Category Archive Mafundisho

MUNGU AKAAYE KATIKA GIZA KUU.

Shalom nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. 

Ukichunguza utagundua kuna mahali ambapo watumishi wa Mungu, kwa namna fulani wanakwazika, hadi wengine wanaanzisha mashambulizi ya wazi kabisa pale wanapoona baadhi ya vitu ambavyo si vya kiungu vinasimama kwenye eneo la Injili au kazi ya Mungu.

Tengeneza picha wacha Mungu wa kweli wakati ule  wanawaona mamajusi (wasoma nyota), wanawaetea habari za kuzaliwa kwa Yesu duniani, unadhani lilikuwa na ladha nzuri kwao?  mchawi wa Endori analeta taarifa za Samweli, Koreshi mfalme wa kipagani Mungu anamwita mchungaji wake? Ni kama mambo yanachanganyikana hivi.

Wakati mwingine unaweza kusema mbona Mungu anajipinga mwenyewe?

Tunasoma katika maandiko..

Wakati fulani Mungu alimtokea Musa katika giza nene sana, na sisi tunajua Mungu ni nuru hakai gizani, ni wazi kuwa wote wanaotokewa na Mungu ni lazima nuru iwaangazie kama kiwakilishi chake mfano Paulo alivyotokewa na Yesu kule Dameski, lakini tunaona hapa Mungu anamwita Musa katika giza nene.

Kutoka 20:21

[21]Basi hao watu wakasimama mbali, naye Musa akalikaribia LILE GIZA KUU MUNGU ALIPIKUWAPO.

[22]BWANA akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli hivi, Ninyi wenyewe mmeona ya kuwa nimenena nanyi kutoka mbinguni. 

[23]Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie. 

Hili ni jambo gumu ambalo huwenda liliwashangaza sana wayahudi, je Musa anaitwa na Mungu gizani? Mbona Mungu anajitokeza mahali pa ajabu hivi, gizani?

Kwanini asingemwita ndani ya mawingu meupe?  Kwenye mwali wa moto kama afanyavyo? Ni kwanini Mungu afanye vile?

Ni kwasababu anataka tufahamu kuwa njia zake hazichunguziki. Yeye hakaririki. 

Warumi 11:33

[33]Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani! 

Tukijua kuwa Mungu ni zaidi ya upeo wetu, basi tusimfunge Mungu katika namna fulani moja, kwamba ili Mungu kumbariki fulani ni lazima awe mtoaji mkubwa sana, ili Mungu ampe yule miujiza mikubwa ni lazima awe mwombaji na mfungaji.

Ili yule awe mtumishi wa kweli wa Mungu ni lazima apite chini ya walezi wa kiroho, kama hana huyo basi hawezi tumiwa na Mungu.

 Ni kweli kwa sehemu kubwa ya wito wa  ki-Mungu hufuata mikondo hiyo, lakini alikuwepo yule mtu anayefanya miujiza kwa jina la Yesu lakini hafuatani na Yesu kabisa wala mitume wake, mpaka mitume wakaanza kumpiga vita..baadaye wakaja kujua kuwa walikuwa wanashindana na kusudi la Mungu.(Marko 9:38-39)

Tafsiri yake ni nini?

Kuna mahali sisi kama watoto wa Mungu tunalazimika kuikubali mipaka na kukiri kuwa si kila njia ya Mungu tutaielezea ipasavyo, kwasababu anaweza kujitokeza pia katika giza  nene, Hivyo tukijua hilo hatupaswi kupoteza muda wetu mwingi kupambana na watu, bali tutumie nguvu zetu nyingi kusimama na kweli, mengine yabaki kwa Mungu tukijua kuwa Iwe kwa hila au kwa nia njema, injili itahubiriwa tu, sisi tutasimama katika njia yetu aliyotuonyesha Bwana.

 Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

VITU VITATU VINAVYOPOTEA SAWASAWA NA LUKA 15

Ukisoma Injili ya Luka utaona Bwana Yesu anafundisha vitu vitatu tofauti vinavyopotea.

 

1) Kondoo: Luka 15:3-7

2) Shilingi: Luka 15:8-10

3) Mwana: Luka 15:11-32

> Kondoo anapotea kutoka kwenye kundi, na kuishi maporini, anaanza kutafutwa na mchungaji.

> Shilingi inapotea ndani ya nyumba, inaanza kutafutwa na mwanamke.

> Lakini mwana anamwacha makusudi baba yake anachagua kwenda nchi ya mbali. Anangojewa na baba yake.

Haya ni makundi matatu ya watu ndani ya nyumba ya Mungu.

Kundi la kwanza ni aina ya watu ambao hutoweka katikati ya jamii ya waaminio, ukichunguza sababu sio kwamba wamedhamiria wao kuwa hivyo, lakini udanganyifu wa dhambi, anasa za kidunia, na mafundisho ya uongo, huwapoteza, na kutokomea huko. wakati wa mwanzoni hawajijui kama wanapotea…lakini baadaye wanapojikuta katika ukame wa kiroho, katika kuharibika, kuvurugwa, ndio wanagundua kuwa njia waliyoiendea sio sahihi.

Wanaanza kutaabika huku na huko, kutafuta msaada lakini hawaupati, mpaka watakaporudi kwenye zizi lao. Sasa Hapa ni wajibu wa kanisa kuwafuatilia, watu na namna hii.

Ndio hapo Bwana Yesu anasema ……

Luka 15:4-6

[4]Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?

[5]Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi.

[6]Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.

Lakini kundi la pili hufananishwa na ile shilingi iliyopotea. Kumbuka ilipotelea ndani, sio nje.

Hili ni kundi la watu ambalo haliondoki ndani ya kanisa, lakini linapotelea likiwa huko huko. Hawa ndio wapo kwenye hatari kubwa zaidi kwasababu wanaweza wakawa wanaendelea kuwa viongozi, wazee wa kanisa, waimba kwaya lakini maisha yao yapo mbali na Kristo, ni wazinzi, walevi, washirikina.

Kama wewe ni mmojawapo, tubu haraka kwasababu kuwa katikati ya kundi haimaanishi umekubaliwa na Mungu, Yuda aliishi na Bwana Yesu miaka yote, na akafanya miujiza lakini bado alikuwa upotevuni.

Halikadhali kanisa linapowagundua watu kama hawa, ni wajibu wao kuwarejesha aidha kwa mafundisho, au maonyo, au makaripio ili wapone.

Ndio hapo Bwana Yesu akasema..

Luka 15:8-10

[8]Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione?

[9]Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.

[10]Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.

Lakini kundi la tatu, ni wale ambao kwa makusudi kabisa wanaamua kumwacha Mungu na kurejea ulimwenguni. Ndio mfano wa yule mwana mpotevu.

Hawa ni wale wanaosema kuanzia leo mimi sipo nanyi, habari za wokovu sitaki. Wanaamua kujiachanisha moja kwa moja na kanisa au habari za kiroho.

Hawa ni kuwaombea, Bwana awape moyo wa kuzingatia wenyewe mioyoni mwao warejee, lakini kanisa linapaswa lifahamu wanaporejea hawapaswi kuwatenga au kuwaona hawafai…kanisa halipaswi kuwa kama yule mwana mkubwa, bali linapaswa liwapokee na kuwajenga upya, kwasababu Mungu anawapokea.

Luka 15:28-32

[28]Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi.

[29]Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;

[30]lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.

[31]Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.

[32]Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.

Je mahali ulipo umemwona aliyemmoja wa kundi hili?

Mfuatilie, mwonye, mwombee.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Je! Naweza nikawa nimepokea Roho Mtakatifu na bado nikataabika na dhambi?

Jibu ni ndio endapo hatutajua tabia za Roho Mtakatifu.

Katika biblia tunaona Petro alipokea Roho Mtakatifu, siku ile ya Pentekoste pamoja na watu wengine, lakini baadaye mtume Paulo anamkemea kwa dhambi ya unafki, ya kula na mataifa, wakati akaapo nao lakini pale wayahudi wanapokuja kuketi naye anajitenga nao.(Wagalatia 2:11-14)

Hiyo ni kutuonyesha kuwa mtu anaweza akapokea kweli Roho Mtakatifu lakini bado akasumbuliwa na dhambi fulani.

Je! Hiyo husababishwa na nini, ilihali tunajua alipo Roho Mtakatifu dhambi haimtawali mtu?

Ni vema kujua kuwa ipo tofauti ya mtu kuwa na Roho Mtakatifu, kujazwa Roho na kuenenda kwa Roho.

Pale mtu anapookoka moja kwa moja hupokea Roho Mtakatifu, lakini ili Roho huyo awe na nguvu ndani ya Mtu, kupokea tu haitoshi bali anapaswa ajazwe, (Waefeso 5:18) lakini sio tu kujazwa bali ajifunze kuenenda kwa Roho, akihakikisha kuwa hamzimishi ndani yake.

Kuenenda kwa Roho ni kutembea na Roho Mtakatifu wakati wote. Ni rahisi mtu kujazwa Roho awapo katika mazingira fulani tu maalumu labda kanisani, au kwenye mifungo au maombi. Lakini kuenenda kwa Roho ni kumruhusu atembee na yeye kila mahali awapo. Ambapo itathibitika kwa tabia ya mtu ya kujikana nafsi, kujichunguza,  kuomba, kujitahidi kuliishi Neno katika mwenendo wake wa kila siku. Mtu wa namna hii akisimama vema Roho wa Mungu humjawa na kumsaidia kushinda wingi wa dhambi.

Na hivyo kamwe hataweza kusumbuliwa na dhambi ya namna yoyote. Hivyo tukirudi kwa Petro. Ni wazi kuwa eneo mojawapo alilegea ndio maana akanaswa na dhambi ya unafki.

Wagalatia 5:16

[16]Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 

Hivyo tujue kuwa kwa jinsi tunavyompa Roho Mtakatifu nafasi mioyoni mwetu ndivyo ambavyo, tunapokea nguvu ya kuzishinda dhambi kirahisi, lakini pale tunapomzuia ndivyo tunavyoanza kulemewa na dhambi.

Pokea Roho, jazwa Roho, enenda kwa Roho, usimzimishe Roho, usimhuzunishe Roho. Utaushinda ulimwengu. 

Tukitembea na mambo yote hayo. Roho ni thabiti kwetu

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

HESHIMA YA KIONGOZI, NI PALE ANAPOJIONYESHA NI DHAIFU.

2 Samweli 6:22

[22]Kisha nitakuwa hafifu zaidi, nami nitakuwa mnyonge machoni pangu mimi mwenyewe; lakini kwa wale vijakazi uliowanena, kwao nitaheshimiwa.

Pale kiongozi anapokubali kuwa dhaifu machoni pake mwenyewe ndio mwanzo wa yeye kuwa na heshima machoni pa watu wake.

Kinyume chake ni kweli pale kiongozi anapotaka kujiwekea heshima yake mwenyewe ndivyo anavyokuwa dhaifu machoni pa watu anaowaongoza.

Mke wa Daudi alidhani Daudi atadharauliwa kwa kucheza cheza na kuruka-ruka mpaka nguo kumtoka mbele za Bwana na watumishi wake. Lakini kinyume chake, kumbe ndivyo walivyompenda na kumthibitisha zaidi.

Daudi alikuwa ni kiongozi wa kiroho wa watu, sio mfalme tu wa watu, haikuwa rahisi kumtofautisha na mtu mwingine yeyote, katika bidii yake ya kumtafuta Mungu, hakukitanguliza cheo alichokuwa nacho, palipostahili kufunga sana na kuomba alifunga, palipostahili kulia alilia na kuvaa nguo za magunia, palipostahili kuimba aliimba kwa nguvu zake zote hadi nguo kumdondoka.

Alitenga mambo ya ufalme na ibada, alionyesha bidii kuwathibitishia watu kuwa yeye ni mnyonge, na mdhaifu, mbele ya macho yake mwenyewe, ndio maana mke wake akamdharau. Akasema mimi siwezi kuitwa mke wa mfalme wa namna hii, asiyejitofautisha na vijakazi wake, ambaye haeleweki kama ni mfalme au mchungaji.

Unyenyekevu aliokuwa nao, alipokuwa  mchungaji wa kondoo, ndio huo huo aliendelea nao alipokuwa mchungaji wa watu. Katika namna ya kimwili alionekana dhaifu, tofauti na wafalme wengine, waliokuwa wanajivunia majeshi, Daudi alijivunia Jina la Bwana.

Halikadhalika wewe kama kiongozi wa kiroho, Je!, unaweza kuwa si kitu, kwa mambo unayoyatenda kwa Mungu wako, yanayopelekea mpaka wengine kukudharau, kwa kusema unajishusha daraja?

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

PALE ADUI YAKO, ANAPOKULETEA ZAWADI YA UPENDO.

Sauli alikuwa ni adui mkubwa sana wa Daudi, kiasi cha kumfanya maisha yake yote yawe ni mafichoni tu na ugenini kwa miaka mingi. Lakini cha ajabu ni kuwa uadui aliokuwa anauongeza kwa Daudi, uliongeza pia upendo mwingi kwa Daudi kupitia mwanawe Yonathani.

1 Samweli 19:1-2

[1]Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi.

[2]Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha;

1 Samweli 20:17

[17]Naye Yonathani akamwapisha Daudi mara ya pili, kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwake; kwa maana alimpenda kama alivyoipenda roho yake mwenyewe.

Upendo ambao Daudi mwenyewe baadaye anashuhudia ulizidi upendo wa mwanamke..

2 Samweli 1:26

[26]Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, Ulikuwa ukinipendeza sana;

Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, Kupita upendo wa wanawake.

Naam, Familia moja inatoa uadui uliozidi na wakati huo huo inatoa upendo usio na kifani.

Na hatimaye upendo ukazidi nguvu uadui wote..

Popote unapojikuta hupendwi, unapigwa vita, unatendewa mabaya, unaonewa wivu, bila sababu yoyote, fahamu kuwa hapo pia pana upendo mwingi sana nyuma yake uliojificha.

Kwanini pengine huuoni?

Ni kwasababu unashindana na maadui zako badala ya kuwaombea mema. Mwangalie Daudi hakudhubutu kushindana na bosi wake, ijapokuwa alijua anawindwa naye ili auawe, hata yule mtu aliyejifanya amemuua mfalme, Daudi hakufurahishwa naye, kinyume chake alimwua huyo, hata alipothibitisha kifo mfalme Daudi hakucheka bali aliomboleza na kulia.

Hatimaye Mungu akampa zawadi ya upendo kupitia mtoto wa huyo huyo adui yake, ndiye Yonathani.

Hii ndio sababu kwanini Bwana Yesu anasema wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi. Kwasababu ndani yao pia upo upendo mwingi sana usiouona.

Mathayo 5:43-44

[43]Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;  [44]lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

Ikiwa ni boss wako, anakupiga vita mwombee kwa kuugua kabisa, sio kinafki mnyororo ulio nyuma yake utakupenda kwa upendo mkuu, unaorudisha kwake.

Mungu anapenda, tuitafute amani kwa bidii zote (Waebrania 12:14). Je! Unamwona adui yako kwa jicho lipi?

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

PALE WATUMISHI WANAPOSHINDWA KUTOA PEPO.

Mwanzoni nilidhani kilichowafanya mitume washindwe kumtoa yule Pepo ambaye alimvaa yule kijana, na kumtupa majini, ni uwezo wa pepo yule. Kwamba alihitaji kiwango cha juu zaidi cha kiroho ili kumshinda ambacho hicho kinakuja katika mifungo na maombi mengi kama Bwana Yesu alivyosema.

Marko 9:28-29

[28]Hata alipoingia nyumbani, wanafunzi wake wakamwuliza kwa faragha, Mbona sisi hatukuweza kumtoa? 

[29]Akawaambia, Namna hii haiwezi kutoka kwa neno lo lote, isipokuwa kwa kuomba.

Lakini uhalisia ni kwamba sio kuwa pepo lile lilikuwa na nguvu nyingi za ukinzani. Bali lilikuwa ni sawa tu na mapepo mengine ambayo walishawahi kukutana nayo huko nyuma, na huwenda hata yale yalikuwa ni yenye nguvu zaidi ya hili, lakini waliyatoa yote, na hapa wameshindwa…walijiuliza sana, mpaka wakaenda kumuuliza Yesu.

Ndipo Yesu akawaambia namna hii haiwezi kutoka isipokuwa kwa kuomba.

Hapo anaposema isipokuwa kwa kuomba, hamaanishi kuwa kiwango chao cha maombi kipo chini, lakini hasaa analenga “Utegemezi” wao kwa Mungu umeshuka.

Ikumbukwe kuwa wakati mfupi nyuma, Yeye alikuwa mlimani siku tatu, uweponi mwa Mungu, usiku na mchana anamtafakari Mungu lakini ni wanafunzi tu watatu walioongozana naye, ambao ni Petro, Yohana na Yakobo. Wengine wote waliosalia hawakuwepo, wapo bize na huduma, muda wa utulivu na Mungu hawana, muda wa kudumu magotini kujinyenyekeza kwa Mungu umefinywa .

Hawakujua kuwa utegemezi wao wa jana sio sawa na wa leo, ndio hapo wakashindwa kutoa pepo.

Hivyo wakajifunza, kuwa pamoja na huduma lakini pia kuwepo uweponi mwa Bwana kimaombi ni muhimu vinginevyo tutashindwa kutatua matatizo mengi  ya kihuduma.

Nasi tujue nguvu za jana, haziwezi kuwa za leo, ikiwa hatatuendeleza utegemezi wetu kwa Mungu.

Inawezekana kabisa ukaitatua hiyo changamoto leo kwa ushindi wote, lakini kesho ikakushinda, ukapona leo, lakini kesho ugonjwa ukakurudia..

Ukatoa pepo leo lakini kesho ukashindwa, angalia utegemezi wako umeyumba kiasi gani..

Kisha rudisha ile namna yako ya ukaribu na Mungu, pata muda wa utulivu mwingi, kutafakari Neno, kuomba, kufunga, kuimba na kuabudu, na kuisikia sauti ya Mungu, hiyo yote ndio inaitwa kuomba…fanya hivyo mara kwa mara..hatimaye kile kilichokuwa kionanekana kama ni changamoto kinatatulika tena.

Tatizo sio nguvu, tatizo ni kiwango cha utegemezi wako. Kwasababu nguvu tayari zipo hazijatengenezewa njia ya kutoka.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JIFUNZE KUTENGA UKUAJI WA KIROHO NA KARAMA YAKO.

Mtu anapookoka, vitu viwili huwa vinaanza kukua ndani yake kwa pamoja cha kwanza ni Karama, na cha pili Roho.

Lakini la kutilia maanani, ni asili ya ukuaji wao, kwasababu karama huwa inatabia ya kukua kwa haraka sana kuliko roho ya mtu.

Karama inaweza ikakua ndani ya mda mfupi sana, baada ya kuokoka, na isiwe na maandalizi mengi, Kwamfano mtu anaweza akawa amepewa karama ya unabii, karama ya uponyaji, karama ya lugha na fasiri za lugha, karama ya miujiza na vikaanza kufanya kazi kwa nguvu sana,. Sasa mahali pa kuwa makini sana ni hapo, kwasababu pale inapoonekana karama wengi hudhani ndio ishara ya ukuaji wa kiroho.

Na pengine huyu mtu anaweza kujiona amepiga hatua kubwa sana, kumbe sio. Ukuaji wa kiroho ni hatua ya taratibu sana, inayochukua safari ya muda mrefu hata miaka. Na ndivyo ambavyo Mungu amekusudia.

Haijalishi utawahi kuelewa maandiko, karama yako itatenda kazi kwa ukubwa kiasi gani, bado Mungu humtengeneza mtu taratibu, kama tu vile mwili wake unavyokuwa taratibu. Ilimchukua Musa miaka  arobaini (40), kuwa mchungaji wa Israeli aliyeaminiwa na Mungu, ilimchukua Paulo miaka kumi na nne (14) mpaka awe mtume wa kiMataifa, ilimchukua Bwana Yesu miaka thelathini (30), mpaka awe mwokozi.

Sio kwamba muda wa hapo katikati walikuwa ni wazembe sana, hawamchi Mungu, ndio maana muda ukapita mrefu hakionekani chochote kilichofanyika hapana, bali matengenezo ya mwanadamu yafanywayo na Mungu huwa yanaenda kwa hatua nyingi ambazo humchukua muda, ijapokuwa sisi tutayataka yawe kufumba na kufumbua, lakini kwa Mungu sivyo.

Je! Ni madarasa yapi ambayo mtu anapitia hapo katikati?

Nyakati za ukimya wa Mungu: Hapa Mungu anamwandaa mtu katika ukimya wake, si rahisi kusikia chochote, kuona chochote, kama ilivyokuwa mwanzo, lakini haimaanishi kuwa Mungu hayupo na mtu huyo, bali anajengewa ndani yake saburi na Imani. Usiishi tena kwa hisia au misisimko bali kwa Imani katika ahadi za Mungu. Jambo hili linaweza kumchukua mamiezi hata miaka.

Nyakati za mafunzo: Hapa Mungu anamweka chini ya waalimu, kumfundisha, ni wakati wa kulishwa Neno, na kupokea maarifa mengi, na uzoefu wa kiroho, kwa waliomtangulia. Kama Kristo alivyokaa chini ya waalimu akiwasilikiliza, akiwatazama, na kuwauliza maswali (Luka 2:46). Vivyo hivyo huyu naye ni lazima tu atapitishwa chini ya watu kumfundisha, na akikwepa darasa hili, hatoona maendeleo yoyote ndani yake.

