LINDA CHEMCHEMI YA MOYO WAKO.

by Devis | 17 June 2025 08:46 am06

Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako CHEMCHEMI ZA UZIMA”.

Chemchemi kazi yake ni kutoa “maji ya kunywa” lakini pia ya maji ya “kustawisha mimea”.

Kama chemchemi ikitoa maji ya chumvi au ya magadi, ni wazi kuwa maji yake hayatafaa kwa matumizi yoyote yale, hivyo mahali hapo hapana uhai, watu hawawezi kuishi wala wanyama wala mimea..

Lakini kama chemchemi ikitoa maji safi yasiyo na magadi wala chumvi, na tena masafi, basi mahali pale kila kitu kitasitawi ikiwemo watu, wanyama na mimea, na hata shughuli zote nyingine za kiuchumi.

Mfano wa maji machungu na yasiyofaa ni yale wana wa Israeli waliyokutana nayo kule ‘Mara’

Kutoka 15:22 “Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.

24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko”.

Sasa Biblia inafananisha “Mioyo yetu na chemchemi zinazotoa maji”… Maana yake yanayotoka mioyoni mwetu yanaweza kukuza, kustawisha au kudhoofisha afya zetu, wanyama wetu, mimea yetu…kwaufupi kila kitu kinachotuzunguka ikiwemo kazi zetu, elimu zetu, nafasi zetu, kibali chetu na mambo mengine yote yanategemea sana yanayotoka mioyoni mwetu.

Sasa najua utauliza haya maji machungu au matamu ni nini?.. Turejee maneno ya Bwana Yesu.

Mathayo 12:34 “Enyi wazao wa nyoka, mwawezaje kunena mema, mkiwa wabaya? Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake.

35 Mtu mwema katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya”.

Tusome tena Mathayo 15:18-20…

Mathayo 15:18 “Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu unajisi.

19 kwa maana MOYONI hutoka MAWAZO MABAYA, UUAJI, UZINZI, UASHERATI; WIVI, USHUHUDA WA UONGO, NA MATUKANO

20 hayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi…….”.

Umeona hapo?.. kumbe moyoni ndiko kunakotoka matukano, uzinzi, wizi, uongo n.k mambo ambayo ndiyo yanayomtia mtu unajisi, na bila shaka hayo ndiyo Maji machungu yatokayo moyoni kupita kinywani, ambayo hayafai kwa kustawisha chochote…

Wengi wamepoteza na kuharibu maisha yao kwasababu ya uzinzi, na wengine kwasababu ya wizi, na wengine kwasababu ya mauaji, wapo waliopoteza kibali kwa Mungu na kwa watu kwasababu ya wizi, au uzinzi, au mauaji..wapo walipoteza kazi zao za mikono na huduma zao zilizokuwa zenye utukufu kwasababu ya uzinzi, au wizi au matukano..

Wapo walioharibu ndoa zao zilizokuwa za heshima na mfano kwasababu ya uzinzi, uongo, na mauaji (utoaji mimba) Kwanini?.. kwasababu chemchemi zao zinatoa maji machungu yanayoua ndoa, kazi, huduma, kibali, heshima na nguvu.

Yakobo 3:8 “Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.

9 Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu.

10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.

11 Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu?

12 Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu”.

Lakini kama moyoni kukutoka mambo masafi, ambayo ni upendo, ukweli, utu wema, uvumilivu (kwa ujumla utakatifu)… hakika hiyo ni chemchemi bora inayostawisha kila kitu, maji yake yatastawisha wokovu, kazi ya Mungu, kazi ya mikono, elimu, heshima, ndoa, nafasi na mambo mengine yote mazuri.

Je wewe chemchemi ya moyo wako inatoa maji ya aina gani?.. machungu au matamu?.. Kama inatoa machungu ipo dawa leo?.. dawa hiyo ni Roho Mtakatifu… Mwamini YESU leo kisha ukabatizwe na Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukutakasa moyo wako Bureeeee kabisa!

Baada ya hapo ndoa  yako iliyokufa itafufua upya, huduma yako, kazi yako, elimu yako au kitu kingine cha thamani ulichopewa na Bwana, kitafufuka kwani tayari maji yatokayo ndani yako ni masafi..

Lakini labda tayari chemchemi yako ni safi, nayo inatoa maji masafi.. bado kuna jambo lingine la ziada la kufanya nalo ni KUILINDA chemchemi yako..

Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako CHEMCHEMI ZA UZIMA”.

Utaulinda moyo wako kwa MAOMBI, kusoma NENO, kujihadhari na ulimwengu na kushiriki ibada pamoja na watu wenye imani moja na wewe kila mara.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Nini maana ya Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu?

Fahamu Maana ya Mithali 15:24 Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu;

MOYO ULIOELEKEA KWA MUNGU.

JE UPANGA UMEINGIA MOYONI MWAKO?.

JIHADHARI NA MANENO YASIYO NA  MAANA 

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/06/17/linda-chemchemi-ya-moyo-wako/