Category Archive Uncategorized

Wana wa Asafu ni akina nani katika biblia?

Kabla ya kuwafahamu wana wa Asafu, ni vizuri kumfahamu Asafu mwenyewe alikuwa ni nani.

Asafu alikuwa ni mmoja wa walawi ambao, mfalme Daudi alimuweka  kama kiongozi wa mbele wa sifa, atakayesimama mbele ya sanduku la Mungu daima kumsifu Mungu. (Soma 1Nyakati 6:31-32, 39).

1 NYAKATI: MLANGO 16

1 Wakaliingiza sanduku la Mungu, na kuliweka katikati ya hema aliyoipiga Daudi kwa ajili yake; wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu.

2 Na Daudi alipokwisha kuitoa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani, akawabariki watu kwa jina la Bwana.

3 Kisha akawagawia kila mtu wa Israeli, waume kwa wake, kila mtu mkate wa ngano, na kipande cha nyama, na mkate wa zabibu.

4 Akawaagiza baadhi ya Walawi kwamba watumike mbele ya sanduku la Bwana, wamfanyie ukumbusho, na shukrani, na sifa, Bwana, Mungu wa Israeli;

5 Asafu mkuu wao, na wa pili wake Zekaria, na Yeieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Matithiya, na Eliabu, na Benaya, na Obed-edomu, na Yeieli, wenye vinanda na vinubi; naye Asafu mwenye kupiga matoazi;

Kulingana na maandiko, biblia inasema huyu Asafu hakuwa tu mwimbaji, bali Mwonaji pia,

2Nyakati 29:30 “Tena Hezekia mfalme na wakuu wakawaamuru Walawi, wamwimbie Bwana sifa kwa maneno ya Daudi, na ya Asafu mwonaji. Wakaimba sifa kwa furaha, wakainama vichwa, wakaabudu”.

Baadaye, uzao wake uliendeleza  nyayo zake, na wote wakawa waimbaji katika hekalu la Mungu lililokuja kujengwa baadaye, na hata baada ya ule uhamisho wa Babeli, waliporudi bado waliweza kuwekwa katika kazi hiyo hiyo ya Sifa..

Soma, Ezra 2:41 “Waimbaji; wana wa Asafu, mia moja ishirini na wanane”.,

Pia Nehemia 7:44

Halikadhalika kuna baadhi ya Zaburi zilijulikana kama Zaburi za Asafu,Ambazo ni Zaburi 50 na ya 73-83. (Baadhi ya tafsiri zinaonyesha hivyo). Hiyo ni kuonyesha kuwa Mungu alimtumia yeye na uzao wake kwa njia ya uimbaji, kutoa nabii ambazo zinatusaidia hadi sasa.

Lakini kwasasa wana wa Asafu ni akina nani? Na tunapata funzo gani?

Wana wa Asafu ni watu wote wanaotumikia madhabahuni pa Bwana katika huduma ya kumsifu na kumwimbia Mungu. Watu hawa wanatenda kazi kubwa inayompendeza Mungu na kwa kupitia wao, Mungu huwa anapitisha, jumbe zake nyingi, na nabii nyingi zinazookoa na kuponya watu kama ilivyokuwa kwa wana  wa Asafu, hii ikiwa na maana, kwamba wakitumika vema katika kazi yao, basi ni utumishi mkubwa sana, hata Zaidi ya huduma nyingine zote.

Lakini, watu hawa walijua kanuni ya kumwimbia Mungu, walimwimbia Mungu katika “uzuri wa utakatifu”, sawasawa 1Nyakati 16:29. Tofauti na sasa, waimbaji wengi, wamekuwa wasanii, wanageuza uimbaji wa injili kuwa Sanaa na sio wito na huduma ya Kristo Yesu.

Wanasahau kuwa huduma yao ndio ya kwanza kabisa inayomkaribia Mungu Zaidi ya nyingine zote,..Huduma ya Maserafi na Makerubi malaika watakatifu wasimamao mbele ya Mungu daima

Lakini kinyuma chake, Mwimbaji wa injili, utamkuta anakata mauno, anavaa vimini, anapamba uso kama Yezebeli, anaimba kwa staili za wasanii wa kidunia.. Twategemea vipi Mungu atasema au atawaponya, au atawafungua na watu wake kupitia uimbaji huo?, Haiwezekani..Inasikitisha kuona, kanisa la sasa, kundi kubwa la watu walioharibikiwa linatoka kwa wanakwaya na waimbaji.

Kumbuka Sababu  iliyowafanya wana wa Israeli,wapelekwe utumwani haikuwa tu kuabudu maashera hapana, ilikuwa pia ni hiyo ya unafki katika kumwimbia.

Amosi 6:5 “ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi;”

Bwana anatuonya vikali, na sisi pia atatuadhibu vikali kama tutakuwa na tabia kama za wao,  anataka anapoimbiwa aimbiwe katika “uzuri wa utakatifu” (1Nyakati 16:29)..Maana yake ni kwamba wewe mwongoza sifa, wewe mwimbaji, wewe mpiga kinanda,wewe mpiga gitaa, uwe kielelezo kuanzia mavazi yako, usemi, hadi tabia, mbele za watu. Utakatifu ndio uwe leseni yako, ya kumwimbia Mungu.

Kama utashindwa utakatifu, ni heri uache tu, ukafanye kazi nyingine, kwasababu utakuwa unajizombea laana badala ya baraka.

Mahali Mungu anasifiwa na kuabudiwa ni kuwa makini sana.. wengine walipoteza Maisha walipojaribu kuvuruga utaratibu pindi Mungu anapokuwa anasifiwa (Soma 2Samweli 6:1-11 ), Vivyo hivyo na wewe mwimbishaji kanisani, usipokuwa siriazi na huduma yako, uwezekano wa kukutwa na hayo upo mkubwa sana.

Bwana anataka sote tuwe wana wa Asafu, ili atutumie kumtukuza yeye, Pamoja na kuzungumza na watu wake, ili aziponye roho za watu..

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MAOMBI YA YABESI.

NI KITU GANI TUNAJIFUNZA KWA RISPA, BINTI AYA?

SOMO no.02 (BINTI WA YEFTHA).

Gongo na Fimbo ni nini? Na vinawezaje kumfariji mtu? (Zaburi 23:4).

Nini maana ya “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi”?

NI SALAMA ROHONI MWANGU Lyrics

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri.

Rudi nyumbani

Print this post

Maongeo ni nini?(Wakolosai 2:19)

Maongeo ni maongezeko,

Kwa mfano Neno hilo utalisoma katika vifungu hivi;

 Kutoka 23:10 “Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kuyavuna maongeo yake;

11 lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni”.

Soma pia Walawi 19:24

Maana yake ni kuwa kwa muda wa miaka sita Mungu aliwaruhusu wana wa Israeli wapande na kuvuna, hata na vile vinavyoongeza katika mavuno yao. Lakini ufikapo mwaka wa saba, hawakuruhusiwa kuvuna chochote bali waviache kwa ajili ya maskini na Wanyama wa kondeni.

Isaya 9:7 “Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo”.

Maana yake ni kuwa maongezeko ya enzi yake, na amani hayatakuwa na mwisho yataendelea kuongezeka na kuongezeka milele. Na anayezungumziwa hapo si mwingine Zaidi ya Yesu Kristo Bwana wetu.

Wakolosai 2:18 “Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili;

19 wala hakishiki Kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na kuungamanishwa kwa viungo na mishipa, hukua kwa maongeo yatokayo kwa Mungu”.

Hapo anaposema, “hukua kwa maongeo yatokayo kwa Mungu”, ana maana kuwa, mwili huo(ambao ndio kanisa la Kristo) ukishakwisha kushikamanishwa Pamoja viungo vyote.. Basi hukua, kwa maongezeko (maongeo), yatokayo kwa Mungu..Sio maongezeko yatokayo kwa mwanadamu.

Hii ikiwa na maana hata sisi kama wakristo, tukishikama Pamoja na Kristo tukamfanya kuwa kichwa chetu, basi, tutakuwa katika ukuaji (maongezeko )unaotoka kwa Mungu mwenyewe..

Lakini kinyume chake ni kweli tukimkataa Kristo, kama kichwa cha kanisa, na kuwafanya wanadamu kuwa ndio vichwa vyetu, basi hatutakuwa na maongezo yoyote ya rohoni au mwilini, na hata kama tukiwa nayo, basi yatakuwa hayatokani na Mungu bali ibilisi.

Hivyo hatuna budi kumfanya Kristo kichwa cha kila kitu.. kwasababu ufalme wake unadumu milele. Lakini tukifanya tunajua kujenga ngome zetu au falme zetu, tufahamu kuwa taabu zetu zitakuwa ni bure mwisho wa siku.

Ukuaji wetu wa ndani na nje, unamtegemea Yesu Kristo tu, zaidi yake hakuna mwingine.

Sifa heshima na utukufu vimrudie yeye milele na milele daima.

Bwana atusaidie.

Shalom..

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Sadaka ya kinywaji ilikuwaje? Na inawakilisha nini?

Mkatale ni nini katika biblia? (Matendo 16:24)

SIFONGO NA SIKI NI NINI?

Pakanga ni nini?

Talanta ni nini katika biblia (Mathayo 25:14-30)

Santuri ni nini? (Danieli 3:5,10)

Bushuti ni nini?

Donda-Ndugu ni nini?

Pango la Makpela ni lipi, je lina umuhimu wowote kwetu?

Rudi nyumbani

Print this post

KWANINI KUWE NA UTAWALA WA MIAKA 1000

Biblia inatuonyesha baada ya tukio la unyakuo, ambapo watakatifu watakwenda mbinguni kwenye karamu ya mwana-kondoo kwa kipindi cha miaka saba, ..watarudi tena duniani wakiwa na Bwana Yesu ili kutawala naye kwa muda wa miaka 1000.

Sasa utajiuliza ni kwanini Bwana Yesu asiwe nao milele mbinguni bali arudi tena dunia kutawala nao. Makusudi ya Bwana ni yapi?

Sasa leo hatupo  kueleza kwa urefu, huo utawala utakujaje kujaje na wakati gani..ikiwa utapenda kupata somo lake kwa urefu basi fungua link hii >>> UTAWALA WA MIAKA 1000.

Lakini nataka tuone sababu za kuwepo kwa utawala huo…

Sababu zipo  mbili kuu

  1. Ni kwamba Yesu anataka kuwapa raha watu wake.

Raha hiyo inajulikana kama raha ya sabato..

Waebrania 4:9-11

[9]Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.

[10]Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.

[11]Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi.

Hichi ndicho kipindi ambacho Bwana atawarejeshea vyote watumwa wake walivyovipoteza kwa ajili yake walipokuwa hapa duniani  kwa kuwapa ufalme ulio bora wenye nguvu na wa kudumu. (Yoeli 2:25)

Watatawala kama wafalme na mabwana, na makuhani,..na Yesu Kristo mwenyewe akiwa kama Bwana wa Mabwana na Mfalme wa Wafalme.

Kipindi hicho dunia hii itarejeshwa na kuwa nzuri sana hata zaidi ya ilivyokuwa Edeni. Dunia yote itajawa na amani..kwasababu kipindi hicho ibilisi atakuwa amefungwa kwa muda wa miaka 1000,

Ikiwa wewe iliishi maisha ya kujikana na huu ulimwengu wa kitambo unaopita, basi kule utakuwa na nafasi kubwa sana kwa Yesu Kristo, tutakuwa na miili mipya ya utukufu isiyougua wala kuzeeka, utaburudishwa kwelikweli,

Na raha isiyo na kifani itatawala nyuso za watu wa Mungu, mtu ambaye ulionekana umerukwa na akili kwa kumtumikia kwako Mungu, binti ulionekana mshamba kwa kujisitiri kwako, Bwana atakupa heshima na faraja yako ya kumiliki.

Wote waliotaabika kwa ajili ya injili ya Kristo kwa namna moja au nyingine huo  ndio utakuwa wakati wa kuburudishwa na kuyafurahia maisha.. Ni lazima Bwana Yesu afanye hivi, ili kuwathibitishia watu wake kwamba hakuna chochote walichokipoteza walipokuwa hapa duniani walipomfuata yeye.

2.   Jambo la pili: Ni ili kuweka maadui zake wote chini.

ambapo wa mwisho atakuwa ni mauti.

1 Wakorintho 15:24-26

[24]Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu.

[25]Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke maadui wake wote chini ya miguu yake.

[26]Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.

Kumbuka hata katika utawala ule watu watakuwa wanaendelea kufa, wale ambao walizaliwa humo..lakini sisi hatutakufa kwasababu tutakuwa na miili ya utukufu tuliyotoka nayo mbinguni.

Hivyo Bwana Yesu atadhibiti maadui zake waliosalia (wa rohoni) na wa mwisho wao atakuwa ni mauti,

Kwasasa, bado maadui baadhi wa Bwana Yesu hawajadhibitiwa, na ndio maana bado utaona watu wanakufa, lakini mambo hayo yote, atayamaliza ndani ya huo utawala wa amani wa miaka 1000.

Hivyo mpaka utalawa unakwisha..mambo yote mabaya yatakuwa yamekwisha kabisa kabisa.

Na baada ya hapo sasa ndio inakija mbingu mpya na nchi mpya..huko hakutakuwa na kilio wala mateso, wala huzuni, wala mauti, kwasababu tayari vilishakomeshwa na Yesu Kristo vyote katika utawala ule.

Na ile Yerusalemu itakushuka sasa kutoka mbinguni, ambapo Mungu kwa mara ya kwanza atafanya maskani pamoja na wanadamu.(Ufunuo 21&22)

Yaani kwa ufupi ni kwamba Mungu atahamishia makao yake hapa..

Uzuri na mambo yaliyopo huko..biblia inasema jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia,

Jua na mwezi havitakuwepo..ulimwengu huu utageuzwa na kuwa sehemu ya tofauti kabisa..

Lakini ikiwa wewe upo nje ya wokovu, unayo hasara ya mambo mengi, ya kwanza ni karamu ya mwana-kondoo mbinguni, ya pili ni utawala wa miaka 1000 na mwisho mbingu mpya na nchi mpya.

Hivyo itakufaidia nini uupate ulimwengu mzima kisha upoteze roho yako.

Kumbuka kwa jinsi hali ilivyo hichi ni kizazi kitakachoshuhudia tukio la unyakuo, hatuweki siku lakini kwa dalili zinavyoonyesha hatuna muda mrefu Kristo anarudi..labda pengine leo usiku.

Hivyo tuanze kuelekeza mawazo yetu mbinguni, tuachane na mambo haya ya kitambo ya ulimwengu. Yesu ameshatuandalia makao, ambayo atakuja kutuburudisha kwa kipindi cha miaka 1000. Tutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kabisa kuziacha. Na Bwana atatupokea na kutusamehe.

Bwana akubariki

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

IMESALIA RAHA YA SABATO KWA WATU WA MUNGU.

UMUHIMU WA KUBATIZWA.

Kiyama ni nini?

JE KANISA LITAPITIA DHIKI KUU?

MAOMBOLEZO YA HADADRIMONI.

USICHELEWE KUMPAKA BWANA MARHAMU!

Kupiga ramli ni nini katika biblia?

NI SALAMA ROHONI MWANGU Lyrics

Rudi nyumbani

Print this post

Tofuati kati ya kifo na mauti ni ipi?

Kifo ni ile hali ya uhai kutoka ndani ya kiumbe hai chochote. Kifo kinaweza kumtokea mtu, mnyama, bakteria, kirusi, mmea, jani n.k. Vyote hivi maadamu vina uhai ndani yao, vinapotokwa tu huo  uhai basi vinakuwa vimekufa.

Lakini Mauti ni nini?

Mauti ni kile kile kifo, isipokuwa ni mahususi tu kwa mwanadamu.. Huwezi kusema “mti” umekumbwa na mauti, au “mbwa” amepatwa na mauti.. Bali utasema, mti umekufa au mbwa amekufa. Ni mwanadamu tu ndiye anayekumbwa na mauti.

Lakini kwanini Kifo kitofautishwe na mauti?

Ni kuonyesha uzito wa hali hiyo kwa mwanadamu.. Kwamfano “Kilio” kinaweza kutokea kwa mtu yeyote yule, iwe ni mtoto au mtu mzima Lakini kikiwa kwa mtu mzima, hakiwezi kuchukuliwa kama kile cha mtoto, kwasababu kama vile wasemavyo wanajamii, “ukiona mtu mzima analia basi ujue kuna jambo”

Maana yake ni kuwa hadi mtu mzima anatoa machozi, ujue hayajaja bure bure tu, bali yana sababu nyuma yake, na matokeo mbele yake, kwasababu si desturi ya mtu mzima kulia. Nyuma yake utagundua aidha kuna msiba, au magonjwa, au kuumizwa moyo kusikoelezeka, kusalitiwa au kupoteza mali zake nyingi, au vitu, n.k.. Lakini mtoto mdogo anaweza akalia kwasababu zisizokuwa na maana au msingi wowote.

Vivyo hivyo katika kifo na mauti ni tendo lilelile..kuondoka kwa uhai.. isipokuwa linapokuja kwa mtu, linakuwa na uzito wa namna yake, kwasababu mwanadamu hakuumbiwa kifo, halidhalika kwa sifa yake na heshima na akili alizopewa na Mungu, jambo kama hilo ni anguko kubwa sana kwake..Mauti ni pigo kwa mwanadamu.

Sababu ya mauti kumpata mtu ni nini?

Ni dhambi..

Warumi 6:23 “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu”.

Sisi wanadamu tulipoasi, adhabu hii ya mauti ilitukumba.. Hilo ni pigo kubwa sana kwetu, tofauti na Wanyama, wenyewe hawajui chochote, wala hawaelewi, kufa na kupotea kwao ni kitu cha kawaida, lakini sisi tunajua kwamba ipo siku uhai utatutoka..

Lakini heri ingekuwa ni kifo cha miili yetu tu halafu basi.. Lakini Huko mbeleni pia baada ya kifo, kuna adhabu ya kifo cha roho. Hiyo ndio inayoitwa mauti ya pili..Ambazo roho hizi zitamalizwa kabisa katika lile ziwa la moto..Hapo ndipo utaona, tofauti ya kifo cha mnyama, na kile cha mwanadamu.

Ndugu, ukikumbwa na mauti sasa, toa yale mawazo kwamba utakuwa kama mnyama tu.. Hapana, ukifa katika dhambi, utanyoshea moja kwa moja hadi jehanamu, ukisubiri siku ya ufufuo ifike uhukumiwe kisha utupwe katika ziwa la moto milele na milele.

Lakini Habari njema ni kwamba, Bwana Yesu alikuja kukomesha mauti kwa mwanadamu, na kwamba yeyote amwaminiye yeye, anakuwa amevuta kutoka katika mauti na kuingia kwenye uzima..

Yohana 5:24 “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani”.

Umeona? Yaani Yesu akikuoa mauti inakuwa haina nguvu tena ndani yake..

Hivyo ndugu, wasubiri nini, leo usimkaribishe Yesu moyoni mwako.? Kumbuka hakuna mtu mwenye garantii ya kuishi milele. Au anayeijua kesho yake kama atakuwa duniani au la. Ukifa katika dhambi ni nani atakayekuponya na mauti ya roho yako? Huko utakapokwenda utakuwa mgeni wa nani. Kama huna uhakika, unajisikiaje kubaki katika hali hiyo?

Lakini nafasi sasa unayo, Ikiwa upo tayari kufanya hivyo leo, yaani kuongozwa sala ya toba ya kumpokea Yesu.. Basi fungua hapa kwa ajili ya mwongozo huo >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa kifo kinampata kiumbe hai chochote, lakini mauti ni mahususi kwa mwanadamu, kwasababu yenyewe inabeba maana kubwa zaidi ya kifo cha kutoka uhai tu. Mauti imebeba uchungu, majuto, masononeko, hukumu, nyuma yake, jambo ambalo kifo hakina.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

jiunge kwenye group la whatsapp la mafundisho ya kila siku kwa kubofya hapa >>> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Jehanamu ni nini?

Kuna hukumu za aina ngapi?

Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?

NINI KINATOKEA BAADA YA KIFO?

UNYAKUO.

DHAMBI YA MAUTI

BALI WANA WA UFALME WATATUPWA NJE!.

Rudi nyumbani

Print this post

UTAKAPOKUWA MZEE, UTAINYOSHA MIKONO YAKO. NA MWINGINE ATAKUFUNGA

Bwana Yesu asifiwe,

Ufukufu na Heshimu ni vyake milele na milele. Amina.

Napenda tutafakari, Pamoja kwa makini maneno haya ambayo Bwana Yesu alimfunulia mtume wake Petro, ni maneno ambayo yatakufaa sasa wewe kijana ambaye bado una nguvu za kufanya utakalo hivi sasa..

Embu Tusome;

Yohana 21:18 “Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na MWINGINE atakufunga na kukuchukua usikotaka”.

Hii kauli ni ya kuitafakari sana, sio ya kuichukulia juu juu, Hapa Bwana anamweleza Petro jinsi ujana wake unavyoweza kumpa uhuru wa ‘nani wa kujifunga chini yake’, na kumtumikia, mfano akiamua, ajifunge na kuwa mtumwa wa mali, uamuzi ni wake, akitaka ajifungue kisha ajifunge kwa mwingine tena, bado uwezo huo anao, leo anaweza akajifunga kwa Mungu, kesho kwa shetani, ni jinsi apendavyo kwasababu nguvu hizo anazo rohoni.

Hapo ndipo lile neno linalosema, “nimewaandikia ninyi vijana kwasababu mna nguvu ya kumshinda yule mwovu”(1Yohana 2:14), linapotimia, maana yake, uwezo wa kujifungua au kujifunga kwa shetani, unao, angali  bado una nguvu..

Lakini tunaona Bwana Yesu anampa angalizo lingine na kumwambia, utakapokuwa mzee, “MWINGINE”..Atakufunga na kukuchukua usikotaka..

Sasa ulishawahi kutafakari huyo ‘mwingine’ ni nani?

Huyo mwingine ni Aidha “Mungu” au “Shetani”.. Maana yake ni kuwa utafika wakati, ambapo kama hutajiweka chini ya Mungu tangu sasa, shetani atakuweka chini yake kipindi hicho, penda usipende,..yaani utamilikiwa na shetani asilimia mia ya Maisha yako, na kukufanyia chochote apendacho juu yako..

Ukishafikia hii hatua, kamwe huwezi tena kumgeukia Mungu, wala hata kuzielewa Habari za Mungu, kwasababu tayari wewe ni mfungwa wa shetani.

Hali kadhalika kinyume chake ni kweli, unapofanyika chombo cha Mungu sasa angali una nguvu..utafika wakati huna nguvu, Mungu atakuchukua moja kwa moja na kukupeleka atakapo yeye.. Huko ndipo wakati ambapo uzee wako unaishia vema..hata kama ni kwa kifo kwasababu ya ushuhuda, lakini kamwe hutakaa upotee tena milele..kwasababu umeshafungwa tayari na Mungu, hivyo hakuna namna yoyote utakaa upotee au uanguke mikononi mwa shetani.

Ndio maana biblia inasema..

Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo”.

Maana yake ni kwamba usipomkumbuka muumba wako leo, wakati una nguvu (wakati wa ujana wako) utafikia wakati, utapoteza furaha yako yote ya maisha.. Hicho ndicho kipindi cha kufungwa na ibilisi, na kupelekwa usipotaka..Angalia vema utaona wazee wengi ambao wamekuwa wakipuuzia injili tangu ujanani, mwisho wao huwa hauwi mzuri, kunakuwa na ugumu mkubwa sana kuwashawishi kwa Habari ya wokovu. Huwa wanapitia wakati mgumu sana kiroho kwasababu tayari “mwingine” ameshawafunga na kuwachukua wasipotaka..

Hivyo Bwana Yesu alikuwa anamtahadharisha Mtume Petro, sio tu kwa Habari ya kifo chake, lakini pia kwa maamuzi anayoyachukua sasa..lazima yawe ya busara.. Utumwa anaouchagua sasa, ndio utakaomuhifadhi baadaye..

Kama ni Kristo, basi Kristo atamwokoa, lakini kama ni shetani basi shetani atampeleka alipo yeye..

Ndugu, siku hizi ambazo waweza kusikia injili, na ukashawishika moyoni, ndizo siku zako za ujana, embu sasa anza kujiweka chini ya Kristo, akuongoze, achana na ulimwengu na mambo yake, wanadamu hawawezi kukufaidia chochote kwa siku zijazo.

Anza kuisafisha njia yako sasa, kama vile biblia inavyotushauri katika..

Zaburi 119:9 “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako”.

Kumbuka, ni kipindi kifupi sana tumebakiwa nacho hadi kurudi kwa Bwana Yesu mara ya pili, Kama unadhani, Unyakuo bado sana, fikiria mara mbili, dalili zote zimeshatimia, injili inayoendelea sasa sio ya kubembelezewa wokovu, bali ni ya kujiingiza katika ufalme kwa nguvu. Huna sababu ya kuendelea kufichwa uhalisia, dakika hizi ni za majeruhi, siku yoyote, parapanda  inalia, PARAPANDA INALIA!!

Bwana atusaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

PETRO AKAMWAMBIA YESU “BWANA NA HUYU JE”?

NI YESU YUPI UMEMPOKEA?, NI ROHO IPI UMEIPOKEA? NA INJILI IPI UMEIPOKEA?

Je! Ni kanisa lipi sahihi kumuabudia Mungu?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita.

Ni sahihi kusema sikuitiwa kuhubiri ubatizo kama Paulo alivyosema (1Wakorintho 1:17)?.

LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE.

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Rudi nyumbani

Print this post

LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE.

Ulishawahi kukutana na kundi la watu ambao linakutafuta tu wakati wa shida, kama ndio, kuna hali Fulani unajisikia ambayo sio nzuri, ni kweli wapo ambao mazingira yanawabana washindwe kukutafuta nyakati nyingine, lakini wapo ambao wewe kwao ni mtu wa kuwatatulia tu matatizo, Habari nyingine na wewe hawana..

Kuna mtu mmoja alikuwa ananifuata nimtatulie tu matatizo yake, lakini baada ya hapo ukimpigia hata simu umsalimie, hapokei, na anabadilisha line ya simu moja kwa moja ili usimpate, baadaye anakuja kukutafuta tena, na jambo linalofuata hapo ni kuomba msaaada..

Unajua hata kama utamsaidia, lakini utasema kwanini iwe hivi, kwanini tusiwe na mahusiano hata na nyakati nyingine zote..

Sasa hiyo hali ndiyo ambayo Mungu anapitia sasahivi kwa wanadamu wengi duniani, biblia inasema..

Yeremia 2:27 “waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE”.

Umeona, wanadamu wengi sasa kinachowapeleka kwa Mungu, si kingine Zaidi ya kuomba, wafunguliwe, kuomba waponywe, kuomba wafanikishwe kiuchumi, kuomba kazi, n.k.

Lakini ukiangalia mahusiano waliyonayo na Mungu ni hafifu sana au hakuna kabisa.. Hana muda wa kusoma biblia kuyajua mapenzi ya Mungu ni nini katika Maisha yake, kumaliza hata dakika 20 kila siku katika kutafakari Neno la Mungu hawezi, kuomba kunamshinda, kwenda ibadani ni mara moja kwa mwezi, ikizidi sana mara mbili, na hata akienda ni ili Mungu amjibu lile ombi lake alilomuomba lakini sio kumwabudu katika Roho na Kweli.

Anachokiona  kirahisi kwake, ni kwenda kununua maji ya upako na mafuta, ili amwage kwenye biashara zake, ili mambo yake yaende sawa.. Au pale anapopitia hali mbaya sana ya magonjwa ndipo anapomfuata Mungu ili amsaidie,. Hapo ndipo atafunga na kuomba, na kusoma Neno kila siku kwa bidii..Lakini siku nyingine zote anaishi maisha ya dhambi.

Ndugu, tujue kabisa Mungu hapendezwe na huo mfumo wetu wa Maisha, Mungu ametuzira watu wengi sana na sisi hatujui, ndio maana inakuwa ngumu sana kusaidiwa na Mungu kwasababu, Maisha yetu ni ya kinafki mbele zake.

Lakini ukiendelea kusoma pale Bwana anasema..

Yeremia 2:27 “waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe.

28 LAKINI WAKO WAPI MIUNGU YAKO ULIOIFANYA? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawasawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda.

29 MBONA MNATAKA KUTETA NAMI? Ninyi nyote mmeniasi, asema Bwana”.

Umeona tusimgeuze Mungu kama ni sehemu ya kutatulia matatizo yetu tu, ili hali Maisha yetu hayaendani na wokovu. Tusitete na Mungu, Mambo hayo kayafanye kwa waganga wa kienyeji lakini usifanye kwa Mungu, kwasababu utajikuta unaangukia tu laana badala ya baraka.

Hivyo tuanze sasa, kumtafuta Mungu nyakati zote, tuhakikishe tunayatenda mapenzi yake, tuonyeshe bidii zetu kwake, kwamba tunampenda sio kiunafiki, bali kwa mioyo yetu kweli. Tunamtafuta sio atufanye kuwa mabilionea, bali atufanye kuwa wana wake kama Yesu Kristo. Na ndio sasa hata hayo mengine atasaidia bila hata kutumia nguvu wala kumwomba..

Kumbuka katika nyakati hizi za mwisho, watakaokwenda kwenye UNYAKUO, sio kila mtu asemaye ninamwamini Mungu tu, halafu basi,..Bali ni watu wayatendao mapenzi ya Mungu kikamilifu sawasawa na Neno la Kristo.

Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”

Bwana atupe jicho la kuona, na kuyatendea kazi.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

USIJARIBU KUMGEUZA MUNGU MGANGA WA KIENYEJI,UTAKUFA.

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?

Talanta ni nini katika biblia (Mathayo 25:14-30)

WAKATI ULIOKUBALIKA NALIKUSIKIA

JINSI UNAJISI UNAVYOMGHARIMU MTU.

Rudi nyumbani

Print this post

Maana vitu vyote ni watumishi wako(Zaburi 119:91)

SWALI: Biblia inamaana gani kusema “ maana vitu vyote ni watumishi wako”?. Je wanaotumia vifaa vya upako kama vile chumvi, maji, udongo, kuombea watu, wanatimiza kusudi lile lile la Mungu kwasababu na vyenyewe vinafanya kazi ya Mungu kwa nafasi hiyo? Je kwa mujibu wa andiko hilo ni sawa?

Zaburi 119:90 “Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa.

91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, MAANA VITU VYOTE NI WATUMISHI WAKO”.


JIBU: Ni kweli kama andiko hilo linavyosema, vitu vyote tunavyoviona katika mbingu na  katika nchi ni watumishi wa Mungu, yaani, jua, mwezi, nyota, mawingu, milima, moto, maji, upepo, mafuta, udongo, mende, mbu, nzi, konokono, kipepeo vyote vinamtumikia Mungu.

Lakini swali ambalo tunapaswa tujiulize je vinamtumkia Mungu katika utumishi gani?

Ulishawahi kwenda kumuomba mjusi akusaidie kuomba rehema mbele za Mungu? Ulishawahi kuliomba jua likupe rizki, ulishawahi kuamka asubuhi na kuuambia mwezi ukuponye magonjwa yako, na ukuepushe na ajali?

Kwanini usifanye hivyo, ilihali vyote vinamtumikia Mungu?.. Lazima ufahamu utumishi wao ni upi mbele za Mungu, kwamfano, biblia inasema..

Zaburi 19:1 “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake”.

Ikiwa na maana kuwa tutazamapo mbingu na anga, basi tunahubiriwa utukufu wa Mungu kwa kupitia hivyo,  hapo tayari vimeshamtumikia Mungu, lakini hatuwezi kwenda kutumia mawingu ili Bwana atujibu maombi yetu.

Mungu kaweka njia kwa kila jambo, Na njia pekee ambayo alituchagulia sisi ili tumfikie Mungu, na kupokea wokovu wetu, na baraka zetu ni kwa kupitia YESU KRISTO tu na JINA LAKE Hapo ndipo tunapoweza kusaidiwa  mahitaji yetu, na dua zetu. Kwasababu hatuna jina lingine au kitu kingine chochote kiwezacho kutuokoa sisi isipokuwa Jina lake tu. . (Matendo 4:12)

Sasa wapo watu wanasema, mbona, Yesu alitumia udongo, mbona manabii walitumia chumvi,..Wanashindwa kuelewa yapo MAINGILIO YA MUNGU. Ambapo  Mungu mwenyewe upo wakati anashuka mahali Fulani kwa muda , kulitimiza kusudi lake Fulani, ndipo anapotumia chochote apendacho, kisha baada ya hapo hakuna kitu kingine cha ziada katika hicho kitu.

Ndio maana utaona wakati  ule alipomtumia punda kuzungumza na Balaamu, hatuona tena, punda wakitumika kuzungumza na watu, kana kwamba ndio kanuni, halikadhalika, Elisha alipoambiwa alale juu ya yule kijana kisha atakuwa mzima, hatuona tena, tendo hilo likifanyika hadi leo hii, tukilala juu ya wagonjwa ili  wapate afya.

Ipo hatari kubwa sana ya kutumia vitu vya Mungu na kuvigeuza kuwa  ndio kanuni za uponyaji, kosa mojawapo lililowafanya wana wa Israeli Mungu achukizwe nao, hadi kupelekwa tena utumwani Babeli, lilikuwa ni kuitumia ile sanamu ya shaba, Musa aliyoagizwa na Mungu aitengeneze kule nyikani, watu waiangaliapo wapone.

Hivyo watu wasiomjua Mungu, na MAINGILIO YAKE YA MUDA, wakaigeuza kuwa ndio sehemu ya ibada, walipofika nchi ya ahadi wakaiundia madhabahu kisha wakaanza kumwomba Mungu kupitia ile, mwisho wa siku wakawa wanaabudu mapepo pasipo wao kujijua na matokeo yake wakapelekwa Babeli utumwani.

Hivyo nawe pia ukiona mahali popote uendapo, vitu kama hivyo vimefanywa kama kanuni, kila wiki ni maji ya upako, mafuta, chumvi, au kingine chochote, ujue kuwa huna tofauti na wale waabudu sanamu, na jua na mwezi, na unayemwabudu hapo sio Mungu bali ni shetani mwenyewe. Na Unamkasirisha Bwana sana.

Jina ambalo tumepewa sisi, tulitegemee kwa kila kitu, na kila saa ni jina la YESU KRISTO TU.. Hilo ndio uligeuze kuwa sanamu yako, na si kitu kingine chochote. Kama ulikuwa unafanya hivyo basi acha mara moja.

Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”.

Hivyo, kwa hitimisho ni kuwa, mstari huo  haumaanishi  maji, au chumvi, au udongo, au kitu kingine chochote kinaweza kufanya shughuli ya upatanisho wa mwanadamu. Hapana ni uongo.  Vinamtumikia Mungu, lakini sio katika mambo ya wokovu wetu.

Bwana atuepushe na sanamu.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NEHUSHTANI (NYOKA WA SHABA).

USIJARIBU KUMGEUZA MUNGU MGANGA WA KIENYEJI,UTAKUFA.

KWA KUWA WASEMA MIMI NI TAJIRI.

Bwana alimaanisha nini kusema“maana mtenda kazi astahili posho lake”

Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani,

Nini maana ya “chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu”?

Unyenyekevu ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

HIZO NDIZO ROHO ZA MASHETANI.

Jina la mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe milele. Karibu tuyatafakari maandiko. Na leo tutaona ofisi kuu tatu za shetani, ambazo, zinafanya kazi humu duniani.

Biblia inasema..

Ufunuo 16:13 “Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.

14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi”.

Hapa, tunaona watatu wanatajwa, ambao ni;

  1. Joka
  2. Mnyama
  3. Nabii wa uongo

Haya ni mapepo makuu matatu ya juu sana na yanayofanya kazi kwa kushirikiana, na kichwa chao akiwa ni ibilisi mwenyewe. Muunganiko huu ndio unaoukamilisha utawala mchafu wa mashetani unaofanya kazi duniani.

Sasa Ofisi ambayo, inafanya kazi sasa kwa nguvu ni hiyo ya JOKA, lakini hizo nyingine mbili zilizosalia yaani ya Mnyama na Nabii wa Uongo, kwasasa zinafanya kazi katika siri, lakini zitakuja kufanya kazi vema, katika kipindi cha dhiki, baada ya unyakuo kupita. Kipindi hicho ndio zitawepa mamlaka kamili ya kujidhihirisha duniani.

Sasa tuone kazi za hizi roho tatu ni zipi;

  1. Tukianzana na huyo wa kwanza yaani Joka.

Kama tunavyofahamu kazi kuu ya JOKA ni kumeza: Biblia inapomtaja joka (shetani), inalenga moja kwa moja katika kummeza Kristo mahali popote anapozaliwa,

soma Ufunuo 12:3-5

“3 Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba.

4 Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.

5 Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi”.

Na ndio maana utaona pindi Kristo anazaliwa duniani, Joka hili lilisimama ndani ya Herode, kutaka kumuua, lakini lilishindwa..Hivyo mahali popote Kristo anapozaliwa, ni lazima joka ajitokeze kuleta vita, hata sasa mtu anapotaka kuokoka kwa kumaanisha kweli kumfuata Kristo, ajue kuwa ni lazima atakutana na vita vya hili joka, kwasababu sikuzote halitaki kumwona Kristo katika mioyo ya watu.

Na ndio mwishoni biblia inasema, likaenda kusimama katika mchanga wa bahari, yaani mahali ambapo, nchi kavu na Habari vinakutana, fukwe (beach), Yaani ikifunua kuwa lipo mpakani, kuwazuia watu wanataoka kutoka katika giza kuja katika nuru, hapo ndipo vita ilipo.. Kwa maelezo marefu juu ya hili fungua link hii usome >>>> NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

Ufunuo 12:17 “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari”.

Hivyo, fahamu kuwa ukitaka kuwa mtakatifu, basi ujue pia joka litasimama kukupinga vikali. Lakini halitaweza kukushinda, ikiwa umedhamiria kweli kumfuata Kristo. Lakini ukiwa nusu nusu, yaani unataka hutaki, litameza Kristo wako, na hutazalisha chochote katika wokovu wako.

          2.  Mnyama.

Biblia inapotaja mnyama, inazungumzia utawala ya ibilisi kupitia falme kubwa za dunia. Alishatumia falme za dunia kadha wa kadha huko nyuma, kama vile Babeli, Umedi, Uyunani na Rumi, kuangusha watakatifu wa Mungu. Na utaunyanyua tena ufalme mwingine ambao utakuwa na nguvu sana, ufalme huu kichwa chake kitakuwa ni RUMI,  na utafanya kazi kwa kipindi kifupi sana yaani miaka pungufu ya saba (7), lakini utaleta, mabadiliko makubwa sana duniani, kiasi kwamba kila mtu atalazimishwa aufuate huo utawala.

Usipoufuata, hutaweza kuuza wala kununua, wala kuajiriwa. Biblia inasema utawala huo wa kishetani ambao utakuwa na chapa ya 666 nyuma yake, utafurahiwa na watu wote watatakaokuwa wamesalia, ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima cha mwana-kondoo kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu. Lakini wale wote watakaoonyesha dalili ya kuukataa au kuupinga, mwisho wao utakuwa ni kifo cha mateso makali sana ya dhiki.

Ufunuo 13:8 “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia”.

Jambo ambalo wengi wetu hatulijui ni kuwa, utawala huu tayari ulishafanya kazi huko nyuma,ambao ni ni Rumi, na ulishawaua watakatifu wengi sana Zaidi ya milioni 80, Lakini sasa Mungu ameuzuia kwa muda, lakini ndio utakaokuja kuzuka tena na kuyaongoza mataifa yote, katika utawala mpya, moyo wa utawala huo ni Vatican, Rumi, utakuwa na nguvu nyingi Zaidi ya ule wa kwanza, kwasababu utakuwa na sapoti ya mataifa yote makubwa unayoyajua leo hii duniani.

Ufunuo 17:8 “Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako”.

   3.   Nabii wa Uongo.

Kama jina lake lilivyo, ni nabii, kazi yake ni kuwapotosha watu, kwa kuwapa maagizo ya uongo, wadhani kuwa wanapokea maagizo kutoka kwa Mungu kumbe ni kwa ibilisi. Biblia inasema hata sasa wapo manabii wa uongo, ambao wanaiga kazi ya mkuu wao, atakayekuja. Nabii huyu ndiye mpinga-kristo mwenyewe.

1Yohana 2:18 “Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho”.

Mpinga-Kristo huyu ambaye atakuja rasmi mara baada ya unyakuo wa kanisa kupita, atapewa uwezo wa kufanya ishara za uongo na shetani mwenyewe,atapewa uwezo wa kutenda miujiza feki kama ile ya Yane na Yambre kipindi cha Musa.

2Wathesalonike 2:6 “Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7 Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.

8 Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;

9 yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo”;

Na kazi yake kubwa itakuwa ni kuwashurutisha watu, waipokee ile chapa ya mnyama, na wengi watamuamini sana na kuipokea kwasababu ya zile ishara atakazokuwa anazifanya duniani.

Ufunuo 13:12 “Naye atumia uwezo wote wa mnyama yule wa kwanza mbele yake. Naye aifanya dunia na wote wakaao ndani yake wamsujudie mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona.

13 Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu.

14 Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi.

15 Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe.

16 Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao;

17 tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake.

18 Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.

Na mwisho kabisa, roho hizi zote tatu, yaani ya joka, mnyama na nabii wa uongo, zitaungana, na kuwaendelea wafalme wote wa duniani, ikiwemo wa hilo taifa lako unaloishi,  ili wapatane kwa kitu kimoja, kupigana na Mungu mwenyezi, pale Israeli, katika vita ile ya Harmagedoni, kipindi hicho ndicho Kristo atahitimisha vyote kwa kuwaua wanadamu wengi sana, na kuanzisha utawala wake mpya wa amani wa miaka elfu moja hapa duniani, naye atatawala kama MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA. Haleluya.

Hivyo ndugu, fahamu kuwa hizi ni nyakati za mwisho, kipindi kifupi sana tumebakiwa nacho,  Unyakuo ni siku yoyote, dalili zote zimeshatimia, mfumo wa yule mnyama upo tayari, unatendakazi tu kwa siri kwa dini ya uongo ya rumi, ni wakati wowote kunyanyuka, Tubu dhambi zako mgeukie Bwana Yesu kwa kumaanisha. Kubali kujitwika msalaba wako umfuate, kwasababu parapanda italia siku yoyote.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

UFUNUO: Mlango wa 12

UFUNUO: Mlango wa 13

UFUNUO: Mlango wa 17

USIPOTEZWE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

DANIELI: Mlango wa 1

NA JINA LAKE AITWA, NENO LA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

Bwana alimaanisha nini kusema“maana mtenda kazi astahili posho lake”

Moja ya maagizo ambayo Bwana Yesu aliwapa wanafunzi wake alipowatuma kwenda kuhubiri injili mbali, lilikuwa ni kutokulipisha fedha katika huduma yoyote watakayoitoa, halikadhalika   kutokubeba chochote katika safari yao. Yaani wasiwe na maandalizi yoyote ya njiani, Lakini mwishoni kabisa mwa maagizo yake aliyasema maneno haya “maana mtenda kazi astahili posho lake”.. Sasa swali linakuja Je hili posho ni lipi alilostahili huyu mtandakazi ili hali ameitwa atoe bure?

Mathayo 10:8 “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu;

10 wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake”.

JIBU: Posho alilostahili ni lile ambalo Bwana Yesu mwenyewe atampa katika kazi ya injili anayoipeleka, kwa kupitia watu wakarimu ambao Bwana Yesu mwenyewe atawagusa moyo huko waendako aidha kwa kuwapa maji, au chakula, au nguo, na wakati mwingine hata fedha.

Hiyo yote ni kuonyesha kuwa Bwana Yesu anaweza kumtunza mtumwa wake, katika mazingira yoyote atakayomtuma. Na ndio maana mwishoni kabisa akawaambia maneno haya;

Luka 22:35 “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!

Ni ni kufunua kuwa hatupaswi kuwa na wasiwasi wa maandilizi yoyote ya huduma ya Kristo, pale ambapo hatuna chochote,  Bwana anataka tuwe wepesi (SIMPLE), tusijali sana tutakula nini, tutavaa nini huko tuendako, kesho tutatolea wapi nauli ya kurudi, hilo jambo Bwana hataki sisi kama watumwa wake tulifikirie, kwasababu ameahidi kabisa ikiwa tunatenda kazi yake kiuaminifu, basi tumestahili posho lake, hivyo anza kutumika.

Lakini haimaanishi kuwa, wakati wote, hata kama unacho, ndio ujifanye hauna, hapana, bali, upo wakati wewe kama mtumishi wa Mungu utabarikiwa na utakuwa na vya kuendea huko katika ziara, hivyo vitumie hivyo, Na ndio maana wakati mwingine Bwana aliwaambia wajibebe fimbo ya njiani, na kujifungia viatu, wakati sehemu nyingine kama tuliyosoma hapo juu aliwakataza.(Marko 6:8-9)

Kwahiyo, kwa vyovyote vile, Bwana atatunza, ilimradi tunamtumkia yeye kwa uaminifu. Tusiwe na wasiwasi na huduma yake.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

ANGALIENI MWITO WENU.

WITO WA MUNGU HAUVUKI NENO LAKE.

MAAGIZO AMBAYO HAYAJAAGIZWA!

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA TITO.

BWANA AWEZA KUKUPA ZAIDI SANA KULIKO HIZO.

HERI WAPATANISHI, MAANA HAO WATAITWA WANA WA MUNGU

Rudi nyumbani

Print this post

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Yapo maombi ya namna tofauti tofauti, lakini yote  ni lazima yaangukie katika mojawapo ya makundi haya Matano (5).

1)   Kusifu na Kuabudu.

Wengi hawafahamu kama sifa zetu ni maombi yanayojitegemea kwa Mungu, haya ni maombi yanayomwasilia Mungu katika mfumo wa nyimbo, halikadhalika pia kwa kumwadhimisha kwa matendo yake makuu aliyoyafanya kwa kuzungumza kwa vinywa vyetu.. ndio maombi ya kwanza yenye nguvu. Tunapomsifu Mungu katika Roho na kweli, ni Zaidi ya maombi mengine yote tunayoweza kuyapeleka kwake.,

Biblia inasema Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu;(1Nyakati 16:29), Na pia Mataifa yote yamsifu yeye. Mambo mengi, na vifungo vingi huwa vinafunguka, pale tu tunapomsifu Mungu kwa kumaanisha katika Roho na kweli, Kwasababu ni maombi yanayouvuta uwepo wa Mungu kwa haraka sana juu ya mtu, Na ndio maana ibada zote lazima zitanguliwe na maombi haya.

2) Maombi ya Upatanisho.

Ni maombi ya kuwaombea wengine, Zaidi ya kwako mwenyewe. Kuwaombea watakatifu,  kuwaombea, wanyonge, kuliombea taifa, viongozi, hata maadui zako n.k. Haya ni maombi ambayo yanampendeza Mungu sana. Danieli alifunga na kuomba kwa ajili ya taifa lake Israeli, na dhambi zao, Na Mungu akamsikia akamrehemu (Danieli 9:1-27).

 Bwana Yesu alipokuwa duniani, sehemu kubwa ya maombi yake ilikuwa ni kutuombea sisi (Yohana 17) hivyo akasema pia, tuombeane sisi kwa sisi ili tupate kuponywa (Yakobo 5:16). Ikiwa na maana wengi hawawezi kuokoka/kufunguliwa wenyewe, ikiwa sisi hatutawaombea, Na pale maombi haya yanapokuwa ya muda mrefu (ya dua), basi huwa yana nguvu Zaidi, kupelekea kutupa kibali cha kupendwa na Mungu, kama ilikuwa kwa Danieli.

3) Maombi ya Mahitaji.

Ni maombi ya kupeleka haja zetu kwa Mungu, ikiwemo, kumwomba Roho wake, rizki, amani, furaha,  uponyaji, kibali, fursa, gari n.k. Bwana Yesu alisema pia, tuombapo tuombe Bwana atupe rizki zetu,(Mathayo 6:11). Na pia alisema tuombe nasi tutapewa. Haya ndio maombi yanayojulikana na kuombwa na watu wengi sana.

Luka 11:11 “Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?

12 Au akimwomba yai, atampa nge?

13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”

4) Maombi ya Shukrani.

Ni maombi muhimu kwa kila mwanadamu, ni maombi ya wakati wote, ya asubuhi, ya mchana, na jioni, tunamshukuru Mungu, kwa uhai, afya, chakula, makazi, Malazi, familia,

Wakolosai 3:15 inasema “….tena iweni watu wa shukrani.”. Ulishawahi kushukuriwa kwa wema Fulani uliomtendea mtu, ukaona hali unayojisikia ndani ya moyo wako kwa shukrani ile..Ndivyo ilivyo kwa Mungu anapoona Sio kila majira tunaenda kumpelekea tu mahitaji yetu..Bali wakati mwingine tunamkaribia kumshukuru kwa vile anavyotufanyia. Inampendeza sana moyo. Na wakati mwingine kupelekea hata kupewa vile vilivyosalia, kwasababu tunaonyesha kuthamini neema yake.

5) Maombi ya Vita.

Ni maombi ya kushindana, na nguvu za giza, kwa mamlaka ya rohoni tuliyopewa katika damu ya Yesu, Hapa tunatangaza ushindi, na pia kutamka kwa Imani katika Neno la Mungu. Yapo mambo mengine ibilisi hawezi kuyaachia kirahisi rahisi. Hivyo inahitaji kukemea, kuamuru, kuvunja, na kubomoa, kwa Imani.

Ufunuo 12:10 “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.

11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa”.

Hivyo kama watakatifu tukijifunza kutumia aina hizi tano za maombi, bila kupuuzia hata moja, basi, tutakuwa ni askari wazuri sana katika roho.

Shalom

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.

Nifanyeje niwe mwombaji mzuri, wa masafa marefu?

YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.

WALA TUSIACHE KUKUSANYIKA PAMOJA

LAKINI SISI HATUKUIPOKEA ROHO YA DUNIA.

Matulizo ya mapenzi ni nini? (Wafilipi 2:1)

Rudi nyumbani

Print this post