Wokovu na furaha ya wokovu ni vitu vinavyokwenda sambamba, palipo na wokovu ni lazima na furaha ya wokovu pia iwepo, vikipishana kidogo, basi ni tatizo kubwa sana ni sawa na chakula kilichokosa chumvi, utakula tu, ili kujaza tumbo lakini hutakifurahia hata kidogo,
Wakristo wengi sasa wameupokea wokovu, lakini , si wote wanayo furaha ya wokovu. Kuwepo katika wokovu ni suala ambalo unapaswa ufurahie, (U-enjoy), kama vile ufurahiavyo maisha ya utajiri. Lakini kama hilo jambo halipo ndani yako sasa, basi kuna tatizo kubwa.
Kuna kipindi ulikuwa unajihisi furaha, na amani na wepesi ndani ya wokovu, haukujali ni magumu kiasi gani unapitia, lakini sasa unajiona kama hiyo raha haipo tena, wokovu unakuwa kama vile wa kujilazimisha, upo tu, unasogeza siku ilimradi, kesho ije.Leo tutatazama, ni vitu gani vya kuzingatia kama mkristo, ili uweze kuirejesha ile furaha ya wokovu uliyoipoteza. Na kama hujawahi pia kuwa nayo basi zingatia kanuni hizi muhimu.
Daudi hakuwahi kupoteza furaha ya wokovu maisha yake yote, isipokuwa siku alipofanya dhambi ya makusudi, ya kuzini na mke wa askari wake(Huria), mwanzoni alidhani ni jambo jepesi tu, lakini aliponaswa katika huo mtego, alikaa muda mrefu sana, bila furaha ya wokovu, japokuwa alishasamehewa hiyo dhambi na Mungu..
Yeye ndio aliyeandika Zaburi ya 51, na katika dua zake alimwomba Mungu amrejezee furaha ya wokovu aliyoipoteza zamani.
Zaburi 51:12 “Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi”.
Nawe pia ikiwa umeokoka, halafu unaendelea kutenda dhambi, furaha hii itaondoka ndani yako, na ukristo wako utakuwa ni mzito na mgumu sana, pengine hata baada ya kutubu. Hivyo kaa mbali na dhambi.
Mahali pekee ambapo pana matumaini, faraja, nguvu ya kuendelea mbele, basi ni katika Neno la Mungu. Kama mkristo ukiwa mvivu wa kuchukua biblia yako na kusoma kila siku, huwezi kusonga mbele katika hii safari ya imani.
Kwamfano katika biblia utamsoma Ayubu, katika majaribu yake, utamsoma Ibrahimu na Sara katika kusubiri kwao, utamsoma Henoko na Eliya katika ukamilifu wao, utajifunza uvumilivu, saburi, upendo, amani, utasoma shuhuda mbalimbali za waliotendewa maajabu na Yesu n.k. Hivyo kwa maarifa hayo, ni ulinzi tosha kwako, wa kuufurahia wokovu wako.
Lakini ukiwa ni mkavu ndani, hapo ndipo ibilisi atakujaza biblia yake, ya hofu ya maisha, mashaka, wasiwasi, huzuni, wivu, chuki n.k.Penda Neno la Mungu kama upendavyo chakula.
Mithali 3:1 “Mwanangu, usiisahau sheria yangu, Bali moyo wako uzishike amri zangu.2 Maana zitakuongezea wingi wa siku. Na miaka ya uzima, na amani.3 Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako.4 Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu”.
Katika eneo ambalo hupaswi kuwa mvivu nalo basi ni hili, hapa shindana na mwili, ukikosa kuwa mwombaji, Kama Yesu alivyosema, Kesheni mwombe msije mkaingia majaribuni (Mathayo 26:41).. Ni kweli kabisa majaribu yasiyokuwa na msingi yatakukuta, na hivyo utakuwa unaishi kila siku maisha ya kujikwaa kwaa..
Ibada ni muhimu sana kwa mkristo, ikiwa umeokoka halafu huna desturi ya kuhudhuria ibadani, kujumuika na watakatifu wengine, utaikosa furaha ya wokovu wako..Bwana alisema..
Waebrania 10:25 “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”.
Pia maandiko yanasema..
Mithali 27:17 “Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake”.
Vipo vitu ambavyo utavipata kwa juhudi zako mwenyewe, lakini vipo ambavyo utaongezewa na wengine, kuna mahali utaishiwa nguvu, mwingine atakushika mkono hata tu kwa karama yake. Binafsi nimeona nikitengenezwa ukristo wangu kwa sehemu kubwa sana nilipokuwa na wengine, zaidi ya nilivyokuwa mwenyewe.
Ibadani pia ni mahali ambapo, utapata fursa ya kumwimbia na kumwabudu Mungu, kwa nafasi na uhuru zaidi kuliko mahali ulipo mwenyewe. Na ukikosa ibada ya Sifa, pia furaha ya wokovu haiwezi kumiiminika ndani yako.Sifa huponya mioyo yetu. Huondoa uchungu na mizigo yetu,.Jaribu kudumu muda mrefu katika sifa, utaona badiliko kubwa sana moyoni mwako.
Ukiridhika na hiyo hiyo hali ya kiroho muda mrefu, tatizo hili ni lazima likukute.. lilishawahi nikuta mimi, na likanisumbua sana.. Embu tengeneza picha mtoto ameshafikisha miaka 5, bado anategemea tu, maziwa ndio yawe chakula chake, Je! atafurahia chakula hicho kama alivyokuwa na miezi 5?, jibu ni la, kinyume chake ndio atadhoofika.
VIvyo hivyo na wewe ikiwa umeokoka, na kitambo sasa kimepita, hakikisha kila siku unapiga hatua mpya, katika kujifunza, kuacha dhambi, na zaidi sana, kushuhudia habari njema kwa walio nje.Moja ya mambo ambayo yananipa furaha moyoni ya wokovu, ni pale napoona siku yangu haijapita bure bure bila kufanya kitu fulani kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Lakini nikipitisha muda fulani mrefu, nipo nahangaika hangaika tu na mambo ya kiulimwengu, huwa furaha hiyo inapotea kabisa, najiona kama Roho Mtakatifu ameniondoka.
Hivyo wewe kama mkristo hakikisha, kila siku unapiga hatua, anza kuwahubiria na wengine na bila shaka utaufurahia mwenyewe wokovu wako.
Hivyo katika mambo hayo matano (5), angalia ni wapi umezembea, kisha uchukue hatua nyingine ili usife kiroho, kwasababu ukiendelea nayo hiyo hali muda mrefu hatma yake itakuwa ni kurudi nyuma au kufa kiroho kabisa. Kubali kuanza upya na Bwana.Kumbuka tatizo sio wokovu wetu, tatizo lipo katika mienendo yetu.Bwana atusaidie.
Shalom
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Furaha ni nini?
IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.
YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.
KIFO CHA MTAKATIFU POLIKAPI (Policarp).
Nini maana ya wokovu watoka kwa Wayahudi? (Yohana 4:22)
Nini maana ya ombeni kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi wala siku ya sabato?.
VIPINDI VINNE VYA MAISHA VILIVYO VIGUMU MTU KUMKUMBUKA MUUMBA WAKE.
Rudi nyumbani
Print this post