Ni kitu gani umekichagua kwenye nyumba ya MUNGU katika mwaka huu?..Je nafasi fulani, au cheo, au umaarufu, au nini?.
Kumbuka Nyumba ya MUNGU ni zaidi ya jengo la Ibada, bali pia Miili yetu ni nyumba ya MUNGU.
Yohana 2:20 “Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?
21 Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake”.
1 Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?”
Soma pia 1Wakorintho 6:19, utazidi kuelewa vyema.
Sasa kama Miili yetu ni HEKALU LA MUNGU, yaani NYUMBA YA MUNGU ni kipi umekiamua juu ya Mwili wako katika mwaka huu mpya?, kwamaana Neno linasema Utakatifu ndio ufaao nyumba ya MUNGU, na tena haufai siku moja tu, bali milele…..
Zaburi 93:5 “Shuhuda zako ni amini sana; UTAKATIFU NDIO UFAAO NYUMBA YAKO, Ee BWANA, milele na milele”.
Chagua utakatifu wa mwilini na rohoni huu Mwaka, usiishi tena kwa kuuchafua mwili wako kama ilivyouchafua mwaka jana, au miaka iliyopita, anza mwaka na mambo mapya.
Anza kujenga ushuhuda mpya, badilika kimwonekano, watu watakapokutazama waone waseme hakika yule ni mkristo, na watakapokuuliza usema “UMECHAGUA UTAKATIFU KWA MAANA NDIO UFAAO NYUMBA YA MUNGU”.
Sema mwaka huu sio mwaka wa Kushindana na mtu kimavazi ndani ya nyumba ya MUNGU, sema mwaka huu ni wakati wa kuipamba nyumba ya MUNGU kwa utakatifu.
Sema mwaka huu ni mwaka wa kuhubiri UTAKATIFU kila mahali, kwamaana pasipo huo hakuna mtu atakayemwona Mungu (Waebrania 12:14).
2 Wakorintho 7:1 “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu”.
Hili ni neno fupi la mwaka kwako.
Bwana atusaidie sana..
Shalom.