WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.

WANA WA MUNGU, NA BINTI ZA WANADAMU.

Wana wa mungu, na binti za wanadamu,ni wakina nani leo hii?


Biblia inaposema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu, Ndivyo itakavyokuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu (Luka 17:26)..Yapo mambo mengi sana tunapaswa tuyachunguze yaliyokuwa yanatokea katika siku za Nuhu, Na leo tutaangazia jambo moja ambalo ndilo lililopelekea wakati ule dunia yote kuangamizwa.

Na jambo lenyewe si lingine zaidi ya kuchanganyikana kwa mbegu kati ya wana wa Mungu na binti za wanadamu. Leo hii nataka ufahamu kuwa wana wa Mungu wanaozungumziwa pale sio malaika, kama wengi wetu tulivyofundishwa, biblia inasema malaika hawaoi wala hawaolewi (Mathayo 22:3), na sisi watakatifu tukishakwenda mbinguni tutafanana na wao..Pamoja na hayo malaika hawajapewa miili ya kiduniani, bali wao ni roho watumikao biblia inasema hivyo (Waebrania 1:14)

Hivyo kusema wale wanaozungumziwa katika Mwanzo..Ni malaika wa Mungu walizini na wanadamu, hilo linakinzana na maandiko. Bali wale wanaotajwa pale kama wana wa Mungu ni wanadamu watakatifu wa Mungu, na binti za wanadamu ni binti za wana wa ulimwengu huu. Ndio maana unaona baada ya tukio lile walioadhibiwa kwa gharika ni wanadamu na si malaika ikimaanisha kuwa ni dhambi walizokuwa wanazitenda wanadamu na si malaika.

Lakini kwanini kulitokea makundi hayo mawili wakati huo?

Biblia inatuonyesha tokea mwanzo, kulikuwa na tofauti kati ya zao mbili kuu..Yaani uzao wa Kaini, na ule uzao wa Sethi.. Ule uzao wa Kaini ulikuwa na tabia zake tofauti kabisa ambazo tabia ya kwanza ulikuwa haumchi Mungu wala hauna habari na Mungu kama Baba yako Kaini alivyokuwa, pili ulikuwa ni mzao wa uuaji, utaona mtoto wa Kaini anashuhudia kuwa alikuwa muuaji hata zaidi ya baba yake (Mwanzo 4:23), tatu ulikuwa ni uzao wa kuoa tu nje ya utaratibu wa Mungu, kuoa wake wengi (Mwanzo 4:19), nne ulikuwa ni uzao wenye ujuzi na maarifa mengi sana ya kidunia..Utaona mwanzoni tu walishagundua vyuma, chuma, vyombo vya miziki na kuvitumia isivyopasa (Mwanzo 4:20-22)..n.k.

Lakini uzao wa Sethi, ulikuwa ni uzao mtulivu, walikuwa ni wafugaji tu, na baada ya kuona dunia imeharibika sana na kajitenga mbali na Mungu wao walienda kinyume na kuanza kuliitia jina la Bwana..yaani ikiwa na maana walikuwa ni watu wanaomtafuta Mungu sana, watu wa ibada, watu waliojitenga na mambo maovu n.k.

Mwanzo 4:25 “Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.

26 Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana”.

Hivyo dunia ilikuwa inajulikana wazi, kuwa kuna uzao wa Sethi, uliokuwa unajulikana ni uzao wa watu wanaojishughulisha na kumtafuta Mungu kwa bidi na wenye msimamo (kwasasa tunaweza kusema ni walokole), na uzao wa Kaini ambao kwasasa tuseme watu wa ulimwengu huu wasioamini hata kama kuna Mungu, wenye elimu na sayansi na teknolojia ya hali ya juu na kwa ujuzi wao huo wote hawamtaki Mungu.

Sasa ilikuwa ni rahisi Mungu kuivumilia dunia maadamu anaona bado uzao wake unamtafuta yeye na kujitenga na uovu duniani , na unajishughulisha na mambo ya imani, (Kama alivyomwambia Ibrahimu wakati Fulani kwamba endapo wakipatika wenye haki 10 hatateketeza mji, Mwanzo 18:32)

Lakini ilifikia wakati huu uzao wa Mungu, ambao ndio wale wanaoitwa wana wa Mungu, wakakengeuka wakajisahau wakashindwa kuvumilia walipoona dunia inavutia, watu waovu wanasitawi ulimwenguni, wakaanza kuwaona hao binti wa wana wa kibinadamu jinsi wanavyoishi kidunia…Jinsi wanavyovaa kizinzi, wakikatiza mitaa yao wakiwa na vimini, na vi-top, migongo wazi, wakiwa wamevaa suruali za kubana, wakiwa wamejipamba kwa ma-makeup za kisasa, na wanja, na mahereni ya dhahabu na chuka za bandia, na mawigi wasio na aibu wala haya, wakiwa wamejichubua na kubadili maumbo yao na mienendo yao kwa ujuzi wote…wakitembea bichi wakiwa na bikini tu.

