Nini maana ya ombeni kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi wala siku ya sabato?.

Nini maana ya ombeni kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi wala siku ya sabato?.

Jibu: Ili tupate kuelewa vizuri, tutaisoma habari hii hii katika vitabu vitatu tofauti vya Injili. Tukianza na kitabu cha Mathayo, biblia inasema…

Mathayo 24:15  “Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),

16  ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;

17  naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake;

18  wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake.

19  Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!

20  OMBENI, ILI KUKIMBIA KWENU KUSIWE WAKATI WA BARIDI, WALA SIKU YA SABATO.

21  KWA KUWA WAKATI HUO KUTAKUWAPO DHIKI KUBWA, AMBAYO HAIJATOKEA NAMNA YAKE TANGU MWANZO WA ULIMWENGU HATA SASA, WALA HAITAKUWAPO KAMWE.

22  Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo”.

Habari hii inazungumzia unabii wa Kuanguka kwa mji wa Yerusalemu, Baada ya wayahudi kumkataa Bwana Yesu. Yesu mwenyewe aliwaambia, kuwa utafika wakati, ambao Mungu atawaadhibu kwa kuikataa hiyo neema, tena akawaambia siku hizo zipo karibu kutokea ambapo, maadui zao (Yaani Warumi ambao wanawatawala sasa), watakapowazunguka pande zote na kuubomoa mji wao pamoja na hekalu, na kuwatawanya baadhi yao huko na huko, kama wakati wa uhamisho wa Babeli, na hayo yote ni kutokana na wao kumkataa Masihi, hivyo ile neema ya ulinzi kutoka kwa Mungu itaondoka juu yao, na adui atawavamia na kuwaharibu…

Habari hiyo tunaisoma katika kitabu cha Luka..

Luka 19:41  “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,

42  akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.

43  Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;

44  watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako”.

Sasa Bwana alipoutoa huo unabii, watu waliokuwa wanamdharau na kumkataa hususani viongozi wa dini, Mafarisayo na Masadukayo, waliyapuuzia maneno hayo, na kumwona kama amerukwa na akili. Lakini wanafunzi wa Yesu walijua kabisa kuwa maneno ya Yesu hayatapita, jambo hilo lazima litimie, ndipo wakamfuata wakamwuliza ni lini hayo mambo yatatokea?. Ndipo Bwana akawaambia…

Luka 21:20 “… hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia.

21  Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.

22  Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.

23  Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.

24  Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia”.

Hapo sasa Bwana Yesu anazungumza na wanafunzi wake  tu, na si watu wote..hapana! bali wanafunzi wake tu, anawaambia jinsi mambo yatakavyokuwa na anawaambia jinsi ya kuepukana na hiyo siku ya mapatilizo.. Anawaambia watakapoona tu mji wa Yerusalemu umezungukwa na Majeshi..basi watambue kwamba ile ule unabii aliowaambia ya kwamba Yerusalemu itateketezwa umekaribi kutimia…

Sasa anaendelea kuwaambia wanafunzi kwamba watakapoona hayo majeshi, wasingoje chochote, waondoke mji wa Yerusalemu wasije na wao wakaangamia huko kwasababu ni siku ya kisasi cha Mungu. Hivyo waondoke wasafiri waende mji mwingine..wakakae huko..

Na pia waombe kuwa siku hizo za kuondoka zisitokee msimu wa Baridi wala siku ya Sabato..

Sasa kwanini siku ya Baridi na sabato?

Maeneo ya Yerusalemu miezi ya Machi na Aprili, kunakuwa na baridi sana, wakati mwingine mpaka kutengeneza barafu, sasa kwa ufahamu wa kawaida tu, kusafiri na punda kwenye barafu au wakati wa joto ipi bora?..bila shaka ni heri kusafiri kipindi cha joto kuliko cha barafu.. Hiyo ndio maana Bwana Yesu akasema waombe hayo yasitokee msimu wa baridi.

Lakini sio hilo tu! Akawaambia pia waombe yasitokee siku ya Sabato?

Sasa kwanini siku ya sabato?…Je Bwana Yesu alikuwa anamaanisha watu waishike sabato?. Jibu ni la.. Kumbuka wayahudi walikuwa wanashika sheria ya Musa, na pia siku ya sabato watu walikuwa hawaruhusiwi kufanya kazi, wala kutembea umbali mrefu…kulikuwa ni kipimo kidogo tu cha mwendo kwa siku, ambacho mtu hapaswi kukizidisha hicho katika siku ya sabato. Kipimo hicho kilikuwa kinaitwa “MWENDO WA SABATO”.

Matendo 1:12 “Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato”.

Ulikuwa ni mita kadhaa tu, Hivyo haikuruhusiwa mtu yeyote kutoka kusafiri, au kwenda kuzurula zurura. Na ilikuwa ni sheria mtu yeyote akionekana anafanya kazi siku hiyo au anatembea tembea hovyo ilikuwa ni kifo. (Unaweza kusoma sheria hiyo ya kutembe vizuri katika kile kitabu cha Kutoka 16:25-30) /www wingulamashahidi org/

Sasa hebu jiulize katika mazingira kama hayo, (yaani siku ya sabato), ndio majeshi yamezunguka Yerusalemu, ambapo ndio wakati wa kuondoka…utawezaje kuondoka?? Maana nchi hairuhusu mtu kusafiri, maana yake utajikuta unakaa huko huko mjini mpaka maangamizi yanakukuta. Ndio maana Bwana akawaambia “waombe kwamba siku hizo za kukimbia zisitokee msimu wa baridi, wala siku ya sabato”. Kwasababu kama zikitokea katika mojawapo ya mazingira hayo, basi dhiki yake itakuwa ni kubwa sana, ambayo haina mfano wake. Na watakaoathirika wa kwanza ni wanawake, tena hususani wale wenye mimba, au wanaonyonyesha…Hebu jiulize tena, mwanamke mjamzito au mwenye kichanga mkononi, ambacho muda wote kinahitaji malezi na joto la mama,  atakimbiaje kwenye baridi na katika mazingira ya mji kuzuiliwa watu kusafiri??..umeona jinsi ilivyo ngumu, ndio maana Bwana akawaambia ole wao wenye mimba, na wanyonyeshao.

Sasa baada ya Bwana Yesu kuwaambia maneno hayo ya unabii, pamoja na maneno mengine mengi…Bwana Yesu siku za kupaa kwake zilifika na aliondoka, lakini wanafunzi wakabaki na ufahamu vichwani mwao, kwamba siku si nyingi Yerusalemu itakuja kuzungukwa na majeshi, na huo ndio wakati wa sisi kuondoka..tusingoje..

Miaka 37 baada ya Bwana Yesu kuondoka, Unabii huo ulitimia.. yaani mwaka AD 70, Wakati ambapo Yerusalemu kunaonekana kuna amani, majeshi ya Warumi yalianza kuizunguka Yerusalemu wakiwa na silaha, watu wakajua ni jambo la kawaida tu, suluhisho la amani kwa mazungumzo litapatikana, pengine wakatokea watu wa kutabiri kutakuwa na amani, hakuna shida, hakuna haja ya hofu, kwasababu wakati huo Rumi ndio uliyokuwa inatawala dunia.

Lakini Mitume wa Yesu baadhi ambao bado walikuwa wanaishi, waliowaonya wakristo juu ya unabii huo wa Bwana, hivyo miongoni mwa wakristo, tukio hilo lilipotokea hawakusubiri wala kupoteza muda.. Wengi wao waliondoka Yerusalemu.. Na kukimbilia nchi za kando kando…waliyakumbuka yale maneno ya Bwana aliyosema.. “hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia  Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie”. Hivyo wakristo waliokuwa na shughuli zao, huko waliziacha na kuondoka Yerusalemu kipindi hicho hicho, ingawa walionekana wendawazimu.

Lakini hao wengine wasioujua unabii  waliendelea kubaki wakijua hayo majeshi yataondoka tu…wengine wakawa wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi, huku mazungumzo ya amani yanaendelea…siku chache mbele, mambo yakabadilika, yale majeshi yaliyokuwa yametulia tu mipakani, yakaingia Yerusalemu kama maji, yakaua watu wengi, na yakaangusha majengo yote ikiwemo hekalu, wala halikubakia jiwe juu ya jiwe, kama Bwana Yesu alivyotabiri, waliosalimika ni wale walioondoka tu. Na hayo yote biblia inasema yaliwapata kwasababu hawakutambua majira ya kujiliwa kwao.

Ndugu huo ni mfano wa dhiki kuu halisi ambayo inakuja huko mbeleni, Dhiki kuu yenyewe ipo karibu kutokea, itaanza ghafla tu, wakati kama huu ambao watu wanasema kuna amani na utulivu…ambapo baada ya unyakuo kupita watakatifu watakapoondolewa duniani, wale waliobaki, ambao wataikataa ile chapa, watateswa kwa mateso yasiyo ya kawaida, na baada ya kuteswa kwa miaka kadhaa bila kuruhusiwa kufa ndipo watakufa..

Hivyo unyakuo sio wa kukosa kabisa… na maneno ya Bwana Yesu kamwe hayapiti. Alisema Yerusalemu itazungukwa na maadui na hakuna jiwe litasalia juu ya jiwe..jambo hilo limetimia… Na maneno mengine yote aliyoyasema ni lazima yatatimia, hakuna ambalo halitatimia.

Marko 13:31 “Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe”

Je umempokea Kristo?..Je una uhakika hata parapanda ikilia leo utanyakuliwa?..Kama huna uhakika basi huo tayari ni uthibitisho kwamba hutaenda, kwahiyo ni vyema ukatafuta uhakika kuanzia leo kwa kuyatengeneza maisha yako katika Yesu.

Bwana akubariki

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

IMESALIA RAHA YA SABATO KWA WATU WA MUNGU.

NYAYO TUNAZOPASWA KUZIFUATA.

NITAFANYA YERUSALEMU KUWA JIWE LA KUWALEMEA .

CHUKIZO LA UHARIBIFU

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments