Je shauri la kuipepeleza Kanaani lilitoka kwa wana wa Israeli au kwa BWANA?

Je shauri la kuipepeleza Kanaani lilitoka kwa wana wa Israeli au kwa BWANA?

Swali: Je lile shauri la kupeleka wapelelezi Kanaani lilitoka kwa nani?..Maana sehemu moja katika biblia inasema lilitoka kwa Bwana (Hesabu 13:1-3) na sehemu nyingine inasema lilitoka kwa wana wa Israeli (Kumbukumbu 1:22-23). Je! lipi ni sahihi, na je biblia inajichanganya?.


Jibu: Turejee mistari hiyo, mmoja baada ya mwingine.

Hesabu 13:1 “Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,

2 Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao.

3 Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na Bwana; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli”.

Hapa tunaona ni MUNGU ndiye anamwamuru Musa apeleke wapelelezi.

Kumbukumbu 1:22 “Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tupeleke watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia.

23 Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila”

Na hapa tunasoma kuwa ni “Wana wa Israeli” ndio waliopendekeza kupeleka wapelelezi Kanaani. Sasa swali ni je!..biblia inajichanganga?.

Jibu ni La!.. Biblia haijichanganyi mahali popote, isipokuwa fahamu/pambanuzi zetu ndizo zinachojichanganya au kuchanganyikiwa.

Sasa ni kwanini hapo sehemu moja iseme ni Mungu na sehemu nyingine iseme wana wa Israeli? Ukweli ni upi?

Ukweli ni kwamba wazo la kupeleka wapelelezi wakaiepeleze Kanaani ni Wana wa Israeli ndio waliolitoa, kamwe Mungu asingeweza kuwaambia wana wa Israeli wapeleke wapelelezi kwasababu yeye ana nguvu nyingi na wala hahitaji utafiti wa wanadamu katika kuokoa au kuharibu!…Kama ndivyo angefanya kwanza kwa Farao, lakini tunasoma Farao alikuwa kama mnyoo tu mbele za Bwana, na Taifa la Misri kwa wakati huo lilikuwa na nguvu Zaidi hata ya Kanaani.

Hivyo kilichowasukuma wana wa Israeli kupeleka wapelelezi ni hali ya ugumu wa mioyo yao, ambayo baada ya kutoka Misri walianza kuusahau uweza wa Mungu na kumdharau Mungu, kiasi kwamba hawakuamini kwamba angeweza kuwashindania kama alivyowashindania walipotoka Misri, lakini kinyume chake wakaukataa uweza wa Mungu, mioyo yao ikawa migumu, wakajitwika silaha, na wakapanga mipango yao.

Hesabu 14:11 “Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao”.

Sasa kwakuwa wana wa Israeli tayari walikuwa wameshamdharau Mungu na uweza wake, hivyo Mungu aliruhusu baadhi ya Mambo wayafanye, katika kiwango cha uweza walichompimia. Na mojawapo ya jambo ambalo aliliruhusu ni hilo la kwenda kupeleleza.

Hivyo Musa aliposikia mpango wa wana wa Israeli kwenda kuipeleleza, alienda kuuliza kwa Bwana, na Bwana akawapa ruhusa sawasawa na hiyo Hesabu 13:1-6. Na sio jambo hilo tu ambalo Mungu alitoa ruhusa bali yapo na mengine mengi ambayo wana wa Israeli walijiamulia na Mungu akaruhusu yaendelee katikati yao, lakini hayakuwa mapenzi makamilifu ya Mungu, baadhi ya mambo hayo ni yale ya wana wa Israeli kujitakia mfalme katika (1Samweli 8:5) na yale ya talaka ambayo Bwana YESU aliyasema katika Mathayo 19:3-8.

Mathayo 19:3 “Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?

4  Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,

5  akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?

6  Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.

7  Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?

8  Akawaambia, MUSA, KWA SABABU YA UGUMU WA MIOYO YENU, ALIWAPA RUHUSA KUWAACHA WAKE ZENU; LAKINI TANGU MWANZO HAIKUWA HIVI.

9  Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini”

Hii ikitufundisha kuwa, kuna mambo ambayo Mungu anaweza kuyaruhusu katika maisha yetu yatokee lakini yakawa si mapenzi makamilifu ya Mungu. Hivyo ni muhimu sana kutafuta kuyajua na kuyafanya mapenzi makamilifu ya MUNGU, na ndivyo tutakavyompendeza Mungu, na kuishi kama atakavyo yeye.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Kanaani ililaaniwa (Mwanzo 9:20-25,) kwanini Mungu awapeleke wana wa Israeli katika nchi iliyolaaniwa?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

EPUKA KUPELELEZA KILA KITU MUNGU ANACHOKUAHIDIA.

NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?

Nini maana ya Mithali 19:21Mna hila nyingi moyoni mwa mtu; Lakini shauri la Bwana ndilo litakalosimama.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments