UNAUELEWA, HISOPO UMEAO UKUTANI?

 UNAUELEWA, HISOPO UMEAO UKUTANI?

1Wafalme 4:32 Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.  33 Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata HISOPO UMEAO UKUTANI; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.

Salaam! karibu tujifunze na kutafakari bahari za mwokozi wetu Yesu Kristo na uzuri wake maishani mwetu.

Habari yetu itaanzia kwa mfalme Sulemani ambaye Mungu alimjalia hekima nyingi zaidi ya wanadamu wote waliokuwa duniani kwa wakati ule. Na moja ya mambo ambayo, aliyatafakari sana, hayawakuwa tu yanayowahusu wanyama na viumbe hai, lakini ni pamoja na mimea mbalimbali.

Hivyo kama tunavyosoma katika vifungu hivyo, aliweza kutambua hekima iliyokuwa imejificha nyuma ya miti mikubwa na yenye umaarifu kama mierezi, lakini, kilichomtafakarisha pia sio katika mimea mikubwa, lakini pia midogo  mfano wa Hisopo, na jinsi inavyomea. Na hapo tunaona anaeleza sifa yake, kwamba ni mmea unaomea ukutani.

Ikiwa na maana, mahali palipo na ardhi ngumu, au mwamba au jiwe, wenyewe unamea, na kukua na kuzaa bila shida yoyote. Tofauti na mimea mingine mingi yenye nguvu, itahitaji  udogo mlaini mwingi, tena tifutifu, lakini huu wa hisopo ni wa kipekee unahitaji mahali pagumu.

Kufunua nini?

Mmea huu unamfunua Bwana wetu Yesu Kristo,yeye  Hakuhitaji mahali palipoandaliwa pa kitajiri, ili kulitimiza kusudi la kifalme duniani,  hakuhitaji familia ya kidini maarufu, au kabila la kikuhani,  ili aishi maisha makamilifu, hakuhitaji kuishi mji mtakatifu Yerusalemu ili ampendeze Mungu. Bali alitokea mahali ambapo ni vijijini (Nazareti), familia maskini, tena nyakati za kipagani, ambazo imani ilikuwa imekongoroka sana, pia, kabila lisilojiuhusisha na mambo yoyote ya kikuhani kabisa. Hivyo Yesu aliishi katika jamii ya wapagani.

Wakati sisi katikati ya dhiki nyingi (yaani penye mwamba mgumu) tunanyauka. Yeye ndio alikuwa anasitawi. Aliweza kustahimili mapingamizi ya kila namna zaidi ya mwanadamu yoyote aliyewahi kutokea hapa duniani. Alichukiwa na ulimwengu, alisalitiwa, alikanwa, aliachwa peke yake, aliaibishwa, alipigwa mpaka kuuawa. Lakini hakuwahi kuanguka au kutenda dhambi yoyote. Haleluya! Anastahili hakika mwokozi wetu Yesu Kristo.

Ni hisopo umeao ukutani. Mahali ambapo mimea mingine imeshindwa, yeye ameweza.

Na ndio maana Neno linasema;

Waebrania 12:2  tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

3  MAANA MTAFAKARINI SANA YEYE ALIYEYASTAHIMILI MAPINGAMIZI MAKUU NAMNA HII YA WATENDAO DHAMBI JUU YA NAFSI ZAO, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.

4  Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi;

Umeona ni kwa namna gani Yesu alivyokuwa mwamba imara wa kutegemea sana?

Na ndio maana maandiko sasa yanasema, kwa kuwa alijaribiwa kama sisi, basi anaweza kuchukuliana na sisi pia katika mambo yetu ya udhaifu.

Waebrania 4:14  Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu.

15  Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.

16  Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

Hivyo ndugu, ni nini unachongoja, usiokoke leo?. Wewe peke yako hutaweza, kuushinda huu ulimwengu, unaihitaji neema ya Yesu Kristo ikusaidie. Mpokee leo, upate ondoleo la dhambi zako,  Akupe na Roho wake mtakatifu ili kukusaidia sasa kuishi maisha ya ushindi kama yeye alivyoishi.

Ukipita katika miamba lakini unaendelea kumea.  Hivyo chukua uamuzi huo leo. Ikiwa upo tayari kuokoka basi fungua hapa kwa mwongozo wa sala ya Toba. >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

ALIFANYIKA SADAKA KWA AJILI YETU!

VITA BADO VINAENDELEA.

TUKAZE MWENDO KWA TULIYOANDALIWA.

TUNAHESABIWA HAKI BURE KWA NJIA YA IMANI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Devis Julius administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments