by Devis | 24 June 2025 08:46 am06
Jambo jingine Kuu la kujifunza kama mkristo ni Kumshukuru Mungu kila wakati na kwa kila jambo, kwamaana maandiko ndivyo yanavyotufundisha..
1Wathesalonike 5:18 “shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu”.
Kuna mambo yanafunguka tu yenyewe baada ya kumshukuru Mungu!..haihitaji nguvu nyingi.. Maombi ya shukrani ni maombi yanayougusa moyo wa Mungu zaidi hata ya kupeleka mahitaji!, kwani ni yanauelezea uthamani wa Mungu katika maisha ya mtu, ni maombi ya kushuka sana na ya kuithaminisha kazi ya Mungu katika maisha yako au ya wengine, na hivyo ni maombi yenye nguvu sana na kuugusa moyo wa Mungu kuliko tunavyofikiri.
Na kiuhalisia maombi ya kushukuru ndiyo yanayopaswa kuwa maombi ya kwanza kabisa kabla haya yale ya toba na mahitaji..kwasababu, uzima tu ulionao ni sababu ya kwanza kumshukuru Mungu, kwasababu usingekuwa nao huo hata maombi mengine usingeweza kuomba..
Leo tuangalie faida moja ya kumshukuru Mungu, kwa kujifunza kupitia Bwana wetu YESU KRISTO.
Kama wewe ni msomaji wa Biblia utagundua kuwa kila wakati ambapo Bwana YESU alitaka kufanya MUUJIZA usio wa kawaida, alianza kwanza kwa kushukuru..
Kwamfano kipindi anaigawa ile mikate kwa watu elfu nne alianza kwanza kwa kushukuru..
Mathayo 15:33 “Wanafunzi wake wakamwambia, Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii?
34 Yesu akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba, na visamaki vichache.
35 Akawaagiza mkutano waketi chini;
36 akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, AKASHUKURU AKAVIMEGA, akawapa wanafunzi wake, nao wanafunzi wakawapa makutano.
37 Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate makanda saba, yamejaa”.
Pengine unaweza usione uzito wa shukrani katika huo muujiza wa mikate… hebu tusome mahali pengine palipoonesha kuwa ni SHUKRANI ya Bwana ndio iliyovuta ule muujiza mkuu wa mikate.
Yohana 6:23 “(Walakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, WAKATI BWANA ALIPOSHUKURU)”..
Hapo anasema.. “wakati Bwana aliposhukuru”… Kumbe! Ile shukrani ilikuwa na maana kwa sana kwa muujiza ule kutendeka.. Na wala pale hapaonyeshi kwamba Bwana YESU alimwomba Baba augawe ule mkate!.. la! Bali alishukuru tu kisha akaumega!, muujiza ukatendeka.
Kuna mambo mengine unahitaji kushukuru tu na kuendelea mbele!, na mambo yatajiweka sawa yenyewe, kuna nyakati hutahitaji kuomba sana.. bali kushukuru tu, na kumwachia Bwana..na maajabu yatatendeka..
Pia utaona kipindi kile kabla ya Bwana kumfufua Lazaro alianza kwanza kwa KUMSHUKURU MUNGU..
Yohana 11:39 “Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne.
40 Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?
41 Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, BABA, NAKUSHUKURU KWA KUWA UMENISIKIA.
42 Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.
43 Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje.
44 Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake”.
Umeona? Ni shukrani tu, ndio iliyomtoa Lazaro kaburini..
Je na wewe unayo desturi ya kumshukuru Mungu?.. Maombi ya shukrani yanapaswa yale maombi marefu sana, kwani tunazo sababu nyingi sana za kumshukuru Mungu, kama umeokoka, huo wokovu ulio nao ni sababu ya kumshukuru Mungu hata masaa sita mfululizo, kwasababu kama ungekufa kabla ya kuokoka leo ungekuwa wapi?.
Kama unapumua hiyo ni sababu ya kumshukuru Mungu, kwasababu wapo walioondoka na wengine ni wema kuliko hata mimi na wewe.
Na zaidi ya yote si tu kushukuru kwa mambo mema au mazuri Mungu anayokutendea, bali hata kwa yale ambayo yameenda kinyume na matarajio yako, ni lazima kushukuru, kwasababu hujui kwanini hiyo jambo limekuja kwa wakati huo, endapo Ayubu asingemshukuru Mungu kwa majaribu aliyokuwa anayapita zile Baraka zake mwishoni asingeziona.
Ni hivo hivyo mimi na wewe, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa vyote, viwe vizuri au vibaya.. kwasababu tunajua mwisho wake utakuwa mzuri.
Yeremia 29:11 “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
UNAZO KILA SABABU ZA KUMSHUKURU MUNGU
Kwanini BWANA awaagize wakoma wakajionyeshe kwa Makuhani?(Luka 17:14
KWA KUWA FURAHA YA BWANA NI NGUVU ZENU.
Maombi kama sehemu ya maisha ya mwamini mpya.
Nini maana ya Selahamalekothi?
Source URL: https://wingulamashahidi.org/2025/06/24/faida-nyingine-ya-maombi-ya-kushukuru/
Copyright ©2025 Wingu la Mashahidi unless otherwise noted.