NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?

NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?

Kazi kubwa shetani anayoifanya kwa mkristo kila siku ni kutaka kumwangusha katika imani yake hivyo anatumia njia ya majaribu kumwangamiza, majaribu ni vikwazo, na kuna vikwazo vya aina nyingi katika safari ya ukristo ambavyo shetani lazima avilete na sio kila mtu atakutana navyo bali ni mkristo tu aliyeamua kujitoa kikamilifu na kumfuata YESU KRISTO kwa moyo wake wote.

kwahiyo shetani akishajua umechagua njia hiyo ndipo atakapoanza kuamua kukupepeta kwa njia zozote zile; anaweza akaja aidha kwa njia ya magonjwa, shida, mafarakano baina yako na watu wanaokuzunguka ili tu kuikana imani yako, au vikwazo vya nguvu za giza, mabalaa, ajali, mikosi, na vishawishi vya kukufanya utende dhambi zisizo za kukusudia, n.k.. haya yote shetani anayaleta kwa dhumuni tu la kukufanya wewe ulegee katika imani, au umkane Mungu, au uteseke na pengine ufe kabla hata hujamaliza kusudi lako uliloitiwa duniani, kumbuka mambo haya shetani anayalengesha kwa mkristo tu aliyeamua kusimama,

Tunaona Bwana YESU aliwaonya wanafunzi wake akiwaambia “makwazo hayana budi kuja”. Lakini pamoja na hayo alitoa njia ya kuweza kuyadhibiti, na ni kwa njia moja tu nayo ni kwa “KUOMBA”.

Tufuatilie mahali pengine alichowaambia wanafunzi wake:

Mathayo 26:40 ” Akawajia wale wanafunzi wake, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, je! hamkuweza kukesha pamoja nami hata SAA MOJA?.

41Kesheni, MWOMBE, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.

Tunaona hapo Bwana YESU aliwasisitiza wanafunzi wake waombe kwasababu majaribu mazito yalikuwa yanawangojea mbeleni, na ndio maana Bwana angali akiyaona hayo ya kwenda kupata mateso alimwomba Mungu amwepushe na kile kikombe cha majaribu, hivyo kwa kufanya vile japo lile jaribu halikuondolewa lakini alipewa nguvu ya kulishinda na ndio maana malaika walimtokea na kumtia nguvu, lakini kwa wale wengine (wanafunzi wake) ambao nao majaribu mazito yalikuwa yanawangojea walila wakidhani kuwa adui yao(shetani) na yeye alilala?. Lakini tunafahamu kitu gani kilichowatokea dakika chache baadaye, tunaona shetani alipomjaribu Petro alimkana KRISTO pale pale na wengine wote walikimbia na kujitenga na Bwana.

Lakini je! mfano wangekesha na BWANA kuomba wasiingizwe majaribuni, unadhani yale yote yangewatokea? La! Hakika Mungu angewaepushia pengine malaika angewaonya waondoke maeneo yale, au mazingira ya wanafunzi kushikwa na wale askari au mazingira ya Petro kutaka kumkana Bwana yasingekuwepo, na kama wangekaa kuomba na YESU wasiingie majaribuni hata kama wangeingia majaribu Mungu angewapa wepesi wa kushinda kama Bwana alivyopewa ule wepesi wa kushinda.

Na jambo hili hili linajirudia hata sasa hivi, kwa mkristo yoyote aliyesimama, wakati wewe umelala fahamu kuwa adui yako hajalala yupo nje anaandaa majeshi ya kukuangamiza wewe, unadhani kama yalimpata BWANA kwanini yasikupate na wewe?, kama alimwomba BABA amwepushe na majaribu inakupasaje wewe?. Na ndio maana hata tunaona pale alipowafundisha wanafunzi wake kusali aliwaambia hivi ” ..USITUTIE MAJARIBUNI, BALI UTUEPUSHE NA YULE MWOVU..” . Haya maombi ni muhimu sana katika maisha ya kila mkristo.

Na ukiwa kama mkristo ni muhimu kufahamu maeneo ambayo adui anapenda sana kutumia kukushambulia na hapo ndipo unapotakiwa kutilia mkazo katika kuomba Mungu atoweshe majeshi ya mwovu katika eneo hilo, yapo maeneo mengi mfano, mara nyingine shetani anaweza kutumia marafiki zako wa karibu au ndugu zako kudhoofisha imani yako unashindwa aidha kusoma NENO, au kuwa huru na imani yako au kusali, na unaona unaishi katika mazingira ambayo hayaepukiki kuwa na hao watu, hapo sasa unatakiwa umwombe BWANA awalinde ndugu zako dhidi ya yule mwovu asipate nafasi ya kuwatumia kuidhoofisha imani yako.

Au mara nyingine shetani anaweza kutumia wafanyakazi wenzako au maboss wako kukuharibu wewe uiache au uikosee imani yako, pengine hata kuikana, maeneo kama hayo ni vema ukeshe katika kuomba BWANA awafunike wafanyakazi wenzako shetani asiwatumie wao kama vyombo kwa kukujaribu wewe. Kwa kufanya hivyo utajikuta imani yako haisumbuliwi hata kama upo katikati ya watu wasioamini kiasi gani na hata kama ikitokea shetani akiruhusiwa kuwatumia kukujaribu wewe Mungu atakupa nguvu ya kuyashinda kama alivyompa Danieli hutaweza kumkana Mungu hata kama utatupwa katika tundu la simba, utashinda kama Bwana YESU hata kama ni kuwekwa msalabani, lakini ni kwanini ? ni kwasababu ULIMWOMBA BWANA AKUEPUSHE NA MAJARIBU.

Lakini usipokuwa mwombaji ndugu, hutaweza kumshinda shetani utabakia tu kutamka ushindi wa mdomoni lakini mwisho utaishia kuikana imani kama vile tu Petro, Kumbuka nia ya Petro ilikuwa kweli sio kumkana BWANA lakini kwasababu alikuwa hana nguvu ya kushinda majaribu alijikuta ameingia katika matatizo makubwa, na nguvu hii ingepatikana kwa njia ya MAOMBI TU!.

Na ndio maana Bwana alisema tuombe walau hata “SAA MOJA” kwa siku. Ni hatari sana kama wewe ni mkristo hata dakika 10 husali, si ajabu unaona ukristo ni mgumu kuuishi, mitego ya adui chungu nzima imetuzunguka, pasipo maombi tutawezaje kuishinda?. Wachawi hawalali wanakesha kila siku kuloga na kuilaani siku yako kwa BWANA, wewe unatakiwa uamke uibariki siku yako.

Utawezaje kushinda tamaa za uasherati, kama Yusufu kwenye maeneo yako ya kazi, au shule, au makazi unayoishi,? katika kizazi hichi cha uzinzi kama sio mwombaji?..NI WEWE AMBAYE UNASEMA KUWA NI MKRISTO.

Yakobo 4: 1″ Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu?.

2Mwatamani wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu KWA KUWA HAMWOMBI.

Hivyo ndugu ni muhimu kutenga walau SAA MOJA kila siku kuomba, kuibariki siku yako, yapo mambo mengi ya kuombea ipo familia yako,ukoo wako, jamaa zako na marafiki zako mwombe Mungu awalinde wasiwe vyombo vya shetani kukuangamiza Katika UKRISTO wako, ombea wakristo wenzako na watumishi wa Mungu shetani asipate nafasi ya kuliharibu kanisa, ombea taifa unaloishi pamoja na viongozi wake ili uishi kwa amani, wasikuingize majaribuni kumbuka usipofanya hivyo wanaweza hata kuibua sheria zilizotungwa kuzimu ushindwe kumwabudu Mungu wako kwa uhuru, ombea kazi yako, vyombo vyako vya usafiri, shule yako, n.k. shetani asivitumie kuharibu imani yako au uhusiano wako na Mungu.,

Wakati mwingine unajikuta muda wote upo buzy hujamaliza hili linazuka lingine, na hali hiyo inaendelea kila siku mpaka inasonga imani yako na uhusiano wako na Mungu, hayo ni majaribu unapaswa UOMBE Mungu ayaepushie mbali hayo majaribu ili shughuli za kidunia zisizoisha ziondoke mbele yako na upate Muda mwingi binafsi na Mungu wako.

Usipofanya hivyo ndugu shetani atakuwa amekushinda utafananishwa na ile mbegu iliyotupwa kwenye miiba, ilipomea shughuli,udanganyifu wa mali na masumbufu ya maisha hayo yakaisonga ikawa haizai(mathayo 13:22). Kwa nyanja zote hizi ukiomba hakika hautashindwa kumaliza saa moja.

Hivyo kwa wewe mkristo ni muhimu sana kumwomba Mungu akuepushe na Majaribu maadamu upo safarini, vikwazo na majaribu Bwana alituonya hatuna budi kukutana navyo na ni kwa MAOMBI tu! tunaweza kudhibiti.

OMBA WALAU SAA MOJA KILA SIKU.

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kwa msaada wa maombi/Ushauri/ubatizo/mafundisho/Whatsapp: Namba zetu ni hizi:

+255693036618/ +255789001312


Mada Nyinginezo:

MAOMBI KWA WENYE MAMLAKA

FAIDA ZA MAOMBI.

HATARI YA KUTOKUITAFAKARI BIBLIA VIZURI?

KWANINI MUNGU HAKUMUUA NYOKA MPAKA AKARUHUSU AJARIBIWE PALE BUSTANI NA EDENI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments