Title May 2019

UFUNUO: Mlango wa 20

Bwana wetu YESU KRISTO apewe sifa, karibu katika mwendelezo wa kitabu cha ufunuo, leo tukiwa katika ile sura ya 20, tunasoma..

Mlango 20.

1 Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake.

2 Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;

3 akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.

4 Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.

5 Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.

6 Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu.

Katika sura iliyotangulia tuliona jinsi Bwana Yesu Kristo alivyoyahukumu mataifa yote ya dunia katika ile vita kuu ya Har-magedoni, na kuharibu utawala wa dunia nzima, na tuliona pia zile roho mbili kati ya zile tatu chafu yaani roho ya yule mnyama na nabii wa uongo zilitupwa katika lile ziwa la moto, ikiwa imesalia roho moja ya lile joka ambalo ndiye shetani mwenyewe,

lakini katika sura hii tukisoma kuanzia mstari wa 1-3 tunaona shetani akikamatwa na kufungwa na kutupwa kuzimu, kwa muda wa miaka 1000, kumbuka huyu hakutupwa katika lile ziwa la moto kama wale wengine, huyu atafungwa kwa kitambo tu akingojea kuja kufunguliwa baadaye kwa kazi maalumu na kisha ndio aje kutupwa katika lile ziwa la moto aliyomo yule mnyama na nabii wa uongo.

Kuna vitu kadhaa vya kuzingatia hapo…

1) Malaika akishuka kutoka mbinguni. Huyu ni mmoja wa Malaika watakatifu, kumbuka kuna malaika walioasi ambao waliungana na shetani, na kuna waliobaki kuwa waaminifu kwa Mungu, na wametofautiana kimaumbile na uwezo, wapo malaika wa vita na wa sifa n.k na huyu ni mmoja wapo wa vita kwasababu tunaona ameshika mnyororo mkononi mwake..

2) mwenye ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake…Kumbuka Bwana Yesu Kristo baada ya kushinda mauti alizitwaa funguo zote za mauti na kuzimu, kwahiyo watu wote walio hai na waliokufa wapo chini yake yeye…anao uwezo wa kumshusha mtu kuzimu na kumpandisha, huo uwezo anao ndio maana siku za mwisho atawafufua watu wote ambapo wengine atawapa uzima wa milele wengine atawafufua kwa hukumu, hivyo kama anao huo uwezo ni lazima atakuwa na uwezo pia wa kumshusha mtu au kiumbe chochote kuzimu, na ndio hapa tunaona anampa huyu malaika funguo hizo ambazo ni amri ya kumkamata shetani na kumtupa kuzimu. Kuzimu iliyozungumziwa hapa ni SHIMO REFU LISILOKUWA NA MWISHO ( Bottomless Pit).

Huko hakuna raha sana, ni sehemu mbaya ya uchungu ambayo iliwekwa maalumu kwa malaika walioasi sio wanadamu…wanadamu walioasi sasa wanaokufa wanakwenda sehemu yao (kuzimu yao ambayo hiyo na yenyewe ina mateso lakini sio makali kama ya hawa malaika walioasi…(Mapepo na yenyewe yanayokuzimu yao ambapo yakifanya jambo lisilopasa yanakwenda kutupwa huko).

Ndio maana wakati Fulani Mapepo yalimsihi Bwana yasipelekwe shimoni, baada ya kumtesa Yule mtu wa Pwani ya wagerasi…yalijua Bwana tayari alichukizwa na jambo lile la kumtesa Yule mtu anazo amri za kufunga na kufungua..na yalijua endapo Bwana angetamka Neno tu la wao kwenda shimoni, habari yao imeisha….huko shimoni ni mahali ambapo wanafungwa na kuna mateso yasiyoyakawaida.

Luka 8: 30 “Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia.
31 Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni.
32 Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa”.

Na mpaka sasa kuna baadhi ya mapepo yamefungwa huko biblia inasema hivyo…kwa maelezo marefu kuhusu roho za mapepo zilizopo kifungoni bonyeza hapa >>  ‘Vifungo vya Giza vya Milele”

Sasa shetani naye atakamatwa na kwenda kutupwa shimoni, mule mapepo yalipomwomba Bwana asiwapeleke. Atakaa kule kwa muda wa miaka 1000, akionja uchungu mkali kuliko wa wanadamu..Na hatakwenda peke yake bali na mapepo yote pamoja naye…duniani hakutabaki na roho yoyote chafu..watakaa kule kwa maumivu kwa miaka 1000..Kumbuka hilo sio ziwa la Moto…ziwa la Moto litakuja kuzinduliwa rasmi na yeye mwenyewe(shetani) baada ya hukumu ya kiti cheupe ambayo tutakuja kuiona huko mbeleni.

Ufunuo 20:3 “akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache”.

Baada ya kufungwa tunaona pia ukatiwa muhuri juu yake, Nia ya kutiwa muhuri ni “ili asiwadanganye tena mataifa hata itimie miaka elfu”…Muhuri kazi yake ni kuzuia kitu Fulani kisiendelee juu ya huyo mtu/kitu kwa kipindi Fulani cha muda…Hapa shetani baada ya kufungwa nguvu za upotevu zinaondolewa juu yake, anakuwa hana kitu tena..

Kadhalika na watu wa Mungu wana Muhuri wanaotiwa na Mungu ambao huo Mungu anawatia ili wasipotee au wasidanganywe tena mpaka siku ya ukombozi wao..Na huo Muhuri sio mwingine zaidi ya Roho Mtakatifu…
Waefeso 4:30 ” Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.”

Baada ya hapo tunaona jambo lingine katika mstari wa nne,

“4 Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.”

Hapa kuna makundi mawili ya kuyatazama: kundi la kwanza ni la wale waliopewa viti vya enzi na kuketi juu yake kisha kupewa hukumu, na watu hawa si wengine zaidi ya wale watakatifu(bibi-arusi safi) waliokwenda na Bwana katika unyakuo, kama biblia inavyosema watakatifu ndio watakaouhukumu ulimwengu na Bwana Yesu pia alisema katika..

Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?

28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.”

Sasa hukumu wanayopewa hapo sio hukumu ya kuwahukumu wengine hapana! Bali hukumu inayozungumziwa hapa ni Mamlaka ya kutawala…hiyo ndio hukumu watakayopewa…Kila mmoja atapewa mji wake wa kutawala (na atakuwa anahukumu juu ya huo mji atakaopewa)..yeye ndiye atakuwa kama mkuu wa huo mji…Hiyo ndio maana ya kupewa hukumu hapo katika mstari wa 4.

Luka 19:16 “Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.

18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

19 Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano”.

Hapo ulimwengu mpya Bwana anaozungumzia ni ule utawala wa miaka 1000, Kristo atakapotawala na watakatifu wake,

Kundi la pili ni wale waliofufuliwa ambao waliuawa na mpinga-kristo katika ile dhiki kuu, kwa kukataa kusujudia sanamu yake na kupokea chapa katika vipaji vya nyuso zao, hapa watakuwa ni wayahudi na wakristo, hawa nao watafufuliwa na kupewa miili ya utukufu na kuingia katika ule utawala wa miaka 1000 pamoja na Kristo,huo ndio ufufuo wa kwanza, lakini wafu wengine wote waliosalia ikiwemo watu wote walioipokea ile chapa ya mnyama pamoja na watu wote waovu, hawatafufuliwa mpaka ile miaka 1000 itakapoisha, biblia inasema Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. Kumbuka hatutakaa mbinguni milele, bali biblia inasema makao yetu yatakuwa na Bwana hapa duniani milele.

Kuna hatari kubwa sana ya kukosa unyakuo, au kufa katika dhambi sasa, kutakuwa hakuna nafasi ya pili, inatisha sana!!

UTAWALA WA MIAKA 1000

Hivyo kwenye utawala wa miaka 1000 Bwana Yesu atairejesha dunia katika hali yake ya mwanzo kama ilivyokuwa pale Edeni, amani itarejea duniani, wanyama wakali hawatakuwa na madhara, simba atakula nyasi, mwanakondoo atachunga na simba. ukisoma

Isaya 11:6 inasema ” Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.

7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe.

8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.

9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.”

Kwahiyo Kifo hakitakuwa na nguvu, ingawa kwa watakaokaidi wachache na kwenda kinyume na utawala adhabu kama kifo zitakuwepo, kwamaana Bwana atawachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma maana biblia inasema ..

Isaya 65:

18 Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.

19 Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza.

20 Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa.

21 Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.

22 Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.

23 Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na Bwana, na watoto wao pamoja nao.

24 Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia.

25 Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng’ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema Bwana.” 

Na Kristo pamoja na watakatifu wake ndio watakaotawala mataifa yote, kumbuka ni wale tu watakaoshinda,

ufunuo 2:26″Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,

27 naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.

28 Nami nitampa ile nyota ya asubuhi. ” na pia BWANA YESU anasema ufunuo 3:21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. “

Amen!.

Kwa maelezo marefu juu ya utawala huu bofya hapa ‘utawala wa miaka 1000”

VITA VYA GOGU NA MAGOGU.

Tukiendelea na mistari inayofuata tunasoma..

Ufunuo 20:7-15

“7 Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;

8 naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.

9 Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala.

10 Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo.

Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.

Hapa tunaona baada ya ile miaka 1000 kuisha shetani sasa anafunguliwa tena ili awadanganye mataifa ambao hawakuwa wakamilifu katika njia zao wakati wa utawala wa AMANI wa BWANA wetu YESU KRISTO , ambao wingi wao ni kama mchanga wa bahari, kwahiyo hili ni kundi la watu waliozaliwa ndani ya ule utawala na ndio hao wataizingira kambi ya watakatifu kutaka kufanya vita nao lakini kabla hawajafanya hivyo biblia inasema moto utashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza wote, na ndipo shetani akakamatwa na kutupwa katika lile ziwa la moto walipokuwepo yule mnyama na nabii wa uongo. Na kilichobaki itakuwa ni hukumu ya watu wote waovu ambao hawakuwepo katika ufufuo wa kwanza. Na ndio tunaendelea kusoma..

HUKUMU YA KITI CHEUPE

Ufunuo 20:11-15″

11 Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.

12 Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.

13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.

15 Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. “

Hii ni hukumu ya mwisho ambayo wafu wote waliosalia makaburini watafufuka kila mmoja atahukumiwa kwa matendo yake, kumbuka hapo vilifunguliwa vitabu vya aina mbili.1)KITABU CHA UZIMA 2) VITABU VINGINE.

Sasa anaposema vitabu anamaanisha ni vingi, na hivi si vingine zaidi ya maisha ya kila mmoja wetu alivyoishi hapa duniani,na kile kitabu cha uzima kipo kimoja tu na si kingine zaidi ya NENO LA MUNGU(biblia), na kama unavyosoma hapo kama jina lako halikuonekana katika kile kitabu cha uzima ikiwa na maana kuwa kama MATENDO YAKO(ambayo ndio kitabu chako) hayaendani na kile KITABU CHA UZIMA(yaani biblia) sehemu yako itakuwa ni katika lile ZIWA LA MOTO. Kumbuka biblia inasema “sisi ni BARUA inayosomwa na watu wote” ikiwa na maana maisha yetu ni “KURASA ZINAZOANDIKWA” na kila siku tunafungua ukurasa mpya, siku utakapokufa kitabu chako kitakuwa kimeisha na kufungwa…kinasubiriwa kufunguliwa tena katika ile siku ya hukumu, sasa jiulize! je leo hii kitabu chako unakiandikaje? je maisha yako ya jana na ya leo yanaendana na kile kitabu (Neno la Mungu). Angalia muda unavyokimbia usije ukasema nitatubu siku nitakayokaribia kufa au nikiwa mzee, wakati huo pengine kitabu chako kitakuwa hakina maana tena au hakikidhi viwango vya kufanana na kile kitabu cha uzima, na hiyo ndio maana ya “KUKOSEKANA JINA LAKO KATIKA KILE KITABU CHA UZIMA”.

Na baada ya haya yote kuisha BWANA YESU atakuwa amekwisha waweka maadui zake wote chini na adui wa mwisho ni MAUTI, Kisha baada ya hapo UMILELE unafunguliwa usio kuwa na dhambi,wala vita,wala shida, wala waovu,wala maumivu,wala shetani wala mapepo. Ni MBINGU MPYA NA NCHI MPYA, tutaendelea kujifunza katika sura zilizosalia juu ya hayo.

Je! Leo hii bado unaendelea kuishi maisha ya kutokujali, unavaa vimini,unakuwa mzinzi,mlevi,mtu wa mizaha,msengenyaji, mpenda anasa, mtukanaji,n.k kumbuka biblia ilishaonya kuwa watu kama hao sehemu yao itakuwa katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti, hivyo ndugu maombi yangu ni utubu umgeukie Bwana Yesu angali bado unayo nafasi ya kukiandika kitabu chako vizuri.

Mungu akubariki.

Kwa mwendelezo >>UFUNUO: Mlango wa 21

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada zinazoendana..


KITABU CHA UZIMA

KITABU CHA UKUMBUSHO

UTAWALA WA MIAKA 1000.


Rudi Nyumbani

Print this post

JINSI EDENI ILIVYOKUWA.

Shalom, mwana wa Mungu karibu tujifunze maneno ya Uzima, yaliyo taa ya miguu yetu (Zaburi 119:105). Leo tutaona mwonekano wa Edeni ulivyokuwa hapo mwanzo na sasa ulivyo. Ukisoma kitabu cha Mwanzo, utaona baada ya Mungu kumaliza kuumba mbingu na nchi na vitu vyote tunaona alifanya tena kazi nyingine ndogo ya ziada, nayo ni kutengeneza BUSTANI. Bustani hii Mungu aliifanya mashariki mwa Eneo linaloitwa Edeni, aliitengeneza kuwa makao ya kiumbe chake maalumu kinachoitwa Mwanadamu. Mungu alikipa heshima ya kipekee mpaka kumtengenezea makao ndani ya makao, Bustani hii ilikuwa ni tofauti kabisa na maeneo mengine ya Dunia yaliyosalia.

Hivyo pale bustanini Mungu aliweka kila kitu ndani yake kinachomfaa na kumtosheleza mwanadamu.. Edeni tunaweza kusema ulikuwa ni kama mji mkuu wa Adamu, na ile Bustani ni Kasri lake. Wanyama wote na viumbe vyote viliweza kuishi nje ya Edeni lakini Adamu hakuishi nje na Bustani ile Mungu aliyompa.

Mwanzo 2:8 “Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.

9 Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

10 Ukatoka mto katika Edeni wa kuitilia bustani maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne.

11Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu;

12 na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham.

13 Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi.

14 Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli; ndio unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati.

15 Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.

Zipo sababu kwanini Mungu hakumwambia Adamu akaishi mahali popote tu anapopapenda duniani. Sababu mojawapo ni kwamba huko kwingine Mungu hakuweka utukufu wake wa kiungu kama ilivyokuwa pale Bustanini Edeni, na ndio maana Mungu alipotaka kuzunguza na Adamu alizungumza naye pale bustanini tu. Na pia kumbuka mahali popote utukufu wa Mungu upo, mahali hapo kunakuwa na (UTAJI) WIGO fulani au ULINZI Fulani. Adui au chochote kisichohusika hakiwezi kupenyeza.

Ili kulielewa hili vizuri tunaweza kujifunza katika mambo yanayotuzunguka ya kila siku. Siku hizi kuna kilimo kijulikanacho kama “ kilimo cha Banda-kitalu” kwa lugha ya kigheni iliyozoeleka na wengi kinaitwa GREEN HOUSE farming. Kilimo hichi hakina tofuati na kile kingine isipokuwa tu, hichi mmea au mboga, au matunda, au maua huwa yanawekwa katika banda maalamu lililozibwa pande zote katika uzalishaji wake. Na wanafanya hivyo sio kwasababu wamependa tu iwe hivyo hapana, lakini kama wewe ni mkulima mzuri utajua kuwa kulima mazao yako katika green-house, kuna faida kubwa kuliko kulima huria, sababu kubwa kwanza ni kinazuia wadudu waharibifu wa mazao kuvamia shamba, pili kinazuia mionzi mikali ya jua kuharibu mimea, hivyo inasaidia kuhifadhi unyevunyevu na kutokutumia gharama nyingi za kupiga madawa, kwa ajili ya wadudu. Na matokeo yake ile mimea huwa inakuwa vizuri, yenye afya, na mwisho wa siku kuleta mazao mengi kuliko hata Yule ambaye yalilimwa mabondeni tu. Huyu anaweza akajiona analoshamba kubwa, lakini mimea ikiaanza kumea tu wadudu waharibifu wanakuja, na hivyo atajikuta anahangaika kupiga madawa, mimea inaliwa na kukosa mvuto na hata akifanikiwa kupeleka sokoni bidhaa yake hainunuliwi kwasababu inakuwa haina ubora unaostahili. Maua mengi ya thamani kama Maua Rose, yanalimwa ndani ya Green house, nje na hapo matokeo yatakuwa hafifu, na ndio maana unaona ubora wake na thamani yake ni kubwa.

Sasa chukua mfano huo huo urudishe pale Edeni, Mungu alimweka Adamu katika GREEN-HOUSE yake, ambayo ndio ile bustani, akamwekea wigo mkubwa wa utukufu wake, na ndio maana chakula na kila kitu kilikuwa kinajiotea tu chenyewe katika ubora wote ndani ya bustani ile, hiyo yote ni kwasababu hakukuwa na viumbe viharibifu vilivyoingia na kugeuza mambo. Lakini sasa baada ya wao kumpa nafasi NYOKA, nyoka akawadanganya walitoboe HEMA lao, na walipofanya vile tu, basi lile hema lote likapasuka, kukawa hakuna ulinzi tena wowote wa bustanini, wanyama hawaribifu wakaanza kuingia. Ndio tunaona pale Mungu anaanza sasa kuwaeleza matokeo yatakayofuatana nao kwa kosa walilolitenda..Adamu atakula kwa jasho, nchi itamzalia michongoma, na mwisho wa siku atakufa tu.

Sasa hayo yote yalikuwa katika mwili, ingekuwa ni heri tu kama yangeishia hapo, lakini fahamu lengo kubwa habari nzima inayoelezwa hapo lengo lake ni kuturudisha katika roho, ni kutuonyesha kwa lugha ya vitendo vya kimwili mambo yaliyofanyika rohoni eneo lile..Sasa katika huu upande mwingine wa roho, ni Shetani mwenyewe alimvaa nyoka ili kumshawishi mwanadamu avunje agano la ulinzi waliowekewa na Mungu katika roho. Kumbuka shetani alipoasi yeye pamoja na malaika zake alitupwa chini, hivyo alikuwa yupo huku chini katika giza, lakini alipoona Mungu kaitengeneza tena nchi upya na kila kitu amepewa mwanadamu, huku yeye hana chochote anasubiri hukumu yake ya mwisho. alitumia ujuzi kutafuta namna ya kuoondoa ulinzi wao ili aingie na kuuharibu uzao wa Mungu kama alivyofanya huko mbinguni..(Yohana 8:44 ….Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo;). kama vile tu wale wadudu wahaaribifu wa mazao.

Na alipofanikiwa kuwashawishi Adamu na Hawa ili wauvunje ulinzi wao kwa Mungu, ndipo akapata nafasi ya kuingia na kuanza kuuwa uzao wa Mungu kiroho. Sasa mambo kama dhambi na uasi vikaanza kuingia, maovu ya kila namna yakaanza kujaa ndani ya wanadamu, vitu ambavyo mwanadamu hakuwahi kuwa navyo, uuaji sio asili wa mwanadamu, uchawi sio asili ya mwanadamu n.k…Vifo vya kiroho vikawa vingi.

Mwanzo 3:22 “Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele;

23 kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.

24 Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka hukona huko, kuilinda njia ya mti wa uzima”.

Lakini ashukuriwe Mungu, Edeni ya rohoni haikufutwa kabisa, bali Mwanadamu alifukuzwa tu, hii ikiwa na maana kuna wakati Mungu aliuweka kuwa watu wake watapata njia ya kuirudia Edeni hiyo. Na leo hii tunafahamu kuwa njia ya kurudia huko ni BWANA YESU TU.

Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”.

Shetani naye hajalala anaendelea kupiga vita ili kuzuia watu wasiirudie Edeni yao anafanya hivyo kwa nguvu ili azidi kuwatesa na kuwaua rohoni na mwisho wa siku waende kuzimu..Ndugu YESU alishalipa gharama kwa ajili yako, kwanini unaruhusu mwingine achezee roho yako kama mpira?. Ukiwa bado unaendelea kuteswa na dhambi hiyo ni umejitakia wewe mwenyewe, ikiwa bado unaendelea kuteswa na mapepo na nguvu za giza hiyo ni umejitakia wewe mwenyewe, ikiwa bado unaishi kwa mashaka na hofu kwamba ukifa leo hujui utakwenda wapi hiyo ni umejitakia mwenyewe.. Kwasababu Yesu alishatuita na kutuahidia raha, tumaini na uzima wa milele bure..yeye ndiye safina yetu sasa, yeye ndiye green house yetu halisi ukiwa ndani yake una uhakika wa ulinzi wa kutosha na roho yako itakuwa salama.

Ushauri wangu ni kuwa kama bado hujayakabidhi maisha yako kwa Bwana kwa kumaanisha kabisa, fanya hivyo leo haraka, kwani shetani hana urafiki na wewe anataka ufe leo katika hali hiyo hiyo na mwisho wa siku uende kuzimu. Ukiwa ndani ya YESU utakuwa na amani na tumaini,..Yeye mwenyewe ameahidi kukupa raha nafsini mwako. Hivyo piga hatua utubu dhambi zako hapo ulipo na yeye atakupokea, Kisha chukua hatua nyingine ya Imani ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamwishwa kwa jina la YESU KRISTO ikiwa bado hujafanya hivyo. Na Mungu atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu.

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

Print this post

UTAWALA WA MIAKA 1000.

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze maandiko matakatifu, kama Biblia inavyosema katika Zaburi 119:105 “ Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.”..Ikiwa na maana Neno la Mungu ni mwongozo wetu, tukilijua Neno la Mungu hata tukikosa vitu vingine vyote bado tutaishi. Amen.

Leo tutajifunza juu ya utawala wa miaka 1000. Swali utawala wa miaka 1000 ni nini?…Utawala wa miaka 1000 ni utawala ambao utakuja kuanza hapa duniani, ambapo Bwana wetu Yesu Kristo atatawala na wateule wake katika hii dunia..Maandiko yanasema mbinguni hatutakaa milele, tutakaa kule kwa kipindi cha Miaka 7 tu na baada ya hapo tutarudi hapa duniani kutawala kwa muda wa miaka 1000, na baada ya hiyo miaka 1000 kuisha, ndipo kitu kinachoitwa MUDA kitasimama, na umilele utaaanza.

Hatua kanisa inayosubiria sasa, ni unyakuo, ambao upo karibuni sana kutokea, watakatifu waliokufa katika Bwana watafufuliwa, wataungana na watakatifu walio hai na kwa pamoja tutakwenda kumlaki Bwana wetu mawinguni. Huko mbinguni mambo yatakayokuwa yanaendelea huko ndio kule (jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia), ni mambo mazuri na mapya..Biblia inapafananisha na mahali pa karamu. Ni kama mahali pa mwaliko, kama ulishawahi kualikwa kwenye sherehe labda harusi unaweza ukaelewa kwa sehemu furaha iliyopo kwenye harusi.

Sasa Wakati karamu ya mwanakondoo inaendelea mbinguni, huku chini duniani Mpinga-Kristo atanyanyuka kuanza kufanya kazi zake, atafanya kazi kwa muda wa miaka 7, ambapo miaka mitatu na nusu ya kwanza ataudanganya ulimwengu mzima kupokea chapa ya mnyama kwa injili yake ya uongo ya amani.

Kwa kivuli cha kuleta amani atafanikiwa kuwadanganya wengi wapokee chapa ya mnyama..na baada ya hiyo miaka mitatu na nusu ya kwanza kuisha itaanza miaka mingine mitatu na nusu, ambayo hiyo itakuwa ni dhiki kwa wale waliokataa kuipokea hiyo chapa yake…Na mwishoni kabisa mwa hiyo miaka mitatu na nusu kuna siku kadhaa zitaongezeka pale, kama siku 75 hivi (Daniel 12:12) ambazo hizo zitahusiana na kumwagwa kwa ghadhabu ya Mungu juu ya nchi kwa wale wote walioipokea ile chapa ya mnyama.(kumbuka hii ghadhabu ya Mungu inahusiana na vile vitasa saba, ufunuo 16, kama utakuwa hujajua vitasa 7 ni nini unaweza ukanitumia ujumbe inbox nikutumie somo juu ya hilo). Na ndani ya hizo hizo siku ndio vita ya Harmagedoni itakapopiganwa.

Hivyo Baada ya hukumu ya Mungu kupita juu ya nchi, na vita vya Harmagedon kupita, duniani watu wengi watakufa sana..biblia inasema watu wataadimika kuliko dhahabu (Isaya 13:12)…kama ilivyoshida kuziona au kuzipata dhahabu ndio siku hiyo itakavyokuwa shida kumwona mwanadamu mmoja chini ya jua…labda siku hiyo mji wa Dar es salaam itabakiwa na watu watano tu! Pamoja na idadi yake ya watu kuwa mamilioni..watu wengi sana watakufa walioipokea ile chapa ya mnyama, na baada ya kufa biblia inasema sehemu yao itakuwa ni katika lile ziwa liwakalo moto (Ufunuo 14:9-10).Hivyo watakaa huko kuzimu pamoja na watu wengine waovu wakisubiria ufufuo wa wafu ambao utakuja mara baada ya ule utawala wa miaka 1000 kuisha, wote wahukumiwe kisha watupwe kwenye lile ziwa la moto.

Sasa utendaji kazi wa Mungu upo hivi, huwa haaribu na kuleta kitu kipya, hapana! Bali huwa anakiponya kile kitu na kisha kukifanya kuwa kipya zaidi…hiyo ndio njia ya Mungu ya kufanya mambo yote kuwa mapya….kwamfano Mtu anapoumwa ili Mungu amrudishe katika hali yake hamwui Yule mtu na kumtengeneza upya..hapana, anachofanya ni kukirejesha kile kitu kama kilivyokuwa hapo kwanza, ndio hapo utaona mtu alikuwa anauvimbe ghafla unapotea, alikuwa ana ugonjwa ghafla anapona n.k..Hata sisi tutakaponyakuliwa hatutauliwa roho zetu na miili yetu na kuumbwa upya hapana! Tutakuwa ni sisi sisi, isipokuwa tutavikwa miili mingine ya utukufu, ile ya kwanza haitauliwa hapana, bali tutavikwa juu mipya juu yake hii, Ndio maana siku ile ya unyakuo wafu watafufuliwa kwanza warudi katika hali zao walizokuwa nazo wakiwa hai. Kisha miili yao ikutane na ile miili ya mbinguni wafanywe kuwa bora zaidi..siku hiyo ndiyo utajua lile neno Bwana alilolisema kuwa hautapotea unywele hata mmoja wa vichwa vyenu, litatumika wapi..(Luka 21:18)

Kadhalika na dunia tunayoishi sasa imeharibiwa sana na shetani na wanadamu…Lakini Mungu hana desturi ya kufuta na kuumba upya, bali anadesturi ya kuponya…yaani kile kile kitu anakirudisha katika hali yake ya kwanza,

sasa kutokana na anguko la mwanadamu, ardhi ililaaniwa, Hivyo aliweka njia ya kuiponya hii dunia na kuirudisha katika hali yake kama ilivyokuwa pale Edeni, ulikuwa ni mpango wa Mungu tangu zamani, kama ilivyokuwa mpango wa Mungu kumrudisha mwanadamu awe karibu na yeye tena.

Kwahiyo kitendo cha kuisafisha dunia, ni kuirudisha dunia katika hali yake ya kwanza,

Ni baada ya vile vitasa vitano vya kwanza vya ghadhabu ya Mungu kumiminwa juu ya wale wanadamu waliobaki duniani walioipokea ile chapa ya mnyama,..na kile kitasa cha sita ndio kinahusu vita vya Harmagedoni (ufunuo 16:12-16) ambayo itapiganwa katika Taifa la Israeli mahali panapojulikana kama Megido..Wakati huo Mataifa yote ulimwenguni yakiongozwa na mataifa kutoka maawio ya jua yaani China, korea, Japani na mengineyo yatakusanyika kwenda kufanya vita na taifa la Israeli, akilini mwao wakidhani wanapambana na Israeli kumbe wanapambana na Bwana Yesu Kristo mwenyewe pamoja na watakatifu wake ambao watakuwepo kwa mfumo wa kimalaika wakati huo…lakini Baada ya muda mfupi sana vita vitakwisha kwasababu Yesu Kristo sio mwanadamu…atawaua wote mara moja kwa Neno lake, na damu nyingi sana zitachurizika kama mto maeneo yale…watashangaa tu kuona maiti zilizochinjika chinjika zimelala chini, na aliyewaua haonekani…

kama ilivyokuwa katika kipindi cha mfalme wa Ashuru katika (2Wafalme 19:35), ambapo alimtukana Mungu wa Israeli, na malaika wa Bwana akashuka kwenye kambi ya jeshi lake, akaua wanajeshi wote ambao idadi yao ilikuwa ni watu laki moja na elfu themanini, walipoamka asubuhi walikuta maiti tu! Na aliyewaua hajulikani..Ndivyo itakavyokuwa katika vita vya Harmagedon, biblia inataja majeshi ya wapanda farasi watakaoanguka siku hiyo watakuwa ni elfu ishirini mara elfu kumi hiyo ni sawa na watu milioni 200, watakutwa wamechinjika vibaya sana na damu yao nyingi…Ndipo ndege wote wanaokula mizoga watakusanyika kuja kula nyama zao.

Ufunuo 19: 11 “Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.

12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.

13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.

14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.

15 Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.

16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA Bwana WA MABwana.

17 Kisha nikaona malaika mmoja amesimama katika jua; akalia kwa sauti kuu, akiwaambia ndege wote warukao katikati ya mbingu, Njoni mkutane kwa karamu ya Mungu iliyo kuu;

18 mpate kula nyama ya wafalme, na nyama ya majemadari, na nyama ya watu hodari, na nyama ya farasi na ya watu wawapandao, na nyama ya watu wote, waungwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa.

19 Kisha nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake”……………..

21 na wale waliosalia waliuawa kwa upanga wake yeye aliyeketi juu ya yule farasi, upanga utokao katika kinywa chake. Na ndege wote wakashiba kwa nyama zao.

Sasa baada ya maangamizi hayo ya mwisho ya duniani kuisha, yatakayofanywa na Bwana mwenyewe , hapo ndipo ishara yake itaonekana mbinguni, jua litazima ghafla, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, nyota zitajificha, kutakuwa na tetemeko kubwa la ardhi, ambalo halijawahi kutokea tangu dunia kuumbwa..siku zote Huwa Bwana Anapojidhihirisha hahitaji mwanga, kwasababu yeye mwenyewe ni NURU kila kitu kitatii chini yake… dunia itakuwa giza tororo na kutoka mawinguni Bwana ataonekana pamoja na kundi kubwa la watu walionyakuliwa waking’aa kama jua…Hapo ndio kila jicho litamwona.(yaani hao watu wachache waliobahatika kusalimika duniani watamwona LIVE akishuka mawinguni), …Litakuwa ni jeshi kubwa, ambalo litatoka mbinguni wakiwa na mavazi meupe na wamepanda farasi..

Bwana atashuka hapa duniani na kuanza kuitengeneza tena upya…Majangwa yatabadilika na kuwa bustani nzuri zenye misitu yenye kuvutia, ardhi haitazaa michongoma tena, jua halitakuwa kali tena, nchi itazaa yenyewe kama hapo mwanzo, maji ya bahari yatapungua na sehemu ya nchi kavu itaongezeka, na maji hayatakuwa na chumvi tena, hakutakuwa na matetemeko wala vimbunga, wala tatizo la maji, nchi itatoa chemchemi nyingi sana…chakula kitakuwa tele…

Kwasababu kwa vile vitasa saba, ghadhabu ya Mungu imetimilika (Ufu.15:1)..hakutakuwa tena na ghadhabu au hasira ya Mungu juu ya dunia baada ya kitasa cha saba…hivyo wale wachache waliosalimika wasiokufa katika yale mapigo, watapata nafasi ya kuingia katika huo utawala wa miaka 1000, wakiwa na miili yao ya asili, yenye kusikia njaa, yenye tamaa ya mwili nk. Wakati huo Shetani atafungwa asiwadanganye tena kwa muda wa miaka 1000, watu hawa watakuwa watu wazuri kwa kitambo kwasababu shetani amefungiwa (Ufu.20:1-3)…Na kwasababu utawala wa amani unaanza wataishi kwa amani, na watazaliana na kuwa na watoto katika Edeni ya Bwana. Na wataongezeka na kuwa wengi mpaka kuijaza dunia.

Na laana Bwana aliyoipiga nayo dunia itafutika…

1) Laana ya kuzaa kwa uchungu.(wanawake hawatazaa kwa uchungu tena).wala wanyama

2) Laana ya kula kwa jasho…(Nchi itazaa yenyewe), hawa watoto waliozaliwa ndani ya huo utawala hawatalima kwa uchungu wala kwa ugumu kama sasa…

3) Uadui kati ya watu na wanyama utaondolewa na Bwana..Biblia inasema katika utawala wa miaka 1000, simba hatakula nyama tena, atakula majani, wala wanyama hawatakulana, na mtoto atacheza na nyoka na wala hawatadhuriana n.k kama ilivyokuwa Edeni.

Isaya 11: 6 “Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.

7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe.

8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.

9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari”.

Isaya 65:25 “Pia inatabiri jambo hilo hilo “ 25 Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng’ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema Bwana.”

Sasa hawa watoto watakaozaliwa katika utawala huo wa miaka 1000, biblia ndio inasema tutakaowatawala….hao ndio watakaoitwa mataifa wakati huo… Sisi tuliorudi na Bwana kutoka mawinguni tutakuwa wafalme juu yao, na Yesu Kristo atakuwa Mfalme wa Wafalme. Sisi hatutakuwa na miili kama ya kwao ya asili, kwasababu sisi tumeshavuka huko, na kupewa miili ya utukufu..miili ambayo ipo kama ya malaika, isiyozeeka, isiyo na tamaa,isiyosikia njaa, isiyochoka, kwetu sisi kutakuwa hakuna kuoa wala kuolewa wala kuzaliana, tutakuwa kama malaika katika hii dunia…utukufu wetu utakuwa mbali sana na hawa watu watakaozaliwa katika utawala huo..

Hapo ndipo litatimia lile neno katika

Luka 19:16 “Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya MIJI KUMI.

18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

19 Akamwambia huyu naye, WEWE UWE JUU YA MIJI MITANO”.

Wale waliokuwa waaminifu kwa Bwana watapewa miji mingi zaidi ya kutawala zaidi ya wale wengine waliokuwa wavivu katika masuala ya Kimungu n.k

 

Mathayo 19: 27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?

28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli”.

Ulimwengu mpya unaozungumziwa hapo ndio huo utawala wa miaka 1000.

Katika utawala huo, Dunia itakuwa na lugha moja na usemi mmoja…Bwana ataiondoa ile laana aliyowalaani wanadamu pale Babeli, ya kuchafuliwa lugha na usemi ambayo mpaka sasa inaendelea kufanya kazi….ndio maana utaona kama kuna nguvu Fulani inayotusogeza mbali sisi kwa sisi tusifanane kiusemi na kitabia inayotokana na lugha…kwamfano utaona hii hii lugha ya Kiswahili tunayozungumza ukienda Kenya ina lafudhi tofauti na Tanzania, vivyo hivyo watu wanaotoka kanda za kaskazini, wanaongea kwa lafudhi tofauti na watu wa kanda ya ziwa na pwani ni tofauti…sasa hii nguvu inayobadilisha lafudhi unaposogea umbali kidogo na jamii ya watu wako ndio hiyo hiyo iliyotokea pale babeli…isipokuwa pale babeli haikuishia kubadilisha lafudhi tu, bali hata maneno kabisa…na kadhalika siku zinavyozidi kwenda lugha moja inavunjika na kuzaa nyingine hivyo hivyo, na itaendelea hivyo mpaka mwisho wa dunia…ndio maana utaona lugha zote za kibantu zinafanana..kuonesha kuwa kwa namna moja au nyingine zilitoka kwenye lugha moja isipokuwa kuna nguvu Fulani iliivunja na inaendelea kuivunja vunja kwa jinsi muda unavyozidi kwenda.

Sasa Mungu aliiachilia hiyo nguvu ya machafuko makusudi kabisa..ili watu wasikae pamoja wakakusudia kutengeneza miungu ya kuiabudu..kama pale babeli. Mungu anatujua sisi wanadamu nia zetu na anaona mbali..Kwa usalama wetu haina budi iwe hivyo tu.

Lakini katika utawala wa miaka 1000 hiyo itaondolewa…ndio maana unaitwa utawala wa Amani wa Miaka 1000…dunia yote itajawa na kumjua Mungu..Kristo atakapotawala kila kitu kitatii..kutakuwa hakuna wakalmani…ni kusikia na kutenda. Kutakuwa hakuna vita wala mafarakano, wala mapishano ya usemi na watu watamtii BWANA YESU na wafalme wake pasipo shuruti..na wakati huo huo itakuwa ni sehemu ya amani na furaha kama ilivyokuwa pale Edeni, wote watakuwa na nia ya kumjua Mungu.

Ufunuo 20:1 “Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake.

2 Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;

3 akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.

4 Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.

5 Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.

6 Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu”.

Sasa mwishoni mwa hiyo miaka 1000 kuisha, Bwana Yesu atamruhusu shetani afunguliwe kwa kitambo kidogo..kwanini aruhusiwe? Ni ili awajaribu mataifa, awajaribu hao watoto waliozaliwa ndani ya huo utawala…Maana ni sheria ya Mungu kila kiumbe chake kijaribiwe…hata sasa tunajaribiwa sasa na huyo huyo shetani…sharti na wao wajaribiwe..shetani atakapofunguliwa wapo baadhi watakaodanganyika naye na wachache watakaomkataa na kudumu katika kuutii utawala wa amani wa Bwana Yesu Kristo..

Wengi watadanganyika kama tu shetani anavyowadanganya wengi leo wasimwamini Bwana Yesu Kristo na uweza wake..kwahiyo wataungana pamoja na kutaka kuleta mapinduzi juu ya utawala wa Kristo..magugu na ngano vitajitenga, kabla hawajajaribu kufanya lolota…litatokea kama lililotokea HARMAGEDON. Moto utawateketeza pale pale walipo na uwingi wao, hatapona hata mmoja..wachache waliokataa kujiunga na hilo jeshi kushindana na Bwana, watahifadhiwa na watakuwa wameshinda.

Ufunuo 20:7 “Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;

8 naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.

9 Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala.

10 Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.”

Baada ya hilo jaribio kuisha..kutakuwa hakuna tena kizazi kingine cha wanadamu kilichosalia kwa ajili ya kujaribiwa, hivyo wakati uliobakia ni wa hukumu. Kila mtu kulipwa kama kazi yake ilivyo.

Kuanzia mwanzo wa wanadamu wote mpaka mwisho, watafufuliwa..walioko kuzimu watafufuliwa…Vitabu vitafunguliwa (ambacho kila mtu ana cha kwake). Na kitabu kimoja cha uzima kitafunguliwa..na endapo mtu hakuonekana jina lake kwenye kitabu cha uzima atatupwa katika lile ziwa la moto,[ kama hujajua nini maana ya jina lako kuonekana kwenye kitabu cha uzima unaweza ukanitext inbox nikutumie somo lake kwa urefu]…

 

Ufunuo 20:11 “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.

12 Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.

13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.

15 Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto”.

Siku hiyo watu wengi wataona sababu ya wao kupelekwa katika ziwa la moto. Itakuwa ni uchungu usioelezeka.Kwasababu kila kitu kitawekwa wazi mbele ya mashahidi wengi.

Na baada ya hukumu kuisha, itakuja mbingu mpya na nchi mpya..Katika mbingu mpya na nchi mpya..Ni hii hii dunia isipokuwa itavikwa na utukufu usioelezeka..itakuwa ni sehemu nzuri zaidi ya mbinguni…Huko kutakuwa hakuna tena muda..ni mambo mapya..wala hakuna bahari tena.

Ufunuo 21:1 “Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena.

2 Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.

3 Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.

4 Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.

5 Na yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi akasema, Tazama, nayafanya yote kuwa mapya. Akaniambia, Andika ya kwamba maneno hayo ni amini na kweli.

6 Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.

7 Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Umempa Bwana maisha yako? Mwisho wa mambo yote umekaribia, hutasema siku hiyo hujasikia, biblia inasema walevi, waasherati, waabudu sanamu, sehemu yao ni katika lile ziwa la moto..

Neema ya Kristo iwe pamoja nawe.

Print this post

JINSI BWANA ALIVYOWACHAGUA MITUME WAKE.

Jina kuu la YESU KRISTO litukuzwe ndugu yangu. Karibu tujinze maneno ya uzima.

Cha kushangaza, Bwana Yesu alipokuwa duniani hakulenga kundi Fulani maalumu la watu ili wawe wanafunzi wake, jaribu kufikiria siku ile alipokesha usiku mzima kumwomba Mungu ampe watu wa kufuatana naye, tulitazamia angekwenda kuchukua watu watakatifu katikati ya waandishi na mafarisayo, lakini cha kustaajabisha alienda kuchukua watu ambao wangeweza kuwa ni hatari sana kwake na katika jamii inayomzunguka.

Embu mtafakari huyu mtu anayeitwa Simoni Zelote. Hilo neno Zelote sio jina la Baba yake, hapana bali jina la CHAMA CHA WAPIGANIA DINI ya kiyahudi kilichokuwa Israeli wakati huo ndio walioitwa WAZELOTE. Ni watu ambao wakati wote walikuwa wanaupinga utawala wa Rumi, na walitumia silaha, na kila mbinu ili kuidondosha dola ya Rumi iliyokuwa inatawala Israeli, na Uyahudi unyanyuke. Hivyo watu hawa walikuwa ni hatari na Simoni huyu alikuwa ni mmojawapo, kwasasa tunaweza kuwaita al-quida wa Wayahudi. Lakini Yesu alikwenda kumchagua na kumfanya kuwa mwanafunzi wake.(Luka 6:12)

Embu mtafakari Mathayo mtoza ushuru. Kumbuka zamani zile watoza ushuru wote walikuwa wanajulikana kama ni watu wenye dhambi, watu wa rushwa na dhuluma sikuzote. Mathayo alikuwa ni tajiri na pia msomi, mtu wa ofisini, aliyekuwa analitumikia taifa la Rumi kule Israeli kwa kulikusanyia Kodi, cha ajabu anakwenda kukutana na maadui wa Warumi, Simoni Zelote. Lakini Yesu anawakutanisha wote pamoja.

Mtafakari tena Yuda: Ni mtu ambaye alikutwa katika tabia zake za wizi na tamaa za viwango vya juu vya fedha, ni mtu ambaye alikuwa yupo tayari kutoa kitu chochote kile ili tu apate fedha, kama alifikia hatua ya kumuuza Bwana, akifahamu kabisa ni mtu asiyekuwa na hatia unategemea vipi, asiwe amefanya mambo mengine maovu huko nyuma kabla ya kukutana na Kristo. Lakini Yesu alimwona pia na kumwita.

Watafakari wale wavuvi: Ni watu ambao hawakwenda shule hata mmoja, Ni kazi za watu waliodharaulika wasio na elimu, vile vile sio kwamba nao walikuwa wanauhafadhali kwa matendo mema, hapana mfikirie mtu kama Petro anafikia hatua ya kutoa panga lake na kumkata mtu sikio, jambo ambalo hata wewe sasa hivi ni ngumu kulifanya,lakini Petro alilifanya japo alishatembea na Kristo muda wote ule na kuona huruma yake na upendo wake..kama aliweza kumkata mtu sikio mbele ya jeshi kubwa kama lile unadhani alikuwa katika hali gani kabla ya kukutana na Bwana, ni wazi kuwa pengine alishaondoa viungo vya watu wengi sana waliomkorofisha… Kuna Wale wanafunzi wawili wavuvi (Yohana na Yakobo) nao pia walimshauri Yesu ashushe moto autekeze mji wote, unaona ni watu ambao hawakuwa na huruma, mpaka Yesu akawaambia hamjui ni roho ya namna gani mliyonayo. (Luka 9:54).

Hiyo yote ni kuonyesha ni jinsi gani Bwana asivyokuwa mbaguzi, aliwachagua watu mbalimbali aliwachagua matajiri, aliwachagua maskini, aliwachagua wenye elimu aliwachagua wasio na elimu, aliwachagua wanafki, aliwachagua kapigania dini.. wote hao, aliwaita sawa sawa wawe mitume wake..Hata na leo hii anaita watu wote, wewe ni fisadi anakuita,wewe ni mpenda fedha ambaye ilifikia hatua ukamtoa mama yako kafara au mtoto wako kwa waganga kwa ajili ya kupata mali, bado KRISTO anakuita leo, wewe ni muuza karanga anakuita, wewe ni mwanasiasa anakuita, wewe ni bilionea bado anakuita uwe mwanafunzi wake, wewe ni tapeli anakuita, wewe ni mlemavu anakuita. Vyovyote vile ulivyo anakuita. Kinachojalisha ni jinsi utakavyomaliza na sio jinsi ulivyosasa.

Tunaona mitume wote wa Kristo mwisho wa siku walikuja kubadilishwa tabia na kuwa mitume waaminifu wenye upendo, mashujaa walioishindania Imani hata kufa, isipokuwa mmoja tu, ambaye ni YUDA huyo peke yake ndiye alikufa na tabia zake zile zile, kwasababu hakuthamini nafasi ya kipekee aliyopewa. Halikadhalika na wewe usipoithamini nafasi hii ya upendeleo unayopewa na Yesu mwenyewe, utakufa katika dhambi zako, na utaishia motoni.

Mathayo 22:14 “Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache”.

Hivyo hapo ulipo anza maisha yako upya na Bwana, anakupokea wewe jinsi ulivyo, haijalishi ni mtenda dhambi kiasi gani, haijalishi una madhaifu kiasi gani, anakuita uambatane naye, uwe mwanafunzi wake kuanzia sasa, anataka akubadilisha uwe MTEULE WAKE kama alivyofanya kwa mitume wake.

Print this post

MBINGUNI YUPO NANI SASA?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze Biblia, ambapo leo tutajifunza kwa ufupi juu ya upeo wa kimbinguni.

Mungu alipomuumba mwanadamu, alimwumba na vitu vitatu NAFSI, MWILI na ROHO…kwasababu Mungu naye ndio yupo hivyo hivyo, anayo nafsi, mwili na Roho, maana alituumba kwa mfano wake…Nafsi yake ndio yeye mwenyewe, roho yake ndio Roho Mtakatifu, na mwili wake ndio ule Uliokuwepo Pale Kalvari, ukafufuka na kupaa mbinguni…Kwahiyo uhai uliokuwa ndani ya Mwili unaoitwa Yesu ndio Mungu mwenyewe(nafsi yake) ukisoma Wabrania 1:3 utaliona hilo…Na Roho iliyokuwepo ndani ya ule mwili wa Yesu ndiye Roho Mtakatifu mwenyewe. Hilo linatuthibitishia kuwa Mungu ni mmoja, na nafsi yake ni moja na Roho yake ni moja, na mwili wake ni mmoja.

1 Timotheo 3:16 “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu”.

Huyo ni Bwana Yesu anazungumziwa hapo, Mungu katika mwili, aliyehubiriwa katika mataifa na akapaa juu mbinguni…kwasababu hakuna mwingine aliyepaa Mbinguni mpaka kwenye kiti cha enzi zaidi yake yeye..

Yohana 3:13 “Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu”.

Utauliza mbona Biblia inasema Nabii Eliya na Henoko walipaa na kuchukuliwa mbinguni…Ndugu Nabii Eliya hakupelekwa mbinguni Bwana alipo sasa, bali alipelekwa mahali panapoitwa Peponi (paradiso), ndio maana sehemu nyingine biblia inasema Henoko alihamishwa, sio alipaa (Waebrania 11:5)….wakati mwingine biblia inapataja paradiso kama mbinguni, kwasababu ya uzuri uliopo huko…Lakini hao watu hawakupelekwa mbinguni Bwana aliko sasa, kule hakuna mwanadamu ambaye ameshafika, ni makao mapya yanaandaliwa kule kwa watu wote waliookolewa kufika siku moja kwa pamoja…hakuna mwanadamu aliyetutangulia kufika kule…Ni Bwana Yesu tu! Peke yake ndio yupo kule akituandalia makao na malaika watakatifu..Sasa kama Eliya kashafika huko kutakuwaje tena… “sehemu ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia”? unaona?.

Utauliza tena, na hao wanaoona maono wakipelekwa mbinguni, ina maana maono yao ni batili?..Wengi wao wanaosema wamepelekwa mbinguni kiuhalisia hawajapelekwa mbinguni kwasababu huko hakuna mtu ambaye ameshafika…wanachokiona ni Maono ya mbinguni…Bwana anawaonyesha maono ya jinsi mbinguni kunavyofanana fanana, lakini sio kwamba wamefika,..Sasa Bwana anaweza kuwapa maono ambayo wakati mwingine ni dhahiri kabisa mtu anaweza akahisi yupo mahali pengine katika mwili kabisa…lakini yakawa ni maono tu sio sehemu halisi…

Hata katika namna za kawaida mtu anaweza kuota ndoto ambayo ni kama dhahiri kabisa, katika ndoto akahisi kabisa vile vitu kama vile haoti, akasikia harufu, akachoka, akahisi baridi ndani ya ndoto, akahisi jua linampiga, akahisi njaa, wakati mwingine akahisi mpaka maumivu katika ndoto, Lakini si kweli kwamba huyo mtu saa hiyo yupo katika huo ulimwengu…Hizo zinaitwa njozi. Na ndivyo Bwana anavyozungumza na watu, anaweza kuwapa watu wake maono kama vile wapo Mbinguni kabisa, wakaona pengine barabara za dhahabu, au almasi, wakaona bustani nzuri, wakaona Malaika watakatifu, wakaona uzuri usioelezeka wa huko, hisia ambazo wanaweza wakadhani ni kweli wamefika kule..Hapana kule hawajafika isipokuwa wamepewa tu maono ya kule.

Lengo la Bwana kuwaonyesha vile ni kutaka kuwaonjesha watu wake uzuri watakaokwenda kukutana nao kule, na wawafikishie wengine ujumbe. Na Bwana anaweza kumpa mtu yeyote maono hayo. Sasa ukikosa maarifa ya kuyaelewa haya, unaweza ukajipiga kifua mbele na kufikiri kwamba umeshawahi kufika mbinguni kabla ya wengine…Mambo yaliyopo kule wala hatuwezi kuyafikiria wala kuyastahimili katika hii miili yetu na akili zetu, mpaka tubadilishwe ndipo tutakapoweza kuyaelezea.

Na maono haya Bwana anayowapa watu, yanatofautiana mwingine ataonyeshwa hivi mwingine vile…mwingine kwenye maono hayo ataonyeshwa barabara za dhahabu, mwingine almasi, mwingine marumaru, mwingine ataonyeshwa makasri, mwingine mahekalu, mwingine ataonyeshwa tunu za kipekee, mwingine ataonyweshwa malaika wamevaa kanzu nyeupe wameshikilia upanga, mwingine ataonyeshwa wamevaa nyeupe zenye mshipi wa dhahabu na wameshikilia matarumbeta, mwingine ataonyeshwa wamevaa blue n.k Nk kwa jinsi Bwana atakavyopenda kumwonesha mtu. Ndio maana utaona kila mmoja anakuja na ushuhuda wake tofauti na mwingine wa mambo aliyoyaona…

Sasa kama wangekuwa wamepelekwa mahali halisi, wasingekuja kila mmoja na ushuhuda wake? Unaona? Wote wangekuja na ushuhuda unaofanana…Lakini kwasababu ni maono, maono hayawezi kufanana…ndio maana utaona Hata kwenye Biblia Yohana wa Patmo alipewa maono yenye maudhui sawa na yale ya Nabii Danieli lakini yalikuwa hayafanani…utaona Danieli anaonyeshwa wanyama wanne wanatoka baharini, mmoja alikuwa mfano wa simba, mwingine chui, mwingine Dubu na mwingine kiumbe kisichojulikana (Danieli 7:3-7)…Lakini Yohana anaonyeshwa mnyama mmoja akitoka baharini aliye mfano wa chui, miguu yake kama ya dubu na kinywa kama kinywa cha simba..(Ufunuo 13:2). Sasa alichoonyeshwa Yohana wa Patmo na Danieli ni kitu kimoja isipokuwa katika maono tofauti..ndio maana utaona kuna utofauti kidogo huyu kaonyeshwa wanyama wanne, lakini huyu kaonyeshwa mnyama mmoja mwenye maumbile ya wanyama wote wanne.

Utaona tena jambo hilo katika Kitabu cha Ezekieli, yeye alionyeshwa makerubi wana nyuso nne kila upande, uso wa mwanadamu, tai, Ndama, pamoja na simba, yaani kerubi mmoja ana nyuso nne..kwenye maono ndivyo alivyoonyeshwa..

Ezekieli 1: 5 “Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu.

6 Na kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne.

7 Na miguu yao ilikuwa miguu iliyonyoka; na nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za miguu ya ndama; zikimetameta kama rangi ya shaba iliyosuguliwa sana.

8 Nao walikuwa na mikono ya mwanadamu chini ya mabawa yao, pande zote nne; na wote wanne walikuwa na nyuso zao na mabawa yao hivi;

9 mabawa yao yaliungana, hili na hili; nao hawakugeuka walipokwenda, walikwenda kila mmoja kuelekea mbele.

10 Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng’ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia”.

Lakini Yohana wa Patmo yeye alionyeshwa Kila Kerubi na uso mmoja, yupo aliyekuwa na uso wa Tai, mwingine Uso wa Ndama, mwingine wa Mwanadamu na mwingine wa Simba, lakini hakuoneshwa kuwa kerubi mmoja ana nyuso nne kama alivyooneshwa Nabii Ezekieli.

Ufunuo 4: 6 “Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma.

7 Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye.

8 Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja”.

Sasa Yohana na Ezekieli sio kwamba wameonyeshwa vitu tofauti, hapana..ni kitu kimoja isipokuwa katika maono mawili tofauti.

Kwahiyo Mbinguni hakuna aliyefika sasa, ni sehemu mpya Bwana anayowaandalia watu wake, na watakaofika ni wale tu waliooshwa dhambi zao kwa damu yake, yaani wale waliomwamini yeye na kutubu na kubatizwa, na kuishi maisha ya utakatifu (Waebr 12:14)..Wapendwa wetu waliokufa katika Kristo sasa wapo mahali pa mangojeo panapoitwa Paradiso au peponi (Ni mahali wamehifadhiwa pa raha sana, lakini ni pa muda tu, wakingoja siku ile ifike)..Na sisi tutakapokufa kabla ile siku haijafika tutakwenda kuungana nao kule, ni sehemu nzuri sana, wote tutakuwa tunaingoja ile siku kwa pamoja.

Biblia inasema siku ile itakapofika wafu wote (yaani wale waliokufa katika haki, waliohifadhiwa paradiso sehemu ya raha na mangojeo)..watafufuka (yaani watarudi katika miili hii ya asili kwanza)..na watakatifu walio hai watawaona na kuungana nao, na kwa pamoja kufumba na kufumbua tutabadilishwa miili yetu na kuvaa ya miili ya utukufu..itakayoweza kustahimili hayo mambo mazuri na mapya tutakayokwenda kuyakuta huko juu…Na ghafla tutavutwa juu mbali sana na hii ardhi (Itakuwa ni shangwe kubwa sana siku hiyo) tutaiingia mbingu ya mbingu….(na mambo tutakayoyakuta huko hakuna awezaye kuyasimulia kwasababu hakuna mtu alishawahi kufika huko kabla)…Lakini kwa walio nje ya Kristo itakuwa ni kilio na kusaga meno na maombolezo makubwa…

Siku ya mwisho yaja! Maran atha maana yake “BWANA WETU ANAKUJA” Na watakatifu waliopo paradiso wanaitamani hiyo siku ifike haraka…siku ya kufutwa machozi yao, na taabu zao na kuingizwa katika umilele.

Ufunuo 22: 20 “Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu”.

Mpe Kristo maisha yako leo, ili uwe na uhakika wa kuwepo miongoni mwa watakaokwenda kuyaona mambo mazuri Bwana aliyowaandalia watu wake..

Bwana akubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:


Mada Zinazoendana:


TOFAUTI KATI YA NDOTO NA MAONO NI IPI?

BASI MUNGU AKAMUADHIMISHA SANA..

UNYAKUO NI NINI?

 SIKU YA BWANA NI NINI?

 NINI HUDUMA YA MALAIKA WATAKATIFU SASA?


Rudi Nyumbani

Home

Print this post

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 3

Karibu tujifunze Neno la Mungu, Biblia takatifu..Kama tunavyojua vitabu hivi vya biblia pamoja na kwamba vimeandikwa wakati mwingine kwa mfumo wa Hadithi, lakini vimebeba ufunuo mkubwa sana ndani yake. Ndio maana tunapaswa tujifunze Biblia na sio tuisome tu!…kwasababu kuna tofauti kubwa kati ya kujifunza na kusoma.

Tumekwisha kuvipitia kwa ufupi vitabu 8 vya kwanza, ambapo cha Mwisho kilikuwa ni kitabu cha RUTHU ambacho kilikuwa kinaelezea chimbuko la Mfalme Daudi lilipotokea, tulimwona mwanamke huyu Ruthu, ambaye hakuwa hata myahudi (alikuwa mtu wa mataifa)kwa Imani aliweza kubeba uzao wa Kifalme ndani yake, kama vile Rahabu kwa imani alivyohesabiwa miongoni mwa wayahudi japo hakuwa myahudi ..na tuliona pia kitabu hiki kiliandikwa na Nabii Samweli ambaye ndiye aliyekuwa mwamuzi wa mwisho kabisa wa Taifa la Israeli.

Na sasa kitabu kinachofuata ni kitabu cha SAMWELI wa Kwanza..Kitabu hichi kiliandikwa na Nabii Samweli mwenyewe kama jina la kitabu lilivyo, sehemu za mwisho wa kitabu baada ya Samweli kufa ziliandikwa na Nabii Gadi na Nabii Nathani ambao tutakuja kuona habari zao huko mbeleni.

Kitabu hichi cha SAMWELI WA KWANZA (au 1 Samweli). Ni kitabu kinachoelezea mabadiliko makubwa ya Taifa la Israeli. Ni kitabu kinachoelezea mabadiliko ya nyakati. Kumbuka wakati wana wa Israeli wanatoka Misri hawakuwa na Mfalme na haukuwa mpango wa Mungu fulani mmoja atawale juu ya wengine…

wangekuwepo viongozi lakini sio Mfalme, kuwepo kwa mfalme ndani ya Taifa la Israeli haukuwa mpango kabisa wa Mungu…kwani kwa kupitia mfumo wa kifalme ndio uliowatesa wao wakiwa Misri, walitumikishwa vikali kwa amri ya Mfalme wa Misri, kwahiyo Bwana alipowaweka Huru mbali na hiyo kamba hakutaka tena watoto wake wafungwe au wajifunge katika katika mfumo huo kwasababu alijua madhara yake…Na sio tu kuwa na mfalme bali hata hakutaka watwae watumwa miongoni mwa ndugu zao na kuwatumikisha kama walivyotumikishwa walipokuwa Misri.

Walawi 25: 38 “Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili niwape nchi ya Kanaani, nipate kuwa Mungu wenu.

39 Tena kwamba nduguyo amekuwa maskini pamoja nawe, akajiuza kwako; usimtumikishe mfano wa mtumwa;

40 kwako wewe atakuwa mfano wa mtumishi aliyeajiriwa, au mfano wa msafiri; naye atatumika kwako hata mwaka wa yubile;

41 ndipo atakapotoka kwako aende zake, yeye na wanawe pamoja naye, naye atairejea jamaa yake mwenyewe, tena atairejea milki ya baba zake.

42 KWA KUWA HAO NI WATUMISHI WANGU, NILIOWALETA WATOKE NCHI YA MISRI; WASIUZWE MFANO WA WATUMWA.

43 Usitawale juu yake kwa nguvu; ila umche Mungu wako.

44 Tena katika habari za watumwa wako na wajakazi wako, utakaokuwa nao; mataifa walio kando-kando yenu, katika hao mtanunua watumwa na wajakazi.

45 Tena katika wana wa wageni wakaao kati yenu mtajinunulia, na katika jamaa zao walio pamoja nanyi, waliowazaa katika nchi yenu; wao watakuwa milki yenu.

46 Nanyi mtawafanya kuwa urithi kwa watoto wenu baada yenu, wawe milki yao; siku zote mtatwaa watumwa wenu katika hao; LAKINI MSITAWALE KWA NGUVU JUU YA NDUGU ZENU, HAO WANA WA ISRAELI, WENYEWE KWA WENYEWE”.

Umeona! Kwahiyo Mungu, alikataza watoto wake wasiwe watumwa katika hiyo nchi waliyoahidiwa…Na zaidi ya yote ukiendelea kusoma utaona Bwana hakuwaruhusu hata pia kutozana RIBA wao kwa wao.

Lakini tunaona wana wa Israeli baada ya miaka mingi kupita walisahau hilo agizo..wakatamani utawala wa kishupavu kama wa Mataifa yaliyowazunguka..Ndipo ukafika wakati waisraeli wote wakakusanyana wakamwendea Nabii Samweli ambaye ndiye alikuwa mwamuzi wa kipindi hicho wakamwambia wanataka mfalme juu yao ili wafanane na mataifa mengine ya Duniani.

Jambo lile likamchukiza sana Samweli na Mungu, na Mungu akawapa mfalme kama walivyotaka, na Bwana akamwongoza Nabii Samweli aandike kitabu cha mambo hayo ili iwe kumbukumbu kwa vizazi vinavyokuja mbele yao na iwe fundisho kwetu sisi watu wa zamani hizi…Kwahiyo sehemu ya Mwanzo wa kitabu hichi inaelezea historia ya Samweli, kuzaliwa kwake na ukuhani katika hema ya Mungu, pamoja na Eli kuhani..Na kuanzia sura ya 8 na kuendelea ndipo tunaona wana wa Israeli wakitaka mabadiliko. Na sehemu iliyobakia inaelezea maisha na matendo ya Mfalme wa Kwanza wa Israeli (Sauli) mwanzo wake na mwisho wake.

1 Samweli 8:4 “Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama;

5 wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote.

6 Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana.

7 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.

8 Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe.

9 Basi sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme atakayewamiliki.

10 Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya Bwana.

11 Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake.

12 Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake.

13 Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji.

14 Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake.

15 Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake.

16 Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng’ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe”.

17 Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake.

18 NANYI MTALIA SIKU ILE KWA SABABU YA MFALME WENU MLIYEJICHAGULIA; BWANA ASIWAJIBU SIKU ILE.

19 Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu;”

Kwa ufupi mwanzo wa matatizo makubwa yaliyowakumba wana wa Israeli yalianzia wakati huu walipojitakia mfalme….huko mbeleni utakuja kuona Wafalme ndio waliowakosesha sana wana wa Israeli na kuwasababisha waingie utumwani na kutapanywa katika mataifa yote duniani.

Na zaidi ya yote utaona Bwana aliwaonya hapo juu, kuwa Mfalme wanayemtaka atawafanya wana wao na binti zao kuwa watumwa, watatumikishwa kwa utumishi mkali..Na watalipishwa ushuru kwa kila kitu, desturi ambayo hapo mwanzo hawakuwa nayo, na wataiona hiyo nchi ya Kaanani Bwana aliyowapa ni chungu! Wataona hakuna tofauti na kule Misri walipotoka..Na Bwana akawaambia siku hiyo baada ya mateso hayo wataomba msaada kwa Bwana lakini Bwana hatawasikia……. Lakini hawakuelewa kama biblia inavyosema! Wakapewa mfalme kama walivyotaka…Na Neno la Bwana likaja kutimia juu yao kama lilivyo miaka kadhaa mbeleni: walitumikishwa kwa utumishi mkali mpaka siku moja wakakusanyika kuomba wapunguziwe makali ya utumishi baada ya Mfalme Sulemani kufa…Tunayasoma hayo katika..

2 Nyakati 10:2 “Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia, (maana alikuwako Misri, ambako amekimbilia mbele ya mfalme Sulemani), Yeroboamu akarudi kutoka Misri.

3 Wakapeleka ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema,

4 Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia.

5 Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao…………………..

9 Akawaambia, Je! Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakisema, Utufanyie jepesi kongwa alilotutwika baba yako.

10 Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliosema nawe, wakinena, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, lakini wewe tufanyie jepesi; uwaambie hivi, KIDOLE CHANGU CHA MWISHO NI KINENE KULIKO KIUNO CHA BABA YANGU.

11 Basi kama baba yangu aliwatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu AKIWAPIGA KWA MIJELEDI, LAKINI MIMI NITAWAPIGA KWA NGE.

12 Basi Yeroboamu na watu wote wakamjia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu.

13 Mfalme akawajibu kwa ukali; mfalme Rehoboamu akaliacha shauri la wazee, akasema nao kwa shauri la vijana,

14 akinena, Baba yangu aliwafanyia kongwa zito, NAMI NITAWAONGEZEA; BABA YANGU ALIWAPIGA KWA MIJELEDI, LAKINI MIMI NITAWAPIGA KWA NGE.

15 Basi mfalme hakuwasikia wale watu; MAANA JAMBO HILI LILITOKA KWA MUNGU, ili alithibitishe neno lake alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa mkono wa Ahiya Mshiloni.”

Umeona? Wafalme wote wa Israeli waliwatumikisha wana wa Israeli kama watumwa, hata Mfalme Sulemani naye, aliwatumikisha wana wa Israeli kupita kiasi…jambo ambalo Mungu hakulitaka.

Kwahiyo kitabu hichi kinaelezea mabadiliko ya Utawala wa wana wa Israeli, kutoka kutawaliwa na Mungu mbinguni mpaka kujitakia mfalme wa kidunia awatawale..Hivyo kina mafunuo mengi sana ndani yake na siri nyingi ni vizuri kama hujakisoma ukisome peke yako, Bwana atakufunulia mambo mengi sana yanayohusiana na wakati huu tunaoishi…lakini jambo moja la kipekee ambalo tunaweza kujifunza juu ya kitabu hiki ni juu ya UBAYA WA KUIGA WATU WA ULIMWENGU HUU..Hekima ya Mungu ni kuu kuliko hekima ya ulimwengu huu, wana wa Israeli walitazama kwa nje jinsi utawala wa kifalme unavyopendeza, hawakujua ndani yake jinsi ulivyo mbaya, mpaka walivyoingia…

Na sisi katika safari yetu ya ukristo tunajifunza, Mambo ya ulimwengu huu, ustaarabu wa ulimwengu huu kwa nje yanaweza kuonekana ni mazuri, yanavutia lakini ndani yake yanamadhara makubwa, Mungu anapotuonya tukae mbali na ulimwengu si kwasababu anatuonea wivu, hapana ni kwa faida yetu wenyewe…anajua madhara tutakayoyapata huko mbeleni endapo tukiuiga ulimwengu, endapo tukienenda kama ulimwengu unavyoenenda…Endapo tukianza kutamani na sisi kuvaa vimini na suruali kama watu wa ulimwengu wanavyovaa, kujipamba kama watu wa ulimwengu wanavyojipamba,..Tutaingia kwenye mtego ambao mwisho wa siku tutaomba Mungu atutoe na Mungu hatatusikia siku hiyo, kama alivyowaambia wana wa Israeli kuwa “18 NANYI MTALIA SIKU ILE KWA SABABU YA MFALME WENU MLIYEJICHAGULIA; BWANA ASIWAJIBU SIKU ILE”.

Tunapoonywa sasa ni wakati wa kusikia, utakapozama kwenye uchawi utafika wakati utalia na Bwana asikujibu!..utakapozama kwenye anasa kupindukia na hali sasa unasikia maonyo hutaki kugeuka itafika wakati utalia na Bwana asikujibu…utakapozama kwenye uasherati na kila siku Bwana anakuonya kwa maonyo haya hutaki kusikia…utafika wakati utalia na Bwana asikujibu!…Unapozama kwenye kuacha uongozi wa Mungu na kufuata uongozi wa mwanadamu, Bwana anakwambia hivi, wewe unasema vile, Bwana anakwambia geuka huku hii ndio njia, lakini wewe unasema dini yangu haisemi hivyo wala watu wote hawasemi hivyo…ndugu yangu utafika wakati utalia na kuomboleza na Bwana hatakusikia!…Unyakuo utakapopita na utakapoachwa utalia na Bwana asikusikie…

Unajua ni kwanini watu wengi wenye magonjwa ya kutisha(japo si wote), Hawaponi? Watu wanaoingia kwenye mitego ya Ibilisi hawanasuki?…Ni kwasababu ya kushupaza shingo wakati wanaonywa..

Mithali 1:29 “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.”

Na imefika wakati wameshazama kwenye matatizo ndipo wanamlilia Mungu,..wengi wanasamehewa makosa yao lakini mauti inakuwa ipo pale pale…sasa hasara zote hizo za nini? Kwanini leo usifanye uteule wako na wito wako imara kama biblia inavyosema katika

2 Petro 1: 10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.

11 Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana wetu, Mwokozi wetu Yesu Kristo”.

Kama hujampa Bwana maisha yako, saa ya wokovu ni sasa, unachotakiwa kufanya sasahivi na hapo ulipo kutubu dhambi zako zote ulizozifanya hapo kabla, na unazozifanya sasahivi…unamwambia Bwana hutaki kuzifanya tena, na wewe mwenyewe ukidhamiria kweli kweli kutokuzifanya tena, kama ulikuwa unakula rushwa unaacha, kama ulikuwa unafanya uasherati unaacha, kama ulikuwa mshirikina unaacha unakwenda kuchoma vifaa vyote vya kishirikina, kama ulikuwa ni mtukanaji, msagaji, mlawiti, shoga, mtoaji mimba, mfanyaji masturbation, mtazamaji pornography, mvaaji vibaya nk. Vyote unaviacha unaanza maisha mapya ndani ya Kristo na Bwana mwenyewe atakusamehe na kukupa maisha mapya ndani yake…Na kama madhara yalikuwa makubwa na ulikuwa hujui kwa mapana madhara yake pia atakuponya ugonjwa wako, atakurejeshea uzima, ila jambo la kwanza ni kutubu kwa kumaanisha kutokufanya tena.

Bwana akuabariki.

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312

 

AMEN.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

KWANINI SAMWELI ALIRUHUSUIWA KUHUDUMU HEKALUNI KAMA VILE WALAWI WAKATI YEYE NI MU-EFRAIMU?

JE! MUNGU ANAWEZA KULETA MAJIBU KUPITIA NGUVU ZA GIZA KAMA ALIVYOFANYA KWA MFALME SAULI?

USIONDOE ALAMA YA MPAKA ILIYOWEKWA NA MABABA.

CHAGUA NI JIWE LIPI LITAKALO KUFAA KWA UJENZI.

‘’MOTO HUFA KWA KUKOSA KUNI’’..NA NDIVYO ILIVYO KWA UASHERATI

UKOMA NA UJANE ULIO NDANI YAKO, UMEUPATIA TIBA?


Rudi Nyumbani:

Print this post

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

Melkizedeki ni nani?


Neno la Mungu linatuambia katika 1Timotheo 3:16 kuwa “bila shaka siri ya utauwa ni kuu.” Au kwa lugha rahisi Neno hili tunaweza kusema “bila shaka siri ya Uungu ni kuu; Hii ikiwa na maana kuwa kuufahamu uungu wa Mungu, si kitu chepesi tu cha kufikirika kibinadamu, bali kipo katika Siri na Siri hiyo ni kubwa sana..Hivyo hiyo inatuhimiza sisi tumwombe Mungu atufunulie ili tuzidi kumjua yeye siku baada ya siku.

Kumbuka Hapa katika hii siri ndipo palipoleta mgawanyiko na mkanganyiko mkubwa kati ya Ukristo na Imani nyingine kama vile uislamu, Na hapa hapa ndipo palipoleta migawanyiko mingine mikubwa katikati ya wakristo wenyewe.

Lakini sisi hatutaingia huko leo, bali kwa ufupi tutamtazama huyu Melkizedeki ni nani, kwa kurejea baadhi ya vifungu vya maandiko. Sasa kumbuka biblia inaweka wazi kabisa, kwamba Kristo alikuwepo kabla hata kabla ya kitu chochote kuwepo duniani.

Yohana 8:57 “Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu?

58 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko”.

Unaona Lakini swali tunajiuliza alikuwepoje? Hili ni swali ambalo hata wakristo wengi leo hii tunashindwa kulijibu ipasavyo. Tutasema Yohana 1:1 Inathibitisha hilo kuwa hapo mwanzo kulikuwepo na Neno naye Neno alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa, ambaye ndio YESU. Hivyo Yesu alikuwepo tangu mwanzo mbinguni na baba yake mpaka ilipofika wakati wa yeye akashuka duniani kuja kutuokoa.

Lakini hatujui kuwa huyu YESU ambaye anaonekana kwa maumbile yale, hakuwepo tangu mwanzo. Safari yake ilianzia AD 1, tutaliona hilo tunavyozidi kusonga mbele.

Kama biblia inavyosema hapo mwanzo kulikuwako “Neno”, Hivyo kwa asili yake NENO sio mtu, Hili ni Neno la kigiriki Logos, likiwa na maana ya WAZO LA MUNGU, /KANUNI au NIA ya Mungu.

Sasa hili Neno kazi yake kubwa ilikuwa ni nini?

Tukisoma:

1Yohana 1:1 “Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya NENO LA UZIMA;

2 (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);

3 hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo”.

Unaona hapo Hili Neno kumbe limebeba UZIMA ndani yake (Yohana 1:4), ambao uzima huo Mungu alitaka kuudhihirisha kwetu tangu zamani. Hapa mitume wanasema walikuwa wanalisikia tangu zamani, hivyo halikuwa jambo jipya katika masikio yao lakini baadaye sasa wakati ulipofika wakaja kupata neema ya kuliona kwa macho yao wenyewe na kulipapasa siku lilipokuja kufanyika mwili ndani ya YESU KRISTO.

Sasa tumeshaona uzima wowote ni Neno la Mungu (Wazo la Mungu) kwa mwanadamu, Kazi yake kubwa ni kurejesha kilichopotea na kukikomboa. Hivyo katika maandiko Neno hili la uzima halikuanzia kwenye Ule mwili wa YESU KRISTO pekee, hapana bali lilianzia tangu mbali sana, isipokuwa lilifichwa tu machoni pa watu wasilitambue kwasababu SIRI ya utauwa ilikuwa bado haijafichuliwa. Hivyo hili NENO Lilichukua maumbile mengi mengi tofauti kwa lengo tu la kutimiza kusudi lile lile kuleta uzima ndani ya watu.

➔Tunaona lilikuwepo kuanzia Edeni, mwanzoni kabisa mwa safari ya mwanadamu kama Ule mti wa Uzima katika bustani, Lile lilikuwa ni NENO LA MUNGU..lilikuwepo pale kuwapa uzima Adamu na hawa, kuwazuia na mauti, lakini walipoasi wakafukuzwa mbali nalo.

➜Baadaye likaja likachukua umbile lingine tena la MERIKEBU(SAFINA), Lilisimama pale ili kuwakomboa wanadamu na uzao wao usipotee kabisa katika uso wa dunia, akaokoka Nuhu na watu wengine 7.

➜Baadaye likaja kuchukua umbo la mnyama MWANAKONDOO, siku ile Ibrahimu alipokwenda kumtoa mwanawe wa pekee kuwa sadaka ya kuteketezwa likasimama kama dhabihu badala ya Isaka kama Yule kondoo aliyekuwa mlimani kichakani, vyote hivyo vilifanyika kwa mafumbo makubwa sana, kufunua UZIMA hasa udumuo utakaokuja huko mbeleni..

➜Ndio baadaye tunakuja kuona linachukua tena maumbile ya wanadamu likaonekana duniani kwa wakati mchache kutimiza kusudi Fulani ndio sasa hapo tunamwona mtu anayeitwa MELKIZEDEKI. Kama kuhani kumpatanisha Ibrahimu na Mungu kwa kitambo tu. Lakini ukuhani halisi ulikuwa bado haujafunuliwa.

Waebrania 7:1”Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki;

2 ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani;

3 hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwana Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele……………….

Waebrania 7:15 “Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki;[anazungumziwa YESU KRISTO]

16 asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo;

17 maana ameshuhudiwa kwamba, Wewe u kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki”.

Mahali pengine tena Neno lilipochukua umbile la kibinadamu, ni pale Shedraka, Meshaki na Abednego walivyotupwa kwenye tanuru la moto Likatokea kwa mfano wa mwana wa Mungu, likawa linazungumza nao kisha likaondoka..Kwasababu lilikuwa bado halijashuka rasmi duniani. Lakini utaona lengo lake ni lile lile kuleta uzima na kuokoa.

Sehemu nyingine lilitokea kama MWAMBA. Kule jangwani wana wa Israeli walipokuwa wanakaribia kufa na kiu lilisimama mbele yao ili kuwaokoa, Na Musa hakulifahamu hilo mpaka alipofanya uzembe ule wa kuupiga ule mwamba mara mbili ndipo alipojua kuwa kumbe alikuwa amesimama mbele ya uzima wenyewe, mbele ya mkombozi mwenyewe.

(1Wakorintho 10:4 “wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo”.)

➜Baadaye likaja kujidhihirisha katika maumbile mengi tofauti tofauti mfano kama Hekalu, Sehemu nyingine kama malaika, sehemu nyingine kama nguzo ya moto. Sehemu nyingine kama NYOKA WA SHABA.

(Yohana 3:14 “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyohivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;
15 ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye”.)

➜Sehemu nyingine likajidhihirisha kama HEKIMA Ambayo aliwavaa waamuzi na wafalme wa Israeli akianziwa na Sulemani na wengineo waliomfuata, ili tu kutimiza lengo la kuwaokoa na kuwatunza watu wake kupita wafalme wale Mungu aliowachagua hekima yake ikae ndani yao.

Ukisoma Mithali sura ya 8 na ya 9 utaona kabisa jinsi Sulemani anavyoilezea hekima kama kitu chenye uhai na kinazungumza, Pia soma (1Wakorintho 1:24) utaona inamtaja KRISTO kama yeye ndio hiyo Hekima ya Mungu yenyewe.

Sehemu hizo hatuna muda wa kuzielezea moja moja, Lakini nataka uone picha Fulani hapo, NENO LA MUNGU jinsi lilivyopana, Na jinsi lilivyokuwepo tangu mwanzo. Hivyo baadaye sasa wakati ulipofika, Mungu kuufunua utimilifu wote, Mungu kuweka wazi WAZO lake lote kwa mwanadamu, Mungu kuufunua uzima wote na Ukombozi wote, akaona ni vyema sasa aunde mwili maalumu, mahususi, uzaliwe na mwanamke bikira, uitwe jina la YESU (Maana yake YEHOVA-MWOKOZI) ili sasa liweze kukaa na wanadamu milele, lizungumze nao, liwajibu maswali yao, liwafundishe, walipapase, walitegemee hilo, liwaongoze katika njia ya kweli na ya haki na ya uzima hata milele. Hapo ndipo tunaona Lile Neno ndani ya mwili unaoitwa Yesu…ambaye kwa ujumla sasa ndio tunamwita BWANA YESU KRISTO HALELUYA! HALELUYA!. 

Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”.

Ndio maana mtume Yohana alikuwa anaoujasiri kabisa kusema maneno haya…

1Yohana 1:1 “Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima;
2 (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);”

Sasa tukirudi kwenye zile kauli za Yesu anaposema kabla Ibrahimu hajawapo mimi nipo, hapo tunaona alikuwa hauongelei ule mwili uliozaliwa na bikira, bali alikuwa anaongelea lile Neno la Mungu ndani yake. Ukilijua hilo hutasema kuwa Mungu anazo nafsi tatu. Wewe na MAWAZO yako au NIA yako hamwezi kuwa vitu viwili tofauti vinavyojitegemea, ni kitu kimoja.Lile Neno ndio Mungu mwenyewe, Yesu Kristo ni Mungu ndani ya Mwili.

Hivyo ndugu tukirudi kwenye kichwa cha Somo je! Huyu Melkizedeki ni nani?. Jibu ni kuwa Huyu Melkizedeki ni Neno la Mungu lililojidhihirisha katika mwili kutimiza kusudi fulani kabla ya wakati wake mtimilifu. Lakini baadaye ndilo liliokuja rasmi kuitwa YESU KRISTO.Hata sasa tunaposema mkaribishe YESU Kristo ndani ya maisha yako, tunamaanisha likaribishe Neno la UZIMA la Mungu ndani ya maisha yako, Kwasababu Neno hilo sasa limefunuliwa ndani ya Kristo Yesu Bwana katika utimilifu wote. Kwahiyo unavyolisikia hili Neno na kulipokea, ni sawa umempokea Yesu Kristo mwenyewe ndani ya maisha yako…

Je! Leo hii bado Upo katika dhambi?, Na hali Tumesharahisishiwa wokovu namna hii bado unauona ni mgumu kuupokea?. Watu wa Agano la Kale japo walilifahamu hili Neno la Mungu kwa sehemu tu kwa kupapasapasa lakini walitii kwa utimilifu wote wakapata wokovu sisi je! Tutapataje kupona tusipouthamini wokovu mkuu namna hii?(Waebrania 2:3). YESU KRISTO ndio  wazo la Mungu, ndio NIA ya Mungu, ndio MUNGU MWENYEWE katika Mwili. Tumfuate yeye tupate kuwa salama, katika safari yetu hii fupi hapa duniani.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP



Mada Zinazoendana:

NEHUSHTANI (NYOKA WA SHABA).

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?

MJUE SANA YESU KRISTO.

SIRI YA MUNGU.


Rudi Nyumbani:

Print this post

MWEZI NI ISHARA GANI KWETU?

Shalom mtu wa Mungu, karibu tujifunze tena maneno ya Mungu.

Kama wengi wetu tunavyojua kuwa, siku ya Bwana inakuja, siku ya hukumu yake ambapo Bwana atauhukumu ulimwengu kwasababu ya ubaya wake..(Isaya 13:11 inasema hivyo)

Na katika siku ya Mwisho,wafu wote watafufuliwa na Kiti cheupe cha Hukumu kitawekwa na Yesu Kristo ataketi juu yake, na kila mtu, mmoja baada ya mwingine atasimama mbele yake atoe hesabu ya mambo yake yote aliyoyafanya tangu siku alipozaliwa mpaka siku aliyokufa, yote hayo yatamulikwa katika kioo kikubwa sana, na kuonekana mbele ya watu wote na hapo ndipo kila mtu atapasa sifa yake, au aibu yake. (1Wakorintho 4:5)

Litaonekana tendo moja baada ya lingine, liovu au la haki litaonekana pale…kama mtu alikuwa ni mwasherati yataonekana matukio yote aliyoyafanya ya uasherati, siku aliofanya, mtu aliyefanya naye, mwaka, mwezi, mpaka dakika na sekunde alizokuwa anafanya…na watu wote wataona hakutakuwa na siri, kama mtu aliyafanya tendo Fulani la haki nalo pia litaonekana mwaka, siku, mpaka sekunde ya tendo hilo. Iwe alifanya kwa siri au kwa wazi yote yatakuwa bayana.

Na ni kwanini Mungu anataka watu wote waone?..Ni kwasababu yeye ni muhukumu wa haki na hivyo asitokee mtu yeyote atakayesema Yule kaonewa au Yule kapendelewa, watu wote watashuhudia matukio ya yaliyokuwa yanaendelea miongoni mwa watu.

Yohana 5: 28 “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.

29 Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, NA WALE WALIOTENDA MABAYA KWA UFUFUO WA HUKUMU”.

Na Leo kwa Neema za Bwana tutaangalia ni kwa namna gani..MATUKIO(AU MATENDO) YA WANADAMU YANAVYOREKODIWA MBINGUNI.

Unajua unapoingia Benki au kwenye duka Fulani kubwa lenye bidhaa nyingi za thamani huwa wanaweka camera Fulani zizazorekodi matukio yote yanayoendelea kule ndani (CCTV). Wakati mwingine zinawekwa sehemu za kujificha wakati mwingine sehemu za wazi kabisa…

Sasa lengo la kuweka hizi camera kwa wazi ni ili watu wote wazione wanaoingia pale na waliopo kule ndani, ili wajue kuwa mambo yao yote wanayoyafanya yanarekodiwa na hivyo iwatengenezee hofu ya kutaka kujaribu aidha kuiba au kufanya kitendo chochote cha uhalifu. Hilo ndio lengo la hizo camera (CCTV) kuweka wazi. Ni ili mtu anapoingia na kuziona zile aingiwe na hofu ya kutaka kujaribu kufanya tukio lolote ovu..

Na ndivyo hivyo hivyo katika maisha haya…Tunapoingia katika huu ulimwengu Bwana Mungu ameweka camera yake juu inayorekodi mambo yote ya wanadamu tangu tunapozaliwa mpaka tunapokufa..na lengo la kuifanya ionekane ni ili watu waionapo waogope kufanya mambo maovu hapa duniani wakijua kuwa siku moja itaweka bayana matukio yote…Na hiyo camera (au CCTV) Ni huu MWEZI TUNAOUONA! Hapa juu ya vichwa vyetu..Huu mwezi tunaouona haupo tu pale juu kutufurahisha sisi wanadamu hapana! Au kutoa tu mwanga wakati wa usiku…ile ni camera Mungu aliyoiweka ionekane wazi ili watu tuogope kuishi maisha yasiyofaa hapa duniani.. Leo nitakuhakikishia kwanini Mwezi ni Camera ya huu ulimwenguni.

Kama ni mfuatiliaji mzuri wa mambo ya Sayansi…utakuwa umekutana au umewahi kusikia kitu kinachoitwa SATELLITE ( au satelaiti). Satelaiti ni kifaa cha kisayansi kinachowekwa juu sana (Maili nyingi sana angani)…ambacho kifaa hicho kinawekwa katika mfumo wa kuizunguka dunia kama vile mwezi unavyoizunguka dunia…Na kinakuwa na kazi nyingi tofauti tofauti…Lakini kazi kubwa satelaiti inayofanya ni KUREKODI NA KUPIGA PICHA ZA MATUKIO YANAYOENDELEA DUNIANI.

Kwa kutumia satelaiti mtu anaweza kukuona mpaka hapo ulipo na shughuli unazofanya si hivyo tu Satelaiti pia inauwezo wa kupiga picha za miji, na mienendo ya watu wengi na shughuli zao…unaweza kuchunguzwa hapo ulipo pasipo wewe kujijua kwa kupitia satellite…na inamatumizi mengine mengi tu.

Sasa wanasayansi walikitengeneza hichi kifaa kwa kujifunza tabia za mwezi, wakatumia fomula ile ile ya jinsi mwezi ulivyo juu na unavyozunguka dunia, wakaitumia na wao pia kupandisha kifaa chao hicho kama MWEZI WAO juu angani. Na kwasababu hiyo MWEZI huu tunaouona sisi wakaupa tafsiri ya kisayansi kuwa NI SATELAITI YA ASILI…Kwahiyo Wanasayansi hawaujui huu mwezi kwa tafsiri nyingine zaidi ya hiyo..wenyewe wanajua kuwa Mwezi ni satelaiti ya asili(kwa kiingereza natural satellite)…na hizo wanazozitengeneza wao wanazijua kama “satelaiti za kutengenezawa (kwa kiingereza artificial satellites)”. Kafuatilie jambo hilo utalielewa zaidi.

Sasa wao wameutafsiri mwezi kama SATELAITI YA ASILI, lakini hawajui kwanini wameutafsiri hivyo.. Lakini sisi Wakristo Bwana katupa macho ya rohoni kujua. Kama wao walitengeneza mwezi wao wa asili na kuupandisha juu sana, na kuzunguka dunia kwa lengo la kurekodi matukio yanayoendelea duniani..kadhalika na huu mwezi wa asili au satelaiti ya asili kama wanavyouita..unafanya kazi hiyo hiyo kama ya kwao…ya kurekodi matukio yote yanayoendelea duniani tena kwa ufasaha zaidi. Ingawa kwa namna ya macho ya kawaida huwezi kulihakiki hilo.

Ndugu yangu…MWEZI NI SATELAITI YETU. … TV unayoitazama matukio unayoyatazama Youtube na internet yote hayo ni kazi ya satellite, sasa hizi wakati mwingine hazina uwezo wa kuchukua kila tukio duniani vizuri…lakini hiyo satellite ya asili iliyotengenezwa na Mungu mwenyewe haina chenga hata kidogo..inarekodi kila kitu hata vile vya sirini.

Ndugu hakuna chochote unachoweza kukificha sasa, Mbingu na Nchi zinarekodi.. huu mwezi ni Jicho la Mungu ambalo kaliweka wazi ili watu wote waone, na wajue kuwa wanatazamwa juu, na waogope kufanya maasi…Waebrania 4:13 “…Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu”….Je! na wewe unaficha dhambi zako? Ni mwasherati kwa siri? Fahamu kuwa matendo yako yanarekodiwa juu, je! Ni mlawiti kwa siri? Mtazamaji wa pornography kwa siri?, ni mfanyaji masturbation kwa siri? Ni mwuaji kwa siri?, mchawi kwa siri? Mwizi kwa siri?…Tambua kwamba hakuna chochote unachoweza kukificha mbele za Mungu…

Siku ile mambo yako yote yatawekwa wazi screen itaonekana mbinguni ukiwa unafanya tukio moja baada ya lingine na utaambiwa ulitolee hesabu na utashindwa na utatupwa katika lile ziwa la Moto, huku moyoni ukijua kabisa umehukumiwa kwa haki…Mgeukie Muumba wako kabla siku za HUU MWEZI KUWA DAMU hazijafika. Kwasababu itafika siku Jua litatiwa giza na mwezi utakuwa mwekundu kama damu…kuashiria mwisho wa kumbukumbu za wanadamu…ndio maana kwenye mbingu mpya na nchi mpya hakutakuwa na MWEZI tena, kwasababu hakutakuwa na kurekodiwa tena kwa matukio ya watu kwasababu watu wote watakuwa wakamilifu.

Biblia Inasema katika Mithali 28: 13 “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. 14 Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote; Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara”.

Unaona inasema MSHUPAVU WA MOYO ATAANGUKIA MADHARA, Hayo madhara ni ZIWA LA MOTO

Ufunuo 21: 7 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Usizifiche dhambi zako leo kwasababu siku moja zitaanikwa mbele ya wote, Tubu leo kwa kukusudia kuziacha kuzifanya, unakusudia kuacha rushwa, ulevi, utukanaji, ulawiti, umalaya, utoaji mimba, uvaaji mbaya, anasa na mambo yote mabaya…Na Bwana atakupokea na kukupa Roho wake mtakatifu atakayekufanya usiwe na hamu ya kufanya hayo mambo tena..ili siku ile ya kutoa hesabu ya mambo yako yaonekane mambo mema tu! Huku

Bwana akubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

SWALI LA KUJIULIZA!

USILITAJE BURE JINA LA BWANA!

TULICHUNGUZE UMBO LA YESU NA MWENENDO WAKE.

NOTI YA UFALME WA MBINGUNI


Rudi Nyumbani

Print this post

SEHEMU YA MAANDIKO ILIYOFICHWA.

Tukisoma biblia kwa utulivu tutagundua kuwa maandiko yamegawanyika katika sehemu kuu tatu, sehemu ya kwanza ni maandiko ambayo yamefunuliwa moja kwa moja kwa wakati wote, na ya pili ni maandiko ambayo yalikuwa yamefungwa lakini yakaja kufunguliwa baadaye. Na sehemu ya Tatu ni maandiko ambayo yalionekena tu kwa sehemu lakini yakaja kufungwa tena.

Ni vizuri tukalielewa hilo ili tusiichukulie biblia kirahisi rahisi tu au kama kitabu kingine chochote cha kawaida ambacho hakina habari mpya ndani yake.

Sasa Maandiko yaliyofunguliwa moja kwa moja kwa wakati wote ndio yapi?, ndio haya ambayo kwa sehemu kubwa mimi na wewe tunayafahamu, ni maandiko ambayo yapo wazi, yalinakiliwa katika vitabu mtu yeyote anaweza akasoma na kwa kupitia hayo akamwomba Mungu na Mungu akamfunulia hekima iliyopo ndani yake, kwamfano unaposema vitabu vya Torati vyote, unaposoma vitabu vya wafalme, Ayubu, Esta, Zaburi, Yeremia, Isaya, Ezekieli, unaposoma vitabu vya Injili ya Yesu Kristo na Injili ya Mitume, n.k. vyote hivyo ni vitabu vilivyofunuliwa kwetu kwa wakati wote havina masharti Fulani au makomeo au mipaka. Yaani kwa lugha rahisi ni vitabu vinavyotufaa kwa wakati wote, kufundishia, kuonya na kufariji, kujenga n.k..sawasawa wakolosai 3:16

Lakini pia kuna aina nyingine ya maandiko ambayo hayo yalikuwepo tangu zamani, yalikuwa yamefungwa mpaka ulipofika wakati Fulani wa kufunuliwa..Na mfano wa haya tunaona ni kile kitabu cha Mihuri 7 katika kitabu cha Ufunuo mlango wa 6 ambacho kilikuwa kimetiwa muhuri ndani na nje, siri zilizokuwa ndani yake, hazikuwahi kujulikana na mtu yeyote mpaka wakati wa kufunuliwa kwake ulipofika, na tunasoma ni Yesu peke yake ndiye aliyestahili kuivunja mihuri ya kile kitabu na kwa kupitia ufunuo ule mkubwa ndipo tulipofahamu sisi ni akina nani, ndipo tulipofahamu tulipotoka na tunapokwenda, ndipo tulipofahamu mwenenendo wa yule mpinga-kristo, Yule Asi, jinsi atakavyoanza mpaka atakapomaliza na mahali kiti chake cha enzi kilipo, atakapotokea na atakapoishi. Mambo hayo hayakujulikana hapo kabla..Isipokuwa kwa wakati husika..

Vile vile yapo maandiko mengine ambayo, yaliyoonekana kwa sehemu tu na baadhi ya watu lakini yalifungwa mpaka wakati husika uliowekwa Na ndio maana utasoma Danieli aliambiwa..

Danieli 12:3 “Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.

4 Lakini wewe, Ee Danieli, YAFUNGE MANENO HAYA, UKAKITIE MUHURI KITABU, HATA WAKATI WA MWISHO; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka”.

Sasa tunaona watu hawa walipotaka kuyarekodi katika biblia walikatazwa wakaambiwa wasiyaandike kwanza, kwani hayo yametengwa mahususi kwa wakati Fulani wa mwisho. Ndugu nataka nikuambie, Mungu anayo Agenda yake kama vile ibilisi alivyo na Agenda yake, Sio kila siri ya ufalme wa mbinguni imerekodiwa katika kitabu hichi cha biblia, mambo mengine Mungu karuhusu makusudi yafichwe kwasasa, ili shetani asielewe chochote Mungu alichokipanga, Embu fikiria maneno yale Bwana Yesu aliyoyasema, msitupe Lulu zenu mbele ya nguruwe, wasije wakazikanyaga chini ya miguu yao, wakageuka na kuwararua.. Ikiwa Mungu ameruhusu sio kila jambo la ufalme wa mbinguni tutalifichua kwa kila mtu tu, kwanini na yeye asitenge fungu lake kwa ajili ya familia yake tu?.

NGURUMO SABA ZIPO MBIONI KUTOA SAUTI ZAO.

Tunaona Yohana alipokuwa Patmo, alionyeshwa maono mengi sana na Bwana Yesu Kristo, na mengi ya hayo aliambiwa ayaandike, ikiwemo ufunuo wa yale makanisa 7 na jumbe zao, ikiwemo baragumu saba, na vitasa saba, Lakini alipofika kwa Yule malaika mwenye nguvu sana aliyeshika kile kitabu kidogo, alipolia na ngurumo saba kutoa sauti zake alipotaka kuandika, alikatazwa asiandike. .Tunasoma hayo katika Ufunuo mlango wa kumi:

Ufunuo 10: 1 “Kisha nikaona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake; na uso wake ulikuwa kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto.

2 Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunguliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, nao wakushoto juu ya nchi.

3 Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. NA ALIPOLIA, ZILE NGURUMO SABA ZIKATOA SAUTI ZAO.

4 Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, YATIE MUHURI MANENO HAYO YALIYONENWA NA HIZO NGURUMO SABA, USIYAANDIKE”.

Ni mambo nyeti sana na ya kutisha vile vile, kwasababu siku zote ngurumo mara nyingi kwenye biblia inaashiria hukumu ya Mungu, sasa hizi ngurumo 7 (ambazo ni Huduma 7/watu 7) zitapoanza kutoa sauti zao, kwa kupitia maubiri hayo ambayo yatasikika ulimwenguni kote, Nguvu ya Mungu itashuka kwa namna ya ajabu juu ya watu wengi wanaume kwa wanawake waliochaguliwa…. ndugu yangu, masikio ya wengi yatawasha, kwasababu mambo yatakayosikiwa yatakuwa ni mpya yatakayoambatana na hukumu na mapigo. Wanaoichezea madhabahu ya Mungu sasahivi na wakiona hakuna chochote kinachotokea siku hiyo ndio watayapojiona kuwa wao kumbe walikuwa ni takataka mbele za Mungu, watajihukumu wenyewe kabla hata ya kufika kwa Mungu, wao wenyewe watakiri kuwa hawakuwa watumishi wa Mungu kwa jinsi mambo yatakayokuwa yanasemwa na hiyo nguvu ya uamsho wa ajabu itakayokuwa inatembea katikati ya Kristo na Bibi-arusi wake duniani.

Zekaria 13:3 “Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la Bwana; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtumbua atoapo unabii.

4 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; WALA HAWATAVAA JOHO YA NYWELE ILI KUDANGANYA WATU;

5 bali atasema, MIMI SI NABII KAMWE; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nalifanywa mtumwa tokea ujana wangu”.

Huu ni unabii Zekaria aliopewa wa kipindi hicho kinachokuja, kutakuwa na utiisho mkubwa katika kanisa la Mungu ambao haujawahi kuwepo, zaidi hata ule wa Petro alipokutana na Anania na Safira, walipoanguka na kufa baada ya kumwambia uongo Roho Mtakatifu, utakuwa ni mkubwa kuliko huo.

Kutakuwa na ishara na miujiza ya ajabu ambayo haijawahi kurekodiwa katika historia yoyote ya kanisa, Mungu atafanya mambo ambayo kila jicho litashangaa, na Mungu atafanya hivyo kumpa Bibi-Arusi wake imani ya kunyakuliwa, hapo ndipo sehemu ya pili ya ule unabii wa Yoeli wa mambo yatakayotokea siku za mwisho utatimia.

Matendo 2:19 “Nami nitatoa ajabu katika mbingu juu, na ishara katika nchi chini, damu na moto, na mvuke wa moshi

20 Jua litageuka kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla ya kuja ile siku ya Bwana iliyo kuu na iliyo dhahiri

21 Na itakuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa”.

Hayo yote yatatimia katika wakati huo, na hiyo itafanyika ndani ya kipindi kifupi sana, na ghafla utanyakuo utapita.

Dunia itabakia imeduwaa ikijiuliza ni nini hiki.. Na ndio maana mambo hayo yalihifadhiwa yasijulikane kwanza, na pia kumbuka kutatamkwa mambo mapya kabisa ambayo hutaweza kuyapata katika biblia, lakini hiyo haimaanishi kuwa yatapingana na Biblia hapana, bali yatakuwa mapya na sio wote watakayo yapokea isipokuwa wale wanawali werevu tu, ambao Mungu mwenyewe atawapa hekima ya kuyapokea. Huo ndio wakati Danieli aliosema Maarifa yataongeza, watu wote wa Mungu wataongezewa maarifa ya kumjua Mungu kwa kiwango cha ajabu.

Mjumbe wa Kanisa hili la mwisho la Laodikia WILLIAM BRANHAM, ambaye Mungu alimtumia kwa ishara nyingi na miujiza mingi Mungu naye pia alionyeshwa maono ya siku hizo zitapofika, kumbuka hapo kabla Bwana alimpa Maono mengi sana yaliyokuja kutokea yakathibitishwa kimataifa, mojawapo ndio lile la vita kuu vya pili vya dunia alionyeshwa jinsi Hitler atakavyonyanyuka na kuipeleka dunia katika vita na mpaka mwisho wake utakavyo kuwa wa kutokueleweka, aliliandika hilo (akamtaja mpaka jina) likisubiriwa litokee, na likaja kutokea vilevile,..na mengine mengi ukitaka kujifunza masomo yake utaniambia inbox niwe nakutumia.

Alionyeshwa kwa sehemu uamsho huo utakavyoja kuwa akasema alitamani na yeye awe mmojawapo wa uamsho huo kwa jinsi alivyoona miujiza ya ajabu iliyokuwa inafanyika. Halikadhalika na wahubiri wengi wengi maarufu walithibitishiwa juu ya hilo na Mungu mwenyewe.

Hivyo ndugu, ikiwa bado haupo ndani ya wokovu, unasubiria nini wakati huu wa neema sasa?. Kumbuka Jambo hilo litakapotokea halitamuhusu kila mtu duniani bali watu ambao tayari walishaanza kutembea na Mungu tayari huko nyuma, watu waliopokea ubatizo wa Roho Mtakatifu, Watu wanaotambua majira wanayoishi, Wengine wote hawataelewa chochote wala hawatasaidiki kwasababu Yule ROHO anayewavuta watu kumwamini yeye atakuwa hayupo ndani yao.

Ukiyajua haya, ufanye uteule wako imara sasa, tubu anza kutembea na Mungu katika muda huu mfupi uliobaki, kabla ya siku za hatari hazijaanza. Kwani kwa jinsi mambo yanavyoonekana tusitazamie sana vizazi vingine mbele yetu, hichi kizazi tunachoishi mimi na wewe kinaweza kushuhudia hayo yote.

Ubarikiwe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MIHURI SABA

HISTORIA YA WILLIAM BRANHAM

NGURUMO SABA

MIISHO YA ZAMANI.

NGUVU ZA ZAMANI ZIJAZO:


Rudi Nyumbani

Print this post

MAVAZI YAPASAYO.

Shalom, Mtu wa Mungu karibu tujifunze Neno la Mungu, Taa pekee ya kweli iongozayo miguu yetu.

Leo kwa ufupi tutajifunza ni kwanini Mwanamume hapaswi kuvaa mavazi yampasayo mwanamke, kadhalika na mwanamke hapaswi kuvaa mavazi yampasayo mwanamume.

Neno hilo linapatikana katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 22:5 “ Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo NI MACHUKIZO KWA BWANA, MUNGU WAKO.”

Jambo la msingi na muhimu ambalo watu wengi hatulifahamu kuhusu huu mstari ni kuwa Biblia haijasema hapo, mwanamume au mwanamke asivae mavazi yaliyotengenezwa mahususi kwa jinsia nyingine hapana bali imesema “YAMPASAYO”.

Neno yampasayo ni Neno linalohusiana na maumbile, yaani mavazi yanayopatana na maumbile ya mtu husika…

Kwamfano maumbile ya mwanamume ni ya misuli, na ukomavu kidogo, na yasiyo na mvuto hivyo mavazi yake yanapaswa yawe yanaendana na jinsi mwili wake ulivyotengenezwa, kadhalika na mwanamke mwili wake ni mlaini kidogo na umbo lake ni la kipekee tofauti na mwanamume hivyo na mavazi yake yanapaswa yaendane na jinsi mwili wake ulivyotengenezwa.

Kwahiyo mwanamume umbile lake linamlazimu avae suruali, wakati mwingine na nguo ngumu hayo ndio mavazi yanayoendana na mwili wake..Na kadhalika mwanamke hana sababu ya kuvaa suruali kwasababu umbile lake sio sawa na la mwanamume..yeye nguo zake ni magauni mazuri, marefu yaliyotengenezwa kwa ustadi mbali mbali ambayo yanamsitiri na sketi zenye heshima…hayo ni mavazi yanayompasa mwanamke

Sasa kwanini ni machukizo kuvaa nguo zisizoupasa mwili wako, leo tutajua ni kwanini ni machukizo..

Machukizo maana yake, ni kitu kinachochukiza, Mfano ukifanya kitu usichokitaka au usichokipenda maana yake hicho kitu kitakuchukiza, na kama tayari kimeshakuchukiza hapo ni rahisi kuchukua uamuzi wowote aidha kukasirika au kutengana na hicho kitu. Huo ni mfano tu!…Na tabia nyingine ya kitu kinachokuchukiza ni kwamba mtu mwingine anaweza asione kama kinakuchukiza, jambo linalokuchukiza wewe kwa watu wengine linaweza kuonekana kama ni jambo la kawaida.

Na ndivyo hivyo hivyo kwa Mungu wetu tunavyoonekana, tunafanya kitu kinachomchukiza tunapovaa mavazi yasiyopasa maumbile yetu. Unaweza ukaona hakuna shida kufanya hivyo lakini ni machukizo. Ni kitu kinachomuudhi sana Mungu ndani ya moyo wake.

Unakumbuka pale Edeni, Adamu na Hawa baada ya kuasi wakashona majani wakajitengenezea mavazi ya majani?…wao waliona wamejisitiri na kupendeza lakini mbele za Mungu wote wawili walikuwa wamevaa mavazi yasiyowapasa na hivyo Mungu hakupendezwa na yale mavazi akawatengenezea mavazi mengine ya ngozi.

Kwahiyo ni machukizo makubwa sana kuvaa mavazi yasiyoupasa mwili wako, jaribu kufikiri leo labda simba wamepewa akili kama mwanadamu..halafu unakwenda porini na kukuta simba kavaa ngozi ya fisi, au unamwona simba jike kaota zile nywele za shingoni kama za simba dume, na simba dume hana zile nywele..Unaona ni kitu kisicholeta picha nzuri ni kitu cha kuchukiza.

Na ndio hivyo hivyo tunavyoonekana mbele za Mungu..

Sasa hivi utakwenda kila mahali mpaka kanisani utakuta wanawake wamevaa suruali, na ukijaribu kuuliza atakwambia hizi ni suruali za kike kwahiyo hazina shida!! Dada yangu mpendwa…shetani asikupofushe macho, hakuna suruali za kike, suruali zote ni za kiume zilitengenezwa mahususi kufuatia maumbile ya wanaume soma kutoka 28:42-43 utathibitisha hilo…sio kwasababu na wewe dada una miguu miwili iliyogawanyika kama mwanamume ndio iwe sababu ya wewe kuvaa suruali, ndugu usidanganyike…hata simba jike ana kichwa kama cha simba dume lakini yale manyoya ya kichwa yamewekwa mahususi kwa ajili ya maumbile ya kichwa cha simba dume tu!!..Kwahiyo usijaribu kulinganisha vitu bila hekima ya macho ya rohoni..Hizi ni siku za mwisho, shetani anakuja kwa ujanja mwingi sana ambao usipokuwa makini unachukuliwa nao.

Hivi unajua kuwa siku hizi kuna SIDIRIA ZA KIUME PIA??…Kama ulikuwa hulijui hilo, hebu katafute kulijua, zipo sidiria za kiume na zinauzwa bei ghali sana, nyingine mpaka kufikia sh. Laki moja za kitanzani, na nyingine zaidi ya hapo, na zipo za mitindo tofauti tofauti.. unaweza ukazi-search kwenye google utaziona, na tena zina maua maua kama zile za wanawake, na zinavalika sana na kuuzika sana duniani, na zinaheshimika…Na watu wanazivaa kama fashion, nk.

Sasa hebu nikuulize wewe mwanamke, umekwenda kanisani na kukuta mchungaji kavaa hiyo sidiria ya kike halafu anakuhubiria na anakwambia hii haina shida! Ni sidiria ya kiume haina tatizo!! Je! Utamwamini?…si utasema dunia imeisha??…Kadhalika na wewe usidanganywe na kuambia ‘‘kuna suruali za kike’’.

Kama mchungaji wako havai sidiria za kiume madhabahuni asikudanganye na wewe uvae suruali za kike kanisani au nje ya kanisa, kama yeye haweki hereni, mabangili, hapaki wanja, lipstick wala havai sketi za kiume ambazo zipo na watu wanazivaa…basi asikudanganye na wewe uning’inize mambo hayo katika mwili wako…Biblia inasema mwanamke avae mavazi ya KUIJISITIRI, na sio ya Kuficha sehemu za siri (1Timotheo 2:9)..Suruali yoyote inafunua maumbile ya mwanamke, hivyo haiwezi kumsitiri, Kwanini avae?

Weka mbali vimini, weka mbali tattoo, weka mbali hereni, mawigi, suruali.. na kila aina ya fashion za ulimwengu huu..Biblia inasema aupendaye ulimwengu hata kumpenda Mungu hakupo ndani yake…

Jehanamu ipo!! Sio hadithi za kutunga..Ni kweli ipo! Ni kitu halisi na dhahiri kabisa..Na ni maelfu ya watu shetani anaofanikiwa kuwapeleka huko.

Ni matumaini yangu kuwa Bwana atakupa macho ya kuliona hilo, ili uiepuke ghadhabu yake..

Bwana azidi kukubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MAVAZI YA NDANI NA YA NJE.

WEWE NI HEKALU LA MUNGU.

JE! KUCHORA TATTOO NI DHAMBI?

MWANAMKE YEZEBELI

KUZIMU NI MAHALI PA NAMNA GANI, JE! HUKO WANAISHI WATU WAKIFA NA KWENDA KUPATA MATESO AU NI VINGINEVYO?


Rudi Nyumbani

Print this post