Nyakati hizi, huambatana na kusikiliza mahubiri, kusoma vitabu, kuwauliza maswali, kuhudhuria semina na vipindi vingi vya mafundisho.

Nyakati za utulivu na kutengwa: Hizi ni nyakati ambazo Mungu atakutenga mbali na ulimwengu, au kukupunguzia mahangaiko, ili upate muda mwingi wa kuomba na kufunga na kujisomea Neno peke yako. Nyakati hizi wengine hata watafute kazi vipi hawapati, ukiona hivyo tumia muda huo kumkaribia Bwana, kwasababu Mungu anakufundisha kujenga mahusiano yako binafsi na yeye. Ili uielewe sauti ya Mungu.

Nyakati za Kunyenyekezwa: Hapa Mungu atakuacha uwe kwenye uhitaji/ utegemezi fulani, atamwagiza kunguru (ndege mchafu), akuhudumie kama ilivyokuwa kwa Eliya, sio kwamba ameshindwa kukuletea mtu mwema, au kukupa tu yeye mwenyewe, hapana, anaweza mtumia yule usiyempenda, usiyemtarajia kukuhudumia eneo fulani, lengo akufundishe unyenyekevu wake, na upendo usio na sharti. Ikiwa mtu atakwepa darasa hili, anaukwepa unyenyekevu wa Mungu.

Nyakati za Majaribio: Ibrahimu alipitishwa kwenye majaribio, lengo sio kuangamizwa, bali kuhakikiwa imani yake, , ijapokuwa Ibrahimu alishinda katika mengi ikiwemo kumtoa mwanawe sadaka, lakini alishindwa kwa kusikiliza sauti ya mkewe Sara akazaa na kijakazi wake. Ni kuonyesha kuwa lile utakaloshindwa lisiwe sababu ya wewe kudhani kuwa Mungu amekutupa, lengo, jirekebishe, jifunze kutokana na makosa, ili uwe mkamilifu. Ibrahimu aliposhindwa kwa Sara Mungu alimwambia uwe mkamilifu mbele zangu (Mwanzo 17:1). Kipindi hichi ni kufanywa mkamilifu.

Nyakati za huduma: Hapa Bwana atakujaribu kwa lililo dogo, atakuweka katika utumishi wake, uwahudumie wengine, hapa anapima uaminifu wako. Je! Utatenda kwa uaminifu? Ndicho alichokifanya kwa mitume wake (Mathayo 10), alipowatuma wawili wawili, kabla ya huduma kamili kuja juu yao siku ya pentekoste.

Wito kamili: Hapa Mungu amekuhakiki na kukuthibitisha, kuwa chombo chake kiteule. Ndipo anapokutumia jinsi apendavyo, yawe kwa makubwa au madogo, Hapa ni rahisi kuona mema mengi sana ya Mungu, katika maeneo mbalimbali ya rohoni.

La kufahamu tu, hatua hizi zinaweza kuingiliana, yaani ukapitishwa tatu, au nne, kwa wakati mmoja, na huweza jirudia rudia, mzunguko ukawa huo huo kwa kipindi kirefu.

Lakini mwisho wa mnyororo huo , utaona mwisho wa madarasa hayo Umefundishwa;

Saburi, Imani, maarifa, Kiasi Uaminifu, ukamilifu (utauwa), upendo

Ambavyo vinaenda sambamba kabisa na lile Mtume Petro aliloliandika kwa uweza wa Roho katika..

( 2Petro 1:5-11)

5 Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa,
6 na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa,
7 na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.
8 Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.
9 Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani.
10 Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.
11 Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Hivyo ikiwa umemwamini kweli Kristo, na kumfuata, basi fahamu kuwa lengo kubwa na Mungu ni wewe  ufikie ukuaji bora wa kiroho, jitahidi kutembea kikamilifu kwenye madarasa yake ambayo huchukua muda,  lakini mwisho wake ni TAJI LA UZIMA lisilonyauka, kwa kufuzu madarasa ya Mungu.

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

PALE MUNGU ANAPOHUDUMU KUPITIA KULALA KWETU.

Usingizi, unapopita kiasi, hutuletea hasara, na umaskini, biblia imeliweka wazi hilo (Mithali 6:9-11), na sio usingizi tu, bali mambo yote yanayoonekana mazuri kama vile chakula, tendo la ndoa kwa wanandoa, yakikosa kiasi huleta uharibifu, Lakini usingizi kama usingizi, sio jambo baya, endapo tutaliona kiroho.

Mungu alipomleta Mwanamke duniani, alitumia njia ya usingizi, kama kanuni ya kumtoa kwa mwanamume, ingewezekana kabisa Mungu kumchukua Adamu kwenye maono kama alivyomchukua Yohana kule Patmo, kisha amuumbe Hawa kwa njia hiyo, au angemwacha macho, ashuhudie kazi yote ya upasuaji inavyofanyika, lakini hilo hakulichagua bali alitumia usingizi.

Robo ya maisha yako, unakuwa usingizini, hivyo huo muda, sio kwamba hakuna chochote kinachoendelea, au muda wako unapotea kama wengi wanavyodhani.

Watafiti wa kisayansi wanasema mtu anapokea taarifa katika ubongo, anapokuwa macho, lakini pale anapolala, taarifa zile ndipo zinapokusanywa, na kuhifadhiwa. Sasa huo ni utafiti wao, ambao tunajua kwa sehemu una uhalisia, lakini sisi wa rohoni tunaona zaidi ya mwilini.

Usipojua kuuandaa usingizi wako vema, basi unaweza kuzuia kazi za Mungu kutimilika vizuri tulalapo, kama tu  vile tunavyoweza kuzuia kazi za Mungu anazotenda ndani yetu wakati wa mchana, tusipofuata kanuni zake.

Ukiona mara nyingi usingizi wako unavurugika, hulali, wakati mwingi unataabika usiku, unaota tu ndoto mbaya kila siku, magonjwa ya usiku yasiyokoma, fahamu kuwa pia hali yako ya kiroho inadhoofika.

Ni nini Mungu hufanya usiku?

  1. Tulalapo Mungu huleta taarifa: Ndivyo alivyofanya kwa Ibrahimu, Danieli, Yusufu, n.k.(Ayubu 33:14)
  2. Tulalapo Mungu hutuponya magonjwa yetu: Udhihirisho wa wazi, Angalia Ushuhuda wa maisha yako, ni mara nyingi umelala na magonjwa umeamka mzima.
  3. Tulalapo Mungu hutukuza kiroho: Ukuaji wa kiroho kama vile wa kimwili, huendelea mchana na usiku (Marko 4:27)
  4. Tulalapo Mungu hutuburudisha: Usingizi ni starehe Mungu alioubuni kwa ajili yetu, ili kutupa utulivu na uchangamfu mpya kwa siku ijayo: (Zaburi 127:2)

Ili mojawapo ya huduma hizi, au zote, zitimie ndani yetu, basi jifunze kufanya yafuatayo.

Siku zote omba, kabla ya kulala,  Kwa kufuata mpangilio huu.

Sema, Bwana Yesu, yote uliyonifundisha kutwa nzima ninaomba usiku wa leo, yazamishe kwenye vyumba vya ndani vya moyo wangu, nisiyasahau.

Bwana Yesu lile agizo kuu, ulilosema nami kutwa nzima, au siku zangu za nyuma, lithibitishe  tena kwa kupitia njozi zangu.

Bwana Yesu nijuze yote kuhusiana na mambo ya kesho na yale yanayokuja mbeleni kupitia njozi zangu.

Bwana ninakwenda kinyume ni mashambulizi yote ya usiku yatokayo kwa yule mwovu, ndoto za kipepo, magonjwa, na madhaifu ninavifuta kwa jina la Yesu Kristo. Amen

Sikuzote ona usiku wako, ni sehemu ya huduma. Jipe muda wa kupumzika, huku umeuandaa kwa maombi mazuri.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

UPANDE WA UKUAJI WA KIROHO, ULIOSAHAULIKA

Ni maswali mengi yanaulizwa na watakatifu,  mbona ninajuhudi sana,  ninahudhuria vipindi vingi vya mafundisho,  mifungo na maombi, semina na mikutano, na makambi makubwa ya ujazo wa Roho Mtakatifu,  ninapokea nguvu, Mungu anatenda makubwa, lakini najiona moyoni bado  sina ukuaji mzuri wa kiroho?

Kwanini, sababu ni nini?

Tukisoma maandiko tunaona kuna upande ambao, tunausahau kuutilia msisitizo katika kumjua Kristo, na pengine hauhubiriwi sana madhabahuni, lakini ni muhimu

Upande huo mtume Paulo aliusema katika kitabu cha Wafilipi,

Wafilipi 3:10 ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na USHIRIKA WA MATESO YAKE, nikifananishwa na kufa kwake;

Zingatia hapo, anataja mambo mawili anasema, ili nimjue yeye na uweza wa kufufuka kwake,

Lakini pia..

Na ushirika wa mateso yake.

Watu wanatazama sana, eneo la kwanza, ambalo ni uweza wa kufufuka kwake, yaani wanatafuta nguvu za Mungu kwa juhudi kubwa, miujiza, uponyaji, baraka, unabii, ujazo wa Roho Mtakatifu, jambo ambalo ni zuri sana, na linapaswa litafutwe, lakini, bado mtu huyu kwa bahati mbaya anaweza asikamilike kama hatataka na sehemu ya pili pia ya kumjua Kristo, ambayo ni ‘ushirika wa mateso yake’.

Paulo alifanya miujiza lakini alifungwa pia kwa ajili ya hiyo, aliponya watu lakini alipigwa mawe, alifanya makubwa lakini bado alitukanwa, na kufanyiwa visa.

Ukuaji mzuri wa kiroho, hautazamii tu, kupokea nguvu za Mungu, unatazama pia Ushirika wa mateso yake.

Tunataka tumjue Kristo, lakini hatutaki kuudhiwa kwa gharama tulizoingia kwa ajili yake, Yesu alisema tutapata mara mia kweli, lakini pia tutapata na udhia (Marko 10:30).

Ndege hawezi kuruka kwa bawa moja, ni lazima yote mawili yafanye kazi, Tukimtaka Mungu kwa nguvu zake, tu lakini hatumtaki na mateso yake, bado maendeleo hayatakuwa makubwa. Haijalishwi tutajazwa Roho kiasi gani.

Ushirika wa mateso ni pamoja na kukubali kuchukiwa kwa ajili ya jina lake, kutengwa kwasababu ya misimamo yako ya kiroho, kumbuka gharama ya Danieli kupendwa ni pamoja na kukubali kutupwa kwenye tundu la simba, Yusufu kuwa mkuu ni pamoja na kuuzwa na ndugu zake kwasababu ya misimamo yake, Ayubu kuitwa mcha Mungu ni pamoja na majaribu aliyoyastahimili. Huo ndio ushirika wa mateso yake.

Usifurahie tu, kuona nguvu za Mungu, jiulize binafsi ni wapi nimeshiriki mateso ya Kristo, kwa kuzikubali gharama?  Palipo na gharama na umakini wa kiroho, ushirika wa mateso ni lazima utaambatana nawe.

Tukue kiroho.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

NINA WATU WENGI KATIKA HUU MJI.

Ziara ya Paulo Korintho ilikuwa ya ukinzani sana, ambapo yamkini kama sio Mungu kumthibitishia neno lake, asingeendelea kubaki kwenye mji ule, kwasababu watu wa mji ule sio tu walipingana naye waziwazi, bali biblia inasema pia walimtukana Mungu. Jambo ambalo lilikuwa gheni sana machoni pa watendakazi wa injili, (Matendo 18:1-6)

1 Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho…
4 Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani..
5 Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo.
6 Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung’uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa.

Lakini katika moyo wa ukinzani ule, ambao alikuwa karibu kuondoka, Bado Mungu alimtokea katika maono usiku akamwambia, baki, kwa kuwa mimi nina watu wengi katika mji huu. Sio ‘watu tu’, bali ‘watu wengi’, idadi kubwa mno, umati wa watu.

Matendo 18:9-11

9 Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze,
10 kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; KWA MAANA MIMI NINA WATU WENGI KATIKA MJI HUU.
11 Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu.

Mara nyingi tunapokuwepo kwenye miji mikubwa, na kuona uzito na ugumu wa mioyo ya watu, na ubize wao, na kiburi chao ni rahisi kukata tamaa na kusema hapa Mungu hana watu tena.

Lakini kaa ukifahamu Mungu bado ana watu wake wengi nje ya kanisa, wanaopaswa waje ndani ya kanisa.  Katikati ya wanaomtukana yeye, wanaopingana na wewe, kwenye mikanganyiko ya kipepo ya kila namna, Mungu bado anaona watu wengi ambao anataka waokolewe.

Badili mtazamo wako kuanzia leo, injili sio macho yetu, ni macho ya Mungu, pale tunapoona hapafai, haimaanishi kuwa hapafai machoni pa Mungu.

Endelea, tena na tena, lipo kusudi kubwa la Mungu nyuma ya mahali ulipo.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.