Luka 17:12 “Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali,
13 wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!
14 Alipowaona aliwaambia, Enendeni, MKAJIONYESHE KWA MAKUHANI. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika”.
Sababu kuu ya Bwana YESU kuwaagiza hawa wakome wakajinyeshe kwa Makuhani ni kwasababu Makuhani ndio watu wa mwisho kutangaza kama mtu ni Mkoma au si Mkoma, baada ya uchunguzi.
Kwani zamani mtu akihisiwa au akijihisi mwenyewe kama ni mkoma basi sheria ilikuwa ni kwamba anaenda kwa Kuhani, na kisha kuhani anauchunguza mwili wake na baada ya uchunguzi akibainika kwamba anao Ukoma, basi huyo mtu anakuwa najisi na anatengwa,
Sheria hiyo tunaisoma katika kitabu cha Mambo ya Walawi Mlango wa 13.
Walawi 13:9 “Pigo la ukoma litakapokuwa katika mtu, ndipo ataletwa kwa kuhani;
10 na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pana kivimbe cheupe katika ngozi yake, na malaika yamegeuzwa kuwa meupe, tena ikiwa pana nyama mbichi iliyomea katika kile kivimbe,
11 ni ukoma wa zamani ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa yu najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye yuna unajisi”
Kwahiyo endapo wale watu kumi wenye ukoma wangefika kwa Kuhani na baada ya kukaguliwa wakakutwa na madhaifu hayo yaliyotajwa hapo juu, basi wangekuwa NAJISI..maana yake ni wenye ukoma ambao haujatakasika/kupona.
Na kama tayari walishachunguzwa zamani na kubainika wanao ukoma, na sasa wanarudia tena vipimo kwa kuhani ili kubaini kama ukoma wao umepona basi endapo wangekutwa. bado wanao basi wangeendelea kuwa najisi na kutengwa….
Lakini tunaona watu hao kumi (10) wakiwa njiani kuwafuata Makuhani ili waangaliwe, wakiwa njiani walijikuta wametakasika ule ukoma, walijikuta ngozi zao zimerudia hali zao za zamani, kama Naamani alivyoponywa ukoma wake. (2Wafalme 5:14).
Luka 17:14 “Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.
15 Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu;
16 akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria.
17 Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?
18 Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu”
Mambo makuu mawili ya kujifunza kufuatia habari hiyo
1.Uponyaji wa YESU unahitaji imani yenye Matendo.
Laiti kama hawa wenye ukoma wangeyadharau maneno ya Bwana YESU aliyowaambia kuwa wakajionyeshe kwa Makuhani, na wangeenda njia nyingine, hakika wasingepona, wangebaki vile vile.
Lakini walipochukua hatua ya kwenda kwa Makuhani, kumbe maili kadhaa mbele muujiza wao ulikuwa unawangoja, kama tu ilivyokuwa kwa Naamani alipoambiwa akajichovye mara saba Yordani.
Hali kadhalika na wewe, shida au ugonjwa wowote ulio nao, kazi uliyobakiwanayo ni moja tu, kuyaamini maneno ya Bwana YESU na kuendelea mbele katika Neno lake, Muujiza wako utakutana nao mbele, usianze kuutafuta dakika hiyo hiyo.
2. Kurudi kumpa MUNGU utukufu na kushuhudia.
Hili ni jambo la pili la kujifunza. MUNGU wetu anapendezwa na watu wa Shukrani.
Angalia mtu huyu alirudi kumshukuru MUNGU na kutoa ushuhuda na Bwana YESU akatafsiri tukio hilo ni kama kumpa MUNGU utukufu..
Huwenda MUNGU alishakutendea jambo fulani kubwa je uliwahi kurudi na kumtukuza mbele ya wengi?..Au je una mpango wowote wa kumtukuza katika hilo unalomwomba sasa akutendee?..Jibu unalo wewe.
Je tayari umempokea YESU?..Unao uhakika Bwana akirudi leo unaenda naye?.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea