwa na ibilisi!.
Na sisi hatuna budi kusimama Imara bila hofu, kwa ujasiri mwingi pale ambapo adui anatumia NDIMI za watu kama silaha yake…
Hiko ni kipindi cha kuwa na imani na ujasiri….mipango inapopangwa ya vitisho au uchonganishi, havitasimama endapo wewe utasimama.
Ni wakati kusimama na kuamini huku tukiomba, na silaha za ndimi zao zitaanguka, na Bwana atatukuzwa.
Ifuatayo ni mistari inayozungumzia hatari ya NDIMI ZA UOVU…
Zaburi 57:4 “Nafsi yangu i kati ya simba, Nitastarehe kati yao waliowaka moto. Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale, Na ndimi zao ni upanga mkali.”
Zaburi 64: 2 “Utanificha mbali na shauri la siri la watenda mabaya, Mbali na ghasia ya watu wafanyao maovu;
3 Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu,
4 Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi.
5 Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona”
Zaburi 140:1 “Ee Bwana, uniokoe na mtu mbaya, Unihifadhi na mtu wa jeuri.
2 Waliowaza mabaya mioyoni mwao, Kila siku huondokesha vita.
3 Wamenoa ndimi zao kama nyoka, Sumu ya fira i chini ya midomo yao”.
Lakini pamoja na kwamba adui anatumia ndimi kutushambulia, vile vile na sisi tunaweza kutumia ndimi hizo hizo, kumharibu.
Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”
Tunampiga shetani kwa ndimi zetu, kwa njia ya KUOMBA, na hususani maombi yanayohusisha mfungo.
Bwana atubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2024/12/19/tutampiga-kwa-ndimi-zetu/
Copyright ©2025 unless otherwise noted.