Simoni Mkirene aliubeba msalaba wa Bwana Yesu au la?

by Devis | 7 June 2025 08:46 am06

Swali: Katika  Mathayo 27:31-32 tunasoma kuwa Simoni Mkirene alimsaidia Bwana kuubeba msalaba wakati anaelekea mahali pa kusulibishwa, lakini tukirudi katika Yohana 19:17-18 tunasoma kuwa hakusaidiwa na mtu badala yake aliubeba mwenyewe mpaka Golgotha, je mwandishi yupi yupo sahihi?.

Jibu: Turejee mistari hiyo..

Mathayo 27:31 “Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake.

33 Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa”

Hapa ni kweli Simoni Mkirene alimsaidia Bwana kuubeba msalaba..

Lakini hebu tusome tena Yohana 19:17-18..

Yohana 19:16 “Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.

17 Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.

18 Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati”.

Hapa inaonyesha ni kama hakusaidiwa na mtu mpaka alipofika Golgotha..

Je kwa mantiki hiyo biblia inajichanganya?…

Jibu ni La! Biblia ni kitabu kisicho na makosa wala mkanganyiko mahali popote, isipokuwa fahamu zetu na pambanuzi zetu ndizo zinazojichanganya.

Sasa tukirejea katika habari hizo mbili, ni kwamba Mwandishi wa kitabu cha Yohana (ambaye ni Yohana mwenyewe) alijaribu kueleza safari ya Bwana kwenda Golgotha kwa ujumla, bila kuhusisha mtukio madogo madogondogo yaliyokuwa yanatokea njiani.

Kwamfano utaona yeye kasema tu Bwana alijichukulia msalaba wake mpaka Golgotha, pasipo kutaja matukio kama ya kutemewa mate njiani, au wale wanawake kumlilia na Bwana kuwajibu kwamba wajililie nafsi zao na watoto wao (Luka 13:26-28).. Sasa matukio kama haya Yohana hajayataja lakini haimaanishi kuwa amesema hayapo, la! Bali ni kwamba kafupisha tu habari.. hata wewe/mimi tunaweza kuelezea jambo kwa urefu au ufupi kutegemea na mapenzi yetu.

Lakini sasa tukirudi kwa Mathayo yeye kataja safari ya Bwana kwa urefu kidogo,akihusisha matukio madogo madogo yaliyokuwa yanaendelea njiani katika safari yake..na mojawapo ya tukio ndio hilo la Simoni Mkirene aliyekuwa anatokea shamba na akashurutishwa kuubeba msalaba wa Bwana YESU.

Na utaona pia ijapokuwa Mathayo alirekodi tukio la Simoni Mkirene kumsaidia Bwana msalaba, lakini pia hakutaja tukio la wanawake waliomlilia Bwana njiani, ambapo tukio hilo linakuja kutajwa na mwandishi mwingine wa kitabu kingine ambaye ni Luka..

Luka 23:26 “Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.

27 Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.

28 Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.

29 Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha”.

Umeona kwahiyo habari ya Bwana YESU kujichukulia msalaba mpaka Golgotha kama ilivyoandikwa na Yohana haipingani na ile ya iliyoandikwa na Luka, Mathayo au Marko.. kinachotofautisha habari hizo ni kwamba moja imeandikwa kwa urefu nyingine kwa ufupi.

Je umempokea YESU, je umeubeba msalaba wako na kumfuata?.. Je unajua ni kwanini Simoni Mkirene aliruhusiwe kubeba msalaba nyuma ya YESU?.. ni ufunuo kuwa tukitaka kumfuata YESU ni lazima tubebe msalaba tumfuate YESU nyuma.

Marko 8:34 “Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.

35 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha”.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MANENO SABA YA YESU MSALABANI.

YESU MNAZARETI,  ANWANI YA MSALABA.

MSALABA NI ZANA YA UJENZI WA MAISHA YAKO.

Je! Bwana Yesu alisulubiwa juu ya msalaba au juu ya mti uliokuwa wima?

Kwanini Bwana Yesu alisema pale msalabani naona kiu?

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/06/07/simoni-mkirene-aliubeba-msalaba-wa-bwana-yesu-au-la/