ALIFANYIKA SADAKA KWA AJILI YETU!

ALIFANYIKA SADAKA KWA AJILI YETU!


Unapomwona maskini na kumhurumia na kuamua kumsaidia kwa kile alichopungukiwa, na kuifanya huzuni yake iondoke, hapo ni sawa na umeichukua huzuni yake, unapokutana na mtu ambaye hana chakula kabisa na ukaamuhurumia na kuamua kumpa kile chakula kidogo ulichokuwa nacho wewe ambacho ungepaswa ukile wewe, hapo ni sawa umeichukua njaa yake na kujitwika juu yako,Unapomwona mtu anakwenda kufa na wewe ukajitoa kufa kwa niaba yake, hapo ni sawa na umeichukua mauti yake.

Na kwetu sisi wanadamu ndio hivyo hivyo, kwa dhambi zetu tulistahili kufa, tulistahili kupotea kabisa lakini alitokea mmoja aliyetuhurumia ambaye hakustahili kufa, hakustahili kupotea, hakustahili kuadhibiwa akachukua hayo matatizo yetu yote na kujitwika juu yetu ili sisi tuwe huru..

Ndio hapo ili kwamba sisi tusife hana budi yeye kufa kwa niaba yetu, ili kwamba sisi tusiadhibiwe hana budi yeye kuadhibiwa kwa niaba yetu na hiyo yote ni kutokana tu na huruma yake kwetu sisi..


2 Wakorintho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”.

Ili kwamba upande mmoja uwe na vingi na lazima upande mwingine upungukiwe, ili kwamba sisi tupone ni lazima mmoja aangamie, hiyo ndiyo sababu Bwana Yesu Kristo alikufa kwa ajili yetu ili kwamba sisi tupate uzima wa milele…kulikuwa hakuna njia nyingine ya mkato ya sisi kuokolewa bila ya njia hiyo ya mmoja kuchukua matatizo ya mwingine…hata mahakamani pasipopatikana mdhamini hakuna kuachiwa huru..Ndio maana Biblia inasema..

Yohana 1:29 “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”.


Na kama alichukua matatizo yetu na kujitwika juu yake ni dhahiri kuwa kwa hali ya kawaida asingepaswa kufufuka tena, kwasababu makosa yetu sisi yalistahili adhabu ya milele…Lakini SIRI iliyopo kubwa hapo ni kwamba, Kristo alifufuka tena, kwa ukamilifu wake alisimama na kushinda hoja! Hivyo mauti ikashindwa juu yake, kuzimu ikashindwa juu yake, na hivyo akavishinda vyote na kufufuka bila dhambi yoyote..Hatia yote aliishinda.

Waebrania 9:28 “Kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu”.

Ni sawa na wewe ukutwe na makosa fulani yanayostahili kufungwa kifungo cha maisha, halafu atokee mtu na kuichukua kesi yako wewe na ashtakiwe kwa kupandishwa kizimbani kabisa na ahukumiwe na kufungwa, na kisha baada ya siku chache unamwona mtaani yupo huru, anakwambia kesi imekwisha! Wote tupo huru wala usiwe na wasiwasi… Lazima utajiuliza ni nini kimetokea?..aidha katoroka gerezani au labda kesi yake imerudiwa kusikilizwa tena na ikatokea kashinda hoja? Yatakuwepo maswali mengi yasiyo na majibu!..Na zaidi ya yote huyo kukuondolea wasiwasi anakwambia nimekabidhiwa UJAJI MKUU wa Taifa lote, hukumu zote zipo chini yake na wafungwa wote wapo chini yake.

Na ndicho kilichotokea kwa Bwana Wetu Yesu Kristo, alijitwika kesi yetu na kuhukumiwa kufa, ambapo sisi ndio tungestahili kufa lakini baada ya siku chache, alifufuka na kutoka kaburini na kuwaambia wanafunzi wake…Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani”.

Bwana Yesu kwasasa ndiye aliye mhukumu wa watu wote walio hai na waliokufa..

Matendo 10:40 “Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,

41 si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.

42 Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu”.

Lakini Neema hiyo Kristo aliyoibeba sio kwa watu wote!..Ni kwanini sio kwa watu wote? Ni kwasababu sio watu wote watapenda au watataka wokovu, wengine hawatataka kuokolewa, hivyo haiwezekani kuwalazimisha..Kila mtu Mungu kampa uhuru wa kuchagua apendalo, UZIMA au MAUTI.

Kumbukumbu 30: 15 “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya;”

Yesu ndio Nuru ya ulimwengu, chagua Nuru leo ambao ndio UZIMA, na si giza..Kwasababu wengi katika siku hizi za mwisho watachagua giza na wala si Nuru kwa hiari yao wenyewe..kama maandiko yanavyosema.

Yohana 3: 18 “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 

19 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. 

20 Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa”.

Kama hujasalimisha maisha yako kwake ni vyema ukafanya hivyo leo kwa kutubu dhambi zako zote kwa kudhamiria kutokurudia kuzifanya tena, na kutafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu Kristo, kwaajili ya ondoleo la dhambi zako(sawasawa na Matendo 2:38 inavyosema).na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi.

Kwa kufanya hivyo utakuwa umeutua mzigo wako wa dhambi na Bwana Yesu atakuwa amekuingiza miongoni mwa wale waliochukuliwa dhambi zao na hivyo utakuwa umenusurika na hukumu ya Mungu itakayoijilia ulimwengu wote kipindi sio kirefu kijacho..

Bwana akubariki sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

SADAKA ILIYOKUBALIKA.

MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.

TOFAUTI KATIKA YA ZAKA NA SADAKA NI IPI?


Rudi Nyumbani

 

 

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments