Category Archive Home

ByAdmin

NIMEOKOKA, ILA MUNGU NDIYE ANAYEJUA NITAKWENDA WAPI.

Je! Ni sahihi kwa mkristo kufikiria hivi?..

Jaribu kufikiria mfano huu..

Mtu mmoja alitamani sana kujua afya ya mwili wake, hivyo akakusudia kweli kwenda hospitali kupima afya yake kama ameathirika na Ukimwi au La, Hivyo  akafanikiwa kwenda kuonana na daktari akachukuliwa vipimo vyote, Lakini alipomaliza kuchukuliwa tu vipimo akaondoka zake akarudi  nyumbani kwake, daktari alipomaliza uchunguzi wake wa vipimo akarudi sasa ili ampe majibu yake, na kumpa ushauri nasaha lakini alipofika hakumwona..

Sasa  akiwa kule nyumbani, siku zikapita, miezi ikapita, miaka ukapita, akawa anaishi Maisha ya furaha na ya amani kabisa, siku moja watu wakamuuliza vipi kuhusu afya yako, tunatumai sasa ipo njema kwasababu siku ile tayari ulishakwenda kuonana na Daktari..

Ndipo yeye akajibu, ndio! Natumai itakuwa ni njema!..Watu waliposikia vile wakashangaa kwa jibu lile,  unatamai vipi tena? Wakati ulishapata uhakika kwa Daktari,..Lakini yeye akawajibu, ndio nilishaonana na daktari akanichukua vipimo vyote, ila majibu anayo yeye mwenyewe, mimi sijui kingine Zaidi ya hapo, Hivyo yeye Mungu ndiye anayejua kuwa mimi ni muathirika au La!. Hilo ni jukumu lake kama daktari, mimi sihitaji kujua sana kwasababu mimi sio daktari..

Fikiria mtu kama huyo wale watu walimwonaje? Ni Dhahiri kuwa watasema huyu atakuwa amerukwa na akili, alikwenda hospitali kufanya nini sasa kama hakupata majibu ya afya yake, ambayo yangempa uhakika wa afya yake kuwa ni njema au la!.

Na ndivyo ilivyo hata leo kwa mtu  ambaye hajapata bado uhakika wa wokovu wake..Watu wengi ukiwauliza Je! Umeokoka watasema ndio, nilishaokoka zamani sana, mpaka nikabatizwa,..Ukizidi tena kuwauliza, sawa Je unaouhakika hata ukifa leo au Yesu Kristo akirudi leo utakwenda naye mbinguni.. hapo ndipo watakapokuambia ninatumai hivyo, wengine watakuambia hilo ni Mungu ndio analolijua..mimi siwezi kujua hukumu zake, na mwingine atakwambia,nikisema hivyo nitakuwa ninajihesabia haki, na kujiona mimi ni kitu fulani mbele za Mungu..wakati bado sijafika lolote linaweza kutokea.

Ndugu Neno WOKOVU ni Neno lenye msingi wa UHAKIKA chini yake, mfano huwezi kusema umeokolewa kwenye moto, na huku bado unajihisi  kama upo bado mule mule motoni, vinginevyo hiyo itakuwa ni ndoto tu au bumbuazi fulani limekushika, lakini mfano ukiokolewa kutoka motoni na mtu fulani, utajiona kabisa jinsi unavyohama kutoka ulipokuwepo kwenye mateso na kwenda sehemu nyingine salama..Hivyo ni jambo la uhakika..

Na ndio maana biblia inaweka  wazi kabisa kwa kutuambia…

2Wakorintho 13:5  “Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu? Isipokuwa mmekataliwa”

Unaona, ukiwa mkristo huendi tu ilimradi, huwi tu kama mshabiki fulani, bali kila hatua inajipima je! Mpaka sasa Kristo yupo pamoja nami au La!, Na je ikitokea leo hii safari yangu ya Maisha imekwisha ghafla Je nitakuwa upande wa haki au hukumu?

Sasa, swali unaloweza kujiuliza ni Je utaupataje Uhakika huo wa wokovu ndani yako?

Unapaswa uangalie mambo mawili la kwanza Ni Je! Tangu uliposema umeokoka, kuna badiliko lolote lililotokea ndani yako?..Je yale matunda ya Roho yamezalika ndani yako?

Sawasawa na Wagalatia 5:22  inayosema..

“Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23  upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Hivyo kama hayo yapo ndani yako, basi hiyo ni hatua ya kwanza ya kukupa uhakika ndani yako.

Na jambo la pili, Je! Tangu ulipoubeba msalaba wako na kumfuata Kristo, Je! Ulipitia vipingamizi vyovyote katika hilo?..Kupitia majaribu sio sifa kwamba ni jambo jema, lakini shetani hawezi kukuangalia umeacha rushwa, akakuvumilia, umeacha ulevi na kuuza pombe kwenye biashara yako akakuangalia tu, umeacha kampani za marafiki wabaya na disko asikuletee udhia, umeacha ulimwengu kwa ujumla wake na mambo yake yote asikuletee dhihaka,  umekatisha ghafla yale madili haramu uliyokuwa umepanga wewe na wenzako kwenda kuyafanya shetani akabaki anakutazama tu!..Umekatisha hayo mahusiano ya kiasherati ghafla anakutazama tu…wakati mwingine utapitia kupigwa au kutengwa, n.k. Sasa kama haya hayakuonekana ndani yako basi uhakika huo kuupata ni ngumu, Kristo na mitume wake waliyapitia hayo, vilevile na wewe utakumbana nayo kwa sehemu fulani katika safari yako ya wokovu.

Sasa Ikiwa hayo mambo mawili makuu yameonekana ndani yako, basi uhakika wenyewe wa kama upo katika njia sahihi ya wokovu utatokea wenyewe ndani yako, wala hautahitaji kuulizia bali Roho Mtakatifu mwenyewe atakushuhudia kuwa wewe ni mwana wa Mungu na umeokoka..

Sawasawa na Warumi 8:16  “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;

Hivyo ndugu, kama  bado mpaka sasa hujapata uhakika huo, Ujue tu, mbinguni hutakwenda haijalishi utasema niliongozwa sala ya toba, au nilibatizwa, au nilikuwa ninahudhuria kwenye maombi..Hutakwenda kwasababu suala la wokovu sio suala la kubahatisha au kuhisi hisi tu bali ni uhakika Mungu anaompa mtu akiwa bado hapa hapa duniani..Na kuwa na uhakika wa kwenda mbinguni sio kujihesabia haki..

Biblia inasema…

2Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.

Ukisoma kwenye tafsiri nyingine hususani zile za kiingereza(kjv) Hilo Neno “jitahidini zaidi kufanya imara” linasema hivi..

“brethren, give diligence to make your calling and election sure…”

Neno SURE, linaamisha uhakika, maana yake ujitahidi  kuufanya kuitwa kwako na uteule wako uwe wa uhakika..

Hivyo na wewe pia hujachelewa, ndani ya kipindi hichi kifupi cha maisha yako uliyobakiwa nayo hapa duniani, na kabla Bwana hajarudi, anza kuuthibitisha tena wokovu wako, kusudia kweli kuanzia leo kumfuata Kristo, anza kuzaa hayo matunda ya Roho, na kuwa tayari kuubeba msalaba wako..Na Bwana mwenyewe atauweka uhakika huo ndani yako. Nawe utaishi Maisha ya amani kila siku, ambapo hata wimbi lolote likisimama mbele yako, hata bunduki ikiwekwa mbele yako, huna wasiwasi kwasababu unajua ukifa tayari moja kwa moja utakuwa mbinguni kwa Baba.

Bwana akubariki sana.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?

UPAKO NI NINI?

MUNGU WETU, JINSI LILIVYO TUKUFU JINA LAKO DUNIANI MWOTE!

MAMBO MANNE,YANAYODHOOFISHA UOMBAJI WAKO.

RABI, UNAKAA WAPI?

UKADHANI YA KUWA MIMI NI KAMA WEWE.

Mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili

Rudi Nyumbani:

ByAdmin

MKARIBIE BWANA ZAIDI ILI UFANYIKE NGUZO.

Mkaribie Bwana.

Shalom, karibu tujifunze Neno la Mungu..

Miongoni mwa watu waliokuwa wanamfuata Bwana Yesu kulikuwa na makundi manne..1) Makutano 2)Wanafunzi 3)Mitume 12 na 4) Nguzo.

Kundi la kwanza ambalo ni makutano, hawa walikuwa tu wanakusanyika kusikiliza mahubiri ya Bwana Yesu ambao mara zote Bwana alikuwa anazungumza nao kwa mifano, na kuwaponya magonjwa yao..baada ya hapo walikuwa wanarejea katika shughuli zao na maisha yao ya kawaida.

Kundi la pili ambalo lilikuwa ni la wanafunzi wa Yesu, hawa walikuwa wapo kama 70 hivi au zaidi kidogo..Kundi hili ni lile ambalo lilikuwa linamfuata Bwana Yesu lakini si kila mahali…Ni baadhi ya watu ambao waliamua kujitoa kumtumikia Yesu sehemu zote alizokuwa anakwenda…na hawa pia Bwana alikuwa anawatuma kuhubiri injili kila mahali ambapo Bwana alipokuwa anataka kwenda. (Soma Luka 10:1).

Kundi la tatu lilikuwa ni Mitume…Mitume hawa walikuwa 12 tu, na waliteuliwa na Bwana Yesu kati ya lile kundi la wanafunzi 70 waliokuwa wanamfuata Yesu.

Luka 6: 13 “Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume”

Kundi la mitume ndio lilikuwa linamkaribia sana Bwana kuliko wale wanafunzi 70 na makutano..Hawa kila mahali Bwana alipokuwa na wao walikuwepo, walikula nae na kunywa naye…na mbele za Bwana ni kama vile walipendelewa zaidi kuliko wanafunzi wengine kwasababu kila mfano ambao Bwana aliokuwa anawafundisha makutano usioeleweka wao ndio walikuwa wanapata fursa ya kwenda kumwuliza akiwa peke yake, maana ya mifano hiyo, nafasi ambayo makutano wala wale wanafunzi wengine hawakuipata.

Lakini lilikuwepo kundi la mwisho ambalo ni la kipekee sana..ambalo hilo lilikuwa karibu sana na Bwana zaidi ya makundi hayo matatu yaliyotangulia…na kundi hilo lilitwaliwa kutoka miongoni mwa wale wanafunzi 12…Na hao walikuwa watatu tu ambao ni (Petro, Yohana na Yakobo)..Hawa watatu walijulikana kama NGUZO.

Wagalatia 2:9 “tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; YAKOBO, na KEFA na YOHANA, WENYE SIFA KUWA NI NGUZO, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;”

Kefa ni jina lingine la Petro(soma Yohana 1:42). Hawa watatu walijulikana kama nguzo…Maana yake walikuwa wanauhusiano wa kipekee na Bwana zaidi ya mitume wote, zaidi ya wanafunzi wote na zaidi ya makutano yote.

Utaona hawa watatu kila mahali ambapo Bwana alitaka kwenda peke yake (labda mlimani kusali, au kuwafunulia siri za ndani sana) aliwachukua hawa watatu tu Yohana, Yakobo na Petro, na si mitume wengine waliosalia..Hebu tuangalie mifano michache kulithibitisha hili..

Luka 9:27 “Nami nawaambia kweli, Wapo katika hawa wanaosimama hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata wauone kwanza ufalme wa Mungu.

28 Baada ya maneno hayo yapata siku nane, aliwatwaa PETRO NA YOHANA NA YAKOBO, AKAPANDA MLIMANI ILI KUOMBA.

29 Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta.

30 Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya”

Unaona hapo walikuwepo mitume wote lakini Yesu aliwachagua tu hao watatu kwenda nao mlimani..kusali na huko akawafunulia ufunuo mkubwa namna ile, na wakaisikia sauti ya Mungu ikisema huyu ni mwanangu mteule wangu, msikieni Yeye. Ufunuo huo waliouona tu hawa watatu, na Bwana aliwaambia wasimwambie mtu mwingine yoyote mpaka atakapofufuka katika wafu. Maana yake ni kwamba wanafunzi hawa walikuwa na siri nyingi ambazo Bwana aliwafunulia ambazo mitume wengine hawakuzijua.

Tutazame mfano mwingine tena..

Mathayo 26:36 “Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.

37 Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka.

38 Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.

39 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.

40 Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?”

Hapo utaona Bwana alitenga makundi mawili..kundi la kwanza ambalo ndilo lile la mitume 9 aliliacha kule kwenye bustani ya Gethsemane….hakuenda nalo kuomba usiku ule, badala yake akawachukua Petro, na wale wana wawili wa Zebedayo ambao ni (Yohana na Yakobo), hao ndio akaenda nao kusali..na hao ndio aliowaambia wakeshe waombe pamoja na yeye wasije wakaingia majaribuni..kwasababu shetani ndio aliokuwa anawawinda zaidi kwasababu walikuwa na Bwana zaidi..Na kama wewe ni msomaji wa biblia utagundua kuwa wakiwa kule waliona tena ishara nyingine wakati Yesu akiwa anaomba jasho lake lilikuwa kama matone ya damu, na pia waliona malaika wakija kumtia nguvu…

mambo hayo mitume wengine waliosalia hawakuyaona…

Na hawa watatu, hata wakati wa Pentekoste na kuendelea ndio mitume Bwana alitembea nao kwa viwango vikubwa sana..mpaka watu wote wakawaita kuwa ni NGUZO YA KANISA. Kitabu cha Ufunuo wa Yohana, ambacho kimebeba siri nyingi za ufunuo wa siku za mwisho, na ujio wa Bwana Yesu kimendikwa na Yohana huyu…ambaye ndiye mmoja wao wa wale watatu.

Sasa kwanini wanafunzi hawa watatu waliteuliwa na Bwana kuwa karibu zaidi na yeye kuliko wengine wote?

Jibu ni kwamba, kwasababu walimpenda Bwana zaidi..Mungu hana upendeleo hata kidogo..kila dakika, kila muda walikuwa wanamtafakari Bwana, wanamfikiria yeye, wanamtumikia yeye, na wamejikana nafsi na kusema lolote liwalo tutamfuata Yesu Bwana wetu popote aendapo, kwa moyo huo Bwana akawapenda zaidi na hivyo kuwakaribisha wamsogelee zaidi kuliko wengine…Kama ni mwanafunzi wa Biblia utamjua Petro alivyokuwa anampenda Bwana…ilifika wakati akamwambia Bwana wajapochukizwa wote kwaajili yako mimi sitachukizwa..ijapokuwa alikuwa ni dhaifu lakini angalau hata alikuwa anaujasiri wa kusema hivyo tofauti na wengine…

Hali kadhalika Yohana na Yakobo ni hivyo hivyo,..walimpenda Bwana mpaka ikafikia wakati wakamwendea Bwana wao na kumwomba katika ufalme wake waketi mmoja mkono wake wa kuume na mwingine wa kushoto…(walimpenda Bwana mno na hivyo Bwana akawapenda zaidi). Yohana ilifika wakati akawa anaegemea kifuani mwa Yesu kila mahali…na ilifika kipindi Bwana akawaambia wazi wazi kuwa mmoja wao atamsaliti..na kila mmoja akawa anawasiwasi ni nani amtajaye..na Bwana akamfunulia Yohana peke yake kwamba ni Yuda kwa sauti ya chini, wengine hawakusikia.. kwasababu alikuwa karibu sana na yeye kifuani mwake…

Yohana 13:23 “Na palikuwapo mmoja wa wanafunzi wake, ameegama kifuani pa Yesu, ambaye Yesu alimpenda.

24 Basi Simoni Petro akampungia mkono, akamwambia, Uliza, ni nani amtajaye?

25 Basi yeye, hali akimwelekea Yesu kifua chake, akamwambia, Bwana, ni nani?

26 Basi Yesu akajibu, Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa. Akatowelea tonge, akalitwaa akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskariote”.

Tabia ya hawa watatu kuwa tayari chochote Bwana alichowaambia ndizo zilizowafanya kuwa karibu zaidi na Bwana kuliko wengine, Bwana alipotaka kwenda kuomba walikuwa tayari kutaka na wao kwenda kuomba..walikuwa hawaonyeshi dalili za uvuvi ingawa walikuwa na madhaifu, walijinyima kila kitu ili tu wampendeze Yesu.

Vivyo hivyo Neno la Mungu linasema..Yakobo 4:8 “Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili”.

Unapojikana nafsi na kumpenda Mungu zaidi, na kumfanya yeye ndio wakwanza kila mahali, hapo ndipo unapojitengenezea daraja zuri la Mungu kukukaribia zaidi..ndipo unapoongeza daraja zuri la Mungu kukupenda zaidi ya wengine, kukufunulia siri nyingi zaidi ya wengine…kukutumia na kukubariki. Unapoutafa uso wa Mungu kwa kusali, kufunga, kutenda mema zaidi ya wengine..mema yako yanapimwa mbele za Mungu kila siku na yanapoonekana yamezidi ya wengine wengi ndipo na wewe thamani yako inapanda mbele za Mungu, lakini kama leo ukiambiwa tu usali..hata dakika mbili humalizi, kusoma tu neno ni mara moja kwa wiki, na hata ukisoma unasoma tu mistari na sio mada nzima..hapo utafanyikaje NGUZO mbele za Mungu.?

Hivyo tusiridhike na uhusiano wetu na Mungu..Tuzidi kumkaribia Bwana..kutoka kuwa wanafunzi wake, hata mitume wake hata Nguzo..

Ufunuo 3: 12 “Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa NGUZO katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Maran atha!


Mada Nyinginezo:

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

INGIENI KWA KUPITIA MLANGO ULIO MWEMBAMBA.

YULE JOKA WA ZAMANI.

KUOTA UNAANGUKA .

NAO WALIOKUWA WAMEKUSUDIWA UZIMA WA MILELE WAKAAMINI.

TIMAZI NI NINI

Rudi Nyumbani:

ByAdmin

Kwanini Ibrahimu analitaja jina la YEHOVA wakati Musa anasema hakujifunua kwa jina hilo kwao?

SWALI: Hujambo mpendwa,naomba nieleweshwe hili tafadhali katika mwanzo 22:14 utaona Ibrahimu alipaita mahali pale YEHOVA-YIRE ambapo alimtoa yule kondoo kuwa sadaka, badala ya Isaka, lakini ukisoma tena katika Kutoka 6:2-3 Mungu anamwambia Musa kwamba hakuwai kujidhihirisha kama YEHOVA kwa Ibrahimu ,Isaka, na Yakobo, bali Mungu mwenyezi. Je! Biblia inajipinga? Asante sana.


JIBU: Kumbuka vitabu vitano vya mwanzo vimeandika na mtu mmoja ambaye ni MUSA (Ambavyo ni Mwanzo, kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na kumbukumbu la Torati ).. Na kama tunavyojua Musa aliviandika vitabu hivi alipokuwa jangwani (yaani akiwa njiani kuelekea nchi ya Ahadi).. Na katika kitabu cha Mwanzo ambacho ndicho tunapata huko habari za Ibrahimu…wakati anaziandika habari hizo akiwa jangwani tayari alikuwa ameshafunuliwa jina hilo jipya la Mungu yaana YEHOVA. Hivyo mahali popote ambapo alisoma habari za Ibrahimu, akimtaja Mungu kwa jina lolote lile yeye Musa ni lazima angeliandika kwa jina YEHOVA, kadhalika mahali popote ambapo Nuhu angemtaja Mungu kwa jina lolote lile yeye Musa angesahihisha katika maandishi yake na kuandika jina YEHOVA badala yake..na hivyo hivyo kwa Lutu, Yakobo, Isaka, Yusufu na wengineo.

Sasa utauliza mbona kila mahali katika vitabu hivyo vitano vya kwanza vya Musa kila mahali Mungu katajwa kama BWANA, na si hilo YEHOVA ??

Kumbuka Katika biblia yetu ya Kiswahili na ya kiingereza na ya lugha nyingine zote…kila mahali ambapo leo hii tunapasoma pameandikwa neno BWANA, Kwa asili hapakupaswa paandikwe hivyo…Sehemu nyingi katika agano la lake unapopaona pameandikwa neno BWANA, kwa asili pangepaswa paandikwe neno YEHOVA. Musa nyingi alizitafsiri kama Yehova..kwa mfano katika

Mwanzo 2:7 biblia inasema

“ Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai”…Mstari huu Musa aliuandika hivi “Yehova Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai ”

Lakini sasa watafsiri wa kwanza biblia waliona ili kuliheshimu zaidi hilo jina la Mungu si vyema kuandika jina hilo Tukufu na kuu kama lilivyo…Hivyo kwa hekima ya Roho ndipo likawekwa jina BWANA badala ya YEHOVA..Kitu ambacho ni kizuri!..kama tu vile isivyo hekima wala heshima kumwita mzazi wako jina lake halisi na badala yake unamwita jina lake la cheo “BABA”..huwezi kusema shikamoo Joseph badala yake utasema shikamoo Baba. Hivyo si dhambi kumwita Mungu BWANA kama inavyochukuliwa leo na ndugu zetu mashahidi wa Yehova wakidhani kuwa kumuita Mungu BWANA ni kumvunjia heshima..

Biblia zote, pale kwenye utangulizi, zimechapishwa na angalizo hilo pale mwanzoni kabisa.. Kuwa BWANA lilimaanisha YEHOVA.

Kwahiyo kitabu cha Mwanzo kimetaja Yehova na kitabu cha Kutoka kwasababu mwandishi ni huyo huyo mmoja, na aliviandika vitabu hivyo akiwa tayari ameshalijua jina la Mungu kamilifu yaani Yehova.

Mada Nyinginezo:

Kwanini Bwana alisema Hakuna aliye mwema ila mmoja?


Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

Kwanini kila nikitaka kusali naingiwa na uvivu?

KWANINI BWANA YESU ALISULUBIWA NA WEZI WAWILI?

Kwanini Mungu aliikubali sadaka ya Yeftha ya kumtoa binti yake kafara?

Rudi Nyumbani:

ByAdmin

OLE WA NCHI NA BAHARI.

Ufunuo 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.

13 Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.

14 Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo.

15 Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule.

16 Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake.

17 Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama JUU YA MCHANGA WA BAHARI”.

Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, kama ukisoma mistari iliyotangulia kabla ya hiyo, utaona kuwa shetani kuna majira alijaribu kufanya vita katika mbingu, lakini alishindwa kama biblia inavyotuambia akatupwa chini na mahali pake hapakuonekana tena mbinguni kuanzia huo wakati.

Lakini biblia inatuambia pia alipotupwa, hakukaa katika eneo la nchi peke yake, au hakwenda baharini moja kwa moja , hapana, bali alikwenda kusimama juu ya mchanga wa bahari….Kwa namna nyingine alikwenda kusimama ufukweni mahali ambapo nchi na bahari vinakutana.

Shetani alifahamu kuwa, hivyo ndivyo vitu viwili vinavyoikamilisha dunia, hakuegemea tu upande mmoja afanye makao yake huo hapana..badala yake alisimama pale ufukweni ili aweze kuyaona na kuyatawala yale yanayotoka katika nchi na yale yanayotoka katika bahari. Na ndio maana baada ya pale biblia inasema “Ole wa nchi na bahari”, Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu..

Unaona? haituambii nchi tu peke yake, au bahari peke yake, hapana bali vyote viwili, kwasababu ndipo alipopania kuwanasa wanadamu.

SASA NCHI NA BAHARI KIBIBLIA VINAWAKILISHA NINI?

BAHARI: au sehemu yenye maji mengi, biblia imeshatupa majibu yake,.Tusome.

Ufunuo 17:15 “Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha”.

Kumbe maji yanawakilisha jamaa, na makutano na mataifa na lugha…Yaani kwa ufupi watu wengi.

Vilevile, tunaweza kuona jambo lingine, pale Bwana Yesu alipochagua mitume wake, wengi wao aliwachagua kutoka katikakati ya wavuvi, akifunua kuwa watakuja kufanya kazi ya uvuvi wa watu wengi, yaani jamaa, na mataifa la Lugha, kama alivyomwambia Petro na Andrea katika (Mathayo 4:19)..

Hivyo Bahari inawakalisha watu wengi, kwahiyo shetani tangu alipoona ameshindwa hawezi tena kupigana yeye kama yeye aliamua sasa kuelekeza macho yake katikati ya watu ili apate nguvu, na chombo kikubwa anachokitumia ili kupata ufuasi mkubwa wa watu ni kupitia kitu kinachoitwa DINI, penye dini ndipo palipo na watu wengi, sio katika siasa au makabila..

Hivyo mpaka sasa yupo katika kilele cha kuzikutanisha dini zote na madhehebu yake yote ambayo tangu zamani yalishautupilia mbali uongozo wa Roho Mtakatifu na kufuata mapokeo yao ya kibinadamu, ili zikubaliane katika kitu kimoja.

Na ndio maana ukisoma ile sura inayofuata ya 13, utaona Yule joka aliposimama tu pale kwenye mchanga wa bahari, wakati huo huo wanyama wawili walitokea, mmoja alitokea baharini, na mwingine akatokea nchi kavu (Soma ufunuo sura ya 13 yote utaona)..Sasa Yule aliyetokea habarini ndiyo huyu atakayepata nguvu ya kuwa na wafuasi wengi sana duniani kwa kupitia dini…

NCHI: NI Hifadhi ya kimwili, tangu mwanzo, Mungu alipomuumba Adamu alimpa ardhi ailime na kuitunza kwasababu huko ndipo alipomchipulia chakula chake kitakachomfanya aishi hapa duniani.

Ayubu 28:5 “Katika ardhi ndimo kitokeamo chakula;…”..

Hata sasa chakula na utajiri vipo katika ardhi..Hivyo kwa lugha ya sasa nchi tunaweza kusema inawakilisha Uchumi,..Fedha, biashara, hazina, vitu vinavyoweza kumpatia mwanadamu Rizki ili aishi hapa duniani n.k…

Kwahiyo shetani kuona hivyo, alisimama pia katika eneo hilo.. tangu huo wakati akajikita kudhibiti mihimili hiyo miwili mikuu, Watu, na uchumi.. nchi na bahari..

Kwanza Ili awapate Watu anatumia kivuli cha dini, ambapo hivi karibu anaenda kutimiza adhma yake ya kuzileta dini zote zilizopoteza uongozo wa Roho Mtakatifu pamoja, zikiongozwa na ile dini mama ya Rumi, na cha ajabu biblia inatuambia watu wote na mataifa yote ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima cha mwanakondoo tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu wataufurahia huo utawala na mfumo mzima wa ibilisi ..

Na sasa ili kuwalazimisha watu wote waufuate huo mfumo wa mpinga-Kristo, shetani atamnyanyua mnyama mwingine ambaye atakuwa na nguvu ya kiuchumi sana,(taifa kubwa) ambalo hilo litayahimiza mataifa mengine yote yapokee maagizo kutoka kwa huo umoja wa dini duniani, na mtu yoyote atakayekataa kuupokea hataruhusiwa kununua wala kuuza, wala kufanya biashara yoyote, wala kuajiriwa mahali popote.. Unaona Jinsi hali itakavyokuwa mbaya.. Ni nani atapona hapo.

Haya ni mambo ambayo tunaweza kuyashuhudia siku za hivi karibuni wala tusidhani bado miaka mingi, jaribu kufikiria jinsi ugonjwa huu wa Corona ulivyozuka tu ghafla, na athari yake ndogo tu inawafanya watu wasiweze kutembea hata nje katika baadhi ya nchi, na imetokea tu ndani ya kipindi kifupi cha miezi mitatu tu, hakuna ambaye angeamini kuwa dunia ingeweza kuwa namna hii, dunia ambayo inashamra shamra za kila namna..Lakini mambo yamekuwa hivyo barabara zipo wazi..Hata matajiri na wana wa wafalme, na watu mashuhuri na fedha zao haziwasaidii wakati huu. Ndivyo mambo yatakavyobadilika ghafla tu wakati huo ukifika.

Shetani ameshajidhatiti vya kutosha, na ghafla tu, dini zote zitafikia muafaka mmoja zikiongozwa na dini ile mama ya Rumi, watafikia muafaka mmoja, watapata sapoti kutoka katika kila pembe ya dunia, watakuwa na kiongozi wao mmoja ambaye ndio atakuwa mpinga-Kristo..Huyo ataishawishi dunia iwe na ustaarabu mpya, Lakini lengo lake ni kuihimiza ile chapa ya mnyama ili awanase wanadamu wote.. Sasa kwa kuwa yeye amejikita katika masuala ya kiimani sana, kama tulivyosema atapata msaada mwingine kutoka katika taifa lenye nguvu ya kiuchumi duniani, ili kuyalazimisha mataifa mengine yote yamtii yeye kwa shuruti.

Mpaka wakati huo umefika ujue unyakuo tayari umeshapita ndugu yangu, sijui utakula nini wewe unayemkataa Yesu leo, wewe ambaye utakuwepo ulimwenguni wakati huo, pona yako itakuwa ni kufia njaa ndani, kama utakuwa hujakamatwa na kuuliwa kwa mateso yasiyokuwa ya kawaida.. Hakuna mtu yoyote atayevumiliwa na mtu au chombo chochote cha dola ambaye ataonekana hajapokea chapa hiyo ya mnyama.. usifikiri utapona..Ni ngumu sana ndugu, usidhani akaunti yako ya benki itakusaidia wakati huo, hilo jambo halitakuwepo, usidhani utakimbilia mafichoni, ondoa hayo mawazo, usidhani elimu yako itakusaidia kupata ajira wakati huo, acha kufikiria hivyo..Chapa utaipokea tu.

Hizi ni nyakati za hatari tunazoishi, ole wa nchi na bahari!…Kimbilio pekee ni Kristo tu saa hii..Ikiwa upo bado nje ya Kristo, basi fanya uamuzi wa Busara leo hii, tubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, omba toba kwa Mungu, nenda kabatizwe ikiwa bado hujafanya hivyo. huu ni wakati sasa wa kuamka usingizini.

Warumi 13:11 “Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini”.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

UFUNUO: Mlango wa 13

UCHAWI WA BALAAMU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

DANIELI: Mlango wa 7

MWISHO WA DUNIA UTAKUJAJE?

Nini maana ya “Siku moja nyuani mwa Bwana ni bora kuliko miaka elfu”?

Rudi Nyumbani:

ByAdmin

UCHAWI WA BALAAMU.

Hesabu 23:23 “Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli”

Wengi tunalifahamu hili andiko na tunalitumia, pale tunapohisi roho za kichawi zinatunyemelea…Na tunapolitumia kwa Imani linaleta majibu hakika kwasababu ni pumzi ya Mungu…Lakini hebu leo tuingie kwa undani kidogo kujifunza juu ya Neno hili ili tupate faida mara mbili Zaidi.

Siku zote tunashauriwa tujifunze biblia na sio tuisome tu…tukichukua tu kipengele cha mstari wa biblia na kukitumia hicho bila kutafuta maana ya mstari huo, kwanini mwandishi aliandika hivyo, na Mungu alikuwa anamaanisha nini juu ya mstari huo..hapo tutakuwa hatujajifunza bali tumesoma tu..ambapo matokeo yake ni madogo kuliko kama tungeketi chini na kujifunza kuanzia juu chanzo cha mstari huo na dhima, na maudhui ya huo mstari ukoje.

Sasa tukirudi katika mstari huo hapo juu, kama ukianza kusoma kitabu hicho cha Hesabu kuanzia sura zilizotangulia kabla ya hiyo ya 23, utaona inahusu safari ya wana wa Israeli (au wana wa Yakobo), walipokuwa wanatoka Misri kuelekea nchi yao ya Ahadi,

Wakiwa njiani jangwani walikutana na kikwazo, Ilikuwa kwamba ili waendelee na safari yao iliwapasa wakatize katika nchi ya watu fulani ambao walijulikana kama wamoabu.

Nchi hiyo ilikuwa na mfalme na huyo mfalme akawakatalia wasikatize katika nchi hiyo, na hakukuwa na njia nyingine ya karibu isipokuwa kukatiza katika nchi hiyo..Ijapokuwa waliwaomba sana na kuwaahidi kwamba watalipia gharama zote za uharibifu wowote kama ukijitokeza katika kukatiza kwao lakini wenyeji wa mji ule walikataa katakata wakiongozwa na mfalme wao..Na kwa hofu Mfalme wao hakuishia tu kuwazuia bali alipanga pia kwenda kupigana nao, hivyo akatafuta pia namna ya kuwalaani(au kwa lugha rahisi kuwaloga) ili atakapokwenda kupigana nao aweze kuwashinda kirahisi bila kutumia nguvu nyingi.

Katika harakati za kutafuta mtu mashuhuri wa kuloga, akampata mtu anayeitwa Balaamu mchawi (Hesabu 24:1), huyu alikuwa ni mchawi wa viwango vya juu sana na aliyejulikana kwa kuloga hata mataifa, ambaye alitumia nguvu za giza, na alikuwa anauwezo wa kuisikia pia sauti ya Mungu..na kabla ya kuloga alikuwa anauwezo wa kupima kiwango cha kiroho mtu alichopo kabla ya kumwangusha…na sio hilo tu, alikuwa anazo mpaka mbinu mbadala zisizo za kuweza kumwangusha mtu bila kutumia uchawi wowote…(na huo ndio mbaya Zaidi ambao ndio alioutumia kuwaangusha wana wa Israeli).

Sasa alipoitwa kama wengi wetu tunavyoijua habari…haraka sana aliwajua wana wa Israeli ni watu gani…alijua ni watu wa Mungu na wamezungukwa na ukingo wa Mungu pande zote…hakuna namna ya kuweza kuwaingia kwa njia ya uganga wala uchawi (hakuna namna yoyote vibuyu na dawa za miti shamba zinaweza kufanya kazi juu yao)..hata hivyo alinusurika kifo njiani wakati anajaribu kutaka kwenda kuwalaani…Ili litimie lile neno la kwanza (akulaaniye atalaaniwa, na akubarikiye atabarikiwa).

Hivyo Balaamu alilijua hilo na alipofika kwa mfalme wa MOABU akamwambia wazi kabisa kwamba “HAKIKA HAPANA UCHAWI JUU YA YAKOBO, WALA HAPANA UGANGA JUU YA ISRAELI”.

Hiyo ndiyo asili ya Neno hilo…Ni mchawi Balaamu ndiye aliyeyasema maneno hayo sio Mungu kama wengi wetu tunavyodhani. Balaamu alikiri kabisa..Hivyo akaacha kujaribu kuwaloga/kuwalaani Israeli ambaye ndiye Yakobo, kinyume chake akawabariki, kwasababu alijua endapo angetaka kuwaalaani ni kujitafutia laana na kifo..hivyo akaamua kuhamia kwenye Mbinu yake ya pili ambayo ndiyo KUBWA NA KUU.

Hesabu 24:1 “Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani”

Mbinu hiyo siyo ya kutumia vitunguli tena/wala vibuyu/ wala ya kuwatamkia maneno mabaya..Mbinu hii ya pili ambayo ndio UCHAWI HASAA ni ya kuwakosesha wana wa Israeli na Mungu wao..Ili Mungu awakasirikie na kuwaadhibu yeye mwenyewe…kwasababu kuwaangusha kwa njia ya uchawi imeshindikana sasa dawa ni kuwachonganisha na Mungu wao..Hivyo akamfundisha Mfalme wa Moabu namna ya kuwakosesha wana wa Israeli ili wapigwe na Mungu wao..

Akamfundisha na kumwambia wawaalike wana wa Israeli baadhi katika sadaka za miungu yao na kuwapa wanawake wao walio wazuri na warembo, hivyo Wana wa Israeli watakapoona hivyo wataingia tamaa na kuzini na wanawake hao katika karamu hizo za miungu na hasira ya Mungu itawaka juu ya wana wa Israeli..Tusome

Hesabu 25:1 “Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu;

2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao.

3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli”.

Ukiendelea kusoma utaona Mungu aliwakasirikia na aliwaua kwa pigo watu elfu 24. Kama sio mtu mmoja kwenda kurekebisha Israeli wote wangeisha siku hiyo mbele ya ghadhabu ya Mungu..Hivyo japokuwa Yule mchawi balaamu hakuwaloga kwa uchawi wa uganga na vibuyu lakini aliwaloga kwa kuwakosesha na Mungu wao.

Jambo hilo hilo linaendelea hata sasa katika nyakati hizi za agano jipya. Ni kweli hakuna uganga wala uchawi juu yako, umelindwa na kuzungukwa na kingo za moto pande zote, katika afya yako, katika kazi zako, katika familia yako, mpaka una ujasiri wa kusema Bwana ndiye anisaidiaye sitaogopa mabaya, wala uchawi wala uganga..Ndio shetani analijua hilo na wala hawezi kukuloga kwa vitunguli, wanaokuendea kwa waganga ni kweli wanapoteza muda..nataka nikuambie shetani akishalijua hilo wala hapotezi muda wake kukutumia watu kutafuta kukuloga wewe…kwasababu hawezi kulaani kilichobarikiwa…hviyo acha kufikiri kwamba wachawi wanakuwinda wewe uliyeokoka kweli kweli, walishaacha siku nyingi wakati ule walipogundua tu unazungukwa na jeshi la mbinguni…

Shetani anachofanya sasa juu yako ni kutafuta njia ya kukukosesha wewe na Mungu wako, ili Mungu akuadhibu…na anatumia watu mfano wa Balaamu..wanaoonekana nje ni watu wa Mungu kumbe ndani ni mbwa-mwitu wa kali…Hao watakwambia kuoa mke wa pili si dhambi, watakwambia kuziangukia sanamu na kuzibusu na kuzipa heshima sio kuzisujudia.

Na biblia imeshatabiri nyakati hizi za mwisho watu wengi wataangukia katika kosa hili la Balaamu..

Yuda 1:11 “Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya Kora”.

Watakwambia kufanya matambiko ya ukoo sio dhambi, watakuwambia kuishi na mwanamke/mwanamume ambaye hamjaoana hakuna tatizo, watakuwambia kuzini ni mapungufu ya kila mtu, watakuweka katika kila kishawishi cha wewe kufanya dhambi, , Zaidi sana watakufariji katika dhambi na watakukemea katika kuwa mtakatifu…lengo na madhumuni ni kukukosesha wewe na Mungu wako ili Mungu akukasirikie na kukuangamiza (Huo ndio uchawi mkubwa shetani anaowalogea watu wa Mungu kuliko hata ule wa vibuyu)..

Bwana Yesu alisema maneno hayo Dhahiri katika Ufunuo.

Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini”.

Je! Na wewe umedanganyika na uchawi huo wa Balaamu? Nabii wa uongo?..Unadhani shetani anahangaika na bati lako usiku na kundi lake la wachawi?..usidanganyike!..anahangaika sasa kukukosesha na Mungu wako. Hataki ulifahamu neno na anafanya juu chini ufe katika dhambi zako ili siku ile uingia katika adhabu ya hasira ya Mungu katika ziwa la moto. Hivyo mwache aende peke yake huko yeye na mabalaamu wake, sisi tujitenge na yeye kwa kutubu leo na kushika amri za Mungu na Neno lake, kwa kujitenga na uasherati wote, wizi, rushwa, anasa, tamaa mbaya, wivu, matusi, na mambo yote machafu na kuzidi kujitakasa kila siku, na kuishi katika utakatifu ndipo tutakapojiepusha na ghadhabu ya Mungu na kupata baraka zote alizozikusudia katika Maisha yetu. Hatuna haja ya kuogopa wachawi wa vibuyu kwasababu huko waliko wanakiri kwamba hakuna uchawi wala uganga kwa waliokoka..

Sisi tupambane kujilinda na dhambi ndilo jukumu tulilolonalo sasa.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.

WAKAMTUKANA MUNGU, WALA HAWAKUTUBU.

NENO NI LILE LILE, LAKINI UJUMBE NI TOFAUTI.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

JINA LA MUNGU NI LIPI?

Rudi Nyumbani:

ByAdmin

UKADHANI YA KUWA MIMI NI KAMA WEWE.

Nakusalimu katika jina kuu la mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima..

Kwanini mara nyingine tunakuwa ni wepesi kufanya dhambi, ni wepesi kuwasengenya majirani zetu, ni wepesi kwenda kuzini, licha ya kwamba tunasema tumeokoka, au tupo karibu na Mungu, lakini bado ni wepesi kutazama picha chafu mitandaoni na kufanya masturbation….

Ni kwasababu tunamdhania Mungu yeye ni kama sisi, kwamba anaelewa tu! Ni madhaifu ya kawaida ya mwili..Na kibaya Zaidi pale tunapoona Mungu hachukui hatua yoyote ya adhabu katika ouvu tulioufanya, pengine pale tulipoenda kutazama picha chafu mitandaoni halafu Mungu akakaa kimya, halafu kesho yake tena tukarudia jambo hilo hilo na bado akawa yupo vilevile, hakuna lolote baya amelifanya katika Maisha yetu, kesho kutwa tena tukaenda kuzini, jambo likawa vilevile, kanisani tunahudhuria, kwaya tunaimba, maombi tunafanya, wala hakuna shida yoyote, wiki ijayo tukaanza kuwazungumizia vibaya majirani zetu, tulikuwa hatuli rushwa wala hututoi rushwa lakini tulipoanza kula rushwa na tukaona hakuna jambo lolote baya lililotukuta basi ndio ikawa desturi yetu kufanya hivyo, licha ya kuwa unasema ni mkristo.

Imekuwa hivyo hivyo miaka nenda miaka rudi, unawaza moyoni na kusema “hata Mungu anaelewa mambo haya”, ndio maana haniadhibu kwa lolote, Unadhani yeye ni kama wewe, Unadhani anavyowaza juu ya maovu ni kama wewe unavyowaza, unamchukulia kama mtu mwenzako asiyeweza kujali mambo madogo madogo kama hayo, unadhani kuwa hawezi kukuacha, wala kukuadhibu kwa vitu kama hivyo..

Lakini leo sikiliza Neno la Mungu linavyosema..

Zaburi 50:16 “Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia, Una nini wewe kuitangaza sheria yangu, Na kuliweka agano langu kinywani mwako?

17 Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.

18 Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, Ukashirikiana na wazinzi.

19 Umekiachia kinywa chako kinene mabaya, Na ulimi wako watunga hila.

20 Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia.

21 NDIVYO ULIVYOFANYA, NAMI NIKANYAMAZA; UKADHANI YA KUWA MIMI NI KAMA WEWE. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako.

22 Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya”

Angalia tena ule mstari wa 21 anasema.. “Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza; ukadhani ya kuwa mimi ni kama wewe”…Unaona, Mungu anapokaa kimya kutokana na dhambi zako unazozifanya kwa siri, usidhani yeye anakufurahia tu!.. Unasema umeokoka na huku unayo mambo yako ya siri ambayo unajua kabisa ni machukizo kwa Mungu, lakini Mungu hakusemeshi kwa lolote na wewe umestarehe tu, unadhani Mungu ni kama wewe, ataendelea na wewe hivyo siku zote..La! Anasema atakurarua na asipatikane mtu wa kukuponya..

Hasemi atakupiga tu, halafu basi au atakuadhibu, hapana anasema atakurarua..Na unajua anayerarua ni mnyama mkali kama vile simba, maana yake ni kuwa atakuharibu vibaya sana, kiasi cha kwamba hutaweza kusimama tena baada ya hapo, hata uombeweje, au uhubiriweje, hutaweza tena kusimama…Ndio maana anasema hapo “asipatikane mtu wa kukuponya”

Na ujumbe huo Mungu anausema kwa wale wote wanaomsahau..Inamaanisha kuwa hapo mwanzo walishawahi kuwa wake, lakini wakamzoelea wakamwona kama yeye ni kama wao, wakawa hawaogopi tena kufanya dhambi mbele zake..

Ndugu ikiwa wewe ni mmojawapo, Basi wakati wako wa kutubu kwa kumaanisha ndio huu, pengine umebakisha kipindi kifupi sana kukumbana na makucha hayo ya Mungu (Usitafute kuujua upande wa pili wa ghadhabu ya Mungu, kwasababu inatisha sana).. Ikiwa unafanya dhambi kisirisiri za kujirudia rudia ambazo hazimpendezi Mungu, na umekuwa ukizifanya kwa muda mrefu sasa na Mungu amekaa kimya tu, ni heri usiendelee kuzifanya, kwasababu kwa kukaa kwake kimya hivyo usidhani yeye ni kama wewe..

Hivyo chukua hatua sasa ya kuuimarisha wokovu wako, na Mungu atakusamehe na kuiahirisha ghadhabu yake kwako.

Kumbuka hizi ni nyakati za mwisho, hakuna haja ya kuthibitishiwa tena kuwa tunaishi katika majira ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hali halisi yenyewe inaonekana kwa mambo yanayoendelea sasa hivi duniani, hivyo huu si wakati wa kuweka mguu mmoja kwa Kristo na mwingine nje, huu ni wakati wa kuzama moja kwa moja kwa Bwana, kwasababu UNYAKUO sasa ni wakati wowote.

2Petro 1:10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI NEEMA YA MUNGU ILIVYOKUWA KUBWA KWA MKE WA LUTU.

MUNGU WETU, JINSI LILIVYO TUKUFU JINA LAKO DUNIANI MWOTE!

 

KWANINI UNAPASWA UJIWEKE TAYARI SASA, KABLA YA ULE WAKATI KUFIKA?.

KWA VILE ALIVYOKUWA MTU WA HAKI.

KRISIMASI (CHRISTMAS) NI NINI? JE IPO KATIKA BIBLIA?

Mitume wote waliopita walikuwa ni watu weupe hata manabii wote waliopita hadi Ma-papa ni ngozi nyeupe. ni kweli ngozi nyeusi ililaaniwa ?

Rudi Nyumbani:

ByAdmin

PASAKA NI NINI? NA JE TUNARUHUSIWA KUSHEHEREKEA PASAKA?

Pasaka ni nini kibiblia?, na je tunaruhusiwa kusheherekea pasaka sisi wakristo kama wayahudi?

Pasaka ni neno la Kiswahili ambalo limetokana na neno la kigiriki “pascha” ambalo tafsiri yake kwa lugha ya kiingereza ni “passover” kwa Kiswahili  ni “pita juu”. Hivyo pasaka kwa Kiswahili tunaweza kusema tafsiri yake ni “pita juu au vuka upite”.

Asili ya Neno hili ni siku ile wana wa Israeli walipokuwa wanatolewa kutoka Misri, usiku ule ambao ndio walikuwa wanatoka Misri, Bwana Mungu aliwaagiza wasitoke nyumba zao kwamba mpaka watakapomchinja yule Mwanakondoo na damu yake kuipaka katika miimo miwili ya Milango…ili wakati yule malaika ambaye alitumwa kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza wote wa wanadamu na wanyama waliokuwepo katika Misri nzima..atakapopita katika kila nyuma na kuiona damu hiyo ya mwanakondoo kwenye miimo ya mlango basi hataingia katika nyumba hiyo kumharibu mzaliwa wa kwanza wa nyumba hiyo “ATAVUKA JUU, AU ATAPITA JUU” Kuendelea na nyumba nyingine…na atakapofika katika nyumba nyingine na kukuta damu juu ya miimo ya mlango kama nyumba ya kwanza vile vile ATAPITA JUU na kuendelea mpaka atakapokuta nyumba ambazo hazina damu hiyo, ndipo ataingia na kuangamiza.

Kutoka 12:12 “Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana.

13 Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, NITAPITA JUU YENU, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri”.

Hivyo hicho kitendo cha kuvuka na KUPITA JUU ndicho kinachoitwa Passover, kwa kigiriki Pascha, kwa Kiswahili PASAKA.

Sasa katika Agano jipya damu ya mwanakondoo yule ndio inayofanananishwa na damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Sisi tuliokuwa dhambini tulipotolewa dhambini(yaani Misri yetu) na tunapoelekea nchi yetu ya ahadi mbinguni…Damu ya Yesu ndiyo iliyotuokoa la laana ya Mungu dhidi ya watu wote walio katika dhambi..Na damu ya Yesu ni ishara ya Agano kwamba kwa kupitia damu yake tunalindwa na hukumu ya Mungu..Hukumu ya Mungu inapoachiliwa au itakapoachiliwa tutakuwa tumefunikwa chini ya damu ya Yesu na Malaika yule wa hukumu ATAPITA JUU YETU, na tutanusurika na hukumu ya Mungu.

Swali ni Je tunaruhusiwa kusheherekea pasaka kama watu wengine?

Tafsiri ya kusheherekea kibiblia ni tofauti na tafsiri ya kusheherekea kama inavyotafsiriwa na ulimwengu. Tafsiri ya sherehe kwa ulimwengu ni kula, na kunywa na kulewa, na kwenda kujiburudisha, kujifurahisha, kufanya uasherati, kujisisimua na kufanya anasa na kufanya kila aina ya mambo ya kimwili.

Lakini kibiblia tafsiri ya kusheherekea sio hiyo…Hata wayahudi wahakushehereka Pasaka kwa hivyo…Kibiblia, kusheherekea ni kujiweka katika ibada, na ibada sio kwenda kanisani tu..bali kujinyenyekeza na kujishusha chini ya uwepo wa Mungu, kwa kuomba, kusali, na kuzidi kujitakasa mbele zake huku tukikumbuka kuwa kwa tukio kama hili lililowahi kutokea miaka mingi iliyopita Bwana alitupa wokovu kwa kupitia damu yake pale Kalvari. Hivyo ni wakati wa kumwekea Bwana nadhiri,  wakati wa kuishiriki meza ya Bwana katika vigezo vya kimaandiko, ni wakati wa kusamehe Zaidi (sio kwamba sasa hatupaswi kusamehe mpaka siku ya pasaka ifike, hapana! tunasamehe kila siku, siku hiyo ikifika ni kumalizia tu kuvisafisha vile vidogo ambavyo tulikuwa hatujavimalizia), kwasababu utakatifu sio tu siku ya pasaka hapana bali kila siku!, siku hiyo ni kumalizia tu kuvisafisha vile vichache ambavyo vilikuwa vimesalia. Hivyo hiyo ndiyo tafsiri ya sherehe. Tukisheherekea kwa namna hiyo kuna amani fulani na furaha ya ajabu ambayo Mungu anaimimina ndani yetu..

Lakini tukishehereka kidunia kwamba ndio siku ya kutafuta kwenda disko, ndio siku ya kwenda kulewa, ndio siku ya kuvaa nguo za nusu-uchi na kutembea nazo barabarani, kwamba ndio siku ya kwenda kwenye dansi,  n.k..Tutakuwa tumejitafutia laana badala ya Baraka..Tutakuwa tumeshirikiana na shetani asilimia mia kuudhihaki na kuuzalilisha msalaba wa Kristo, na damu yake ya thamani. Hivyo tutakuwa tumejiharibia wenyewe. Lakini tukishehereka kibiblia tutapata baraka.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

Je! mtu anapofunga kwa muda wa SAA 24,anapaswa kunywa maji au kitu chochote?

SALA YA ASUBUHI

UTHABITI WA AGANO LA MUNGU KWA MKRISTO.

KIJITO CHA UTAKASO.

Kiungo chako kimoja kikikukosesha kikate.

Kiungo chako kimoja kikikukosesha kikate.

CHAPA YA MNYAMA

Rudi Nyumbani:

ByAdmin

Biblia inamaanisha nini inaposema “Tusitweze unabii”?

SWALI: Nini maana ya  “Tusitweze unabii”?


JIBU: Tusome..

1Wathesalonike 5:19 “Msimzimishe Roho;

20 msitweze unabii;

21 jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema;

22 jitengeni na ubaya wa kila namna”.

Maana ya neno “kutweza” ni kudharau au kupuuzia jambo fulani…Hivyo biblia inaposema msitweze unabii maana yake ni “msiudharau/msiupuuzie unabii”..Na unabii unaozungumziwa hapo ambao haupaswi kutwezwa (maana yake haupaswi kudharauliwa/kupuuziwa)..ni unabii wa kurudi kwa Bwana mara ya pili.. ambao Mtume Paulo aliwaonya Wakristo hao waliopo Thesalonike mwanzoni kabisa mwa sura hiyo ya tano(5). Tusome..

1 Wathesalonike 5:1 “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie.

2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.

3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.

Huu ndio unabii wa kwanza ambao haupaswi kupuuziwa hata kidogo, na haukuandikwa kwa Wathesalonike tu peke yao, bali hata kwetu sisi, kwasababu ndio tunaoishi ukingoni mwa nyakati kabisa kuliko vizazi vyote vilivyotangulia. Ukisoma sura yote ya 5 hiyo ambayo ndio ya mwisho kabisa ya kitabu hicho cha 1Wathesalonike utaona jinsi biblia inavyotuonya kwa msisitizo mkubwa kujiweka tayari na siku hiyo ya kurudi kwa pili kwa Kristo, Kwamba siku hiyo inakuja kama mwivi na tusilale usingizi kama wengine walalavyo, na TUSIUUPUUZIE WALA KUUDHARAU HUO UNABII…Kwasababu ni kweli siku hiyo yaja na Mungu hawezi kusema uongo…wote wanaoudharau huo unabii siku hiyo itawajia kama mwivi na kutakuwa na maombolezo makubwa na majuto makubwa, watatamani warudishwe dakika tano nyuma warekebishe mambo yao, lakini itashindikana.

Na hautwezwi kwa midomo tu bali matendo pia…Mtu ambaye hajajiweka tayari kwa kumwamini Yesu Kristo na kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha, na kuishi kulingana na Neno la Mungu, ingawa kila siku anasikia injili lakini anapuuzia mtu huyo ANAUTWEZA UNABII, hali kadhalika mtu ambaye kila siku anasikia habari za kurudi kwa Kristo mara ya pili na anadhihaki na kudharau na kuwaona wanaomgoja Bwana ni watu waliorukwa na akili, na wanaopoteza muda wao, au wamepoteza dira ya Maisha, huyu naye anafanya dhambi hiyo hiyo ya kuutweza unabii ambapo siku moja atajuta majuto makuu na hatapata nafasi ya kurekebisha mambo yake, na mambo hayo yatakuwa hivi karibuni, moja ya hizi siku hii dunia itakuwa si dunia tena..

Vilevile Na unabii mwingine wowote wa kwenye biblia sio wa kuudharau kabisa, kwasababu kila alilolisema Bwana lazima litatimia.

Hivyo kama hujaokoka, saaa wokovu ni sasa, sio baadaye wala kesho..Tubu sasa na Kristo atakusamehe bure kama alivyoahidi.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

IELEWE SAUTI YA MUNGU.

MUNGU WETU, JINSI LILIVYO TUKUFU JINA LAKO DUNIANI MWOTE!

MAMBO MANNE,YANAYODHOOFISHA UOMBAJI WAKO.

Rudi Nyumbani:

ByAdmin

MWACHE YESU, NDIO AWE WA  KWANZA KUKUHURUMIA.

Siku zote mwache Yesu, ndio awe wa  kwanza kukuhurumia!.

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo.

Ni jambo la kawaida kila mmoja wetu kuijali kwanza hali yake binafsi, na si dhambi kufanya hivyo, japo hilo halitufanyi tuonekane kuwa wa maana sana mbele za Mungu.. Kuna wakati Bwana Yesu aliitisha mkutano mkubwa sana, pengine eneo la mjini lilikuwa ni dogo la kuuketisha umati mkubwa wa watu, au pengine palikuwa na usumbufu fulani ambao ungewafanya watu wasimsikilize vizuri, Hivyo akaamua kuwaitisha eneo la mbali kidogo na mji, mahali ambapo hapana makazi ya watu, eneo la nyika tupu,..mahali ambapo hakuwaandalia mahema ya kukutania wala hakuwachagulia penye miti mingi, ambapo walau wangekaa chini yake wapate uvuli, bali alichagua eneo la jangwa lenye nyika tupu.

Na mkutano huo ulikuwa ni Mkutano wa siku tatu..

Lakini biblia inatuambia wengi waliposikia habari ile wakatoka mbali sana, wakaenda eneo hilo la jangwa ili kwenda kuyasikiliza maneno ya uzima ya Bwana Yesu,..Watu wale walifikia pengine asubuhi sana na mapema, wakijua kuwa siku zote tatu zitakuwa ni siku za kufunga, za kumsikiliza tu Bwana Yesu si vinginevyo, hivyo walifika mahali pale wakilijua hilo asubuhi sana, wakakaa chini kwenye jua lile, kuanzia asubuhi mpaka jioni,..

Jaribu kutengeneza picha, masaa 12 ya mchana wanamsikiliza tu Bwana Yesu akiwafundisha, na usiku vivyo hivyo.. siku ya kwanza, siku ya pili, mpaka siku  tatu zinakwisha, wamekaa tu pale, nyikani wakimsikiliza Bwana Yesu kwa makini bila kuondoa miguu yao, huku njaa zikiwauma, lakini waliona kile wanachokisikiliza ni Zaidi ya chakula cha mwilini.. Walijua mtu hawezi kuishi kwa mkate tu, bali kwa kila Neno linalotoka katika kinywa cha Bwana..

Embu tengeneza tena picha Bwana alikuwa anajua kabisa watu wale, walikuwa katika hali ngumu kweli kweli katika eneo lile la ukame na jua kali, alijua kabisa walikuwa hawajala kwa muda wa masaa mengi sana, alijua kabisa hali zao zinakaribia kuwa mbaya..lakini aliendelea kuwafundisha bila kuwahudumia kwa lolote, kwasababu aliona utayari wao wa kumsikiliza yeye bila kuchoka, mpaka siku tatu kamili zilipokwisha..

Lakini siku ile alipomaliza kuwafundisha, biblia inatuambia Bwana Yesu hakuwaacha hivi hivi waondoke waende zao katika hali zile za njaa bali aliona umaskini wao, aliona njaa zao, aliona mateso yako, aliona kiu yao, aliona mahitaji yao na pale pale  maandiko yanatuambia AKAWAHURUMIA ..embu tusome:

Marko 8:1 “Katika siku zile, kwa vile ulivyokuwa mkuu tena ule mkutano, nao wamekosa kitu cha kula, akawaita wanafunzi wake, akawaambia,

2  NAWAHURUMIA MKUTANO kwa sababu yapata siku tatu wamekaa nami, wala hawana kitu cha kula;

3  nami nikiwaaga waende zao nyumbani kwao hali wanafunga, watazimia njiani; na baadhi yao wametoka mbali.

4  Wanafunzi wake wakamjibu, Je! Ataweza wapi mtu kuwashibisha hawa mikate hapa nyikani?

5  Akawauliza, Mnayo mikate mingapi? Wakasema, Saba,

6  Akawaagiza mkutano waketi chini; akaitwaa ile mikate saba, akashukuru, akaimega, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; wakawaandikia mkutano.

7  Walikuwa na visamaki vichache; akavibarikia, akasema wawaandikie na hivyo pia.

8 Wakala, wakashiba, wakakusanya mabaki ya vipande vya mikate makanda saba.

9  Na watu waliokula wapata elfu nne. Akawaaga”.

Unaona hapo?..Walipaswa waondoke vile vile, lakini kwa jinsi alivyoona “WAMEKAA NAYE” siku zote tatu bila kuondoka uweponi mwake, bila kwenda kuhangaika hangaika kuyajali maisha yao, familia zao, biashara zao, miradi yao, ili wapate chakula wao na Watoto wao, badala yake wamedumu pamoja naye kwa siku kadhaa bila kuchoka..basi tukio hilo lilimfanya Bwana Yesu AWAHURUMIE hata kwa yale mengine waliyoyakosa..

Na kama tunavyosoma kitu gani kilifuata.. Wote walishibishwa mikate wakiwa pale nyikani, wakapata na ya kuondokea, mpaka ikabaki na wale samaki vivyo hivyo…Sasa unaweza ukafikiri Bwana Yesu aliwashibisha pale tu…La! Alikuwa anawadhihirishia kuwa baada ya pale na Maisha yao pia yatabarikiwa kwa mfano ule ule wa vikapu, na wala hawatapungukiwa kabisa…Lakini hiyo yote ilikuwa ni kwasababu ya yale maneno ya uzima waliokuwa wanayasikia bila kuchoka ndio yakazaa vikapu vile vya mikate na baraka walizoziendea baada ya pale.

Na sisi tujiulize Je tunaweza kufikia hatua kama hii ya hawa watu?…Je tunaweza kuwa tayari kufunga kutokula kwa ajili tu ya kuutafuta uso wa Bwana kwa kipindi kirefu?, Je tunaweza Kufunga mihangaiko yetu, na shughuli zetu tukatenga wakati wa kuhudhuria ibada na semina ndefu za Neno la Mungu?..kwa kutokujali eneo lenyewe, kutokujali mazingira yanaruhusu kiasi gani, kutokujali umbali, kutokujali hata uzima wako na afya yako?.. Ikiwa tu tutaalikwa mahali ambapo tumewekewa mahema, chini kuna vivuli, lakini bado hatutakwenda ikiwa tunayo makanisa mazuri tena mengine yana feni lakini hatuwezi kukaa hata masaa 2, Je tutawezaje ikiwa tutalikwa mahali penye njika tupu kama pa hawa watu?..Na wakati huo huo bado tunataka Bwana Yesu azihurumie hali zetu,?

Mungu anatuambia tumkaribie yeye na yeye atatukaribia sisi (Yakobo  4:8)..Hivyo tukiwa hatupo tayari kujinyima nafsi zetu na kujitesa katika kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii, katika kuutafuta ufalme wake na haki yake, basi tujue itakuwa shida sana kuyaona matendo makuu ya Mungu maishani mwetu.

Usikazane kutafuta kujihurumia kwanza wewe unapoutafuta uso wa Mungu, subiri kwanza mwache Yesu akuhurumie yeye..jukumu letu ni kuutafuta uso wa Mungu kwa bidii mengine tumuachie yeye, kwasababu anajua shida zetu, na mahitaji kabla hata sisi hatujamwambia. (Mathayo 6:32).

Bwana atusaidie katika hilo. Na atujalie tuchukue hatua zinazostahili katika hilo.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MIILI YA UTUKUFU ITAKUWAJE?

USIWE NA HOFU, USHUKAPO CHINI.

MUNGU AKIKUPITA LEO, HAIMAANISHI KUWA HAJAKUCHAGUA.

MAMBO MANNE,YANAYODHOOFISHA UOMBAJI WAKO.

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

SAKRAMENTI NI NINI, NA JE! IPO KATIKA MAANDIKO?

Rudi Nyumbani:

ByAdmin

KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.

Kipindi kifupi kabla ya ghadhabu ya Mungu kumwagwa juu ya dunia, biblia imetabiri kuzuka kwa mambo ya ajabu sana na ya kutisha ulimwengu…na mambo hayo yapo mengi ikiwemo kuzuka kwa manabii wa uongo na makristo wa uongo, lakini pamoja na hayo yapo mengine matatu ya muhimu, ambayo ni …1) VITA 2) TAUNI na 3) NJAA.

Luka 21:10 “Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; 11 kutakuwa na MATETEMEKO MAKUBWA YA NCHI; NA NJAA NA TAUNI mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni”.

Kama tujuavyo mgonjwa kabla hajaanza kuumwa anakuwa anaanza kuonyesha dalili kwanza, labda ataanza kusikia kichefuchefu na baadaye akawa sawa, muda kidogo atasikia kichwa kinamuuma lakini si sana..na baadaye tena homa lakini si sana..kiasi kwamba anaweza akazivumilia dalili zile na kuendelea na shughuli zake kipindi cha mwanzoni..na wakati mwingine hata akajisikia nafuu kabisa kana kwamba haumwi tena….

Lakini siku ikifika yenyewe ambapo ugonjwa ule utanyanyuka..huo ndio wakati ambao kila siku kwake itakuwa ni afadhali na jana kuliko leo…zile dalili alizokuwa anazisikia mwanzo, kama kichwa kuumwa kidogo, homa kidogo, sasa vinazidi na kujizidisha na kuwa vikali mara nyingi zaidi..hapo atasikia kichwa kikiumwa hata mara kumi ya kile alichokuwa anakisikia hapo mwanzo..Homa inajizidisha mara nyingi kuliko mwanzo na mara nyingine anajikuta anaishia tu kalala kitandani. Mtu anapofikia hali ya kuumwa kiwango hiki huwa anatamani hata afe atokane na mateso hayo.

Sasa mambo hayo yanafananishwa na siku za maangamizi ya dunia zitakavyokuwa …Wengi wetu hatujui nini maana ya dalili ya siku za mwisho…Dalili maana yake ni mwanzo wa kitu…Hivyo biblia inavyosema kuwa dalili za siku za mwisho ni hizi au zile, inamaanisha kuwa mwisho wa siku mambo yatakuwa ni mabaya kuliko hata mwanzo.

Sasa Bwana Yesu alisema dalili mojawapo ya siku za mwisho ni kuwepo kwa matetemeko makubwa ya nchi(Luka 21:11)…maana yake ni kwamba siku yenyewe ya mwisho wa dunia ikifika kutakuwepo na tetemeko kubwa lisiloelezeka mara nyingi zaidi ya yale ya dalili..

Kadhalika Bwana Yesu alivyosema kwamba vita ni dalili mojawapo ya siku za mwisho, maana yake ni kwamba Siku yenyewe ya mwisho wa dunia ikifika kutakuwa na vita kubwa na kali na ya ajabu ambayo haijawahi kutokea, ambayo madhara yake hayajawahi kufananishwa na vita yoyote huko nyuma..na vita hiyo itakuwa si nyingine zaidi ya vita vya Har -magedoni.Kama hizi vita zilizopo sasa tumezoea kusikia watu elfu kadhaa wamekufa..vita hiyo ya mwisho ya Harmagedoni itamaliza mamilioni ya watu.

Pia alisema dalili nyingine ni NJAA, na njaa hiyo inasababishwa na kukosekana kwa mvua na kunyanyuka kwa wadudu wanaoharibu mazao kama nzige waliotokea wakati wa Farao, na waliopo sasa..Siku ya kuharibiwa dunia Itatokea Njaa ambayo haijawahi kuwa mfano wake…Baada ya watu kuifurahia chapa ya mnyama kwa kitambo..Mungu ataipiga dunia nzima kwa njaa..ambapo maji yote yatageuka kuwa damu na mifereji na mito..na mvua itaacha kunyesha(Ufunuo 16:4-6).

Kadhalika Bwana Yesu alisema dalili nyingine ya siku za mwisho ni KUZUKA KWA MAGONJWA MABAYA ambayo yanafanishwa na Tauni kibiblia(Luka 21:11)...magonjwa hayo yatakuwa hayana tiba na yanayoambukiza kwa kasi…Dalili za magonjwa hayo zimeanza kuonekana tangu mwanzo mwa karne ya 21, na mpaka kufikia sasa yameshaongezeka idadi..Kama ijulikanavyo kuna ugonjwa sasa unaoitwa Corona ulimwenguni.. Ugonjwa huu ni dalili tu (mwanzo wa utungu)..ambapo siku yenyewe ya mwisho ikifika ambayo inaweza kuwa hata leo..utazuka ugonjwa mpya ambao utakuwa ni mbaya kuliko huu uliopo sasa…utakuwa ni ugonjwa wa virusi mfano wa huu wa sasa…

Ugonjwa huu utashambulia ngozi na kusababisha majipu ya vidonda ambavyo vinaoza(Biblia inasema majipu yake yatakuwa ni mabovu, maana yake ni ya kuoza) na utakuwa unateseka kwa muda mrefu..Utakuwa ni tofauti na huu uliopo sasa ambao baada ya siku kadhaa mtu anaweza kupona…ugonjwa huo wa majipu utakuwa hauna tiba na wala hautakuwa unapona wenyewe, utampata kila mtu ambaye atakuwepo ulimwenguni wakati huo…

Ufunuo 16: 2 “Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake”.

Mambo haya sio hadithi bali ni mambo ambayo yatakuja kutokea dhahiri kabisa. Siku za ugonjwa huo jua litashushwa pia na kuwaunguza wanadamu wote wenye ugonjwa huo, duniani kutakuwa sio sehemu ya kuishi tena..kila mtu atakuwa kivyake akiugulia na kuteseka kivyake vyake kutakuwa hakuna hospitali itakayopokea wagonjwa kwasababu hata wauguzi wenyewe watakuwa na ugonjwa huo..(Hiyo itakuwa sio siku za dalili tena bali ya ugonjwa wenyewe, dalili ni wakati huu wa sasa).. Unyakuo upo karibu sana kutokea!..Kwasababu kabla ya siku hizo..watakatifu watanyakuliwa kwanza.

Ishara za magonjwa haya ni kutuonyesha kuwa Hukumu tayari imeshatamkwa juu ya ulimwengu..kama vile ambavyo ugonjwa unavyomwingia mtu..na hatua za kwanza ni dalili..na sasa tupo katika dalili ya ghadhabu ya Mungu. Hii hofu iliyopo sasa si hofu, hofu hasaa itakuja wakati huo wa mapigo hayo ya Mungu.

Ni nini kifanyike sasa? Katika hatua hii ya dalili?

Kinachopaswa kufanyika sasa ni kujiweka tayari tu…Tunajiwekaje tayari?..ni kwa kutubu, kujiosha mioyo yetu, kuacha dhambi na kuzidi kujitenga na ulimwengu kila siku… Kuacha kuziabudu sanamu na kuzisujudia , Kuacha ulevi, kuacha rushwa, kuacha wizi, kuacha matusi, kuacha kutazama picha za ngono, uasherati, kuacha kwenda ma disko, kuacha kuvaa nguo za kuonyesha maungo, na vimini na suruali kwa wanawake….mambo haya ndiyo yanayoisukuma ghadhabu ya Mungu imwagike haraka ulimwenguni na juu yako wewe..ni kama mgonjwa ambaye tayari kashaanza kuonyesha dalili, halafu bado hazingatii tiba..pasipo kujua kuwa ndio anazidi kujiharibu na kuuvuta ugonjwa zaidi..

Wakolosai 3: 5 “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; 6 kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu”.

Umeona mstari wa 6, usemavyo?… “kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu”..Soma tena..

Waefeso 5:5 “Maana neno hili mnalijua hakika, ya kwamba hakuna mwasherati wala mchafu wala mwenye tamaa, ndiye mwabudu sanamu, aliye na urithi katika ufalme wa Kristo na Mungu.

6 Mtu asiwadanganye kwa maneno yasiyo na maana; kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi”.

Unaona tena? mstari wa mwisho huo wa 6.. “kwa kuwa kwa sababu ya hayo hasira ya Mungu huwajia wana wa uasi”

Hiyo pekee ndiyo njia ya kujikinga na kujiepusha na ghadhabu ya Mungu…

Utauliza kutokana na tatizo hili lililopo sasa…je ! ni sahihi kunawa mikono na kutosalimiana na mtu kwa kushikana mikono njiani?

Kama tunavyoambiwa ni wajibu wa kila mtu kusimama pindi wimbo wa Taifa unapoimbwa…na wakristo pia wanatii agizo hilo..Hivyo na agizo la kunawa mikono popote tufikapo, tuingiapo na tutokapo wakristo tunatii bila shuruti kwasababu hakutupunguzii chochote katika Imani yetu…Tukijua ya kwamba mioyo yetu tayari imeoshwa kwa sabuni ya kimbinguni (Damu ya Yesu)..Na tumaini letu halipo katika maji na sabuni za mwilini bali katika maji na damu ya Yesu Kristo. Hiyo ndiyo inayotutakasa na kutulinda na kutuepusha na ghadhabu ya Mungu. Hivyo hatuna hofu, na hatuogopi kwasababu tunamtegemea Bwana, wakati ulimwengu unaogopa magonjwa, na njaa na vita sasa…sisi tunaigopa dhambi tu!..

Zaburi 125:1 “Wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, Ambao hautatikisika, wakaa milele.

2 Kama milima inavyouzunguka Yerusalemu, Ndivyo Bwana anavyowazunguka watu wake, Tangu sasa na hata milele”.

Lakini kama tukinawa mikono na mwili mzima mahali popote tuingiapo na tutokapo na huku mioyoni mwetu bado kuna uasherati, bado kuna wivu, hasira, wizi, ufisadi, ibada za sanamu, rushwa, na ulevi hakuna chochote tunachoweza kuepuka…Maji na sabuni na mlo kamili kamwe haviwezi kutuepusha na ghadhabu ya Mungu…Havijawahi katika agano la kale na hata katika agano jipya.

Hivyo kwa hitimisho kama hujampa Yesu Kristo maisha yako, Hizi ni siku za mwisho..huhitaji kuhadithiwa na mtu tena..leo hii ile mipira uliyokuwa unajitumainisha nayo kuwa itakupatia faraja iko wapi? Kule kubet ulikokuwa unajitumainisha nako kuko wapi?…Zile visa na zile biashara zako ambazo ulikuwa unajitumainisha nazo unazifanya ulimwenguni kote ziko wapo leo?, elimu unayojitumainia iko wapi?, disko unayojitumainishia nayo iko wapi? Katika mataifa makubwa zimeshafungwa labda na kwako inaweza kuwa hivyo siku sio nyingi, wale waliokuwa wanakuambia kwamba dunia haitafikia mwisho wako wapi leo?..Uliwahi kufikiri kwamba ingetokea siku moja miji mikubwa mikubwa ingekosa watu barabarani?, mashule mengi ulimwenguni yangefungwa?,

umewahi kutafakari kwamba siku moja ingefika mamilioni ya watu hawataruhusiwa kwenda kazini wala makanisani?..Naam Hali inaweza kurudi kama kawaida na maisha yakarudi kama mwanzo na hata zaidi ya pale..lakini je! Umejifunza nini?…bado upo tu nje ya safina?

Huu ni mwanzo tu kwamba tutubu kwasababu siku yenyewe… ikifika hata hii Neema ya kutubu na ya kusikia mahubiri haitakuwepo?….Siku yenyewe ikifika itakuwa haiwezekani kabisa hata kwenda kanisani, licha ya kutafuta mtu wa kukuhubiria, hata kwa njia ya mitandao halitapatikana…wanaohusika na mitandao watakuwa matatizoni, vituo vya satellite vyote vitafungwa…Chapa ya mnyama itakuwa inafanya kazi na kipindi kifupi baada ya kuipokea chapa hiyo magonjwa hayo yataanza..

Yeremia 28:7 “Lakini lisikilize sasa neno hili nilisemalo, masikioni mwako, na masikioni mwa watu wote, 8 Manabii waliokuwako kabla ya zamani zangu, na zamani zako, walitabiri juu ya nchi nyingi, na juu ya falme kubwa, habari ya vita, na ya mabaya, na ya tauni”.

Kabla ya dunia kufikia maharibifu hayo..waliokuwa ndani ya Kristo watakuwa wamenyakuliwa je utakuwa miongoni mwao?..

Kama hujatubu..Na upo tayari kufanya hivyo leo hii, Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, . NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji Mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ubarikiwe sana

Maran atha!

Mada Nyinginezo:

SIKU YA BWANA INAYOTISHA YAJA!

UFUNUO: Mlango wa 16.

NENO NI LILE LILE, LAKINI UJUMBE NI TOFAUTI.

MWISHO WA DUNIA UTAKUJAJE?

KWANINI UNAPASWA UJIWEKE TAYARI SASA, KABLA YA ULE WAKATI KUFIKA?.

Rudi Nyumbaani: