UNAZO KILA SABABU ZA KUMSHUKURU MUNGU

UNAZO KILA SABABU ZA KUMSHUKURU MUNGU

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.’

Kama unaishi, basi unayo kila sababu ya kumshukuru Mungu, hata kama huna shilingi 10 mfukoni mwako, unazo kila sababu za kumshukuru Mungu.

Kwasababu dakika hii tunayozungumza, wakati wewe unaumwa kichwa tu!..yupo mtu ICU, kapoteza fahamu, yupo mwingine kalazwa unaugua sana. Na wakati pengine wewe upo kitandani umelazwa, ukitafakari matatizo unayoyapitia, kuna mwingine sehemu nyingine ndio yupo katika hatua ya kukata roho.

Wakati wewe hujala tangu asubuhi, yupo mwingine tangu jana hajala kabisa. Wakati wewe unao wazazi na ndugu, yupo mwingine hana hao, yupo peke yake..

Wakati wewe macho yanakusumbua (unavaa miwani), yupo mwingine hana macho kabisa. Wakati unatembea kwa kuchechemea, yupo mwingine hata hiyo miguu hajawahi kuwa nayo. 

Wakati wewe huna fedha wala mali, lakini unao uhuru wa kuamka asubuhi na kwenda unapotaka, wapo wengine sasahivi wamefungwa magerezani na tena kwa miaka mingi, hawana uhuru kama ulionao wewe, wanatamani wangeupata hata walau kwa siku moja tu, lakini hawana… 

Wakati wewe leo siku yako imeenda vizuri, wapo wengine dakika hii hii wapo misibani, wameamka na taarifa za misiba, wanazika wapendwa wao, watu wao wa thamani na wa muhimu. Na sio kwamba wamemchukiza Mungu ndio maana yamewapata hayo hapana! wengine ni watumishi wa Mungu wa thamani kabisa mbele zake, lakini ni wagonjwa, wengine wamefungwa, wengine wametengwa, na wengine hata hawana chakula n.k Lakini wewe hupitii hayo mazito kama ya kwao..Tafakari mara mbili!!..Mshukuru Mungu wala usiwe mtu wa kulalamika kabisa!.

Kitendo cha wewe kuimaliza siku unaishi, huo tayari ni muujiza mkubwa sana. Hivyo katika hali yoyote ile uliyopo, maadamu unao uzima mshukuru Mungu. Siku zote usijilinganishe na yule aliyenacho, bali jilinganishe na yule asiyenacho, ndipo utakapokuwa na kila sababu za kumshukuru Mungu. 

Tena mshukuru Mungu kwa kumwimbia, kumshangilia na kumtolea. Unapofanya hivyo, unaonyesha kumheshimu Mungu na kutambua uwepo wake katika maisha yako. Na pia ni mapenzi ya Mungu sisi tumshukuru yeye.

1Wathesalonike 5:17  “ombeni bila kukoma;  shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu”.

 

Wakolosai 3:15 “…tena iweni watu wa shukrani”.

Siku hizi za kumalizia, shikilia imani kwa nguvu zaidi, kamwe usiruhusu, taabu za dunia kukukatisha tamaa, Mwisho upo karibu sana.

Bwana atubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JIOKOE WEWE NA NYUMBA YAKO.

BWANA MUNGU NASHANGAA KABISA lyrics

BWANA MUNGU NASHANGAA KABISA lyrics

YAKINI NA BOAZI.

BWANA SI MWEPESI WA HASIRA, LAKINI BWANA NI MWINGI WA HASIRA.

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments