CHUKIZO LA UHARIBIFU

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Jina la Bwana wetu YESU KRISTO libarikiwe sana. Karibu tuongeze maarifa katika kulichambua Neno la Mungu leo tutajifunza juu ya chukizo la uharibifu, natumai ujumbe huu utakutoa sehemu moja ya kiroho hadi nyingine, sasa ili tuweze kwenda kwa uzuri ni vema uwe na biblia pembeni ili kukusaidia kufuatilia baadhi ya mistari tutakayokuwa tunaipitia katika somo hili.

Kwa kuanza ni vizuri tukifahamu nini maana ya “chukizo la uharibifu”: Kwa lugha nyepesi tunaposema chukizo la uharibifu ni sawasawa na kusema “chukizo linaloleta uharibifu” au “Chukizo linalopelekea uharibifu”..Kwahiyo hapo kuna mambo mawili, la kwanza ni CHUKIZO, na la pili ni UHARIBIFU. Sasa chukizo ni nini? Na uharibifu ni nini?.

CHUKIZO: Kwa tafsiri ya kibiblia hilo neno chukizo maana yake ni kuudhi/kuleta hasira, hususani pale panapohusishwa na uzinzi, Hivyo mambo yote yaliyokuwa yanafanywa na watu wa Mungu ambayo yalikuwa kinyume na sheria zake mfano kuabudu miungu mingine, kujichongea sanamu, kufanya uchawi, n.k. hayo yote mbele za Mungu yalijulikana kama MACHUKIZO (mambo ya kuudhi au kukasirisha).

Kwa mfano tunaweza kuona Bwana aliwaambia wana wa Israeli katika Kumbukumbu 18: 9-13 akisema:

“9 Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa MACHUKIZO ya mataifa yale.

10 Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,

11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.

12 KWA MAANA MTU ATENDAYE HAYO NI CHUKIZO KWA BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.

13 Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako”.

Unaona hapo mambo waliowafanya wafukuzwe (“mataifa yaliyokuwa Kaanani”) na kuondoshwa kabisa ni MACHUKIZO yao mbele za Mungu, hivyo Mungu akatangulia kuwaonya mapema watu wake kwamba watakapofika katika hiyo nchi ya Ahadi wasijaribu kutenda mfano wa mambo hayo. Kwani Watu wa mataifa walikuwa wana loga, wanaabudu miungu mingi, wanaabudu masanamu, wanapitisha watoto wao kwenye moto, wauaji, n.k. Kwasababu hiyo basi wana wa Israeli walionywa sana wakae mbali na hivyo vitu, kwani vitawasababisha wao nao yawapate yale yale yaliyowapata mataifa mengine.

UHARIBIFU: Kama tulivyoona hapo juu, sababu kubwa iliyowapelekea mataifa yale makubwa yafukuzwe na KUHARIBIWA kabisa haikuwa kwasababu ya kwamba Mungu anawachukia tu!au anawapenda Israeli kuliko wao hapana bali ni kwasababu ya machukizo yao na ndiyo ikawapelekea kuharibiwa na kutolewa katika ile nchi ya Kaanani na kupewa wana wa Israeli. Na kama tunavyojua siku zote kitu kikiwa kinachukiza mara kwa mara kinachofuata ni kuangamizwa au KUHARIBIWA kabisa.

Bwana aliwaaonya tena wana wa Israeli na kusema:

Mambo ya walawi 18: 24 “Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote;

25 na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa.

26 Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye MACHUKIZO hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu;

27 (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya MACHUKIZO HAYA YOTE, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;)

28 ili kwamba hiyo nchi isiwatapike na ninyi pia, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu.

29 KWANI MTU AWAYE YOTE ATAKAYEFANYA MACHUKIZO HAYO MOJAWAPO, NAFSI HIZO ZITAKAZOFANYA ZITAKATILIWA MBALI NA WATU WAO.

30 Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi ZICHUKIZAZO mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.”

Unaona hapo, machukizo yote yaliyokuwa yanazungumiziwa mwisho wake yote yalipelekea UHARIBIFU kwa namna moja au nyingine kwa hilo taifa au mtu mmoja mmoja aliyeyafanya.. Sasa kumbuka vitu hivi kama uchawi, ulawiti, uuaji, uongo n.k. haya yote yalikuwa ni machukizo yanayoleta uharibifu lakini LIPO CHUKIZO MOJA, lililozungumziwa na BWANA YESU, na katika kitabu cha DANIELI, ambalo litakuja kusimama sehemu patakatifu na kuleta uharibifu mkubwa kwa watu wengi wa Mungu litakalosababisha kuwepo na dhiki kubwa ambayo haijawaki kutokea tangu ulimwengu kuwako, na ndilo litakalopelekea hata uharibifu wa dunia.

Kumbuka wakati wana wa Israeli walipokuwa wanaingia katika nchi ya Kaanani, Mungu hakuteua mahali popote katikati ya miji yao pa kuliweka jina lake, na kuwa sehemu takatifu, hivyo wakati huo wote waisraeli walipokuwa wanafanya machukizo Bwana aliwaharibu mara nyingine kwa kuwatia katika mikono ya maadui zao kama wafilisti na walipotubu Bwana aliwanyanyulia waamuzi ambao waliwaokoa na mikono ya maadui zao lakini hawakuwa wanaondolewa taifa lao. Lakini ulipofika wakati Bwana alipojiteulia mahali PATAKATIFU pake pa kuwekea Jina lake yaani YERUSALEMU, zamani za mfalme Daudi, mambo yalianza kubadilika, siku ile HEKALU LA MUNGU lilipokamilika kujengwa kwa mikono ya Sulemani mwana wa Daudi, Baraka na bila kusahau LAANA pia ziliongezwa makali, Na ndio maana Bwana alimwambia Sulemani baada ya kuijenga ile nyumba maneno haya..

1Wafalme 9: 6 “Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, TENA MKIENDA NA KUITUMIKA MIUNGU MINGINE NA KUIABUDU,

BASI NITAWAKATILIA ISRAELI MBALI NA NCHI HII NILIYOWAPA na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa MITHALI NA NENO LA TUSI KATIKA MATAIFA YOTE.

8 Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atasituka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini Bwana ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya?

9 Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha Bwana, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu Bwana ameleta mabaya haya yote juu yao”.

Unaona hapo?. Baada ya Mungu kuichagua YERUSALEMU, kama mahali pake patakatifu na HEKALU kama mahali atakapoweka Jina lake alitarajia muda wote Israeli wakae katika hali ya usafi wa hali ya juu kuliko hapo kwanza, kwamba wakifanya machukizo mbele za Patakatifu pa Mungu, wakatakatiliwa mbali, na kutawanywa katika mataifa yote, na watakuwa mithali kwa kila wawatazamao.

Lakini tukirudi katika kitabu cha Wafalme tunaona hawakuisikia hiyo sauti ya Mungu, badala ya kudumu katika usafi kwa Mungu wakaanza kidogo kidogo kuingiza ibada nyingine katika Israeli na katika nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu, licha ya kwamba Mungu aliwatumia manabii wengi kuwaonya lakini hawakutaka kubadilika (Kuyaacha machukizo yao mbele za Mungu) ikapelekea Mungu kutamka UHARIBIFU WAO. Kama alivyoahidi katika NENO lake, pale Nebukadneza Mfalme wa Babeli Bwana alipomruhusu kwenda kuuteketeza mji wa Yerusalemu, na kuliharibu kabisa lile hekalu la Sulemani, wakauawa majemedari wengi wa Israeli kwa upanga, wengine njaa, na wengine magonjwa, Dhiki ilikuwa kubwa sana, wakachukuliwa utumwani na Israeli ikabaki kama ukiwa, Kutokana na MACHUKIZO waliyoyasimamisha wao wenyewe hivyo yakawapelekea UHARIBIFU MKUBWA namna hiyo.. Naamini kidogo kidogo utakua umeanza kuelewa nini maana ya chukizo la uharibifu.

2Mambo ya nyakati 36:14 “Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na MACHUKIZO YOTE YA MATAIFA; WAKAINAJISI NYUMBA YA BWANA ALIYOITAKASA KATIKA YERUSALEMU.

15 Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;

16 lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, HATA ILIPOZIDI GHADHABU YA BWANA JUU YA WATU WAKE, HATA KUSIWE NA KUPONYA.

17 Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo{Wa-babeli}, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake.

18 Na vyombo vyote vya nyumba ya Mungu, vikubwa kwa vidogo, na hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za mfalme, na za wakuu wake; vyote pia akavileta Babeli.

19 WAKAITEKETEZA NYUMBA YA MUNGU, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, WAKAVIHARIBU vyombo vyake vyote vya thamani.

20 Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babeli; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi;

Tukio hili lililiathiri Taifa la Israeli kwa vizazi vingi, Kama ukifuatilia historia utaona kuwa Israeli halikuwahi kuwa tena taifa huru kwa muda wa miaka 2500, tangu ule wakati walipopelekwa Babeli mpaka juzi juzi tu mwaka 1948, ndio wamekuwa taifa huru tena, siku zote hizo walikuwa wanaishi kama wageni mahali popote walipopelekwa au kukaa. Na hata walipotoka Babeli walikuwa chini ya mataifa yaliyokuwa yanamiliki dunia kwa wakati huo. Unaweza ukaona ni MACHUKIZO MAKUBWA kiasi gani yaliyowasababishia kupitia uharibifu na adhabu kali kaisi hicho… Mungu ni Mungu mwenye WIVU hapendi mahali pake patakatifu panajisiwe kwa namna yoyote ile..

Na tunaona baada ya kutoka Babeli, Bwana aliwarehemu akawajalia kujenga tena hekalu la pili baada ya lile la kwanza lililotengenezwa na Sulemani kubomolewa na mfalme Nebukadneza wa Babeli. Kadhalika Mungu aliwaonya pia yale masalia ya wayahudi waliorudi wasifanye machukizo kama waliyoyafanya mababa zao. Mwanzo walitii lakini kilipopita kipindi Fulani walikengeuka, wakaanza kufanya mfano wa machukizo ya mataifa. (Kumbuka wakati huu Israeli ilikuwa haijiongozi yenyewe kama hapo kwanza) ilikuwa chini ya utawala wa wafalme wengine. Hivyo njia pekee shetani aliyoitumia kusimamisha machukizo katika nyumba ya Mungu kiurahisi sio kuwatumia wayahudi peke yake, bali alianza kuwatumia pia wafalme wa mataifa kwasababu wao ndio waliokuwa na nguvu juu ya taifa la Israeli,

Tukisoma katika kitabu cha Danieli tunaona Danieli akionyeshwa katika maono juu ya mfalme atakayenyanyuka katika utawala wa Umedi & Uajemi ambao ndio kwa wakati huo ulikuwa unatawala dunia, alionyeshwa kiongozi mkatili akilisimamisha chukizo la uharibifu tena katikati ya wayahudi na patakatifu na huyu hakuwa mwingine zaidi ya ANTIOKIA IV EPIFANE (Kumbuka mpaka Antiokia kuja kulitia unajisi hekalu ilikuwa ni matokeo ya kukengeuka kwa wana wa Israeli,mfano wasingeasi Bwana angewaepusha na hayo mambo) Tukisoma

Danieli 11: 31 Na wenye silaha watasimama upande wake, nao watapatia unajisi mahali patakatifu, ndiyo ngome, nao wataondoa sadaka ya kuteketezwa ya kila siku, NAO WATALISIMAMISHA CHUKIZO LA UHARIBIFU..

Kulingana na historia inavyoeleza, kiongozi huyu alinyanyuka na kuingia katika hekalu la Mungu na kufanya maasi yote ambayo hayapaswi kuwepo katika nyumba ya Mungu, aliweza kusitisha sadaka zote za kuteketezwa ambazo zilikuwa zinafanywa na makuhani katika nyumba ya Mungu, na kuiweka sanamu ya ZEU mungu ambayo ilikuwa inamwakilisha yeye, kadhalika akawa anatoa dhabihu ya viumbe najisi kwa wayahudi kama nguruwe katika madhabahu iliyokuwa ndani ya Hekalu la Mungu na kuwalazimisha wanywe damu zao hivyo viumbe, mambo ambayo yalikatazwa katika Torati ya Musa, hakuishia hapo tu, aliwaua wayahudi wengi sana na kuwakosesha kuabudu katika dini yao, hivyo ikawa ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu…Lakini Mungu alikuja kumuua Antiokia, kwa mambo hayo lakini hekalu halikubomolowa,(Ni sadaka tu ya kuteketezwa ndio iliyokomeshwa) kwahiyo kile kitendo cha yeye kwenda pale pamoja na majeshi yake na kutia unajisi patakatifu pa Mungu, ni CHUKIZO LA UHARIBIFU,.kama Danieli alivyolinena.

Sasa huyu Antiokia alikuwa anatimiza sehemu ya kwanza ya chukizo la uharibifu juu ya Hekalu la pili..Sehemu ya pili ambayo ilipelekea tena Uharibifu mkubwa mpaka Hekalu la Mungu kubomolewa na wana wa Israeli kutawanya katika mataifa yote ilitokea mwaka wa 70WK. Wakati jeshi la Rumi chini ya jenerali TITO alipouzunguka mji wa Yerusalemu na kuuchoma moto, na kulibomoa hekalu na kuliteketeza kabisa, na kuwatawanya wana wa Israeli kutoka katika nchi yao, hii ikawa ni mara ya pili ya hekalu la Mungu kuteketezwa baada ya lile la kwanza lililobomolewa na mfalme Nebkadreza wa Babeli.

Na kama vile lile la kwanza lilivyoteketezwa kwasababu ya maovu na maasi ya wana wa-israeli kadhalika na hili la pili lilibomolewa kwasababu hiyo hiyo,? Tunasoma wana wa Israeli walianza kwa kumkataa Yohana mbatizaji kisha wakaja kumkataa BWANA YESU mwenyewe, na kibaya zaidi wakamsulibisha, Bwana aliwaambia katika Yohana 8: 24 “Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu”..Na ni kweli hawakumsadiki Bwana, na ndio maana siku ile alipoukaribia mji wa Yerusaleu aliulilia na kusema.

Luka 19: 41 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,

42 akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.

43 Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;

44 watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako”.

Unaona hapo? Sababu ya kwanza iliyowapelekea wana wa Israeli mpaka kuharibiwa mji wao tena pamoja na Hekalu na jeshi la Rumi ni zile zile kwani waliwakataa manabii wa Mungu kwa kuwaua (soma Luka 13:34) na kuwasulibisha na zaidi ya yote walimkataa aliyemkuu wa uzima wakamkataa mfalme wao (ambaye ni Yesu) wakamkubali mfalme mwingine wa kidunia (KAISARI) na kumkiri hadharani kuwa huyo ndiye mfalme wao.

Yohana 19: 15 “Basi wale wakapiga kelele, Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Je! Nimsulibishe mfalme wenu! Wakuu wa makuhani wakamjibu, Sisi hatuna mfalme ila Kaisari”.

Hivyo wakaendelea na maovu yao, pamoja na wafalme wao wa kipagani, Ndipo wakati wa mapatilizo ulipofika mji kuteketezwa na watu kuuawa na dhiki kubwa ikatokea. Lakini kabla ya huo wakati kufika Bwana alishawaonya wale waliokuwa tayari kumsikiliza kwamba watakapoona ishara Fulani (Yaani majeshi ya Rumi) kuuzunguka Yerusalemu waondoke katikati ya mipaka ya Yerusalemu. Hivyo wale waliomwamini Bwana Yesu na maneno yake (yaani Wakristo) waliepuka hiyo dhiki kwa kuondoka Yerusalemu lakini wale waliosalia waliangamia wote, Yerusalemu iligeuka kuwa ziwa la damu. Jeshi la Rumi liliwaua watu wote na kubomoa Hekalu la Mungu.

Na ndio maana Bwana alisema hivi.

Luka 21: 20 “Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba UHARIBIFU wake umekaribia.

21 Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.

22 Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.

23 Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.

24 Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia”.

Kwahiyo yale maasi waliokuwa wanayafanya katika (nyumba ya Mungu) pamoja na kuwaua manabii wa Mungu kadhalika na kumkataa Masihi wao, ndio lililokuwa CHUKIZO lililopelekea UHARIBIFU wao.

Baada ya hapo wayahudi wote walitapanywa katika mataifa mengi duniani, pasipo kuwa na makao maalumu kama hapo mwanzo, lakini tunaona Bwana aliwakumbuka tena, akawahurumia mwaka 1948, pale Mungu alipowarudishia taifa lao tena. Na sasa wameshaanza kujitambua wao ni wakina nani mbele za Mungu ile neema imeshaanza kuwarudia kidogo kidogo Hivi karibuni wataenda kujenga HEKALU LA TATU, na hili litakuwa ni la mwisho. Maandalizi yote ya kulijenga yapo tayari, kinachongojewa ni kujengwa tu, na zile dhabihu walizokuwa wanatoa kama zamani, zitaanza kutolewa tena. Na mahali patakatifu pa Mungu patawekwa wakfu tena, Na Mungu ataikumbuka Israeli tena kama zamani.

 Lakini kumbuka shetani yupo katika kazi siku zote,..Alilokuwa analifanya nyuma ndilo atakalokuja kulifanya katika siku za mwisho, tena na zaidi ya pale. Kumbuka “machukizo ya uharibifu” yote ya nyuma yaliyotangulia yalikuwa ni kivuli tu cha CHUKIZO LA UHARIBIFU hasaa litakalokuja katika siku hizi za mwisho.

Bwana Yesu alisema katika Mathayo 24: 15 “Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (ASOMAYE NA AFAHAMU),

16 ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;

17 naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake;

18 wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake.

19 Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!

20 Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.

21 KWA KUWA WAKATI HUO KUTAKUWAPO DHIKI KUBWA, AMBAYO HAIJATOKEA NAMNA YAKE TANGU MWANZO WA ULIMWENGU HATA SASA, WALA HAITAKAKUWAPO KAMWE.

22 Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo”.

Kumbuka kutakuwepo CHUKIZO LA UHARIBIFU la tatu na la mwisho litakalokuja kusimamishwa huko Yerusalemu katika Hekalu la TATU. Wakati ule wana wa Israeli kwasababu ya makosa yao Ikasababisha Nebukadneza kuja kuliteketeza hekalu la kwanza, na kwasababu ya makosa yao tena ya kumkataa Masihi ndipo Jeshi la Rumi likaja kuuteketeza mji na Hekalu la pili. Kadhalika na kwa makosa yao tena ndiyo yatakayokuja kupelekea Mpinga-kristo kunyanyuka na kupatia unajisi patakatifu na kuleta uharibifu, pamoja na dhiki kuu katika hekalu la tatu.

Sasa kosa lenyewe litakuwa ni lipi?

Danieli alionyeshwa kosa hilo, tunasoma katika 

Danieli 9:26 “27 NAYE {mpinga-kristo} ATAFANYA AGANO THABITI NA WATU WENGI KWA MUDA WA JUMA MOJA; na kwa nusu ya juma hiyo ataikomesha sadaka na dhabihu; na mahali pake litasimama CHUKIZO LA UHARIBIFU; na hivyo, hata ukomo, na ghadhabu iliyokusudiwa imemwagwa juu yake mwenye kuharibu”.

Kwahiyo unaona hapo kuna AGANO ambalo mpinga-kristo ataingia na watu wengi, na hawa watu si wengine zaidi ya wayahudi ambao wataingia agano hilo na huyu mpinga-kristo ambalo litakuwa kwa kipindi cha miaka 7, agano hili litahusisha kupewa nafasi mpinga-kristo katika Hekalu la Mungu, jambo ambalo Mungu alishalikataza kwamba kisionekane kitu chochote katika hekalu la Mungu isipokuwa wayahudi tu tena makuhani wa uzao wa Walawi, lakini hawa wayahudi baadhi watampa heshima mpinga kristo wakijua tu ni mtu anayeheshimika duniani, hivyo anastahili kuwa na sehemu katika hekalu la Mungu, kama tu wale wa wayahudi wa kipindi cha Bwana Yesu walivyompa Heshima Kaisari, lakini hawatajua kama Yule ndio mpinga-kristo mwenyewe (ambaye atakuwa ni PAPA wa wakati huo) , na hiyo itapelekea kuwa CHUKIZO KUU kuliko yote, na ndipo Mungu ataruhusu hili agano livunjwe, lakini Yule mpinga-kristo ataghadhibika na kuleta dhiki kuu, ambayo haijawahi kuwako tangu ulimwengu kuumbwa.

Na ndio maana biblia inamtaja..katika

 2Thesalonike 2: 3 “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi{MPINGA-KRISTO}, mwana wa uharibifu;

4 yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe KUKETI KATIKA HEKALU LA MUNGU, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.

5 Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?

6 Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7 Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.{kumbuka bibi-arusi wa Kristo ndiye azuiaye mpaka atakapoondolewa kwa kwenda kwenye unyakuo} 

8 Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;

9 yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo;

10 na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa”.

Hivyo huyu mpinga-kristo ataleta dhiki duniani kwa kuihimiza chapa ya mnyama kutenda kazi,ataua wayahudi wengi sana, japokuwa sio wote kwasababu wapo ambao wataiepuka ile dhiki kwa kupitia ile injili ya manabii wawili (Ufunuo 11),na kwenda kujificha hawa watakuwa ni wale wayahudi 144,000 wanaozungumziwa katika (Ufunuo 7), lakini waliosalia wote wataungana na wale wanawali wapumbavu (yaani watu wa mataifa ambao hawakwenda kwenye unyakuo) kwa pamoja watapitia dhiki kuu ambayo itakudumu kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Kama inavyosema katika Danieli:

Danieli 12:11 “Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini”.

Kwahiyo hilo chukizo ni pale wayahudi watakapokuja kuingia agano na mpinga-Kristo, ambaye atataka kuja kuabudiwa kama Mungu..Hayo ni Machukizo makubwa ambayo yatasababisha Uharibifu kwa Wayahudi na kwa Dunia nzima, na kwa mpinga-kristo mwenyewe kwa kupatia unajisi patakatifu pa Mungu.( kumbuka pia Msikiti wa OMAR(Al-aqsa) uliopo pale Yerusalemu sio chukizo la uharibifu kama inavyodhaniwa na wengi .)

Kwahiyo ndugu hili chukizo la uharibifu sio tu kwa Yerusalemu peke yake hapana hata kwa KANISA, maana Kanisa ni HEKALU la Mungu biblia inasema hivyo. Na hili chukizo pia limesimama patakatifu pa Mungu, mahali ambapo pangepaswa YESU KRISTO peke yake aabudiwe, pamekuwa sehemu ya kuabudiwa sanamu pamoja na wanadamu. Bwana anasema Ufunuo 18: 4 “……..Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake. Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake”.

Tukijua kuwa tunaishi katika siku za hatari ni wakati wa kujiweka sawa, je! Bwana akija leo utaenda nae kwenye unyakuo?. Umeamini na kubatizwa?, je! wewe Ni miongoni mwa watakatifu?. Kama sivyo fanya hima katika muda huu wa nyiongeza tuliopewa. Weka mambo yako sawa siku ile isije ikakujia kama mwivi.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
18 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Paphilius patrick
Paphilius patrick
11 months ago

Katika daniel amezungumzia majuma 70 ambayo ni sawa na miaka 490 na siyo miaka 70 kama unavosema.lakini pia isome daniel 9 vizuri,anaxema atafanya agano thabiti na watu wengi kwa mda wa juma moja.huo ulikuwa ni utabiri juu ya masihi.ameanza kwa kukwambia masihi atakatiliwa mbali.juma 1 ni sawa na siku 7 ambapo katika unabii siku 1 inasimama kama mwaka 1 (ezekiel 4:6 na hesabu 34:14) hivyo alikuwa anazungumzia miaka 7.anasema katika nusu yake atafanya agano ambayo nusu ya 7 ni 3 na nusu ambayo ndo mda wa kazi ya masihi.KASOME UNABII VIZURI

Silvest
Silvest
1 year ago

Barikiwa mtumishi nimejifunza mengi kuhusu somo hili.

Anonymous
Anonymous
1 year ago

Amen barikiwa sana.

Simon Nicolas
Simon Nicolas
1 year ago

Haya maarifa unafunuliwa na Roho Nini? Mungu akutunze mtumishi wa Mungu ..hii source ya maarifa hasa Kwa nyakati hizi za mwisho ni nzuri sanaaaa …

peter
peter
1 year ago

Mungu akubariki sana nimejifunza mengi juu ya chukizo la uhalibifu na kuna vitabu vilikuwa vinanichanganya sasa nime patiwa ufumbuzi

Nsaji geofrey
Nsaji geofrey
1 year ago

Ubarikiwe sana kwa somo hili kuna maneno maana yake nilikuwa sijajua lakini roho wa bwana kanifunulia kupitia somo lako hili

JOSIAH MURUVE
JOSIAH MURUVE
1 year ago

Asante kwa neno Mungu awabariki

Rehema
Rehema
2 years ago

Ameen mbarikiwe saana

Geofrey Tarimo
Geofrey Tarimo
3 years ago

Mungu akubariki Sana mtumishi, nashukuru nimepata kitu Cha kujifunza. Mungu atukumbuke na kutuokoa na chukizo la Uharibifu… Amina

Buziku Ndolile Msanga
Buziku Ndolile Msanga
3 years ago

Mungu akubariki zaidi

Mohamed kassim
Mohamed kassim
3 years ago

BWANA YESU akubariki sana. Ubarikiwe zaidi

Eveline william
Eveline william
4 years ago

God bless you ninetafuta maana kwa muda mrefu leo nimefunguka pakubwa