Title September 2022

Amali, na kila kazi ya ustadi, inatokana na mtu kupingana na mwenzake.

SWALI: Naomba kufahamu mstari huu unamaana gani?

Mhubiri 4:4 “Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo”.


JIBU: Sulemani ni mtu ambaye alipewa na Mungu uwezo wa kutambua hekima ya mambo yote yanayotendeka huku duniani.. Na moja ya jambo ambalo aliliona na kutolea habari zake ni kuhusiana na chanzo cha mafanikio mengi ya watu ni nini?.. Na ndio hapo anasema..

“Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana na mwenzake”.

Kwamba kila utajiri, au kazi za ustadi, yaani nyumba nzuri, magari mazuri, mavazi mazuri, hatua zote za mafanikio, asilimia kubwa hutokana na mtu kupingana na mwenzake, kwa tafsiri iliyo nzuri ni kwamba hutokea mtu kushindana na mwingine..ambacho chanzo chake ni wivu.

Kwamfano, mtu atasema mbona Fulani amenunua gari, mimi sijanunua, ngoja nikakope pesa nifanye kazi juu chini na mimi mwaka huu ninunue la kwangu zuri kuliko lile.. Sasa mtu kama huyu atapata gari kweli, lakini chanzo cha gari lake sio malengo yake, bali ni kwasababu wenzake wanayo magari yeye hana.

Hata mashirika makubwa, kufanikiwa kwao ni kwa mashindano, utaona kampuni moja la simu limetoa ofa hii, kesho lingine linaiga ofa ile ile na zaidi, ili lisipoteze wateja.. Hivyo yamefanikiwa kwa njia hizo hizo, za mashindano.

Tajiri mmoja atashindana na tajiri mwenzake ili awe namba moja, hivyo atafanya kazi kwa bidii usiku kucha, ili asishindwe na mwenzake, watashindana kibidhaa n.k.. Mchungaji mmoja atashindana na mchungaji mwingine kwa wingi wa washirika, au kwa ukubwa wa kanisa,

Sasa hayo yote Sulemani ameyaona na kusema ni ubatili, ni sawa na kujilisha(kuufuata) Upepo. Maana yake ni kuwa mafanikio yanayokuja kutoka katika wivu, au mashindano, hayana afya yoyote kiroho.

Hii inatufundisha nini?

Wafilipi 2:14-15 inasema..

“14 Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano,

15 mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu”

Kama watakatifu, hatupaswi kutafuta kitu chochote kwa kushindana, utasema mwenzangu ana neema kubwa kama ile, ngoja na mimi nikafunge na kuomba nimpite,. Hapana, bali tunapaswa tuishi kwa kumtazama Mungu,kila mmoja katika nafasi yake aliyopewa na Mungu, na kuitendea bidii hiyo, kwasababu kwa kupitia hiyo ndio Mungu atatufanikisha, na sio kwa neema za wengine..

Bwana atubariki.

Shalom.

Tafadhali share na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “Amali” na “Ijara” katika biblia?

Na alaaniwe ampigaye mwenzake kwa siri.

Nini maana ya mstari huu: (Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.Mithali 27:14 )?

Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe;(Mithali 16:2)

Kuwaogopa wanadamu huleta mtego,(Mithali 29:25)

Mego ni nini kama tunavyosoma katika biblia? (Mithali 17:1)

Rudi nyumbani

Print this post

NITAJUAJE KAMA MAOMBI YANGU YAMEFIKA (YAMEJITOSHELEZA)?.

Biblia inatufundisha kuomba bila kukoma…

Wathesalonike 5:17  “ombeni bila kukoma”

Leo tutatazama ishara chache ambazo zitatutambulisha kuwa kiwango cha maombi yetu kimejitosheleza au kimemfikia Baba yetu.

1.MZIGO KUPUNGUA NDANI YAKO.

Hii ni ishara ya kwanza itakayokutambulisha kuwa maombi yako yamefika kwa Bwana.

Unapoomba na kuona mzigo wa kile unachokiombea umepungua ndani yako, basi hiyo ni ishara kuwa kiwango chako cha maombi kimefikia kilele kwa muda huo.

Sasa swali utauliza utajuaje kuwa mzigo umepungua ndani yako?. Tuchukue mfano rahisi, Ulikuwa una jambo la muhimu au la siri ambalo ulikuwa umepanga kumweleza mtu Fulani (labda rafiki yako), na hujapata nafasi, ila unaitafuta kwa bidii, kiasi kwamba huwezi kutulia mpaka umemweleza jambo hilo, au umpe taarifa hiyo, sasa kipindi utakapokutana naye na kumweleza yote ya moyoni mwako, kuna hali Fulani unajiona mwepesi baada ya hapo, (unajiona kama huna deni tena, umeutua mzigo), unaona amani inarudi, na unakuwa huru.. Sasa hiyo hali unayoisikia baada ya kufikisha ujumbe kwa uliyemtarajia ndio kwa lugha nyingine ya (Mzigo kupungua ndani yako).

Kwahiyo hata sisi tunapoomba, yaani tunapopeleka hoja zetu mbele za Mungu, kabla ya kuzipeleka tunakuwa na mzigo mzito ndani yetu, lakini tunapokaa katika hali ya utulivu na kusema na Mungu kwa unyenyekevu mambo yetu na hoja zetu, basi kuna hali/hisia fulani ambayo Bwana Yesu anaiachia ndani yetu, inayotupa wepesi katika roho zetu, na kupunguza ule mzigo, kiasi kwamba, kama ulikuwa unamwombea Mtu, kuna hali Fulani inakuja ndani yako kuwa maombi yako yamemfikia Mungu, na hivyo amani ya kipekee inashuka ndani yako, na unajikuta ile hamu ya kuendelea kuombea hilo jambo inaisha, badala yake inakuja hali nyingine ya kumshukuru Mungu na kumshangilia na kumfurahia.

2. ANDIKO KUKUJIA au KUMBUKUMBU YA JAMBO FULANI.

Hii ni ishara ya pili ya maombi yetu kumfikia Baba..

Unapokuwa katika maombi, halafu ghafla likaja andiko katika ufahamu wako, na andiko hilo linauhusiano mkubwa na kile ulichokuwa unakiombea.. basi fahamu kuwa maombi yako yamefika, na hivyo Bwana anakuthibitishia kwa kukupa hilo andiko. Au unaweza kuwa unaomba halafu ghafla ukaletewa kumbukumbu Fulani ya kisa Fulani katika biblia, ambapo kupitia kisa hiko imani yako ikanyanyuka na kujikuta unapata amani au furaha kubwa.. basi hiyo ni ishara kuwa maombi yako yamefika, na hivyo katika hiyo hatua na kuendelea ni wakati wa kumshukuru Mungu na kuutafakari ukuu wake, kwasababu Bwana kashajibu na kusikia.

Vile vile unapokuwa katika maombi na moyoni una mzigo mkubwa kwa kile unachokiombea, halafu ghafla ikaja kumbukumbu Fulani ya kipindi Fulani cha maisha ambacho Mungu alikupigania ukauona mkono wake, au ukaja ushuhuda Fulani kichwani mwako wa mtu mwingine, na ghafla ukajiona umepata nguvu nyingine basi hiyo ni ishara kuwa hoja zako zimefika mbele zake na hivyo Bwana amekuthibitishia kwa kukukumbusha uweza wake na mkono wake.

3. NGUVU MPYA.

Unaweza usisikie chochote unapokuwa katika maombi, (yaani usisikie mzigo kupungua ndani yako) au usiletewe andiko lolote, lakini ukajikuta  unapata nguvu ya kuendelea mbele zaidi….

Maana yake kabla ya maombi ulikuwa umekata tamaa, hata nguvu ya kuendelea mbele ulikuwa huna, lakini baada ya maombi..unaona kuna ujasiri umeongezeka ndani yako, kuna nguvu ya kuendelea mbele imekuja ndani yako, ingawa moyoni mzigo bado hujapungua..

Sasa hiyo hali ya kutiwa nguvu kabla ya kupokea majibu ya maombi yako ni ishara kuwa Maombi yako YAMEMFIKIA BWANA, ila wakati wa kupokea majibu yako bado!…Hivyo Bwana anakutia nguvu ili usije ukazimia kabisa, au ukaanguka kabisa…wakati huo zidi kujisogeza mbele zake kwa maombi ya shukrani…

Kwamfano unaweza kuwa unasumbuliwa na ugonjwa ambao ni mbaya sana, na umemwomba Mungu kwa muda mrefu, akuponye na hapo ulipo upo katika hali ya mauti uti, lakini ukajikuta unapata unafuu mkubwa sana, na hata kuendelea na shughuli zako kana kwamba huumwi kabisa.. lakini ule ugonjwa bado haujaondoka!.. sasa hiyo hali ya kupata unafuu baada ya maombi, ni ishara kuwa Bwana alishasikia maombi yako, ila siku kamili ya muujiza mkuu bado!, (na itafika tu)..lakini amekutia nguvu ili kukuonyesha kuwa yupo pamoja na wewe na ili usije ukazimia kabisa..

Vile vile unaweza kumwomba Bwana akupe kazi fulani nzuri ambayo kupitia hiyo utayafanya mapenzi yake, lakini badala ya kukupa hiyo shughuli unayoiomba muda ule uliomwomba, yeye anakupa riziki za kukutosha tu wakati huo.. (ulitegemea upewe kazi lakini yeye anakupa riziki tu)…Ukiona hivyo jua ni ishara ya kuwa maombi yako yameshamfikia yeye, Ndio maana anakutia nguvu…ni suala la muda tu!, mambo yote yatakaa sawa..

Isaya 40:27 “Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie?

 28 Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. 

29 Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo

30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; 

31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”.

Zipo ishara za kutambulisha kuwa maombi yetu yamemfikia Baba yetu, lakini kwa hizi chache itoshe kusema kuwa Bwana Mungu wetu anatupenda na anatujali na anasikia maombi yetu. Lakini kumbuka kuwa kama bado hujampokea Yesu, (yaani hujaokoka), basi fahamu kuwa Mungu hasikilizi maombi yako wala hajibu. (Yohana 9:31)

Sasa ni kwanini hajibu, wala hasikilizi maombi ya watu ambao hawajampokea?.. Ni kwasababu mtu wa namna hiyo hawezi kuomba sawasawa na mapenzi yake, (kwasababu yeye mwenyewe alisema kuwa mafanikio ya mpumbavu yatamwangamiza, Mithali 1:32) na Mungu hapendi mtu yeyote aangamie wala apotee, bali wote wafikie toba na wafanikiwe..Hivyo atahakikisha kwanza unapata wokovu ndipo mengine yafuate..

Kwahiyo suala la kwanza ni wokovu kabla ya mambo mengine yote.. Kama hujampokea Yesu, kwa kutubu dhambi zako, na kubatizwa katika ubatizo sahihi, basi ni vizuri ukafanya hivyo mapema iwezekanavyo, ili uwe mshirika wa Baraka za Mungu.

Lakini kama tayari umeshampokea Yesu na umesimama vizuri katika imani, basi fahamu kuwa yote unayomwomba Mungu atakupatia sawasawa na ahadi zake, hivyo zidi kumwamini na wala usiishiwe nguvu.

Bwana akubariki

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.

SAUTI NYUMA YA ISHARA.

MAOMBI KWA WENYE MAMLAKA.

Rudi nyumbani

Print this post

JE NI KUTII AU KUPATA KWANZA MAARIFA?

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo Bwana wetu, Karibu tuzidi kuyachambua maandiko;

Mwanadamu anasongwa na mambo mawili pale linapokuja  suala la kuamua hatma ya maisha yake ya milele. Je! Atii au apate maarifa kwanza?. Pale Mungu anapomwambia Usizini? Je, asifanye hivyo? Au achunguze kwanza ni nini kipo nyuma ya tendo hilo, ndipo awe huru sasa kuchagua kuzini au kutokuzini?

Ukweli ni kwamba asili ya mwanadamu ni kutaka maarifa kwanza, ya kitu ndipo baadaye atii, Lakini Je! Biblia inatufundisha nini kuhusiana na maamuzi sahihi na Salama ambayo Mungu aliyaweka kwa mwanadamu.

Tukisoma ile habari ya pale bustanini biblia inatuambia,.. Mungu alipanda miti yake, kisha alipomaliza akatoa maagizo kuhusiana nayo akasema..

Mwanzo 2:16 “Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, 17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika”.

Lakini mwanadamu akaona, hayo maelezo ya Bwana Mungu hayajitoshelezi, kwanini atuzuie tusile, hajui kuwa sisi tunataka tupate sababu kwanza, (tupate maarifa), kujua ni nini kwanza kipo nyuma ya mti huo, ndipo tuwe sasa huru kuchagua kuula, au kutoula. Ndipo wao wakauendea na kuula.

Mwanzo 3:4 “Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. 6 Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni MTI WA KUTAMANIKA KWA MAARIFA, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala”.

Lakini walipofanya vile, hawakuvuna chochote, matokeo yake wakajikuta tayari wameshaingia kwenye matatizo ambayo mpaka sasa tunayashiriki, yale maarifa waliyoyategemea kuwafanya  wawe bora, yakawa mauti kwao.

Hii inatufundisha nini?

Asili yetu sisi wanadamu hatukuumbwa kwenye  kupata maarifa kwanza, ndio tuishi, bali kwenye kutii kwanza.. Ndivyo tulivyotengenezwa na Mungu.. Kwamba tukitembea katika kutii tutakuwa salama sikuzote,..hayo mengine yatakuja baadaye. Ndicho alichokifanya Ibrahimu alipoambiwa akamtoe mwanawe sadaka ya kuteketezwa alitii kwanza, hakudadisi na kusema kwanini huyu Mungu atoe maagizo ya kishetani kama haya ya kuua watu, yeye alitii, ndipo akaja kujua sababu baadaye.

Hii ikiwa na maana kuwa,..Kama Yesu katuambia wazinzi wote, na waongo wote, hawataurithi uzima wa milele, bali sehemu yao ni katika lile ziwa la moto. Tunahitaji nini tena, kutafuta uzuri uliopo nyuma ya uzinzi, mpaka tukaujaribu.au kutafuta eneo la kijeografia la jehanamu, tulione ndio tuamini?

Ufunuo 21:8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Bwana Yesu anasema.. Yeye ndio njia, na kweli na uzima, mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yake yeye (Yohana 14:6), FULL STOP!..Sasa  kwanini tutafiti njia zetu wenyewe za kutupa wokovu? Kwanini uishi kwa mitazamo yako, au ya wanadamu, wanaokuambia hakuna mwisho wa dunia, au hakuna maisha baada ya kifo

Katika nyakati hizi za hatari ambazo biblia inazitaja (2Timotheo 3:1), ni lazima “tuongeze maarifa ya kulijua Neno la Mungu, na sio maarifa ya kuyadadisi maneno ya Mungu, kama Adamu na Hawa”..Tutapotea haraka sana, tukiwa watu wa namna hii, kutilia mashaka maneno ya Mungu, kila andiko tunalolisoma, tunasema kwanini iwe hivi, au iwe vile?, kwani kuna shida gani, nikinywa bia yangu na simdhuru mtu? Acha kabisa hayo mawazo ya ibilisi..Utapotea…Wewe tii sasa, sababu utakuja kuzijua mbeleni. Sayansi itakuambia haipo hivyo, ukweli ni huu, mwanadamu wa kwanza alikuwa ni sokwe, uthibitisho umepatikana, hakuna Mungu..Ndugu hapo ndio umepotea kabisa, Kumbatia Neno la Mungu.

Tunapohubiriwa tuache anasa, jambo la kwanza ni kutii, hilo Neno, haijalishi itatugharimu kiasi gani..Tunapohubiriwa tuvae mavazi ya kujisitiri, tuache vimini, tuache rushwa. Tusiulize ulize kwanini..Ni kuweka kando kwanza..Sababu tutakuja kujua huko mbeleni.

Tunusuru roho zetu…Tulipokee Neno la Mungu kama lilivyo.

Bwana atusaidie sana.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Tofauti kati ya Hekima, ufahamu na maarifa, ni ipi?

Maana ya watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa.

AINA SABA (7) ZA UNAFIKI, AMBAZO UNAPASWA UJIEPUSHE NAZO.

Bilauri ni nini kibiblia?(Ufunuo 21:11,22:1)

TUYATENDE MAMBO YOTE KWA UZURI NA UTARATIBU.

Je mke wa Musa alikuwa ni Mweusi?

Rudi nyumbani

Print this post

NI NINI BWANA ANATAKA KUTOKA KATIKA MUUJIZA ALIOKUFANYIA?

Shalom, karibu tuyatafakari maandiko.

Bwana Yesu ameruhusu miujiza itokee kwenye maisha yetu kwa malengo makuu mawili (2), Lengo la Kwanza ni ili SISI TUPATE FAIDA (TUNUFAIKE) na lengo la pili; ni ili TUTUBU.

Wengi wetu tunalijua hili lengo la Kwanza, na ndilo tunalolitafuta kwa bidii, pasipo kujua kuwa Lengo la pili ndio kuu kuliko la Kwanza, na ndilo Mungu analoliangalia kuliko yote.

Ndugu unaweza kumwomba Bwana Yesu akuponye kansa, na kwa huruma zake akakuponya, unaweza kumwomba Bwana Yesu akupandishe cheo kazini na kwa huruma zake akakufungulia mlango huo, ukapata fursa kazini, unaweza kumwomba Bwana Yesu akufungulie mlango wa riziki au kazi, au akupe uzao na kweli akakufanyia muujiza huo mkubwa ukapata uliyoyahitaji, unaweza kumwomba akufanikishe katika ndoa au masomo, na ikatokea kama ulivyomwomba..

Sasa fahamu kuwa Bwana Yesu kakufanyia muujiza huo au miujiza hiyo, lengo lake ni ili wewe uwe na furaha, na uishi maisha mazuri sawasawa na maneno yake haya..

Yohana 6: 23 “Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.

24  Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu”

Hilo ni lengo la kwanza la Bwana kuruhusu miujiza maishani mwako, lakini sio lengo kuu. Kwasababu unaweza kuponywa Kansa, au Ukimwi lakini bado ukaenda kwenye ziwa la Moto, unaweza kupata kazi nzuri, na kufunguliwa tumbo na kuzaa watoto wengi, lakini bado siku ile akakukana. Kwahiyo lengo kuu la miujiza ya Bwana si kutimiza furaha zetu, au mapenzi yetu. Bali lengo lake kuu ni ili sisi TUTUBU TUNAPOIONA MIUJIZA HIYO!!.

Je unakumbuka Mtume Petro kilichomtokea baada ya Bwana kumfanyia muujiza ule mkubwa wa kupata samaki wengi?..Petro hakufurahia tu kupata riziki, hakufurahia kupata fedha za kwenda kununua kiwanja cha kujenga, kwasababu ya ule wingi wa samaki, hakufurahia mikopo atakayokwenda kukopesha hapo baadaye kwasababu ya wingi wa wale samaki.. bali utaona alikimbilia toba..

Luka 5:4  “Hata alipokwisha kunena, alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki.

5  Simoni akajibu akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.

6  Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao zikaanza kukatika;

7  wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama.

8  Simoni Petro alipoona hayo, alianguka magotini pa Yesu, akisema, ONDOKA KWANGU, KWA KUWA MIMI NI MTU MWENYE DHAMBI, BWANA.

9  Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata”

Umeona?.. Simoni hakusema hapo “ondoka kwangu Bwana kwa kuwa mimi ni mtu maskini” au kwakuwa mimi ni mtu mwenye matatizo mengi ya kiuchumi au kibiashara.. bali alisema “kwakuwa mimi ni mtu mwenye dhambi” (maana yake alitubu).. Na ndipo Bwana akamwambia tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.

Lakini jambo la kushangaza ni kwamba katika miji ile ile ambayo Petro alikutana na Bwana mara ya kwanza, yaani miji mitatu ya (Bethsaida, Kapernaumu na Korazini), Miji hii yote ilikuwa kando ya bahari ya Galilaya..Bwana Yesu alikuwa akitembea huku na huko katika miji hiyo, na kufanya miujiza kama hiyo hiyo, aliyoifanya kwa Petro.

Lakini tofauti ya Petro na watu wengine wa miji hiyo, ni kwamba Petro alitubu kwa miujiza ya Bwana, lakini wengine wengi wa miji hiyo, waliifurahia tu miujiza ya Bwana lakini hawakutubu.

Walifurahia tu watoto wao kuona wanatokwa na mapepo, lakini hawakufikiri kuacha dhambi zao, ingawa Bwana alikuwa anawahubiria toba, walifurahia kubarikiwa kazi zao na biashara zao lakini hawakufikiria kutubu, hawakufurahia kuacha ulevi wao, wala kuacha uzinzi wao, wala kuacha rushwa zao wala kuacha mambo mengine mabaya, ingawa waliifurahia miujiza ya Bwana.

Na hatimaye Bwana Yesu akawaambia maneno yafuatayo…

Mathayo 11:20  “Ndipo akaanza kuikemea miji ile ambamo NDANI YAKE ILIFANYIKA MIUJIZA YAKE ILIYO MINGI, KWA SABABU HAIKUTUBU.

21  Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.

22  Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.

23  Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.

24  Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe”

Hapo anasema alianza kuikemea kwasababu haikutubu “si kwasababu haikushukuru baada ya kufanyiwa miujiza”, au si kwasababu waliitumia vibaya ile miujiza, kwamba baada ya kubarikiwa katika shughuli zao walitumia vibaya fedha!.. La!!.. lakini iliikemea kwasababu moja tu kwamba HAIKUTUBU!!

Na tena anasema itakuwa ni rahisi kwa Sodoma kustahimili adhabu yake siku ile ya hukumu kuliko miji hiyo, maana yake ni kwamba kumbe pamoja na kwamba watu wa Sodoma na Gomora waliadhibiwa kwa moto katika mwili, lakini kumbe kuna bado kuna adhabu nyingine inawangojea huko!! Hii inaogopesha sana..

Lakini Bwana Yesu anazidi kusema, itakuwa ni rahisi watu wa Sodoma kustahimili adhabu kuliko watu wa miji hiyo ya Korazini, na Bethsaida na Kapernaumu. Maana yake adhabu ya watu wa Kapernaumu na Korazini na Bethsaida itakuwa ni kubwa sana, katika ziwa la moto.

Ndugu unayesoma ujumbe huu, Tumwogope Mungu!.. Miujiza anayotufanyia kila siku ambayo tunaiona kwa macho yetu sio kwa lengo la kutuburudisha bali ni kwa lengo la sisi Kuamini kwamba yupo na kwamba yeye hapendi UCHAFU, hivyo tutubu!, tuyatakase  maisha yetu, ili tusipate hasara siku ya mwisho ya hukumu.

Ukiaona Bwana kakujibu maombi yako, ni kwasababu anataka uache usengenyaji wako, ukiona Bwana kakujibu maombi yako kimuujiza ni ujumbe kwako kwamba anataka uache kuvaa unavyovaa nguo za kubana na zisizo na heshima, anataka uache ulevi wako, na si kwamba anakusapoti na ulevi wako au uzinzi wako, au uuaji wako, amekuonyesha miujiza hiyo ili wewe ujue kwamba yeye yupo na anakutazama.

Lakini ukidharau sauti ya Mungu hiyo, ambayo inakutaka utubu, na kuifurahia miujiza tu na ishara, basi fahamu kuwa unajiwekea akiba ya hasira ya Mungu..

Warumi 2:4 “Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa WEMA WA MUNGU WAKUVUTA UPATE KUTUBU?

5  Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu”

Mpokee Yesu leo na tubu kwa kudhamiria kuacha dhambi na kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu, na Bwana atakukubali na kukupatia kipawa cha Roho wake mtakatifu.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NAYE ALIKUWA HANA BUDI KUPITA KATIKATI YA SAMARIA.

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 5)

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

MIUJIZA YA KRISTO, HAITEGEMEI KANUNI ZA KIBINADAMU.

Furaha ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.

SWALI: Naomba kufahamu maana ya huu mstari;

Mithali 17:17 “Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu”.


JIBU: Huu mstari unaeleza rafiki wa kweli anapaswa aweje, pia rafiki ambaye atazidi  kuwa kama ndugu anapaswa aweje?

Anasema ‘Rafiki hupenda sikuzote’, Ndio.. hii ni tabia ya rafiki wa kweli, hupenda nyakati zote, ziwe ni nzuri , au ni mbaya, kwamfano, rafiki ambaye siku umemfurahisha anakupenda, lakini siku pia umemuudhi anakupenda, siku umempa anakupenda, lakini siku umemnyima bado anakupenda zaidi. Rafiki ambaye wakati mnawasiliana anakupenda, lakini wakati mlipopotezana kimawasiliano kwa muda mrefu bado anakupenda.

Huyo ndio rafiki wa kweli..

Lakini hapo anaposema “Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu” ..Maana yake ni kuwa Yule ambaye anakuwa na wewe bega kwa bega, katika wakati wa shida zako, na taabu zako, na misiba yako huyo si rafiki tena bali ni ndugu..

Unamwona anakujali, wakati unaugonjwa wa hali ya juu, unamwona, anakushika mkono wakati umefilisika, unamwona unakufariji sana wakati wa msiba wako, unamwona anatafuta kila mbinu, kukusogeza mahali wakati upo katikati ya mateso. Huyo ni rafiki aliyefanyika ndugu.

Kwasababu kama hapo inavyosema ‘ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu’..Maana yake ili mtu aitwe ndugu, ni lazima awe amezaliwa mahususi kwa ajili ya siku za shida zako.

Je! Na sisi tunapoitana ‘ndugu’ na ‘rafiki’ tunatambua wito wetu katika hayo?

Lakini tunamwona mmoja ambaye, ni zaidi ya rafiki, ni pia ni zaidi ya ndugu, ambaye sio tu amekuwa karibu na sisi katika shida zetu, na mateso yetu na hukumu zetu.. Lakini pia aliyatoa maisha yake yote, pamoja na uhai wake, ili kufa kwa ajili yetu.

Yohana 15:13 “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.”

Hivyo basi, hatuna budi na sisi kuuthamini upendo mkuu namna hii, kwa kukubali kukombolewa na yeye, ili tuoshwe dhambi zetu. Kumbuka hakuna ukombozi nje ya Yesu Kristo, vilevile hakuna uwezekano wowote wa sisi kumpendeza Mungu kwa matendo yetu wenyewe. Na ndio maana ilimpasa aje, ili atukomboe, kutoka dhambini.

Waebrania 2:3 “sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia”;

Ikiwa upo tayari kumkabidhi Bwana Yesu maisha yako, basi waweza wasiliana nasi kwa namba zetu hizi, +255693036618/ +255789001312 kwa ajili ya mwongozo huo, bure, na hakika Bwana atayaokoa maisha yako, na kukufanya kuwa mpya tena.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

RAFIKI MWEMA.

JIRANI YANGU NI NANI?

KAMA VILE UMEME UTOKAVYO MASHARIKI UKAONEKANA HATA MAGHARIBI.

Mretemu ni mti gani?

Je ni halali kupiga kura kanisani kuchagua viongozi?

Je Malaika Mikaeli ndiye Yesu mwenyewe?

Je Kauli ya Mungu katika Warumi 11:4 na 1Wafalme 19:18 inajichanganya?.

Rudi nyumbani

Print this post

WALIKUWA WAMECHOKA NA KUTAWANYIKA KAMA KONDOO WASIO NA MCHUNGAJI.

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo.  Nakukaribisha tena tuzidi kuyatafakari maandiko.

Moja ya mambo ambayo, yalimuhuzunisha sana Bwana Yesu ni pale alipowatazama watu wake na kuwaona wanafanana  na kundi la kondoo wafugwao waliopoteza tumaini kabisa na kutawanyika, kila mmoja mahali pake anapopajua yeye..Ina huzunisha sana..

Embu Tusome; kwa utulivu habari hiyo; 

Mathayo 9:35-36

[35]Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.

[36]Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa WAMECHOKA na KUTAWANYIKA kama kondoo wasio na mchungaji.

Hapo biblia inasema walikuwa WAMECHOKA..na KUTAWANYIKA.

Kuchoka kunakozumgumziwa hapo, sio tu kule kwa kutembea umbali mrefu, katika kutafuta  chakula / maji…hiyo ni sehemu ya kwanza..Bali kuchoka kunakolengwa hapo hasaa kunakuja kutokana na kukandamizwa, kujeruhiwa, na kufukuzwa, kutishwa..pamoja na hofu na wasiwasi wa mashaka ya kuraruliwa na mbwa mwitu wakali.

Hii ndio hali halisi yasasa.. Watu wa Mungu WAMECHOKA. Sio kidogo bali wamechoka kwelikweli, Kutokana na kudanyanywa, kuumizwa na watumishi wa uongo, wameharibiwa, wametawanywa.., manabii wa uongo wamechukuliwa fedha zao wakiwaahidia kubarikiwa na kufunguliwa, lakini mwisho wa siku wanajikuta wapo katika matatizo zaidi, wanahangaika huku na kule kutafuta msaada wa kumkaribia Mungu, lakini hawauoni,

 badala wapewe tiba ya Neno la Mungu wanapewa maji ya upako, wanafika makanisani badala wahubiriwe Yesu, wanahubiriwa bikira Mariamu na watakatifu wa kale, na sala za wafu, badala wahubiriwe neema iliyo katika Kristo Yesu, wanahubiriwa siri zilizo ndani ya wachawi.

Imefikia hatua watu wamekata tamaa kabisa, kila mmoja anaona ni heri, asiamini kanisa lolote, ajisalie tu peke yake nyumbani..kuliko kwenda na kusikiliza madanganyo. Ni ni mbaya sana..

Ndio jambo ambalo Bwana Yesu analiona sasa hivi ulimwenguni..na kulihurumia kundi lake  jinsi lilivyotawanyika…na kuonewa sana..

Ikiwa wewe ni mhubiri, halafu hutimizi wajibu wako wa kuwaongoza watu katika njia sahihi..ujue kuwa utawajibishwa siku ile mbele za Bwana.

Kama tunaigeuza  kazi ya Mungu biashara, hatujali maisha ya kiroho ya watu wa Mungu, hata wakija watakavyo kanisani tunaona ni sawa, …tufahamu kuwa tutawajibishwa na Bwana siku ile.

Yeremia 23:1-4

[1]Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! Asema BWANA.

[2]Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu, Mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema BWANA.

[3]Nami nitakusanya mabaki ya kundi langu, katika nchi zile zote nilizowafukuza, nami nitawaleta tena mazizini mwao; nao watazaa na kuongezeka.

[4]Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, asema BWANA.

Tujiulize, sisi tunaosema tumeitwa kumtumikia Bwana.. Ni utumishi gani tunaoufanya? Tunadhani watu wa Mungu watapotezwa sikuzote?

Mungu anajua kuwakusanya watu wake. Na atawanyanyulia watumishi waaminifu. Sawasawa na Neno lake. Lakini sisi wengine tutawajibishwa.

Bwana atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Gongo na Fimbo ni nini? Na vinawezaje kumfariji mtu? (Zaburi 23:4).

JE! UNAMPENDA BWANA?

USIYADHARAU MARUDIA YA BWANA.

“Nitampiga mchungaji na kondoo wa kundi watatawanyika”,Maana yake nini?

NI LIPI KATI YA MAKUNDI HAYA, WEWE UPO?

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

KANUNI RAHISI YA KUPOKEA BARAKA MARA DUFU.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, Mkuu wa mbingu na nchi libarikiwe.

Kitabu pekee chenye mwongozo kamili wa maisha ni biblia takatifu, Mtu mmoja wa Mungu aliwahi kusema “endapo nikifungiwa katika chumba chenye giza, nikapewa mshumaa na biblia, basi ninaweza kueleza yote yanayoendelea nje katika ulimwengu”.

Hakika hiyo ni kweli kabisa..kwasababu biblia ndio kitabu pekee kinachoelezea uhalisia wa nyakati na majira tunayoishi, na mambo yajayo..

Leo napenda tujifunze kanuni moja rahisi ya kupokea baraka..Wengi wetu, tunategemea maombi tu, tunakuwa tunatumia nguvu nyingi katika kuomba ili kusudui tupokee baraka katika mwili, lakini ipo kanuni moja rahisi ya kupokea baraka.. Na kanuni hiyo Bwana Yesu aliisema katika Marko 4:24..

Marko 4:24 “Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho NDICHO MTAKACHOPIMIWA, na TENA MTAZIDISHIWA”.

Hapo nataka tuyatazame hayo maneno miwili. 1)Kipimo mpimacho ndicho mtakachopimiwa. na 2) tena mtazidishiwa

Maana yake ni kwamba Kama utampimia mwingine kwa kumpa “sh.elfu moja”..basi Bwana atahakikisha anakurudishia kwa njia nyingine hiyo “elfu moja” uliyoitoa. (Huenda ikawa siku hiyo hiyo, au wakati mwingine ambao haupo mbali sana).

Lakini haiishii hapo tu kukurudishia hiyo elfu moja..bali anaendelea kwa kusema “na tena mtazidishiwa”.

Ikiwa na maana kuwa Bwana akishakurudishia kile ulichokitoa, sasa kinachofuata ni yeye kukulipa wema ulioufanya kwa “kwa kukuzidishia”.

Maana yake atakupa na kingine kingi zaidi ya hiyo elfu moja uliyoitoa,

Sasa ili tuelewe vizuri ni kiasi gani tutazidishiwa, hebu tuyatazame tena maneno ya Bwana Yesu katika Luka 6:38.

Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”.

Hapa nataka tuugawanye tena mstari huu katika sehemu mbili.

1) Wapeni watu vitu nanyi mtapewa na 2) Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa kifuani mwenu.

Maana yake tunapowapa watu, kipimo fulani labda elfu moja na sisi Bwana ataturudishia hichohicho kipimo cha sh elfu moja…lakini hataishia hapo, kwasababu akishaturudishia kipimo kile tulichokitoa, ndipo anaanza kutubariki kwa wema tulioufanya, sasa swali anatubariki vipi?..

Anatubariki kwa kutumia hao hao watu kutupa sisi vitu vifuani mwetu kwa kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika..Haleluyaa!!

Kwahiyo kama umetoa elfu moja kwa moyo mzuri na mwema Basi Bwana atakurudishia hiyo elfu moja yako, na atakuzidishia na nyingine nyingi kwa kiwango cha kujaa na hata kumwagika…(unaweza kutafakari jinsi zilizvyo nyingi fadhili zake)..huenda ikawa zaidi ya mamilioni..

Jifunze kuwa mtoaji, kama unataka kupata baraka maradufu.

Maran atha

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano.

Ni lini na wapi Ibrahimu aliioona siku ya Bwana akashangilia?.

JINSI YA KUMSIKIA MUNGU, NA KUPOKEA MAFUNUO AU JUMBE KUTOKA KWAKE.

JINSI YA KUPOKEA UPONYAJI, TUNAPOMWOMBA BWANA ATUGUSE MARA YA PILI.

Talanta ni nini katika biblia (Mathayo 25:14-30)

Rudi nyumbani

Print this post

Mretemu ni mti gani?

Swali: Ule mretemu ambao Nabii Eliya alijilaza chini yake ulikuwa ni aina gani ya mti, na je una muujiza wowote kiroho? (1Wafalme 19:4).

Jibu: Mretemu ni aina ya mti ujulikanao sasa kama “MTARAKWA”. Zipo jamii nyingi za mitarakwa kulingana na mahali na mahali. Mtarakwa unaomea katika bara la Afrika ni tofauti kimwonekano na ule unaomea katika bara la Ulaya, (kutokana na hali ya hewa). Lakini yote inamatawi yanayofanana na tabia zinazofanana, kinachoitofautisha ni unene na urefu.

Mti wa Mtarakwa (au Mretemu) ni mti unaovumilia ukame sana, na kamwe matawi yake hayapotezi rangi yake ya ukijani, hata kama yatapitia ukame mkali.

Ndio maana utaona kipindi Eliya anamkimbia Yezebeli, tayari dunia nzima ilikuwa ni jangwa kwasababu mvua haikunyesha kwa miaka mitatu na nusu, na Eliya anauona mretemu na kukaa chini ya uvuli wake, sasa kikawaida mti uliokauka na ukame hauwezi kuwa na uvuli.

1 Wafalme 19:4 “Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi CHINI YA MRETEMU. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee BWANA, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.

5 Naye akajinyosha akalala chini ya MRETEMU; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule”

Kutokana na sifa hiyo, na jinsi malaika alivyomtembelea Eliya alipokuwa chini ya huo mretemu(au mtarakwa), basi inaaminika kuwa mti huo, una miujiza fulani kiroho.

Vile vile miti hii ya Miteremu/mitarakwa inatumika katika tamaduni nyingi kama miti ya Krismas (Chrismass tree).

Asili ya mti huo kutumika kama alama ya Krismasi ni hadithi ya inayoaminika na baadhi ya watu kuwa kipindi Herode anataka kumwua mtoto Yesu, pale alipotoa amri ya kuuawa kwa watoto wote walio chini ya umri wa miaka miwili, inaaminika kuwa askari wa Herode walipomkaribia Yusufu na Mariamu ili wamwue mtoto, walikuwa karibu na huu mti wa Mteremu, na ghafla ukawafungukia matawi yake yakawaficha, askari walipokuja hawakumwona Yusufu, Mariamu pamoja na mtoto.

Hiyo ndio maana mpaka leo, watu wanautumia mti huo kama alama au nembo  ya Krismas.

Lakini swali ni je!. Ni kweli mtu huo umebeba miujiza yoyote kiroho?.

Jibu ni la!. Mti wa Mretemu/Mtarakwa hauna muujiza wowote kiroho, ni mti tu kama miti mingine, sifa yake ya kuvumilia ukame ndiyo inayowachanganya wengi, lakini kiuhalisia ni mti tu kama miti mingine.

Na zaidi sana, si kweli kwamba mti huo ulimsaidia Mariamu na Yusufu kuwalinda dhidi ya Mauaji ya Bwana Yesu.. Hizi ni hadithi za kutunga, ambazo zimetungwa kwa uerevu wa akili za watu, uliovuviwa na shetani mwenyewe.

Kwasababu Yusufu tayari alikuwa ameshaondoka Bethlehemu kabla ya Herode kuanza mauaji. Hivyo kusema kwamba mti uliwasaidia huo ni uongo wa shetani.

Na si tu mti huu ni wa kawaida, bali hata miti mingine yote haina miujiza yoyote kiroho, kitu pekee ambacho kinaweza kutuletea miujiza chanya katika maisha yetu ni KUISHI MAISHA MAKAMILIFU na kitu pekee kinachoweza kutuharibia maisha yetu ya hapa na yajayo ni MAISHA YA DHAMBI..Na si miti wala kitu kingine chochote.

Hivyo kwa hitimisho, ni kuwa Mretemu ni mti wa kawaida, na hauna muujiza wowote kiroho.

Kama hujaokoka, kumbuka hizi ni siku za mwisho, na Yesu yupo mlangoni kurudi. Mwamini leo, akuoshe dhambi zako, na kukupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Mwaloni ni nini? Na je unafunua nini rohoni?

Mti wa MLOZI alioonyeshwa nabii Yeremia 1:12 tafsiri yake ni nini?

Mti wa Mshita ni mti wa namna gani?

Uasherati wa Kiroho maana yake nini?

ALITOKA HUKO, AKAENDA MAHALI KARIBU NA JANGWA.

Rudi nyumbani

Print this post

Mtu asiye na akili ni nani kibiblia?

Kwa tafsiri za kidunia mtu asiye na akili ni mtu ambaye hawezi kufiriki, kuelewa, kuwasiliana, kupanga au kutatua matatizo. Hivyo, mwanadamu mwenye mtindio wa ubongo, anajulikana kama hana akili, mtu anayefeli darasani, anajulikana kama hana akili, mtu anayeshindwa na wenzake katika maisha anajulikana pia kama asiye na akili.

Lakini je! Biblia nayo inasemaje kuhusiana na mtu asiye na akili. Sifa zake ni zipi.

Zifuatazo ndizo sifa za mtu asiye na akili mbele za Mungu, ikiwa wewe unayo mojawapo au zote, basi fahamu huna akili, haijalishi utakuwa ni wa kwanza, kimaisha, au kielimu, au kicheo. Mungu anakuona unao mtindio wa ubongo, hujakamilika. Na matokeo yake utashindwa kutumia akili zako zote kumpenda yeye kama alivyotupa maagizo katika ‘Mathayo 22:37’

1) Kutomtafuta Mungu:

Zaburi 14:2 “Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu. 3 Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja”.

Ukishaona Mungu hana umuhimu kwako, ni uthibitisho tosha,akili zako zimepunguka kwa kiasi kikubwa mno. Ni sawa, na mbwa asiyemjua bwana wake anayemfuga siku zote. Au mtoto asiyemtambua mama yake amnyonyeshaye kila siku. Fanya bidii kumtafuta Muumba wako, kwasababu hilo ndio jaribio la kwanza alilotuumbia Mungu, ili kuthibitisha kwamba kweli sisi ni wanadamu tuliokamilika, tunaweza kumtafuta aliyetubuni.?

2) Kuwadharau wengine:

Mithali 11:12 “Asiye na akili humdharau mwenziwe; Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza”.

Ukishajiona wewe ni bora kuliko mtu mwingine, au unamwona mwenzako hana lolote jipya la kukufaa wewe, tambua kuwa tayari akili yako imeathirika, fanya haraka sana, kujirekebisha katika eneo hilo, ili usipoteze upeo wako wa kufikiri vema, na wa kupambanua mambo. Kamwe usimdharau mtu yeyote duniani. Hata kama ni mpumbavu wa mwisho.. Kwasababu Mungu naye hamdharau mtu aliyemuumba  japokuwa ni mnyonge (Ayubu 36:5)

3) Kuwaonea watu:

Mithali 28:16 “Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana; Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake”.

Kumuonea mtu kwasababu ya unyonge wake, au udhaifu wake, ni jambo la hatari sana. Ukimdhulumu mwenzako, au kumnyima haki yake, au kutumia hila kumwibia kisa tu hana maarifa ya jambo hilo, kumpiga mkeo, au watoto bila sababu, basi fahamu kuwa wewe ni sawa ni mjinga mbele za Mungu.. Tukae mbali na uonevu wa aina yoyote.

4) Kufanya uasherati:

Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake”.

Uzinzi, ni kipingamizi sio tu cha kiroho, bali pia cha kiakili. Watu wazinzi, wanajiharibia sana uwezo wao wa kupambanua mambo ya kiroho kwa sehemu kubwa sana. Kwasababu Roho Mtakatifu huwa anategemea miili yetu kutenda kazi, hivyo mwili wako unapochafuliwa, hawezi kupata nafasi ya kuwa mwalimu wako. Ndio hapo Unabaki tu kuwa wewe kama wewe, kama mnyama tu. Epuka uzinzi kwa gharama zote, ni hatari..

5) Kutokuwaza  juu ya hukumu:

Mithali 15:24 “Kwa mtu mwenye akili njia ya uhai huenda juu; Ili atoke katika kuzimu chini”.

Hapo biblia inatueleza wazi, mtu mwenye akili, huwaza ni jinsi gani atakavyoepukana na kuzimu iliyo chini, huwaza kwenda mbinguni, huwaza kuepukana na ziwa la moto. Lakini kinyume chake ni kweli, mtu asiyewaza hatma ya maisha yake baada ya kufa itakuwaje, badala yake yupo tu, anachowaza ni ajengeje magorofa hapa duniani, ukimweleza habari za kuzimu hata hashtuki, huyo kwa Bwana hana akili.

6) Kutopenda maagizo:

Mithali 10:8 “Aliye na akili moyoni mwake atapokea agizo; Bali mpumbavu mwenye maneno mengi ataanguka”

Ukiwa ni mtu wa kupinga maagizo mema, unayopewa, bali unajiona upo sawa machoni pako mwenyewe, ukielezwa, uvaaji vimini ni dhambi, unasema hatupo agano la kale, unapoelezwa ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo ni lazima, unasema sisi hatuamini hilo. Ujue kuwa unajiangamiza mwenyewe. Kila agizo lililo kwenye Neno la Mungu linapaswa lipokelewe na kukubaliwa kama lilivyo pasipo kuuliza uliza.

7) Kusahau sahau, sheria za Mungu:

Mithali 10:14 “Watu wenye akili huweka akiba ya maarifa; Bali kinywa cha mpumbavu ni uangamivu ulio karibu”.

Ukiwa mtu wa kutozingatia, au kutotendea kazi kile unachoambiwa au kukisikia, kuhusiana na mafundisho ya adili, yaani unasahau sahau, amri au fadhili za Mungu, unakuwa mwepesi kuanguka ovyo katika dhambi, ni uthibitisho kuwa huna akili kwa mujibu wa kibiblia. Tunapaswa tuwe watu wa kuzitafakari sheria za Mungu wakati wote, kama vile mwanafunzi akaririvyo kila siku masomo yake, ili yamsaidie kufaulu mitihani yake ya mwisho.

Mithali 3:3 “Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.

4 Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu”.

8) Uvivu:

Mithali 24:30 “Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.

31 Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake”.

Ukiwa mvivu, wa kufanya kazi ya Mungu.  Bwana anasema huna akili, yaani Ikiwa hujishughulishi na chochote, unajitafutia matitizo yako mwenyewe. Tumeumbwa, tujishughulishe, kama Mungu alivyojishughulisha..Kama huwezi mtumikia Bwana kwa kujitoa kwa asilimia zote kwenye kazi yake, ni lazima ufanye kazi ya mikono, ili ufanikiwe. Lakini tukishindwa kujishughulisha, ni kwa hasara yetu wenyewe.

Hivyo tukiwa tuna mojawapo ya tabia hizo ni busara tukazidhibiti ndani yetu. Ili tuweze kuishi kwa akili Bwana anazotaka tuwe nazo.  

Zingatia: Mungu anazungumza na mtu mwenye akili timamu, rohoni. Ni lazima tufikie hapo ili Bwana aseme na sisi.

Bwana atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Mpumbavu ni nani katika biblia? (Zaburi 14:1, Mithali 10:14)

Kutia mkono chini ya paja kama ishara ya kiapo, kulimaanisha nini?

Watu wenye ulemavu wa akili, wataenda mbinguni?

Nini maana ya ‘Hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma’?

HAKUVAA NGUO SIKU NYINGI.

NI NINI BWANA ANATAZAMIA KILA TUNAPOSHIRIKI MEZA YAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

FANYIA KAZI KILE UNACHOKISIKIA.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu YESU Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia (Neno la Mungu wetu) lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Zaburi 119:105).

Biblia inasema katika kitabu cha Yakobo…

Yakobo 4:17  “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi

Kumbe haihitaji kwenda kuua, au kuiba, au kuzini ndipo ihesabike kuwa ni dhambi, bali hata “kujua tu kitu kilicho sahihi na kutokukifanya hicho” tayari ni dhambi mbele za Mungu!!!. Hii inaogopesha sana!!.

Ukijua kuwa unapaswa umtumikie Mungu, halafu humtumikii hiyo tayari inahesabika kuwa ni dhambi.

Ukijua kuwa unapaswa Uwe mwombaji, halafu hauombi hiyo tayari kwako ni dhambi.. Na watenda dhambi wote hawataurithi uzima wa milele, kulingana na maandiko.

Ukijua kwamba unapaswa uwe unawaombea wengine, halafu hufanyi hivyo, aidha kwasababu ya chuki au vinyongo au hasira, fahamu kuwa unatenda dhambi..

1Samweli 12:23 “Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi..”

Ukijua kuwa unapaswa uhubirie wengine habari njema za wokovu, wawe kama wewe, na hufanyi hivyo, basi fahamu kuwa unafanya dhambi!. Na watenda dhambi wote ni wana wa ibilisi na hawataurithi uzima wa milele.

1Yohana 3: 8  “Atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi”.

Ukijua kuwa unapaswa ukabatizwe na hautaki kubatizwa au unapuuzia ubatizo, basi fahamu kuwa unafanya dhambi kulingana na andiko hilo “yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi”.

Ukijua kabisa kwamba unapaswa “ulisome Neno (yaani biblia)”, lakini hufanyi hivyo, kwa visingizio Fulani fulani.. Fahamu kuwa unatenda dhambi, na wewe ni muasi kulingana na biblia.

1Yohana 3:4  “Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi”.

Ukijua kuwa  unapaswa ufanye ibada na kukusanyika na wengine kanisani, kumfanyia Mungu ibada kulingana Waebrania 10:25, lakini wewe hufanyi hivyo, badala yake unabaki  nyumbani umelala, au unaenda kufanya shughuli zako nyingine, basi fahamu kuwa unafanya dhambi..

Waebrania 10:25  “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”

Kaka/Dada usilipuuzie kamwe Neno la Mungu,..Unaposikia maonyo ya Neno la Mungu, usiyasikilize tu kama taarifa ya habari, na kuyaacha yapite, au kuyaweza akiba moyoni, bali yafanyie kazi kuanzia wakati ule ule unapoyasikia.. Kwasababu usipoyafanyia kazi baada ya kuyasikiliza basi kwako inahesabika kuwa dhambi, na hivyo utahukumiwa sana siku ile, Bwana Yesu alisema maneno yafuatayo..

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana”

Jiepushe na hukumu ya Mungu!!, Litendee kazi Neno baada ya kulisikia.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

JE UNA MATUMAINI YA KUPATA TENA KILE ULICHOPOTEZA?

Liwali ni nani?

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?

Rudi nyumbani

Print this post