IMESALIA RAHA YA SABATO KWA WATU WA MUNGU.

IMESALIA RAHA YA SABATO KWA WATU WA MUNGU.

Bwana YESU asifiwe sana, karibu tujifunze Neno la Mungu.

Awali ya yote ni vizuri tukaweka msingi kwanza wa kufahamu nini maana ya Sabato.

Sabato maana yake ni pumziko/kuacha kufanya kazi/ kustarehe/kuingia rahani mwako. Mungu alifanya kazi yake ya kuumba kwa muda wa siku sita mfululuzo kama tunavyosoma katika kitabu cha Mwanzo, na ilipofika siku ya saba kazi yote ilikuwa imeshamalizika, ndipo akastarehe/ akapumzika, hivyo akaibariki siku hiyo na kuifanya kuwa kama kumbukumbu la pumziko lake, na baadaye akawaagiza wana wa Israeli walipokuwa kule jangwani kwamba kila itakapofika siku hiyo waifanye kuwa ni sabato yao.

Lakini Sabato haikuwa ile siku yenyewe ya saba, bali sabato ilikuwa ni lile  pumziko lenyewe, Lakini “SABA” yenyewe inawakilisha pumziko la Mungu, kwasababu katika saba ndipo Mungu aliingia katika pumziko lake. Na ndio maana ukisoma kwenye biblia, Mungu hakuiwekea sabato yake mipaka kwamba iwe tu ni katika siku ya saba ,hapana.. Bali  utaona alikwenda mpaka kwenye mwaka wa Saba, ilikuwa kila mwaka wa saba, hakuna kupanda, wala kwenda kufanya kazi yoyote mashambani, bali waipumzishe ardhi, watulie majumbani kwao. Utalisoma hilo katika..

Walawi 25:1 “Kisha Bwana akanena na Musa katika mlima wa Sinai, na kumwambia,

2 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapoingia katika nchi niwapayo, ndipo hiyo nchi itashika Sabato kwa ajili ya Bwana.

3 Panda shamba lako miaka sita, na miaka sita lipelee shamba lako la mizabibu, na kuyachuma matunda yake;

4 lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi, ni Sabato kwa Bwana; usipande shamba lako, wala usipelee shamba lako la mizabibu.

Unaona, haikuishia hapo tu kwenye mwaka wa 7, bali pia miaka hiyo miaka 7, ikipita mara saba tena, kuna sabato nyingine itakayokwepo katika mwaka unaofuata..yaani 7×7 =49, ikiwa na maana, mwaka wa 50 ni sabato ya kumziko na maachilio, inayojulikana kama YUBILEE.

Walawi 25:11 “Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni yubile kwenu; msipande mbegu, wala msivune kitu hicho kimeacho chenyewe, wala msizitunde zabibu za mizabibu isiyopelewa.

12 Kwa kuwa ni yubile; utakuwa mwaka mtakatifu kwenu; mtakula maongeo yake yatokayo shambani.

13 Mwaka huo wa yubile mtairudia kila mtu milki yake”.

Haiishii hapo tu, tutakuja kuona mbele kidogo, sabato nyingine ambayo Mungu ameificha katika maandiko, ambapo ipo katika miaka 1000 kwa ajili ya wateule wake.

Sasa ikiwa tumeshafahamu, sabato ni PUMZIKO, na sio siku fulani, au mwezi fulani, au mwaka fulani, tutafahamu sasa kuwa hata wana wa Israeli kutolewa Misri na kupelekwa Nchi ya Kaanani, ni kwamba walikuwa wanaingizwa katika Sabato yao, (yaani rahani mwao,) ambayo Mungu alikuwa amewaandalia.

Lakini biblia inatuonyesha kuwa sio wote waliweza kuingia katika hiyo raha ya sabato yao, kutokana na kutokuamini kwao na matendo yao kuwa maovu. Si wote waliweza kuingia katika nchi ibubujikayo maziwa na asali isipokuwa wale wawili tu  lakini wengine wote waliosalia Mungu aliwaua kule jangwani.

Waebrania 3:8 “Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha, Siku ya kujaribiwa katika jangwa,

9 Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arobaini.

10 Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu;

11 KAMA NILIVYOAPA KWA HASIRA YANGU, HAWATAINGIA RAHANI MWANGU.

12 Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.

13 Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.

14 Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho;

15 hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha.

16 Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?

17 Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?

18 Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale”.

Unaona? Wengi wao walishindwa kuingizwa katika pumziko lao, kutokana na kuasi kwao.. Lakini sasa bado biblia inatuambia, sabato yao ilikuwa ni kivuli tu cha sabato halisi inayokuja huko mbeleni ambayo Mungu aliwaandalia watu wake, waaminifu.  Mtume Paulo alisema kama ingekuwa Yoshua amewapa raha yenyewe, basi Daudi asingeandikaa tena mahali fulani huko mbeleni juu ya watu wa Mungu kuingia rahani mwa Mungu.

Waebrania 4:7 “aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo,kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu.

8 Maana kama Yoshua angaliwapa raha, asingaliinena siku nyingine baadaye.

9 Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu”.

Umeona? Sisi kama watakatifu tunaomngojea Bwana bado hatujaingia kwenye raha yetu, au sabato yetu, ambayo Mungu alituandalia tangu zamani.. Sasa kumbuka Mungu huwa anapenda kutumia namba SABA, hasaa kuwakilisha sabato yake, kwa kustarehe kwake siku hiyo.

Na biblia inatuambia kwa Mungu miaka elfu moja ni sawa na siku moja. (2Petro 3:8). Sasa kama ulikuwa hujui ni kwamba tangu wanadamu tuumbwe, hadi sasa imeshapita miaka 6000, aidha inaongezeka kidogo sana, au inapungua kidogo sana. Lakini tupo katika mduara huo huo wa miaka elfu 6. Yaani Tangu Adamu mpaka Nuhu, inakadiriwa ni  miaka elfu 2 ilipita, na tangu Nuhu Mpaka kuzaliwa kwa Yesu vilevile inakadiriwa ni miaka elfu 2 ilipita, na tangu kuzaliwa kwa Yesu hadi sasa tunajua ni miaka elfu 2 tupo, kwahiyo jumla ni miaka elfu sita.

Na kama tunavyofahamu kwa Mungu miaka elfu ni sawa na siku moja, kwahiyo mpaka sasa ni kama siku 6 tu kwa Mungu zimepita, na siku ya saba ni sabato yake. Hivyo miaka elfu moja ijayo itakuwa ni sabato ya Mungu kwa watu wake.

Hapo ndipo lile Neno la UTAWALA WA MIAKA ELFU MOJA linakuja kutimia, ambalo Kristo atatawala na watakatifu wake hapa duniani, dunia ikiwa katika hali ya amani na furaha tele.. Kwa maelezo marefu juu ya utawala huu wa amani, tutumie ujumbe inbox tukupe somo lake.

Wakati huo dunia hii itakuwa kama paradiso, kwasababu hakutakuwa na shida wala taabu, wala mateso, tutamfurahia Mungu wetu kwa Muda mrefu sana wa miaka elfu moja, wakati huo sio wa kukosa ndugu yangu..lakini inasikitisha kuona kuwa wengi wetu hatutaingia katika raha hiyo kwa mfano tu wa kuasi kwa wana wa Israeli kule jangwani..

Hizi ni nyakati za za kumalizia hakutakuwa na kanisa lingine zaidi ya hili, yaani sisi ndio tutakaoshuhudia tendo zima la UNYAKUO, Jiulize wewe utakuwa wapi wakati huo utakapofika ndugu yangu, Na ndio maana mtume Paulo ametuonya na kutuambia..

Waebrania 3:12 “Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.

13 Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi”.

Waebrania 4:11 “Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi”.

Huu sio wakati wa kutanga tanga na huu ulimwengu, Huu ni wakati wa kuelekeza macho yetu mbinguni, tuhakikishe kuwa hata tukifa tutakuwa katika ufufuo wa kwanza, na unyakuo ukipita basi tunaenda kumlaki Bwana Yesu mawinguni, ambapo tutakula ile karamu ya mwana kondoo kisha tutarudi kutawala na Bwana hapa duniani.

Je! Umeokoka? Kama bado unasubiri nini? Tubu dhambi zako mfuate Yesu, akupe uzima wa milele.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UTAWALA WA MIAKA 1000.

TAFAKARI SANA KABLA YA KUAMUA HATIMA YAKO.

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

Nini maana ya “yasiyokuwapo hayahesabiki”(Mh 1:15)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments