Title May 2024

MISTARI YA KUOMBEA AMANI YA FAMILIA.

UTANGULIZI: Neno la MUNGU ni DAWA, iponyayo Nafsi, Mwili na Roho.. Maombi yanayosimamiwa na Neno la MUNGU yanakuwa na nguvu kuliko yasiyo na msingi wa NENO, Hivyo wakati wa kuomba au kuombea jambo fulani, ni vyema Mwamini akawa na maandiko machache ya kusimamia wakati wa Maombi.

MAOMBI YASIYO NA NENO LA KUSIMAMIA ni kama BENDERA ISIYO NA MLINGOTI!!….Hivyo ni vyema kulijua Neno la kulitumia wakati wa Maombi.

        AMANI:

Ikiwa Amani imepungua au imepotea kabisa katika nyumba, ambapo inafikia hatua Baba haelewani na Mama, au wazazi hawaelewani na watoto, au watoto kwa watoto hawaelewani, vurugu imekuwa nyingi jambo ambalo hapo mwanzo haikuwa hivyo…. Na wewe kama Baba, au Mama, au Mtoto uliye na Kristo unaliona hilo na unatamani msaada kutoka kwa Baba wa mbinguni, kurejesha mambo yote yawe sawa.

Basi mistari ifuatayo inaweza kukufaa wakati wa maombi baada ya kuitafakari kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Zaburi 4:8 “KATIKA AMANI nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, Bwana, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama”.

Zaburi 29:11 “Bwana atawapa watu wake nguvu; Bwana ATAWABARIKI WATU WAKE KWA AMANI”.

Zaburi 122: 7 “AMANI NA IKAE NDANI YA KUTA ZAKO, Na kufanikiwa ndani ya majumba yako.

8 Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu Niseme sasa, AMANI IKAE NAWE”

Zaburi 147: 14 “Ndiye afanyaye AMANI mipakani mwako, Akushibishaye kwa unono wa ngano”

Ayubu 25:2 “Enzi na hofu zi pamoja naye; HUFANYA AMANI katika mahali pake palipoinuka”

Zaburi 35:27 “Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe Bwana, Apendezwaye na AMANI YA MTUMISHI WAKE”.

Zaburi 37: 37 “Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, MAANA MWISHO WAKE MTU HUYO NI AMANI”.

Zaburi 72:7 “Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, NA WINGI WA AMANI hata mwezi utakapokoma”

Zaburi 85:8 “Na nisikie atakavyosema Mungu Bwana, MAANA ATAWAAMBIA WATU WAKE AMANI, Naam, na watauwa wake pia, Bali wasiurudie upumbavu tena”.

Zaburi 85: 10 “Fadhili na kweli zimekutana, Haki na amani zimehusiana”

Isaya 9:6 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa Amani”.

Ikiwa utaomba maombi hayo kwa Imani, na kwa ufunuo, na ukiwa umejihakika kwamba njia zako zimetakasika mbele zake basi tegemea majibu yake, kwamaana Neno la MUNGU halijawahi kupita kamwe!, wala kushindwa.

Bwana akubariki.

Usikose sehemu inayofuata juu ya Mistari ya kusimamia katika MAOMBI YA UPENDO WA FAMILIA.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

FAMILIA TAKATIFU: Marimu na Yusufu.

TUNA WAJIBU WA KUOMBEA MAHALI TULIPO.

Sadaka ya Amani ilikuwaje?

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake

Rudi Nyumbani

Print this post

UTUKUFU WA MUNGU, UPO KATIKA UMOJA

Umoja katika Ukristo ni jambo linalokimbiwa na wengi lakini ndilo jambo pekee lililobeba UTUKUFU WA MUNGU wa moja kwa moja. Na maana ya Utukufu wa Mungu ni “MUNGU KUTUKUZWA”.. Maana yake Mungu anatukuzwa katika Umoja.

Labda utauliza ni kwa namna gani?.. Tusome maandiko yafuatayo..

Yohana 17:22 “Nami UTUKUFU ULE ULIONIPA nimewapa wao; ILI WAWE NA UMOJA kama sisi tulivyo umoja.

23  Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”

Kumbe Utukufu Kristo aliotuachia lengo lake la kwanza ni ili tuwe na UMOJA.. Na si kutenda miujiza, na maajabu.. Maana yake Mungu anatukuzwa Zaidi katika UMOJA kuliko katika MIUJIZA na ISHARA. Na ndicho kitu pekee kilicho na nguvu ya kuwafanya watu wamwamini Mungu kuliko ishara na miujiza.

Watu watakapoona umoja wetu katika Mungu, ndipo watavutwa kumwamini Mungu kuliko hata kuona ishara na miujiza halafu hamna Umoja… Na ndicho kitu pekee kinachotufanya sisi tumwamini BWANA YESU, ni kwasababu alikuwa na Umoja na Baba.

Laiti Bwana YESU asingelikuwa na umoja na Baba, ingelikuwa ngumu kumwamini kwa ishara na miujiza pekee, lakini ule Umoja wa Roho kati yake na Baba, umetutengenezea sisi Upendo wa ajabu, na Imani kuu kwa BWANA YESU KRISTO, Kwamba yeye ni kweli na hamna uongo ndani yake.

Na vile vile sisi tukiwa na Umoja na Mungu, na tukiwa na umoja sisi kwa sisi ndipo USHUHUDA WETU UTAKAPOTHIBITIKA ZAIDI kuliko kukaa katika matengano.

Yohana 17:21 “WOTE WAWE NA UMOJA; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI YA KWAMBA WEWE NDIWE ULIYENITUMA.

22  Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.

23  Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi”.

Hapo mstari wa 21 anasema.. “WOTE WAWE NA UMOJA ….ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI YA KWAMBA WEWE NDIWE ULIYENITUMA”.

Kumbe UMOJA WETU ndio utakaowaaminisha watu kuwa KRISTO ni BWANA! Na si mahubiri yetu kuwa mengi, au miujiza yetu kuwa mingi…ni UMOJA TU!.

Tukilikataa Neno hili, na kufuata njia zetu za matengano, tutakuwa tunajipunguzia wenyewe utukufu wa Mungu, kwasababu KRISTO hakujitenga na Baba, wala hakujitenga na wanafunzi wake.

> Unapochagua kuomba peke yako kila mara na huku ipo nafasi ya kuomba na mwingine mmoja au wawili ni roho ya matengano inayoondoa utukufu wa Mungu. (Bwana wetu YESU KRISTO mara nyingi alipanda mlimani kuomba na wanafunzi wake, na hata katika sehemu za faragha soma Mathayo 17:1, na Marko 14:33-34).

> Unapochagua kila mara kwenda kuhubiri peke yako na wakati kuna nafasi ya kwenda na mwingine mmoja au wawili, ni roho ya matengano ambayo inapunguza utukufu wa Mungu juu yako (Bwana YESU aliwatuma wawili wawili kuhubiri katika miji na vijiji soma Luka 10:1 na Matendo 13:2).

> Unapochagua kila mara kutosema na ndugu yako, kumfariji, au kumtia moyo au kukaa karibu naye, ili hali ni mtu wa Imani moja nawe, mnamwamini Bwana mmoja, mmepokea roho mmoja, na hata ubatizo mmoja hiyo ni roho ya matengano inayoharibu utukufu wa Mungu juu yetu.

Hivyo ni lazima tuuhifadhi Umoja wa Roho kama Neno la Mungu linavyotufundisha ili tusipungukiwe na utukufu wa Mungu.

Waefeso 4:3 “na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

4  Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.

5  Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.

6  Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote”

Bwana atusaidie na kutuwezesha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

TUUTAFUTE UMOJA WA ROHO.

JE UNAMHUBIRI KRISTO KATIKA KWELI YOTE?.

TAFUTA UZIMA WA MILELE NA SI UZIMA TU!.

MARINDA KATIKA BIBLIA NI KITU GANI?

BWANA ni mtu wa vita,  BWANA ndilo jina lake.(Kutoka 15:3)

Rudi Nyumbani

Print this post

Maana ya Mithali 21:30 Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri,  juu ya Bwana.

SWALI: Nini maana ya Mithali 21:30 Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri,  juu ya Bwana ?


JIBU: Mstari huo unaweza ukasemwa hivi; “Hapana hekima, wala ufahamu, wala shauri linaloweza kufanikiwa/kusimama kinyume na Mungu”.

Ikiwa na maana iwe ni mwanadamu au malaika, atumie uwezo wake wote, kufanya jambo la hila kinyume na yeye haliwezi kufichika kwasababu yeye ni mkuu zaidi ya vyote. Mpango wa shetani kuliharibu kanisa huawezi kufanikiwa hata azidishe kufanya kazi mara elfu zaidi ya mwanzo hilo haliwezekani kama lilivyoshindikana mbinguni.

Mambo yote yanayotokea hayafiki kwake ghafla tu bila hodi, kama ilivyo kwetu sisi wanadamu. Elimu ya darasani haiwezi pindua ukweli wake wa uungu, wajaposema mwanadamu ametokana na nyani, mwishoni wanarudia kule kule kwenye ukweli wa uumbaji wa kiungu, kwasababu atabakia kusimama kuwa Mungu wa daima, na ataabudiwa vizazi vyote haijalishi dunia itaelimika kiasi gani.

Mungu Anajua mawazo yetu yote tokea mbali, wewe kama mwanadamu huwezi mficha dhambi zako, ukajifanya  mbele zake umesahau, au ulikuwa hujui, hata utumie hekima nyingi kiasi gani kuficha ukweli bado anatambua nia ya mioyo yetu.

Anasema;

Zaburi 50:17 Maana wewe umechukia maonyo, Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako.  18 Ulipomwona mwivi ulikuwa radhi naye, Ukashirikiana na wazinzi.

19 Umekiachia kinywa chako kinene mabaya, Na ulimi wako watunga hila.  20 Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia.

21 NDIVYO ULIVYOFANYA, NAMI NIKANYAMAZA; UKADHANI YA KUWA MIMI NI KAMA WEWE. Walakini nitakukemea; Nitayapanga hayo mbele ya macho yako.

22 Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya.

Pale tunapomwona Mungu ni kama sisi ndio unakuwa mwanzo wa kuto-mhofu  yeye. Unapokuwa na udhuru wa kuifanya kazi yake halafu unasingizia sina muda, lakini una muda wa kufanya mambo yako, ukidhani yeye hajui nia yako ya ndani, unajidanganya mwenyewe. Unapoepuka maombi, kwa kisingizio umechoka, na bado unataka Mungu akuhudumie, fahamu Mungu anakuelewa vizuri sana, atakuonyesha ambao wanachoka zaidi yako, lakini hawana udhuru. Jambo lolote tulifanyalo, tutambue kwanza kwa Mungu halifichiki.

Kwasababu Hapana hekima, wala ufahamu, wala shauri litakalosimama kinyume cha Mungu

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Nini maana ya Mithali 19:21Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.(Opens in a new browser tab)

Je shauri la kuipepeleza Kanaani lilitoka kwa wana wa Israeli au kwa BWANA?(Opens in a new browser tab)

Tofauti kati ya Hekima, ufahamu na maarifa, ni ipi?

(Opens in a new browser tab)Maana ya Mithali 11:17 Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake(Opens in a new browser tab)

Rudi Nyumbani

Print this post

Maana ya Mithali 21:17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini;

SWALI: Nini maana ya  Mithali 21:17 Mtu apendaye anasa atakuwa maskini; Apendaye mvinyo na mafuta hatakuwa tajiri.


JIBU: Mstari huo unamaana mbili.

Maana ya kwanza ni ya mwilini, ni ukweli watu wanaopenda maisha ya anasa, mwisho wao huwa ni kutofanikiwa. Kwasababu kile wanachokipata ambacho kingepaswa kiwekwe akiba kwa wakati wa baadaye au kiwekezwe kizalishe zaidi, wao hutumia chote katika starehe mfano wa pombe, uasherati, na kununua vitu vya gharama kubwa, lengo tu asionekane amepitwa na wakati, au aonekane wa kisasa.

Hapo anaposema apendaye mvinyo na mafuta, hayo mafuta yanayozungumziwa hapo ni marashi ya gharama ambayo zamani waliokuwa wananunua ni matajiri. Ni sawa na leo labda mwajiriwa analipwa mshahara wa laki tatu (3) kwa mwezi, halafu anakwenda kununua perfume (marashi), ya  laki 2, ili tu aonekane wa kisasa, hiyo ni anasa, na mwisho wake ni umaskini.

Anasa ni tunda la majivuno, na kukosa adabu. Hivyo biblia inamfundisha mwanadamu yoyote kuwa, anasa ni kinyume cha mafanikio.

Lakini pia rohoni, anasa ni zao la ufukara wa ki-Mungu. Mtu wa anasa, hutumia muda wake vibaya, kwasababu nyakati zake za ziada huishia kwenye starehe za kimwili na sio kwenye mambo ki-Mungu.

Bwana alisema;

Luka 8:14  Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote.

Umeona? Anasa husonga mbegu ya Mungu ndani yako.

Katika kizazi cha sasa anasa ni pamoja na kushinda kwenye tv kutazama muvi kila kukicha, ni pamoja na kushinda mitandaoni kufuatilia vipindi vinavyokupa raha za kimwili na kihisia lakini havikujengi rohoni,  ni kuwekeza muda wako katika matanuzi ya mijini na kwenye sherehe-sherehe za kila mara ambazo hazina mpangalio. Muda wote akili yako ipo katika kile kitu wanachosema “ku-party weekend” na marafiki. Ushikapo simu yako, usiku wote ni kuchat, na wale wanaowaita ma-boyfriend na ma-girlfriend. Muda ambao ungepaswa kusoma Neno na kuomba.

Sasa ikiwa wewe umeokoka, na una mwenendo huo wa maisha, usitazamie hapo utazalisha kitu. Utabakia kuwa Yule Yule milele. Biblia inasema ni heri kuona kwa macho kuliko kutangatanga kwa tamaa(Mhubiri 6:9). Sio kila taarifa uifuatilie, sio kila kitu ukitende, viache vingine vikupite, ili upate nafasi ya kuwa karibu na Mungu wako, uwe mtu wa matunda. Komboa wakati.

Shalom..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa.

(Opens in a new browser tab)APENDAYE FEDHA HASHIBI FEDHA.

Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 4)(Opens in a new browser tab)(Opens in a new browser tab)(Opens in a new browser tab)

Rudi Nyumbani

Print this post

MAMBO NANE (8), AMBAYO WEWE KAMA KIONGOZI UTAIGWA.

Uwapo katika nafasi yoyote ya uongozi, katika kanisa au kwenye huduma, labda mchungaji, mwalimu, mtume, nabii, shemasi, askofu, mzee wa kanisa. Na una watu walio chini yako, fahamu mambo ambayo utaigwa, Na hivyo kuwa makini sana katika maeneo hayo uyajenge.

Mtume Paulo aliyaona kwa mwanawe Timotheo, akayaandika;

2 Timotheo 3:10-11

[10]BALI WEWE UMEYAFUATA mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu, 

[11]na upendo, na saburi; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote. 

Paulo ametaja mambo saba ambayo Timotheo aliyaona kwake akayaiga, ni kama yafuatayo;.

la kwanza ni 

1) Mafundisho yake:

Wewe kama kiongozi kumbuka unachofundisha ndicho watakachofundisha wafuasi wako, ikiwa injili yako ni ya mafanikio, hicho hicho watakifuata na kukifundisha, ikiwa ni mafundisho ya wokovu watakifundisha hicho hicho, ikiwa ni shuhuda za wachawi nao pia watakuwa nazo hizo hizo kama kiini cha injili yao. Hivyo kuwa makini na fundisho lako vinginevyo utajikuta  unapotosha jamii yako ya waaminio, na utatoa hesabu juu ya hilo, mbele za Bwana siku ile.

2) Mwenendo wake:

Ukiwa ni mtu wa kidunia, usitazamie utazaa watu wa rohoni, uvaaji wako, unawafundisha wafuasi wako, kauli zako zitazungumzwa hizo hizo na washirika wako, ukiwa na tabia ya maombi, wanaokufuata nao pia wataiga mwenendo huo wa maombi, ukiwa ni mtakatifu nao pia watakuwa hivyo hivyo. Jichunge mwenendo wako, wewe ni kioo unaigwa mpaka hatua zako. Hivyo usifanye mambo kiwepesi wepesi, ukidhani wote wamekomaa wanaweza kujiamulia tu mienendo bila kukuangalia wewe. Liondoe hilo kichwani.

3) Makusudio yake:

Makusudi ya mtume Paulo, yalikuwa ni kuhubiri injili kwa mataifa kotekote wamjue Mungu (2Wakorintho 1:15-20). Hakuwa na kusudio la umaarufu, fedha, kuheshimiwa na wanadamu, hapana, bali kuhubiri injili tu peke yake, bila kujali dhiki, au kupungukiwa, ilimradi watu waokoke. Hivyo Timotheo naye alipoliona kusudi hilo akaiga, naye pia akawa mhubiri tu wa injili, asiyetafuta vya kwake ndani ya kazi ya Mungu. Halidhalika na wewe pia, nia yako hutakumbulikana mahali ulipo, Je! Unachokifanya ni injili ya Mungu kweli au una lengo lingine. Ikiwa ni Yesu wa mikate, basi ujue watu wako pia watakuwa hapo kumtafuta Mungu huyo huyo wa kwako. Kuwa na kusudi la Kristo ambalo aliliweka pia ndani ya mitume wake, yaani kulitumikia na kulichunga kundi, kama mtendakazi asiyekuwa na faida. Ukijua kuwa thawabu yako ipo mbinguni, usiwe na makusudio mengine, kwasababu wewe ni kioo.

4) Imani yake:

Imani, katika mambo yote, wewe kama kiongozi ukiwa ni mtu wa mashaka juu ya mambo ya rohoni.  Ikiwa huamini uponyaji wa ki-ungu, na wale pia watakuwa hivyo hivyo, huamini miujiza, na karama za Roho, vivyo hivyo na washirika wako watakuiga, ikiwa huamini katika mifungo, ikiwa huamini kuwa duniani kuna watakatifu, au mtu hawezi kuwa mtakatifu, vivyo hivyo watu wako nao watakuwa hivyo, Ikiwa unaamini katika ibada za sanamu, watakuwa kama wewe.  Jenga imani yako kwenye neno la Mungu tu, kuwa mtu wa imani usiwe Sadukayo. Fahamu kuwa mtumishi wa Mungu tafsiri yake ni kuwa mtu wa Imani.

5) Uvumilivu wake:

Kama kiongozi ni ukweli usiopingika utapitia vipindi mbalimbali vya kushinda na kushindwa, vipindi vya kukatishwa tamaa, kusemwa vibaya,  vipindi vya kuachwa peke yako n.k. Mtume Paulo alipitia vipindi vyote, na wanafunzi wake wakawa wanamwangalia, wakaiga mwenendo ule walipoona mafanikio yake yalipotanguliwa na vipindi vingi vya kuvunjwa moyo lakini akastahimili. Hivyo na wewe pia kama kiongozi wa wengine, simama imara, uvumilivu wako ni funzo kubwa kwa wengine. Wakati mwingine Mungu anaruhusu uyapitie hayo ili kuwaimarisha wengine katika dhiki zao, wakuonapo wewe unasimama katika changamoto, na wao pia hupokea nguvu ya kushindana na changamoto zao.

6) Upendo wake:

Kama kiongozi, upendo ni sehemu, kubwa sana, ambalo mtume Paulo alifanya bidii kulionyesha kwa wanafunzi wake na kanisa.  Unapolipenda kundi lako, vivyo hivyo na wale wataiga tabia hiyo na kuidhihirisha kwa wengine. Unapoonyesha chuki, nao pia watakuwa watu wa chuki, unapowajali nao pia watawajali wengine. Unapowasikiliza, tafsiri yake ni kuwa unawafundisha kuwasikiliza na wengine. Hivyo ni kuangalia sana na kuongeza bidii katika eneo hilo, uwe kielelezo.

7) Saburi yake:

Saburi ni kitendo cha kungojea ahadi za Mungu hata katika mambo magumu yanayokinzana na wewe, bado unasubiria tu. Kama kiongozi watu watatazamia jinsi unavyoyashikilia maono yako, bila kuyumbishwa, waige, na wenyewe kushikilia ya kwao. Kamwe usiwe mtu wa kusita-sita, utawavunja moyo wengi, na hatimaye watashindwa kusimama aidha pamoja na wewe, au wao wenyewe. Ijenge saburi yako, wala usiidharau, ni nguvu kwa mwingine aliye chini yako. Leo unaona jinsi gani saburi ya Ayubu ilivyo na fundisho kubwa kwetu. Vivyo hivyo na yako ujue ni darasa kwa wengine.

8) Adha na mateso yake:

Ukweli ni kwamba watu watatamani kusikia ushuhuda wa mapito yako au kuyaona mapito yako hususani yale magumu sana. Lakini waweza kudhani, haliwafahi sana kiroho, lakini wengine pia wakaiiga njia hiyo ya mateso kama yako, kwasababu wameona mwisho wake ulivyo mzuri. Hivyo usiogope kupitia mateso kwa ajili ya Bwana wala usione haya wakati mwingine kueleza shida ulizopitia kwa wengine, hilo nalo huigwa, Leo hii tunaposoma mapito ya mtume Paulo ni wazi kuwa yanatutia nguvu na sisi, kuwa tusonge mbele.

Hivyo, zingatia mambo hayo saba, kwa faida yako na wale walio chini yako. Kwasababu ndicho Paulo alichokiona kwa watoto wake.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

Fahamu maana ya Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.

IMANI “MAMA” NI IPI?

Bwana alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?

Rudi Nyumbani

Print this post

Ipi tofuati kati ya UTAKATIFU na UKAMILIFU?

Swali: Ipi tofuati kati ya kuwa MTAKATIFU (1Petro 1:15-16) na kuwa MKAMILIFU (Mathayo 5:48)?

Jibu: MTAKATIFU ni Mtu aliyetakaswa, aliye safi, asiye na mawaa na anayefanya matendo mema.. Na biblia inatufundisha tuwe watakatifu kama Baba wa mbinguni alivyo mtakatifu…

1Petro 1:15  “bali kama yeye aliyewaita ALIVYO MTAKATIFU, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;

16  kwa maana imeandikwa, MTAKUWA WATAKATIFU KWA KUWA MIMI NI MTAKATIFU”.

Na tena Mambo ya Walawi 19:2  inarudia jambo hilo hilo..

Walawi 19:2 “Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu”.

Lakini MKAMILIFU ni Mtakatifu aliye kamilika….. Wapo Watakatifu waliokamilika na ambao hawajakamilika.

Mtakatifu aliye kamilika ni yule ni anayefanya JAMBO LA ZIADA katika UTAKATIFU WAKE linalomtofautisha na wengine na kufanya afanane na MUNGU … Mfano wa mambo hayo ni kama yale yote Bwana YESU aliyoyataja katika Mathayo 5.

Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

44  lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

45  ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

46  Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47  Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, MNATENDA TENDO GANI LA ZIADA? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

48  Basi ninyi MTAKUWA WAKAMILIFU, KAMA BABA YENU WA MBINGUNI ALIVYO MKAMILIFU

Kwahiyo na sisi ni Lazima tuutafute UKAMILIFU na si UTAKATIFU TU!.

> “Mtakatifu” anafunga na kuomba kwaajili yake peke yake, lakini “Mkamilifu” anafunga na kuomba kwaajili yake na kwaajili ya wengine,

> “Mtakatifu”  anasoma neno na kuomba basi!…Lakini “Mkamilifu”  anasoma Neno na kuomba na kuwafundisha wengine mambo aliyojifunza, ili nao wabarikiwe kama yeye.

> “Mtakatifu”  anafanya kazi ya Mungu kwa moyo ili akapate thawabu mbinguni, lakini “Mkamilifu”  pamoja na kufikiri thawabu mbinguni lililo kubwa zaidi analolifikiri ni ndugu zake wasiangamie katika moto wa milele (moyo wake unaugua juu ya roho za wengine kupotea).

> “Mtakatifu”  atampa Mungu siku moja katika wiki ya kukusanyika nyumbani kwa Mungu, lakini “Mkamilifu”  atafikiri Zaidi ya siku moja.

> Mtakatifu” atazishika AMRI ZOTE ZA MUNGU, lakini Moyo wake utakuwa pia katika mali…. Lakini “Mkamilifu” Atazishika Amri zote na Moyo wake hautakuwa katika mali kama yule kijana aliyekutana na Bwana YESU.

Mathayo 19:16 “Na tazama, mtu mmoja akamwendea akamwambia, Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?

17  Akamwambia Kwani kuniuliza habari ya wema? Aliye mwema ni mmoja. Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.

18  Akamwambia, Zipi? Yesu akasema, Ni hizi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo,

19  Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.

20  Yule kijana akamwambia, Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?

21  Yesu akamwambia, UKITAKA KUWA MKAMILIFU, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.

22  Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi”.

Hivyo hatuna budi kuutafuta UKAMILIFU na sio UTAKATIFU tu peke yake!!.

Biblia inasema Nuhu alikuwa mtu Mkamilifu katika vizazi vyake ndio maana akapona katika ile gharika (Mwanzo 6:9),  Daudi alikuwa mkamilifu ndio maana alipendwa na Mungu zaidi ya wafalme wote (2Samweli 22:24), Ayubu alikuwa mkamilifu ndio maana alimwona Mungu katikati ya majaribu (Ayubu 1:1).

Na hata sisi tukiwa WAKAMILIFU tutamwona Mungu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MADARAKA YA WAKATI MKAMILIFU.

BABA UWASAMEHE

NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

Nini maana ya Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu?

NENO LA MUNGU NI UFUNUO MKAMILIFU.

Rudi Nyumbani

Print this post

Ipi tofauti kati ya KUHANI na MCHUNGAJI.

Jibu: Makuhani ni watu waliokuwa wanahudumu katika “Hema ya Mungu” wakati wana wa Israeli wakiwa jangwani na katika “Hekalu la Mungu” baada ya wana wa Israeli kuingia katika nchi ya ahadi na kumjengea Mungu nyumba.

Kazi ya Makuhani ilikuwa ni “kuwapatanisha watu na Mungu wao” kupitia damu za wanyama. Vile vile Makuhani walikuwa na kazi ya kuwafundisha wana wa Israeli torati, na wote walitoka katika kabila moja lililoitwa Lawi.

Kwa mapana na marefu kuhusu makuhani wa agano la kale, pamoja na kazi zao na tofauti yao na walawi wengine fungua hapa >>>Tofauti kati ya makuhani na walawi ni ipi?

Lakini tunapokuja kwa “Wachungaji” wenyewe ni watu maalumu walioteuliwa na kuchaguliwa na MUNGU kulichunga na kulilisha kundi lake kupitia Mafundisho ya Neno la Mungu, maonyo na Maombi!. (Soma Yohana 21:15-17).

Na hawa wanafanya kazi mfano wa zile za kikuhani katika nyumba ya Mungu. Isipokuwa wenyewe hawawapatanishi watu kwa damu za wanyama bali kwa damu ya BWANA YESU kupitia Neno lake. Hivyo Wachungaji nao ni MAKUHANI WA BWANA.

Lakini si tu wachungaji walio makuhani wa Bwana peke yao, bali hata watu wengine wote waliojazwa Roho Mtakatifu wana sehemu ya huduma ya kikuhani… Kwani ndivyo maandiko yasemavyo kwamba sote tumechaguliwa kuwa MAKUHANI KWA MUNGU WETU.

Ufunuo 1:5 “tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,

6  na kutufanya kuwa ufalme, NA MAKUHANI KWA MUNGU, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina”

Hivyo kila mmoja aliyejazwa Roho Mtakatifu anayo huduma ya upatanisho (ambayo ndiyo ya kikuhani) ndani yake kupitia ile karama aliyopewa, ndio maana sote tuna uwezo wa kuhubiri injili na kuchungana sisi kwa sisi kupitia Neno la Mungu.

2Wakorintho 5:18 “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho;

19  yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.

20  Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu”.

Kama wewe ni Mchungaji, unayesimamia kundi kama kiongozi,  basi simama katika nafasi yako ya kuchunga na kulisha kwani kuna hatari kubwa ya kutokufanya hivyo..

Ezekieli 34:1 “Neno la Bwana likanijia, kusema,

2 Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?

3 Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo.

4 Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala.

5 Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyama- mwitu, wakatawanyika.

6 Kondoo zangu walitanga-tanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo zangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta.

7 Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana;

8 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo zangu walikuwa mateka, kondoo zangu wakawa chakula cha wanyama-mwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo zangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo zangu;

9 kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana;

10 Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao”.

Bwana YESU atusaidie sana.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

WACHUNGAJI WA BWANA MAKONDENI.

TOFAUTI YA MITUME, MANABII, WAINJILISTI, WACHUNGAJI NA WAALIMU NI IPI?

JE! UNAMPENDA BWANA?

Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)

JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?

Rudi Nyumbani

Print this post

Ipi tofauti kati ya maasi na maovu?

Swali: Kuna tofauti gani ya kufanya maasi na kufanya maovu?


Jibu: Maovu ni mambo yote mabaya mtu anayoyafanya yaliyo kinyume na Mungu, na haya yanatokana na shetani (ndio maana anajulikana kama Mwovu, Mathayo 5:37)…mfano wa maovu ni mauaji, uasherati, dhuluma, wizi, ulawiti, ufiraji, ibada za sanamu na mambo mengine yanayofanana na hayo..

Lakini “Maasi” ni mabaya yote yanayofanywa na watu waliokuwa ndani ya Imani kisha wakatoka!!!. (kwa ufupi ni maovu ya watu waliokwisha kumjua Mungu).

Maana yake kama mtu alikuwa ndani ya Imani, na baadaye akakengeuka na kuisaliti ile Imani au kurudi nyuma kwa kuanza kufanya mambo mabaya… basi mambo hayo maovu ayafanyayo ndiyo yanayoitwa MAASI.

Mtu wa kidunia ambaye hajamjua Mungu bado, huyo hawezi kufanya MAASI!.. Kwasababu hakuna ALICHOKIASI!... Mpaka mtu afanye Maasi ni lazima awe AMEASI!..Sasa mtu ambaye hajamjua Mungu anakuwa anafanya MAOVU tu na si MAASI.. lakini akishamjua Mungu na akamwacha Mungu na kurudia maovu aliyokuwa anayafanya,.. basi yale maovu ayafanyayo ndiyo yanayoitwa MAASI.

Na watu wanaofanya Maasi wana hukumu kubwa kuliko wanaofanya Maovu, kwasababu tayari walishamjua Mungu na kisha wakamwacha kwa kurejea nyuma. Mfano wa watu waliokuwa wanatenda MAOVU na si MAASI katika biblia ni watu wa Sodoma na Gomora.

Mwanzo 19:15 “Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika MAOVU YA MJI HUU.”

Na mfano wa watu waliokuwa wanafanya MAASI ni wana wa Israeli (kwasababu walikuwa walianza na Mungu lakini wakakengeuka baadaye)

Yeremia 3:22 “21 Sauti inasikiwa juu ya vilele vya milima, ni kulia kwao na maombi yao wana wa Israeli; kwa kuwa wameipotosha njia yao, wamemsahau Bwana, Mungu wao.

22 RUDINI, ENYI WATOTO WAASI, mimi nitaponya maasi yenu. Tazama, tumekuja kwako; maana wewe u Bwana, Mungu wetu.”

Na katika siku za mwisho biblia inatabiri KUONGEZEKA KWA MAASI!.. Maana yake watakaokuwa wanarudi nyuma na kuisaliti imani na kufanya vitu kwa makusudi watakuwa ni wengi kuliko wale walio wa kudunia wafanyao maovu pasipo kuijua njia ya kweli.

Mathayo 24:12 “Na kwa sababu ya KUONGEZEKA MAASI, upendo wa wengi utapoa”.

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba “Maasi” ni “Maovu” yanayofanywa na watu waliorudi nyuma au waliomwacha Mungu!… Na watendao MAASI wana hukumu kubwa Zaidi ya watendao Maovu tu.. kwasababu wameyajua mapenzi ya Bwana wao halafu wakaasi.

Luka 12:47 “Na mtumwa yule aliyejua mapenzi ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana.

48  Na yule asiyejua, naye amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi; naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na Zaidi”.

Ukitoa mimba na huku unamjua KRISTO na unasema umeokoka ni UASI, ukiiba na huku unajua kabisa wizi ni dhambi na tena unajiita Mkristo huo ni UASI, ukifanya uzinzi na unasema umeokoka wewe ni Muasi, ukiabudu sanamu na huku unajua kabisa si sawa kufanya hivyo ni Uasi!..Na roho ya kuasi ni ROHO YA MPINGA KRISTO! (2Thesalonike 2:7).

Bwana atusaidie tusiwe WAASI wala tusifanye MAASI baada ya kumjua yeye, bali tudumu katika ukamilifu na utakatifu katika Roho wake Mtakatifu.

Lakini ikiwa wewe bado haujaokoka fahamu kuwa pia MAOVU yako uyafanyayo hayatakufikisha popote, mwisho wake ni katika ziwa la Moto..

Ni heri ukayasalimisha maisha yako kwa BWANA YESU ili akusafishe na kukupa uzima wa milele.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MUNGU HAJARIBIWI NA MAOVU BALI MEMA.

IMANI “MAMA” NI IPI?

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

Je Adamu na Hawa, walikuwa hawafanyi mema kabla ya kula tunda?

MAMBO (2) YATAKAYOKUTENGA NA IMANI SIKU HIZI ZA MWISHO.

Rudi Nyumbani

Print this post

Kasirani ni nini? (Kutoka 23:21)

Swali: kumtia mtu au malaika kasirani ndio kufanya nini? (Kutoka 23:21).

Jibu: Turejee..

Kutoka 23:20 “Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea.

21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; WALA MSIMTIE KASIRANI; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake.

22 Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao”.

Kumtia mtu “Kasirani” ni kumfanya mtu “Akasirike”. Hivyo hapo biblia iliposema msitie Kasirani yule malaika maana yake “wasimkasirishe” kwasababu hatawasamehe.

Na ni vitu gani ambavyo vingemtia yule malaika kasirani?.. si vingine Zaidi ya “kumwacha Mungu na kuabudu miungu mingine, pamoja na kutolishika Neno lake”.. Utaona wana wa Israeli mara kadhaa walimtia kasirani yule malaika walipokuwa jangwani na hata walipoingia ile nchi ya ahadi.

Tukio moja la wazi lililoonesha dhahiri, malaika wa Bwana kutiwa kasirani na wana wa Israeli ni kipindi ambacho walikawia kuyaondoa yale mataifa waliyoyakuta katika nchi ya ahadi na walipoingia agano na miungu yao.. jambo ambalo lilikuwa ni chukizo kubwa mbele za  Mungu na kwa malaika wake ambaye aliyempeleka awaingize katika ile nchi ya ahadi.

Waamuzi 2:1 “KISHA MALAIKA WA BWANA ALIKWEA JUU KUTOKA GILGALI KWENDA BOKIMU. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi;

2 nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani?

3 Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu.

4 Ikawa, hapo huyo malaika wa Bwana alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia

5 Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia Bwana sadaka huko”.

Hata leo watu wanawatia kasirani Malaika wa Mungu.. Kwani maandiko yanasema kila mtu aliyeokoka anaye malaika wake asimamaye mbele za Mungu kupeleka habari zake njema na kumhudumia mtu huyo soma (Mathayo 18:10 na Waebrania 1:13-14).

Hivyo inapotokea mtu anafanya mambo yaliyo kinyume na Neno la Mungu, basi Malaika asimamaye naye anachukizwa na kuhuzunishwa pia.

Lakini pia si Malaika tu wanatiwa kasirani, bali pia hata Mungu wetu tunamtia Kasirani kwa maovu yetu.. Wana wa Israeli walimtia BWANA MUNGU kasirani walipokuwa jangwani na hata sasa sisi wa wakati huu tunamtia KASIRANI kwa maovu yetu.

Kumbukumbu 9:7 “Kumbuka, usisahau ulivyomtia Bwana, Mungu wako, KASIRANI JANGWANI; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hata mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya Bwana

8 Tena mlimkasirisha Bwana katika Horebu, Bwana akakasirika nanyi hata akataka kuwaangamiza.

9 Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano Bwana alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji”.

Soma pia Kumbukumbu 31:29.

Bwana atusaidie tusivuke mpaka wa Neno lake na kumkasirisha.

Amen.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JE! MUNGU NI NANI?

HUDUMA YA MALAIKA WATAKATIFU.

MUNGU MWENYE HAKI.

Malaika wa maji ni yupi na Je kuna aina ngapi za malaika?

KAA MAJANGWANI.

Rudi Nyumbani

Print this post

Fahamu maana ya Mithali 18:22 Apataye mke apata kitu chema

SWALI: Je andiko hili humaanisha nini? kupata mke ni kujipatia kibali cha kumkaribia Mungu tofauti na  hapo mwanzo?

Mithali 18:22

Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA. 

JIBU: Andiko hili hutafsiriwa vibaya na watu wengi, wakiamini kuwa pale mtu anapoingia kwenye ndoa basi ndio amejizidishia kibali cha kukubaliwa na Mungu katika maisha yake. Jibu ni hapana, kibali kwa Mungu sio ndoa, kibali kwa Mungu ni “kufanya vema mapenzi ya Mungu” .

Mungu alimwambia kaini maneno haya

Mwanzo 4:7

[7]Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. 

Zaidi pia, maandiko yanaeleza ipo nafasi kubwa kwa mtu  kumkaribia Mungu anapokuwa hajaoa/kuolewa kuliko yule aliyeoa au kuolewa.Kwasababu ambaye hajaoa/ olewa hupata nafasi ya kutosha kumtafuta Bwana na kumfikiria yeye ampendezeje.

1 Wakorintho 7:32-33

[32]Lakini nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana; 

[33]bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe. 

Lakini je! andiko hilo humaanisha kibali gani?

“Apataye mke apata kitu chema; Naye ajipatia kibali kwa BWANA”. 

Tafsiri ya Neno hilo ni kuwa Mungu analikubali jambo hilo(Ndoa), analibariki, na pia analiona ni jema. Hivyo mtu asidhani kuwa aingiapo katika ndoa atamkosea Mungu, au Mungu atapunguza ukaribu naye. Hapana, kinyume chake atapata kibali tu. Hivyo awe na furaha na amani afanyavyo hivyo.

kwasababu pia zipo faida zinazoambata na mtu aliyeoa, mojawapo ni kujiongezea heshima kwa jamii lakini pia kuaminiwa zaidi. Na hilo ni jema husasani katika utumishi & huduma.

Lakini haimaanishi kuwa unapooa ndio Mungu anakukubali zaidi ya ule wakati ambao ulikuwa hujaoa/kuoelewa, au zaidi ya yule mtu ambaye hafikirii kuoa.

Mtume Paulo, Barnaba hawakuoa na zaidi mwokozi wetu Yesu Kristo hakuoa lakini tunaona ni jinsi gani walivyojirahisishia nafasi zao  kwa Mungu. 

kwa mafundisho zaidi kuhusu ndoa pitia masomo chini;

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAFUNDISHO YA NDOA.

MWANAMKE UKITAKA KIBALI, USIWE MTU WA KUPENDA VITU. (Esta 2:17)

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

Rudi Nyumbani

Print this post