UMEITIKIA WITO INAVYOPASWA?

UMEITIKIA WITO INAVYOPASWA?

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.

Karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu, Taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu.

Moja ya masomo mapana sana ni ‘Namna ya kusikia sauti ya Mungu na kuielewa’..Mungu huwa anazungumza na sisi kila siku, lakini ugumu unakuwa ni namna ya kuielewa sauti ya Mungu..Ni kweli sio kila kitu Mungu atakachozungumza na sisi tutakielewa..sio kila kitu kwasababu tuna mipaka Fulani ya kiufahamu kutokana na hii miili tuliyonayo ya kidunia…lakini tutakapoivaa ile miili mipya ya utukufu basi tutamsikia na kumwelewa Mungu kwa mapana Zaidi. Lakini ni muhimu kutafuta kuisikia na kuielewa sauti ya Mungu kwa kadri tuwezavyo sasa, kwasababu Mungu kila siku anazungumza na sisi.

Zipo sababu nyingi zinazofanya tusisikie sauti ya Mungu kabisa..mojawapo ni maovu yetu (Isaya 59:1-2) na kingine ni kusongwa na mambo mengi…masumbufu ya Maisha haya…hizo ni kama kelele masikioni mwetu zinazozuia tusisikie sauti ya Mungu…Unapokuwa unasongwa na sauti nyingi nyingi za mambo ya ulimwengu huu inakuwa ni ngumu sana kuisikia sauti ya Mungu, mtu anayejihusisha na utazamaji wa movies muda mrefu, anakuwa anajisikilizisha sauti nyingine ambazo zinazuia masikio yake kusikia sauti ya Mungu…ni sawa na Mtu aliyeweka earphones kwenye masikio yake…hawezi kusikia sauti ya mtu anayezungumza naye akiwa nje…au kama ataisikia ataisikia kwa mbali sana…au anaweza akasikia isivyopaswa.

Kadhalika mtu anayekuwa katika shughuli nyingi za utafutaji wa mali kuanzia asubuhi, mpaka jioni anafanya hivyo siku saba katika wiki na miezi 12 katika mwaka..ni ngumu sana kuisikia sauti ya Mungu ikizungumza naye..purukushani za huku na kule za Maisha, anakutana na watu hawa, wale..anakumbana na tatizo hili au lile, watu hawa wanamweleza hivi au vile n.k hiyo inazuia sana kuisikia sauti ya Mungu.

Lakini leo hatutaingia sana huko. Leo tutajifunza ni kwa namna gani tunaweza tukaitikia vyema wito wa Mungu..yaani wakati Mungu anapotuita.

Kwanza ni muhimu kufahamu kuwa, Mungu anapozungumza sio kama wengi wetu tunavyotazamia..kwamba atazungumza nasi kwa radi mbinguni au mingurumo, au tutasikia sauti Fulani ya kipekee ya ajabu ikitunong’oneza masikioni. Inaweza ikatokea hivyo lakini hiyo sio njia ambayo Mungu anaitumia kusema na watu siku zote…wengi wanaitafuta hiyo njia lakini Mungu hatumii njia hiyo, sauti ya Mungu inapokuja ni kama ‘’mawazo Fulani yanaingia ndani yako ambayo yanakuwa yanakupa ufunuo fulani’’..Mawazo Fulani yanayokufumbua macho ya kuelewa jambo Fulani ambalo ulikuwa hulielewi au ulikuwa hulijui. Na hayo mawazo yanakuwa ni kama vile wewe umeyatengeneza…unaweza ukadhani ni wewe unajiambia mambo hayo, lakini sio wewe ni Bwana anazungumza na wewe…Sauti yake wakati mwingine inafanana na sauti yako kabisa, isipokuwa ya Mungu inakuja na ufunuo Fulani wa kimaandiko, ambao huo ukiupata unasikia kusisimka katika roho, unajisikia furaha kulijua hilo jambo, unajisikia amani, unajisikia kumgeukia Mungu Zaidi na kumpenda…unajisikia kutolewa sehemu moja hadi nyingine kiimani…Hiyo ni sauti ya Mungu imezungumza na wewe. Na mara nyingi hii inakuja ukiwa sehemu ya utulivu sana ukimtafakari Mungu, au ukiwa katika kulisoma Neno lake. Kwa jinsi unavyokuwa mtulivu zaidi na kulitafakari Neno la Mungu zaidi ndivyo wigo mpana wa kuisikia sauti ya Mungu unavyokuja.

Pia licha ya sauti ya Mungu kufanana sana na sauti yako, lakini pia inafanana na sauti ya Mtu mwingine ambaye yupo karibu na wewe kiimani..Mtu anaweza kuzungumza na wewe Neno Fulani la kiMungu ukaona limekupa msisimko fulani ndani yako ya kutaka kumjua Mungu Zaidi, au kumpenda Mungu, au kumtafuta..Huyo ni Mungu anazungumza na wewe, ingawa unaweza kudhani ni yule mtu kazungumza na wewe, lakini kiuhalisia si Yule mtu bali ni Mungu.

Unaweza pia kuwa katika utulivu..Bwana akaanza kuzungumza na wewe kupitia mahubiri ambayo ulishawahi kuyasikia huko nyuma, ukasikia kabisa kama vile yule mtu anakuhubiria masikioni mwako saa hiyo…ukapata kufunguliwa macho na kuona kitu kipya ambacho ulikuwa hukijui…Sasa huyo ni Mungu anazungumza ndani yako kupitia sauti ya yule Mtumishi uliyemsikia. Na kwasababu bado hujaijua sauti ya Mungu wewe utadhani ni yule mtumishi anazungumza na wewe na hivyo utatafuta njia yoyote ya kwenda kukutana naye au kujiunga katika dhehebu lake au kanisa lake..

Lakini nataka nikuambie hapo utakuwa hujaitikia vyema wito wa Mungu. Ingawa uliisikia kweli sauti ya Mungu. Lakini huko uendako unakwenda kupotea….Hebu tujifunze kidogo katika maandiko juu ya jambo hilo.

1 Samweli 3: 1 ‘Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.

2 Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona),

3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu;

4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.

5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.

6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena.

7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.

8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto.

9 Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake.

10 Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.

11 Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha.

12 Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho.

13 Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia.

14 Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele.’’

Katika habari hiyo tunamwona kijana Samweli…Na siku moja Mungu alipotaka kujifunua kwake, hakuzungumza naye na sauti mpya ya ajabu ya kipekee…bali alizungumza naye moyoni mwake na sauti inayofanana kabisa na ile ya Eli…’yaani kwa ufupi aliisikia sauti ya Eli ikimwita’..Na yeye kwasababu alijua Eli ni Mtumishi mteule wa Mungu, aliyechaguliwa na Mungu atumike katika nyumba ya Mungu…aliitikia wito isivyopaswa akamfuata Eli kwasababu tu ile sauti aliyoisikia ilikuwa kama ya Eli..akaenda kwa Eli lakini hakukipata kile alichokuwa anakitafuta kwa maana alitegemea aambiwe sababu ya kuitwa kwake lakini hakuambiwa..Akarudi kulala tena…akaisikia ile ile sauti kama ya Eli ikimwita mara tatu, bado akarudia kosa lile lile la kwenda kumfuata Eli mpaka Eli alipomsaidia kupata ufahamu kuwa Sauti aliyoisikia sio ya Eli ni ya Mungu, japokuwa inafanana na ya Eli mtumishi wa Mungu.

Na alipotulia kwa makini, na kuitikia vyema wito wa Mungu, ndipo Mungu akaanza kumwambia kusudi la wito wake…Samweli akaja kugundua kuwa kumbe huko kwa Eli alikokuwa anakwenda ndipo Mungu alipopachukia na ndiko Mungu anapotaka kumtuma akawaambie makosa yao.

Na sauti hiyo hiyo inawaita wengi leo hii…Lakini inapoita sio wakati wa kuitikia na kwenda kumfuata huyo mtumishi au dhehebu la huyo mtumishi unayesikia ujumbe kutoka kwake..Bwana ametumia tu sauti ya huyo mtumishi au sauti ya hilo dhehebu kukuita wewe…Lakini Bwana hayupo huko hata kidogo..Yupo hapo hapo ulipo?. Anapokuita ndugu usiende kujiunga na madhehebu utapofuka macho. Hutamsikia Mungu huko hata kidogo. Ndicho kilichomtokea Samweli mpaka alipoelewa somo.

Ndugu udhehebu ni mnyororo mbaya sana, ambao unawakosesha wengi na kuwapeleka kuzimu..Samweli hakujua uovu uliokuwa unaendelea kwenye nyumba ya Mungu ambao ulikuwa unaongozwa na Eli pamoja na wanawe..mpaka siku alipotoka na kuisikia sauti ya Mungu, akagundua kuwa kumbe Mungu ametukasirikia, kumbe japo watu kwa nje wanaona kila kitu kipo sawa lakini kumbe Mungu katukasirikia sisi tuliopo ndani…na hata huyu Eli ambaye Mungu alitumia sauti yake kuzungumza nami..kumbe hata yeye tayari kashaharibu mambo siku nyingi…hayo yote Samweli aliyajua baada ya kutoka kwenye udini na udhehebu wa Eli.

Hivi unajua chapa ya mnyama inauhusiano mkubwa sana na dini na madhehebu…Roho ya Mpinga-Kristo sasa inatenda kazi katikati ya madhehebu, kuhakikisha inawafunga matita matita watu na kuwapeleka watu jehanamu..sawasawa na Mathayo 13:30. Ndio maana unaona madhehebu yanaongezeka kila kukicha…Huo sio mpango wa Mungu kabisa…. Itafika siku moja baada ya unyakuo kupita, madhehebu yote yatasajiliwa katika umoja wa madhehebu duniani..na watu hawataweza kununua wala kuuza wala kuajiriwa wasipokuwa washirika wa mojawapo ya madhehebu yaliyosajiliwa katika umoja huo wa dini na madhehebu duniani…Siku hiyo mamilioni ya watu wataipokea chapa pasipo kujua kuwa wameipokea. Maelezo yake juu ya hayo ni marefu kidogo lakini..Kama hujafahamu kuhusu hayo basi yafuatilie na uyajue au unaweza ukanitext inbox nikutumie somo juu ya hayo.

Lakini huu sio wakati wa kujisifia dhehebu wala dini, ni wakati wa kutoka huko na kurudi kwenye Neno,(Ufunuo 18:4) huu sio wakati wa kusema mimi ni Muanglikana, Mlutheri, Mkatoliki, Mlokole, Msabato, Mbaptist, Mbranhamite, Mmennonites n.k Huu ni wakati wa Kuwa Mkristo wa kweli wa kimaandiko, Bibi arusi safi, aliyeisikia sauti ya Mungu kweli na kuitikia wito inavyopaswa kwa kuzaliwa mara ya pili na kuishi kulingana na Neno la kwenye biblia(Maisha ya utakatifu na yanayompendeza Mungu).

Mungu anapokuita itikia wito ipasavyo, Rudi kwenye Neno lake ndipo mahali salama, ujifunze ukue kiroho, Ona fahari juu ya Roho Mtakatifu anakushuhudia kila siku kuwa wewe ni mwana wa Mungu kuliko dini au dhehebu hivyo havitakufikisha popote.

Bwana akubariki sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Zinazoendana:

WITO WA MUNGU

JE! UMECHAGULIWA KABLA YA KUWEKWA MISINGI YA ULIMWENGU?

IELEWE SAUTI YA MUNGU.

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

SADAKA ILIYOKUBALIKA.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
yohana
yohana
2 years ago

Upo vizuri mtumishi wa MUNGU je vizuru kukuuliza kuhusu maagizo ya mungu (amri10) maana sifaham sijajifunza vizuri kuhusu amri za mungu na 7to iliyopo katikati ya amri10 kwahiyo ukitoa moja zinabaki 9 je unakua uposahihi au umekosea?

Asheri Stephen
Asheri Stephen
3 years ago

Ndugu Shalom,
Mungu akubariki sana kwa huduma nzuri ya Neno la Mungu. Nimepitia sehemu ya masomo yako kidogo na nimependa sana tena ubarikiwe. Naomba kwa kadri ya upatapo nafasi unitumie masomo yanayo husu madhehebu namna Shetani anavyo yadanganya na kuyatumia katika kipindi hiki cha mwisho. Lakini pia nakusihi katika Bwana unitumie pia masomo mbalimbali ili niendelee kujifunza kupitia kusoma kumbe hizi zenye Ufunuo wa Mungu sahihi. Ameni. Simu yangu ni 0626619369, au kwaziada 0621036527 hii zaidi sana ni WhatsApp.