Monthly Archive Mei 2022

TAFUTA MSAMAHA HALISI, NA SI MSAMAHA TU!

Jina la Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo libarikiwe.. Karibu katika kujifunza Neno la Mungu wetu, ambalo ni Taa iongozayo miguu yetu na Mwanga wa Njia yetu. (Zab. 119:105).

Kuna tofauti ya kusamehewa makosa, na kuondolewa Dhambi.. Watu wengi sana wanasamehewa makosa yao na Mungu..lakini bado wanakuwa hawajaondolewa dhambi, Kusamehewa  ni kitu kingine na kuondolewa ni kitu kingine..

Mtu wa kidunia, ambaye hata hamwamini Kristo anaweza kufanya kosa fulani, labda la kuiba na akastahili kufungwa, mtu huyo anaweza kumlilia Mungu, na Mungu akamsamehe kosa hilo na kumwepushia mbali adhabu ya kufungwa, lakini hiyo haimaanishi kuwa ndio kashapata ondoleo la dhambi zake zote.

Utakumbuka wale watu waliomsulubisha Bwana msalabani.. Bwana Yesu aliwaombea Msamaha.. Lakini kwa kuowaombea kule msamaha, haikumaanisha kuwa tayari wameshaokoka na kwamba wakifa wanaenda mbinguni. La! bado walikuwa wana dhambi, ya asili, ambayo hiyo haiondoki kwa kuombewa au kutamkiwa bali kwa mtu mwenyewe kuamua kuchukua hatua ya kufanya maamuzi..

Ingekuwa inaondoka kwa kutamkiwa tu, basi kazi ya wokovu ingekuwa ni rahisi sana, BWANA YESU Asingetuambia tujikane nafsi, asingetuambia tukabatizwe, ANGETUTAMKIA TU DUNIA NZIMA KUWA, TUMESAMEHEWA DHAMBI, na sisi tungekuwa tumestarehe.

Lakini haikuwa hivyo, bali kulikuwa na kanuni maalumu, Na kanuni hiyo ndio ile tunayoisoma katika.. Matendo 2:38, ya KUTUBU NA KUBATIZWA!.

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”.

Kwahiyo wale Makuhani, na Maaskari waliomsulubisha Bwana hawakupata Ondoleo la Dhambi, kwasababu formula la kupata ondoleo la dhambi, ili kupata uzima wa milele, na kuokoka na ghadhabu ya Mungu ya ziwa la Moto, ndio hiyo ya kutubu na kubatizwa.

Wao walichokipata ni msamaha tu, wa lile tendo walilolifanya la kumsulubisha Bwana, lakini kama kulikuwa na uzinzi walioufanya juzi, au uuaji walioufanya wiki iliyopita, au wizi walioufanya mwaka uliopita, ambao hawakuutubia, bado walikuwa na hatia ya dhambi hizo, Hivyo walisamehewa kosa hilo moja tu, la kumsulubisha Bwana aliyekuwa mwenye haki, lakini makosa mengine yalibaki pale pale.

Maana yake ni kwamba, kama Bwana Mungu alikuwa amepanga kuwaadhibu kwa kosa hilo la kumsulubisha Bwana Yesu, basi alighairi kwa kuwa waliombewa msamaha. Lakini Msamaha huo walioupata sio Ule wa kuepukana na ziwa la Moto, au wa kuwapatia uzima wa Milele..bali wal lile kosa tu!

Msamaha uletao uzima wa milele, na utuepushao na ziwa la Moto, ni ule tuupatao kwa sisi wenyewe kuamua kutubu dhambi zetu zote kwa kumaanisha kuziacha, na kubatizwa katika ubatizo sahihi, kama ishara ya kufa na kufufuka na Kristo katika upya wa roho, na kupokea Roho Mtakatifu. (Msamaha huu ndio utuleteao uzima wa Milele, na ndio wa muhimu).

Je na wewe umepokea msamaha upi?..Umepata msamaha tu!, au Msamaha kamili..

Inawezekana kila siku unaamka asubuhi na kuomba toba!, ni kweli Bwana ni Mwingi wa Rehema atakusamehe, lakini kama USIPOPATA  MSAMAHA KAMILI WA ONDOLEO LA DHAMBI ambao huo unakuja kwa wewe kuamua kutubu, kwa kumaanisha kuacha Dhambi zako zote.

Kama bado hujapata Msamaha kamili, basi utafute leo kwa bidii.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

NINI MAANA YA KUTUBU

Bwana aliposema “sikuja kutangua torati bali kuitimiliza” alikuwa anamaanisha nini?

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

Rushwa inapofushaje macho?

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

NJIA NYINGINE YA KUPATA REHEMA NA KIBALI KUTOKA KWA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

Je Mkristo kutembea na walinzi (Bodyguards),ni sawa?

SWALI: Je Mkristo kutembea na walinzi (Bodyguards), katika huduma ni sawa? Kama sio mbona Bwana Yesu alitembea na mitume wake?


JIBU: Tufahamu kuwa mitume hawakuwa walinzi wa Bwana Yesu, Bali waliitwa kwa kazi ya kumshuhudia Yesu duniani.

Na ndio maana utaona wakati Fulani walijaribu kumtetea kwa silaha zao, Lakini Bwana Yesu alimkemea Petro, na kumwambia sikushindwa kuwaagiza Malaika wa Baba yangu kuja kunipigania,(Mathayo 26:52) hiyo ni kuonyesha kuwa kazi ya ulinzi ni ya Malaika sio ya wanadamu. Na pia hakuwaita, ili wamlinde, bali wajifunze kwake.

Kitendo cha mkristo, au askofu kutembea na askari wenye silaha, mikononi mwao wenye lengo la kumlinda, kama vile walindwavyo wanasiasa au watu mashuhuri, hiyo si sawa. Kwasababu hizo sio nyendo za Bwana wetu Yesu Kristo,alipokuwa hapa duniani.

Ndio upo wakati ambapo huduma itakuwa kubwa, na hivyo kutahitajika kuwekwe mipaka ya watu kukufikia, ili huduma itendeke kwa utaratibu, Lakini hiyo bado haikufanyi uwaajiri walinzi, bali  unapaswa uwaweke watendakazi wenzako katika shamba la Bwana walio chini yako, hiyo ndio kazi yao, kama Kristo alivyofanya kwa mitume wake, hakuwaweka  maakida wa kirumi, au watoza ushuru, au watu mataifa kuwa wahudumu wake.

Yohana 12:20 “Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.

21 Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu.

22 Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu”.

Hivyo kibiblia sio sahihi, mtu wa Mungu kuwaajiri maaskari wa ulinzi, kumlinda. Ni vizuri Zaidi akawachagua watakatifu wenzake ambao atakuwa anahudumu nao, kila aendapo.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Wale mamajusi walikuwa ni wakina nani?

Je! dhambi zote ni sawa Kuna dhambi kubwa na ndogo?

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?

Talanta ni nini katika biblia (Mathayo 25:14-30)

Gongo na Fimbo ni nini? Na vinawezaje kumfariji mtu? (Zaburi 23:4).

Mti wa MLOZI alioonyeshwa nabii Yeremia 1:12 tafsiri yake ni nini?

Mshipi wa dhahabu matitini ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

Talanta ni nini katika biblia (Mathayo 25:14-30)

Talanta ni nini katika biblia.

Katika agano la kale Talanta kilikuwa ni kipimo cha uzito cha juu zaidi ya vyote (kilitumiwa hususani katika  kupima madini ya  dhahabu na fedha)..Talanta moja ina uzito wa Kg 34.2.

Neno hilo utalisoma katika vifungu hivi..

Kutoka 25:39, 38:25, Samweli 12:30, 1Wafalme 10:10.

Lakini katika agano jipya haikutumika tu kama kipimo cha uzito bali pia kama cha fedha.

Ambapo biblia inatuambia..Talanta 1 ilikuwa na thamani ya sh5,000 ya wakati ule.

Hivyo kulingana na mfano ule wa yule mtumwa ambaye alisamehewa deni lake lililokuwa kubwa sana la talanta 10,000, ambayo tukiibadili katika pesa ya sasa si chini ya Tsh. Bilioni 6…Tunaona yeye  akashindwa kumsaheme mdeni wake aliyekuwa na deni dogo..la Tsh. Laki 1.

Kama tunavyosoma habari Matokeo yake ikawa ni kukamatwa  na kwenda kutupwa gerezani kwa watesaji. (Mathayo 18: 21-35)

Mfano mwingine ni habari ya yule mtu aliyesafiri, kisha akawaita watumwa wake na kuwapa talanta wafanyie biashara.mmoja akampa tano, mwingine mbili, mwingine moja. (Mathayo 25:14-30)

Hivyo katika vipimo vyote viwe ni vya kifedha au vya kiuzito bado ni vipimo vikubwa na  vya  juu sana.

Lakini tunaona jambo lingine katika kitabu cha Ufunuo..juu ya ile ghadhabu ya Mungu atakayoishusha juu ya dunia nzima siku za mwisho.

Anasema mawe yatakayoporomoka kutoka mbinguni yatakuwa ni makubwa kama talanta..Tengeneza picha jiwe moja lenye uzito wa kg 34.2 linaanguka juu yako ..ni mawe yenye uwezo wa kuvunja fuvu la kichwa..

Ufunuo wa Yohana 16:20-21

[20]Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena.

[21]Na mvua ya mawe kubwa sana, ya MAWE MAZITO KAMA TALANTA, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno.

Si ajabu watu wataomba wafe haraka..Ili tu kujisitiri na hiyo ghadhabu kali ya Mungu mwenyezi juu ya waovu wote.

Ufunuo wa Yohana 6:14-17

[14]Mbingu zikaondolewa kama ukurasa ulivyokunjwa, na kila mlima na kisiwa kikahamishwa kutoka mahali pake.

[15]Na wafalme wa dunia, na wakuu, na majemadari, na matajiri, na wenye nguvu, na kila mtumwa, na mwungwana, wakajificha katika pango na chini ya miamba ya milima,

[16]wakiiambia milima na miamba, Tuangukieni, tusitirini, mbele za uso wake yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na hasira ya Mwana-Kondoo.

[17]Kwa maana siku iliyo kuu, ya hasira yao, imekuja; naye ni nani awezaye kusimama?

Ni mambo ya kutisha sana yanayokuja huko mbeleni

Jiulize unyakuo ukikupita leo, tumaini lako litakuwa ni nini… Ni majuto na vilio vya kusaga meno, ukijua kabisa hata baada ya kufa huko kwa mateso, ni safari ya moja kwa moja hadi kuzimu.

Ni heri ukampa Kristo maisha yako leo maadamu neema ipo..Unyakuo ni wakati wowote, usipumabazwe na huu ulimwengu…achana nao kwasababu Bwana Yesu anasema siku hiyo wao itawajia kwa ghafla tuwala hawatatambua lolote kwasababu wapo gizani..Na sisi tusiwe kama wao gizani ..dalili zote zimeshatimia, tunachosubiria hapa ni unyakuo basi! Hakuna mtu asiyejua hilo. Injili tuliyonayo sio ya kubembelezewa tena wokovu, ni kujionea hali halisi na kuamka usingizini mwenyewe ..

Tengeneza taa yako. Maanisha kuishi maisha wokovu, kwasababu watakaoachwa pia ni wale wanawali wapumbavu, wakristo vuguvugu (Mathayo 25).

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

VIPIMO MBALIMBALI VYA KIBIBLIA.

Ratli/ Ratili ni nini katika biblia?

ANGALIA JINSI USIKIAVYO:

KWA KUWA WASEMA MIMI NI TAJIRI.

HERI WAPATANISHI, MAANA HAO WATAITWA WANA WA MUNGU

Marago ni nini? ( Waamuzi 10:18)

Wahiti ni watu gani?

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

KWA KUWA WASEMA MIMI NI TAJIRI.

Hebu tusome Habari ifuatayo kwa utaratibu halafu tutafakari Pamoja…

Ufunuo 3:15 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona”.

Hayo ni maneno ya Bwana Yesu aliyowaambia watu wa kanisa la Laodikia, ambalo kanisa hilo kiroho ni sisi wakristo wa siku hizi za mwisho.

Utaona anawashutumu watu wa kanisa hilo na kuwaambia kuwa WANAJIOTA KUWA NI MATAJIRI, kumbe ni MASKINI. Lakini Pamoja na hayo utaona anawashauri wakanunue kwake DHAHABU ili wawe matajiri!!!

Sasa swali la kujiuliza hapo, ni lini MTU AKINUNUA DHAHABU ANAKUWA TAJIRI??.. Ni heri angesema NJOO  NIKUPE DHAHABU BURE!, Lakini yeye anasema NJOO UNUNUE!..Maana yake unatoa kitu ili uipate hiyo dhahabu.

Na kama wewe ni mtafakariji mzuri wa Maandiko utaona Bwana Yesu alichokuwa anakimaanisha hapo, ni kwamba ukainunue dhahabu hiyo kwake, kwa bei ya chini, na kisha ukaiuze kwa bei kubwa ILI UPATE FAIDA UWE TAJIRI. (Ndicho alichokuwa anakimaanisha hapo!).

Sasa tatizo ndio liko hapo, kutoa gharama kuinunua hiyo dhahabu iliyosafishwa kwa Moto. Ingekuwa ni bure wengi wangeenda kuichukua tu!.. lakini Bwana anaiuza!..na inahitajika gharama kuinunua. Sasa swali gharama hiyo ni ipi?

Gharama hiyo tunaisoma katika mfano mmoja Bwana alioutoa katika kitabu cha Mathayo Mlango wa 13.

Tusome..

Mathayo 13:45 “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;

46 naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua”.

Lulu, ni kama dhahabu tu kwa gharama, kwasababu zinakaribiana thamani!.. Kwahiyo ni sawa  kusema “ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara aliyeona dhahabu nzuri au lulu nzuri akaenda akauza alivyonavyo vyote, akainunua”

Sasa kumbuka huyu ni mfanya biashara, lengo lake ni apate faida awe Tajiri, hivyo katika pitapita zake akakutana na lulu mahali Fulani ambayo inauzwa kwa bei ya chini, na yeye anajua soko la mahali inapouzwa kwa bei ya juu.. na akaona endapo akienda kuinunua kwa bei hiyo ya chini na kwenda  kuiuza kwenye soko la juu atapata faida nyingi sana…sasa kwa busara akaenda kuuza shamba lake, na vyote alivyonavyo ili aipate fedha ya kutosha kuinunua hiyo lulu inayouzwa kwa bei ya chini… Lengo la kwamba atakapoenda kuiuza kwa bei ya juu itamrudishia fedha ya kutosha ya kununua vyote alivyovipoteza na Zaidi sana kubakiwa na faida nyingi.

SASA UMEONA GHARAMA HIYO?

Maana yake kama hatakubali kuuza vyote alivyonavyo ili apate fedha za kuinunua hiyo Lulu hataweza kuinunua na ataendelea kuwa maskini hivyo hivyo hata kama anajiona hana mahitaji yoyote…

Ndicho Bwana Yesu alichokuwa anamaanisha hapo katika hiyo Habari ya dhahabu.. Kwamba mtu yeyote akitaka kuwa Tajiri basi aende kwake akanunue dhahabu hiyo, kwa bei ya chini, ili akaiuze kwa bei ya juu, na kubakiwa na faida ambayo ndio utajiri wenyewe.

Sasa mfano huo kiroho inamaanisha nini?

Tukitaka kuupata ufalme wa mbinguni ambao ndio unaofananishwa na Dhahabu na Lulu. Hatuna budi kuacha vyote tulivyonavyo vinavyozuia sisi kuupata  huo uzima wa milele (Hiyo Ndio maana ya kuuza vyote na kwenda kuinunua lulu/dhabahu).

Tukishaacha vyote yaani Ulevi wetu, uongo wetu, wizi wetu, anasa zetu, kiburi chetu, uasherati wetu, umaarufu wetu, ujuzi wetu ambao unatuletea kiburi, ujuaji wetu, na biashara zetu haramu, kama za madawa ya kulevya, au uuzaji wa pombe, au utapeli au rushwa n.k Tunapoviacha hivi vyote, na kumfuata Yesu hapo ni sawa na tumeuza vyote, na katika viwango vya kimbinguni tumejipatia credit tosha za kuupata Ufalme wa mbinguni (ambao ndio unaofananishwa na ile lulu au dhahabu safi).

Mathayo 19:20 “Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?

21 Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.

22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

23 Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni”.

Umeona gharama za kuinunua ile DHAHABU ILIYOSAFISHWA KWA MOTO!!!.. Suluhisho ni kuacha vyote, kuvitoa ndani ya moyo wako..

Luka 14:33 “Basi, kadhalika kila mmoja wenu ASIYEACHA VYOTE ALIVYO NAVYO, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.

Unaacha vyote na kumfuata Yesu kama ulivyo.. Bwana Yesu anawapenda watu wanyenyekevu, ambao wameamua kabisa kuanza moja katika Maisha yao, ambao wamejikana nafsi, ambao wamedhamiria kabisa kuzaliwa upya.. Leo Bwana anakuita, anataka akutumie kama chombo kipya, hivyo vua ujuzi wako leo, vua kiburi chako, acha dhambi zako, na mambo yote yanayokusonga  na mfuate…naye atakupenda!, na kukupa zawadi ya Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia katika kushinda dhambi, na kukufanya kuwa mtumishi wake..

Usijione kuwa ni Tajiri, na huna haja ya kitu!.. (usiojione kuwa humhitaji Yesu kwa sasa) bado unamuhitaji sana, bado unaihitaji ile Dhahabu.. nenda kainunue kwa Bwana, kwasababu inapatikana kwa bei ya chini.. na ukiinunua na kwenda kuifanyia biashara, yaani kuwafundisha wengine Habari za ufalme wa mbinguni, utakuwa Tajiri sana katika ufalme wa mbinguni.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

GHARAMA YA UFALME WA MBINGUNI.

VIACHENI VYOTE VIKUE HATA WAKATI WA MAVUNO.

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

NUNUA MAJI YA UZIMA.

Je! Ni kweli Yesu alirejesha kila kitu kama pale Edeni?

Rudi nyumbani

Print this post

Babewatoto ni nani katika biblia?(Isaya 34:14).

Babewatoto ni jina lingine la mapepo yanayotembea usiku (yenye mfano wa ndege wa angani).

Hawa wametajwa mara moja tu katika biblia..

Isaya 34:14 “Na hayawani wa nyikani watakutana na mbwa-mwitu, na beberu anamwita mwenziwe; naam, babewatoto anakaa huko na kujipatia raha”.

Bwana alitoa unabii juu watu wote wa ulimwengu waliomwacha yeye, kuwa makao yao yatakuwa ni makao ya hayawani wa porini na ya mapepo hayo (Babewatoto).

Utaona unabii kama huo Bwana aliutoa pia kwa Babeli kwamba utaanguka na makao yake yatakuwa ukiwa na hayawani wa mwituni watakaa huko na MAJINI yatacheza huko.

Jambo ambalo lilikuja kutimia kama lilivyo..ulipofika wakati wa unabii huo kutimia, Babeli ilikuja kuanguka na mahali pale ambapo palisifika kwa uzuri na bustani zinazoelea leo hii tunapozungumza ni jangwa, hayawani wa porini wanapita na majini wanakaa huko.

Isaya 13:19 “Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza.

20 Hautakaliwa na watu tena kabisa, wala watu hawatakaa ndani yake tangu kizazi hata kizazi. Mwarabu hatapiga hema yake huko, wala wachungaji hawatalaza makundi yao huko.

21 Lakini huko watalala hayawani wakali wa nyikani; na nyumba zao zitajaa bundi; mbuni watakaa huko; na MAJINI watacheza huko”.

MAJINI yanayozungumziwa hapo ni mapepo yenye maumbile kama ya Mbuzi-mwitu.

Hiyo ikifunua kuwa tukimwacha Mungu haijalishi tulikuwa tumestawi kiasi gani, Bwana ataushusha utukufu wetu na makao yetu yatakuwa ni makao ya majini (mapepo) na babewatoto.
Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:

Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au

Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

MAJINI WAZURI WAPO?

AINA ZA MAJINI, MAJINA YAO, KAZI ZAO, NA TIBA ZAKE.

IMESALIA RAHA YA SABATO KWA WATU WA MUNGU.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU WATOTO.

Makao ambayo Yesu alikwenda kutuandalia ni yapi?

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya ugonjwa wa kufisha? (Yeremia 17:9)

SWALI: Nini maana ya ugonjwa wa kufisha? Yeremia 17:9

Yeremia 17:9 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua”?


Kufisha; maana yake ni kusababisha kitu kife.

Hivyo hapo anaposema..moyo una ugonjwa wa kufisha.. Maana yake ni kuwa una ugonjwa wa kupelekea mauti, yaani ugonjwa usioponyeka.

Akiwa na maana kuwa, udanganyifu wa moyo ni mbaya sana, unaweza kukupeleka sio tu mauti ya mwili wako, bali mpaka roho yako pia. Kwamfano waweza kujiuliza shetani alidanganywa na nani kule mbinguni?. Jibu ni kuwa hakudanganywa na mtu yeyote, bali alidanganywa na moyo wake mwenyewe kwamba na yeye anaweza kuwa kama Mungu.

Na mwisho wa siku akapata hasara ambayo mpaka leo hii anaijutia ndani ya moyo wake. Hata sasa udanganyifu wa kwanza hautoki kwa shetani, bali unatoka ndani yetu wenyewe. Baadaye tukishadanganyika, ndipo shetani anapata nafasi ya kuuchochoa udanganyifu huo.

Biblia inasema,

Mithali 14:12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”.

Unaweza kuona kuvaa vimini na kujichubua ni sawa kwasababu moyo wako unakuambia hivyo, lakini kumbe ndio unakwenda kujiangamiza mwenyewe. Unaweza kudhani kumwabudu Mungu kwa kupitia chochote ni sawa tu kumbe, mwisho wake ni mauti.

Njia ni moja tu, nayo ni Yesu Kristo.

Hivyo andiko hilo, linatupa tahadhari kuwa, tumsikilize Mungu, kuliko mioyo yetu. Kwasababu wengi wamepotea, kwa kutii tamaa za mioyo yao, na sio Neno la Mungu.

Bwana atusaidie sana.

Neno “kufisha” utalisoma pia katika vifungu hivi;

Luka 16:17 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;

18 watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya”.

Zaburi 7:13 “Naye amemtengenezea silaha za kufisha, Akifanya mishale yake kuwa ya moto”.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Herode aliliwa na chango, Je, chango ni nini kibiblia?

Je Elisha alimdanganya Ben-hadadi kuwa hatakufa kwa ugonjwa wake?

Jehanamu ni nini?

Ni lini na wapi Ibrahimu aliioona siku ya Bwana akashangilia?

JIWE LILILO HAI.

VIPIMO MBALIMBALI VYA KIBIBLIA.

ZIFAHAMU NAMBA KATIKA BIBLIA NA MAANA ZAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

KIASI NI NINI KATIKA UKRISTO?

Kiasi kama tafsiri yake  ilivyo ni  kuwa na uwezo wa kudhibiti jambo/tendo lisipitilize mipaka yake, yaani litendeke kwa sehemu tu.

Katika Ukristo, kiasi ni moja ya matunda tisa (9), ya Roho Mtakatifu.

Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, KIASI; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Ikiwa na maana ukipungukiwa nacho (kiasi), ni uthibitisho mojawapo kuwa Roho wa Mungu hayupo ndani yako.

Kwasababu huu  ulimwengu una mambo mengi, ambayo, pengine sio mabaya, lakini yakipitiliza matumizi yake, yanabadilika na kuwa mabaya na sumu kubwa sana, kuliko hata matendo yenyewe mabaya.

Sasa swali ni Je, tunapaswa tuwe na kiasi katika mambo gani?

Zifuatazo ni sehemu muhimu, ambazo, Roho Mtakatifu anataka sisi tuwe nazo na kiasi.

  1. Katika ndoa.

1Wakorintho 7:4 “Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.

5 Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu”.

Kukosa kiasi katika tendo la ndoa, hupelekea watu wengi sana kumtenda Mungu dhambi, wengine wanatenda mambo hayo hata kinyume na maumbile, wengine kutafuta njia za visaidizi n.k. wengine muda wao wote wanachowaza ni tendo lile tu, akili zao zote zinafikiria humo, mpaka inawapelekea kukosa muda kusali. Hivyo kiroho chao kinapungua sana kwasababu ya kuendekeza tamaa za mwili.

Biblia inasema..

1Wakorintho 7:29 “Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana;

Ikiwa na maana, tuishi kama vile, hakuna jambo jipya tumeongeza, pale tulipooa au kuolewa, hiyo itatusaidia sana, kuishi Maisha ya utakatifu na kumcha Mungu, katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho duniani.

2. Kiasi katika shughuli za ulimwengu;

Bwana ametuweka duniani tufanye kazi, pia tujitafutie rizki, lakini anatutahadharisha, tusipitilize, mpaka kufikia hatua ya mioyo yetu kuzama huko moja kwa moja tukamsahau yeye, hata muda wa ibada, au kuomba au kuwaeleza wengine Habari njema tukakosa..Hiyo ni hatari kubwa sana.

1Wakorintho 7:31 “Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita”.

Yaani fanyakazi huku ukijua mahusiano yako, au ratiba yako na Mungu haivurugwi hata kidogo.. Kwasababu ukiupeleka moja kwa moja moyo wako huko, ni lazima tu ulale kiroho, na matokeo yake, utakufa na bado hujayatengeneza mambo yako vizuri na Mungu.

1Wathesalonike 5:6 “Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, NA KUWA NA KIASI.

7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.

8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu”.

Usihangaishwe sana na shughuli za dunia hii.. Kuwa na kiasi katika hayo, ili mbegu yako imee vizuri. Zingatia sana hilo. Kama unatingwa na mihangaiko ya duniani, na moyoni mwako unaona ni sawa, basi ujue moyoni mwako Roho Mtakatifu hayupo.

3. Kiasi katika huduma

Mungu anataka watumishi wake pia wawe na kiasi.. Hamaanishi kiasi katika kumtumikia hapana, anataka sana tuzidi kumtimika kwa bidii,  bali anamaanisha kiasi katika karama.

Anasema..

Warumi 12:3 “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; BALI AWE NA NIA YA KIASI, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.

4 Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja;

5 Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.

Hii ni kutuonyesha kuwa hakuna hata mmoja wetu mwenye karama zote, Ni YESU tu peke yake. Hivyo ridhika, na ulichokirimiwa, ukiwa ni mchungaji, usitake wewe wewe ndio uwe ni nabii, na mwalimu, na mwimbaji, na mwinjilisti, na mtume n.k. Huwezi kuwa Yesu.

Jifunze kuwapa wengine nafasi, na kunyanyua karama zao, pia fahamu kuwa wapo watakaokuwa na karama bora kukuzidi wewe. Ukilijua hilo utajifunza kuwa mnyenyekevu, na ndivyo Mungu atakavyokutumia Zaidi.

     4. Kiasi katika haki:

Mhubiri 7:16 “Usiwe na haki kupita kiasi; Wala usijiongezee hekima mno; Kwani kujiangamiza mwenyewe?

Hapa pia Mungu hamaanishi kwamba tusiwe na haki nyingi kupitiliza hapana, anapenda sana tuwe hivyo. Lakini anachomaanisha hapo ni kuwa tusiwe watu wa kujihesabia haki kupitiliza,(yaani kujisifia) kwani matokeo yake ni kujiangamiza wenyewe.

Bwana Yesu alitoa mfano wa yule Farisayo na mtoza ushuru waliokwenda kusali kule hekaluni, lakini yule Farisayo akaanza kumwambia Mungu mimi ni mkamilifu kuliko huyu mtoza ushuru, mimi ninafunga mara mbili kwa juma, mimi natoa zaka, mimi nahudhuria mikesha kila wiki, mimi nahubiri sana n.k. Lakini yule mtoza ushuru akasema Bwana nirehemu mimi ni mwenye dhambi..Matokeo yake yakawa yule mtoza ushuru akahesabiwa haki kuliko yule Farisayo..

Ndipo Yesu akasema..

Luka 18: 14 “…kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa”.

Uendapo mbele za Mungu, au mbele za wanadamu kuwa na kiasi.. Mwache Mungu akuhesabie haki mwenyewe. Usijifisie kwa lolote.

5. Kiasi katika kunena.

Biblia inasema..

Mithali 10:19 “Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili”.

Kwanini haisemi, katika Uchache wa maneno, hapakosi kuwa na maovu?..Ni kuonyesha kuwa, unapokuwa mzungumzaji kupitiliza, ni rahisi sana kujikwaa ulimi, lakini ukiwa si mwepesi wa kuzungumza zungumza,  yaani kila Habari au kila jambo unachangia, basi utajiepusha na maovu mengi.

Mhubiri 5:2 “Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache”.

6. Kiasi katika vyakula, na vinywaji.

Vinywaji kama divai, vilikuwa ni vya kitamaduni Israeli, wakati ule, kwasababu pia ndani yake waliamini kuna tiba, (1Timotheo 5:23) hivyo vilikuwa vinanyweka kwa kiasi sana, kwasababu vilikuwa na kiwango cha  kileo ndani yake.

Paulo akamwagiza Timotheo kuhusiana na Mashemasi na wazee wa kike katika makanisa, akamwambia.

1Timotheo 3:8 “Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana,si watu wanaotamani fedha ya aibu.

Lakini sasa kwa watu kukosa kiasi, leo hii, wanakwenda kunywa pombe ambayo haiwasaidii chochote, wala haina umuhimu wowote katika mwili, Wakati wa sasa tunazo dawa, kwanini ukanywe divai.

Na biblia imeweka wazi kabisa, walevi wote sehemu yao itakuwa katika lile ziwa la moto (1Wakorintho 6:10).

Sio kila kitu ule, au unywe. Zuia koo lako, zuia tumbo lako. Wakati mwingine funga, Litunze hekalu la Mungu. Utaona faida yake

 7.Kiasi katika mwenendo.

Hapa anatoa angalizo, katika mienendo yetu na mionekano.  Hususani kwa vijana.

Tito 2:6 “Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi”;

Jiulize kwanini hasemi, wazee au Watoto? Anasema vijana kwasababu Anajua kabisa vijana wengi wakike na wakiume  waliokoka wanakosa, kiasi katika ujana wao.

Hakuna sababu ya kukesha katika muvi au magemu, au mipira kutwa kuchwa. Ukiwa umeokoka, ili hali unajua kabisa kusoma biblia, kuomba na kuhubiri kunakusubiria.

Hakuna sababu ya  binti wa Mungu avae/ aonekane kama mabinti wa ulimwengu huu. Unaweka mawigi, unavaa suruali, uweka kucha za bandia, n.k. Kuwa “natural”..

1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, NA MOYO WA KIASI; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani”;

Soma pia (1Timotheo 3:11)

Kijana, huna sababu ya kunyoa kiduku, uonekane kama msanii fulani, kwenye tv. Kumbuka Mwonekano wako unakupunguzia utukufu wako.

Kwahiyo, kwa kuhitimisha ni kuwa KIASI katika mambo yote ni muhimu sana. Hivyo tujitahidi kwa upande wetu kila mmoja aangalie ni wapi amekosa kiasi, basi arekebishe mapema, na Roho Mtakatifu atajaa tena ndani yetu kutusaidia kuushinda ulimwengu.

Kumbuka hizi ni nyakati za mwisho, Biblia inasema..

1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze”.

Umeona! Ibilisi anawatufuta watu wanaokosa kiasi ili awemeze, Usiwe mmojawapo!

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MATUNDA 9 YA ROHO MTAKATIFU

Unyenyekevu ni nini?

Je ushabiki wa mpira ni dhambi?

Wibari ni nani?(Mithali 30:26)

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

Nini maana ya mstari huu: (Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.Mithali 27:14 )?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

Je! Mtu ambaye hajaoa anaruhusiwa kulichunga kundi?

“Vya Kaisari mpeni kaisari”  ni vipi hivyo tunavyopaswa tumpe?

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Mungu aseme “Alaaniwe azuiaye upanga wake usimwage damu” (Yeremia 48:10).

Yeremia 48:10 “Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu; NA ALAANIWE AUZUIAYE UPANGA WAKE USIMWAGE DAMU”.

Je kufuatia mstari huo, Mungu anahimiza mauaji?

Jibu: Awali ya yote ni muhimu kuelewa tofauti ya Amri, Sheria na Hukumu za Mungu, sasa kuelewa juu ya mambo hayo, na tofauti zao kwa mapana, unaweza kufungua hapa >>>Nini tofauti kati ya Amri, sheria na Hukumu?

Lakini kwa ufupi ni kwamba, sheria zote na amri zote zilizotolewa katika agano la kale, zilikuwa na hukumu.. Maana yake ni kwamba, ikitokea mtu kavunja sheria au amri mojawapo basi alistahili hukumu. Na hukumu hiyo ilikuwa ni lazima itekelezwe…isipotekelezwa ilikuwa ni dhambi mbele za Mungu kama tu ilivyo dhambi ya kuvunja amri.

Mfano mmojawapo wa hukumu ni ile hukumu ya mtu kupigwa mawe mpaka afe anapokamatwa katika uzinzi..

Mfano wa hukumu nyingine ni hii..

Kutoka 21:15 “Ampigaye baba yake au mama yake, sharti atauawa”.

Kwahiyo mtu yeyote aliyeonekana akimpiga mzazi wake, hukumu ilikuwa ni kifo..wasipomuua mtu huyo, Mungu alikuwa anawaadhibu!..kwahiyo ili waendelee kukaa salama, Bwana Mungu asiwapige, ilikuwa ni lazima wamuue huyo kijana aliyempiga mzazi wake.

Hali kadhalika ilikuwepo hukumu nyingine ya mtu yeyote anayekwenda kuabudu miungu mingine.. ilikuwa ni sheria kwamba mtu akienda kuabudu miungu mingine sharti auawe, haijalishi ni mzazi wako au ndugu yako, ni lazima utamwua aidha kwa kumpiga mawe au kwa upanga.. Usipomwua ulikuwa unalaaniwa na Mungu.

Kumbukumbu 13:6 “Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako;

7 katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia;

8 USIMKUBALIE WALA USIMSIKIZE; WALA JICHO LAKO LISIMWONEE HURUMA, WALA USIMWACHE, WALA USIMFICHE;

9 MWUE KWELI; MKONO WAKO NA UWE WA KWANZA JUU YAKE KATIKA KUMWUA, NA BAADAYE MIKONO YA WATU WOTE.

10 Nawe mtupie mawe hata afe; kwa kuwa alitaka kukupotoa na Bwana, Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.

11 Na Israeli wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako”.

Vile vile ilikuwepo hukumu ya kwamba, mtu yeyote au kikundi chochote kikizuka katikati ya jamii ya Israeli, ambacho kinawashawishi watu kuabudu miungu mingine mbali na Mungu wa Israeli. Bwana Mungu alitoa ruhusa ya watu hao kuuliwa kwa makali ya upanga.

Kumbukumbu 13:12 “Ukisikia yasemwa habari ya miji yako mmojawapo, akupayo Bwana, Mungu wako, ukae humo, ukiambiwa,

13 KUMETOKA KATIKATI YAKO MABARADHULI KADHA WA KADHA, WAMEWAPOTOA WENYEJI WA MJI WAO, WAKISEMA, TWENDENI TUKAABUDU MIUNGU MINGINE MSIYOIJUA;

14 ndipo nawe uulize na kutafuta, ukiuliza kwa bidii; nawe angalia, ikiwa kweli, na jambo lile halina shaka, kwamba machukizo mfano wa haya yafanyika katikati yako;

15 HAKIKA YAKO UWAPIGE WENYEJI WA MJI ULE KWA MAKALI YA UPANGA, KWA KUWAANGAMIZA KABISA, PAMOJA NA VITU VYOTE VILIVYOMO, NA WANYAMA WALIO HUMO, KWA MAKALI YA UPANGA

Umeona?.. Hiyo ndio sababu Bwana kasema hapo kwenye Yeremia 48:10 “..ALAANIWE AUZUIAYE UPANGA WAKE USIMWAGE DAMU”.

Damu inayomwagwa ni ya watu waliomwacha Mungu wa Israeli na sheria zake kwa makusudi.

Lakini swali ni je!..  Hata sasa katika agano jipya hii sheria ipo??.

Jibu ni la!. Katika agano jipya hatuna hiyo amri!..haturuhusiwi kumwua mzinzi, wala mlevi, wala mwizi.. bali tunapaswa tuziue zile roho zilizopo ndani yao, zinazowashawishi wao kufanya mambo hayo.. na roho hizo ni roho za mapepo..hizo ndio tunazozipiga kwa Upanga wa Roho, huku na sisi tukiwa tumejivika silaha zote za roho.

Waefeso 6:11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, JUU YA MAJESHI YA PEPO WABAYA KATIKA ULIMWENGU WA ROHO.

13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;

18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote”.

Tukiweza kuzivaa hizi silaha na kuutumia vizuri upanga wa roho, ndipo tutakapoweza kuziadhibu roho zote, zilizopo ndani ya watu na kuwaacha watu huru.

2Wakorintho 10:3 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;

4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;

6 tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

JE UPANGA UMEINGIA MOYONI MWAKO?.

Na alaaniwe ampigaye mwenzake kwa siri.

KUNA NGUVU YA ZIADA KATIKA KULING’ANG’ANIA KUSUDI LA MUNGU.

Kwanini Bwana Yesu aliwaagiza wanafunzi wake wakanunue upanga?

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

REKEBISHA YAFUATAYO ILI MAMBO YAENDE SAWA.

Rudi nyumbani

Print this post

Je ni halali kupiga kura kanisani kuchagua viongozi?

Jibu: Ndio ni jambo la kimaandiko kabisa kupiga kura kuchagua viongozi wa kanisa!.

Lakini ni lazima kuzingatia wanaopiga kura na anayepigiwa kura. Wanaopaswa kupiga kura kuchagua viongozi ni lazima wawe viongozi au watu waliodumu muda mrefu katika Imani (yaani watu ambao hawajaongoka hivi karibuni).. Kwasababu watu waliookoka hivi karibuni bado hawajajua imani vizuri, na sifa za viongozi wa kiimani, vile vile bado hawajazijua hila za shetani, na bado hawajui mambo mengi ya kiimani, hivyo endapo wakipewa nafasi hiyo wanaweza kuchagua watu kutokana na hisia zao tu!, au mitazamo yao tu, na si sawasawa na Neno!.

Vile vile mtu anayepigiwa kura ni lazima awe Mkristo aliyedumu muda mrefu katika Imani na aliyesifika kwa sifa njema, na sio mtu aliyeokoka hivi karibu, ambaye bado hajajua mbinu na hila za shetani.

Katika biblia utaona mtume wa 12, aliyechukua nafasi ya Yuda, aliteuliwa kwa kupigiwa Kura!.

Matendo 1:21 “Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu,

22 kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, INAPASA MMOJA WAO AWE SHAHIDI WA KUFUFUKA KWAKE PAMOJA NASI.

23 WAKAWEKA WAWILI, YUSUFU, AITWAYE BARSABA, ALIYEKUWA NA JINA LA PILI YUSTO, NA MATHIYA.

24 Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili,

25 ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe.

26 WAKAWAPIGIA KURA; KURA IKAMWANGUKIA MATHIYA; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja”.

Umeona hapo?..Mathiya alichaguliwa kwa Kura!.. na alichaguliwa na Mitume 11, ambao wana uzoefu wa kutosha wa kimaandiko kujua kiongozi bora anapaswa aweje, hawakuhusishwa waamini wote wa Yerusalemu waje kupiga kura!..bali walipiga kura wao viongozi tu! (ili kuzuia upenyo wa shetani)..

Vile vile aliyepigiwa kura, hakuwa mtu aliyekuwa maarufu au mwenye pesa, au mwenye ushawishi.. utaona sifa ya aliyetuliwa ni “mtu aliyefuatana nao mitume tangu wakati wa Yohana hadi wakati wa kuchukuliwa kwa Bwana juu mbinguni”..jumla miaka mitatu na nusu. Kwahiyo walimchagua mtu aliyekuwa mkongwe katika Imani na vile vile aliyekuwa mwaminifu.. Ndio maana utaona Yusufu na Mathiya wote walikuwa wakongwe, lakini Mathiya alikuwa mwaminifu Zaidi ya Yusufu ndio maana alichaguliwa.

Vile vile na sisi tunajifunza namna ya kuchagua viongozi wa kanisa kama Mashemasi, wazee wa kanisa, waangalizi wa Watoto, waweka hazina, waalimu wa vijana n.k kutumia kanuni hiyo.. Kwamba baada ya kusali na kufunga, basi wawekwe wanaostahili kupigiwa kura yule anayestahili, aliye mwamifinu na ateuliwe. Kwa sisi kumteua, basi ni Bwana kamteua..kwasababu sisi tuliomchagua tumetumia vigezo vya Neno kumchagua anayestahili na si macho yetu, Ndio maana na yeye anakuwa ni chaguo la Bwana.

Huo ndio ulikuwa utaratibu wa kanisa la kwanza..Ndio maana utaona Paulo kuna mahali anawaagiza akina Tito na Timotheo vigezo vya kuchagua viongozi..

Tito 1:4 “kwa Tito, mwanangu hasa katika imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu.

5 Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru;

6 ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii”.

Je umeokoka?.. je una uhakika KRISTO akirudi leo unakwenda naye mawinguni?, kama huna huo uhakika basi ni uthibitisho kuwa atakapokuja utaachwa!.. Tubu leo kwa kudhamiria kuacha dhambi zako na tafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu, na upokee Roho Mtakatifu.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi”?

Je!Sisi kama wakristo Tunaruhusiwa kuchangia ujenzi wa Imani nyingine?

Nini maana ya kupiga Kite! Katika biblia.

KWANINI UPIGE MISHALE CHINI?

JE! KUNA UMUHIMU WOWOTE WA KULIPA ZAKA?

Rudi nyumbani

Print this post

Je tunaruhusiwa kutumia vidonge wakati wa kufunga?

Je ni tunaruhusiwa kunywa dawa wakati wa kufunga, au kuonja chakula wakati wa kupika kwaajili ya wengine?

Jibu: Unapofunga unakuwa unajizuia kula chakula au kunywa chochote, kwa lengo Fulani la kiroho. Lakini hatufungi kwa sheria au kanuni Fulani maalumu (biblia haijatupa kanuni yoyote maalumu), wala agizo la Sharti ya kufunga. Isipokuwa imesema tu “mambo mengine hayatoki isipokuwa kwa kufunga na kuomba”.

Mathayo 17: 21 “Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga”

Lakini tukirudi kwenye swali, je tunaruhusiwa kunywa dawa wakati wa kufunga?

Jibu ni NDIO! Kama kuna ulazima huo, kwasababu “Vidonge sio chakula” huwezi kula vidonge ukashiba, au ukakata njaa. Vidonge kazi yake ni kutibu tatizo Fulani lililopo ndani ya mwili (yaani vimetengenezwa kwa lengo la matibabu). Kwahiyo mtu anaweza kuwa amefunga na huku anatumia dawa.

Vile vile kuonja ladha ya chakula, kama kimekolea chumvi, au viungo hakubatilishi mfungo!..Kwamfano unaweza kuwa umefunga, lakini unalo jukumu la kupika chakula kwa wengine ambao hawajafunga! Mf.watoto, katika mazingira kama hayo, unalazimika kuonja chakula kama kimeiva, au kimekolea chumvi..(lakini kwa kiwango kidogo tu! Cha kuishia kwenye ulimi).

Ukionja kwa namna hiyo hufanyi dhambi, wala hakuharibu mfungo wako.. Kwasababu hapo umeonja na hujala. Lengo lako ni kuonja kama chakula hicho kipo sawa au la!.. Ungekuwa umeonja kwasababu unayo njaa, hapo ingekuwa ni tatizo, lakini hujaonja kwa lengo hilo.

Kwasababu ingekuwa hilo ni tatizo, basi hata mswaki asuhuhi, ingekuwa si ruhusa kupiga!..kwa maana ile dawa ya meno, tunapoiweka mdomoni, tayari tunaionja, hata kama hatutaki, vile vile tusingepaswa tusikie hata harufu ya chakula, lakini hayo mazingira hatuwezi kuyaishi.. Ni lazima tusafishe vinywa vyetu kila siku, na pia tutakutana na mazingira tofauti tofauti mahali tunapoishi..

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba kutumia dawa wakati wa mfungo si kosa, wala kuonja chakula kwakiwango kidogo kinachoishia ulimini si dhambi.

Lakini Zaidi ya yote, mfungo kwa mkristo unapaswa uwe ni jambo la mara kwa mara, inasikitisha mtu anayejiita ni mkisto lakini hana rekodi yoyote ya kungunga angalau wiki moja mfululizo.

Mkristo wa namna hii nguvu zake za kiroho zipo chini sana, kuna mambo katika Maisha yake, hawezi kuyapokea kwasababu Bwana Yesu mwenyewe alisema “kuna mambo hayawezekaniki isipokuwa kwa kufunga na kuomba”.

Bwana atusaidie tuwe waombaji na vile vile wafungaji!

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.

Je mama mjamzito anaruhusiwa kufunga?

Je! ni halali kwa mtu wa Mungu kutumia njia za uzazi wa mpango,ikiwamo mipira?

Je sisi wakristo tunaruhusiwa kufanya 40 za marehemu?

Easter ni nini?..Na je tunaruhusiwa kuisheherekea?

Rudi nyumbani

Print this post