Wakaingiwa na tamaa, hapo ndipo na wao wakaenda kuwaoa watu ambao Mungu alishawalaani..Na unajua kwasababu gani Mungu aliwakataza hata wana wa Israeli wasioe binti za mataifa mengine? Ni kwasababu hii hii aliyoiona kwa wakati wa Nuhu, ambayo ni kugeuzwa mioyo. Sulemani hakulisikia hilo pamoja na kuwa alikuwa ni mtu mwenye hekima na aliyependwa na Mungu sana, lakini wanawake hawa walimgeuza moyo mpaka akaenda kufanya ibada za miungu..Na kufarakana na Mungu.

Nehemia 13:25 ‘Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang’oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.

26 Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye’.

Vivyo hivyo, na hawa wana wa Mungu (Uzao wa Sethi) walipooana na binti za wanadamu (uzao wa Kaini) kuwa ni warembo na wazuri….wakabadilika tabia moja kwa moja, na wao pia wakamsahau Mungu, hivyo dunia nzima ikafanana na kuwaa kitu kimoja..Wote ni waovu. Mungu akiangalia haoni wa kumuhurumia, Na hapo ndipo Mungu alipofikia hatua ya kughahiri na kuiteketeza dunia nzima kwa maji.

Mwanzo 6:1 “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,

2 wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.

3 Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.

4 Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile;tena ,baada ya hayo ,wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu,wakazaa nao wana;hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani ,watu wenye sifa.

5 Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.

6 Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.

7 Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya.

8 Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana”.

Unaona mambo yale yale yanajirudia leo hii duniani, wewe kama mwanamke, mwonekano wako unakutambulisha wewe ni binti wa nani? Kwamba wewe ni binti wa Kaini..Na wewe ndio unaowakoseshwa wana wa Mungu wengi kuwapeleka kuzimu..Unategemea vipi adhabu yako siku ile isiwe kubwa zaidi ya wote?. Kuambiwa hivyo sio kuhukumiwa kasome Mathayo 18:6 na Marko 9:42..Hujali leo nani anakutamani nani hakutamani… siku ile utalia na kuomboleza na hakutakuwa na nafasi ya kurekebisha makosa.

Vilevile wewe unayejiita mwana wa Mungu, unajichanganya na mambo ya ulimwengu huu, kuzini kwako ni jambo la kawaida, disko unakwenda, kwenye starehe upo hujui kuwa unajichanga mbegu yako na mbegu za kaini, nawe pia utaangamizwa pamoja na wao, ukifa leo hii..

Ezra 9:2 “Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao, na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na mashehe umetangulia katika kosa hili”.

Kumbuka hili neno “kama zilivyokuwa katika siku za Nuhu”. Hizi ndio siku hizo…Urembo na udunia uliopo leo hii ndio uliokuwa katika siku za Nuhu, upo viwango vya juu, huwezi katika kona mbili tatu ukakosa kuona duka au kituo cha kuuza urembo wa wanawake…mambo haya hayakuwepo wakati wowote kipindi cha nyuma. Fashion, ni moja ya silaha kuu ya ibilisi katika wakati huu.

Ni dua yangu kuwa utabadilika na kumpa Kristo maisha yako, uanze upya, ili ndani ya muda huu mfupi tuliobakiwa nao Bwana ayatengeneze maisha yako na kukufanya kuwa mwana au binti wa Mungu kweli kweli, kama alivyosema katika Neno lake..

Yohana 1:12 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”

Hivyo uwezo huo wa kubadilishwa na kuwa mtoto wa Mungu kutoka kuwa mtoto wa KAINI ule uzao wa nyoka, hauji hivi hivi kwa nguvu zako, bali kwa kuzaliwa mara ya pili..Na kuzaliwa mara ya pili ni pamoja na kutubu na kukubali kubatizwa sawasawa na (Yohana 3:5). Hivyo Kama upo tayari leo hii kusema Bwana Yesu nataka uyageuze maisha yangu nikuishie wewe milele..

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE,SITAKI KUFANYA DHAMBI TENA. NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo, Hapo ndipo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu…usiende mahali panapoabudiwa sanamu..Neno Mahali Mungu anapoabudiwa katika Roho na kweli.. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA.

UZAO WA NYOKA.

WANA WA MAJOKA.

JE! UMECHAGULIWA TANGU ASILI?

NGUVU YA UPOTEVU.

DALILI NYINGINE INAYOUTAMBULISHA UZAO WA NYOKA

JE! Kaini alimpatia mke wake wapi?

UZAO WAKO UTAMILIKI MALANGO YA KUZIMU;

Uzao wa Mwanamke ni upi? Unaozungumziwa katika Mwanzo 3:15?

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
5 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
amanyisye
amanyisye
11 months ago

wanawaMungu niwatakatifu waliopo duniani?

Anonymous
Anonymous
1 year ago

Sasa unaposema watoto Mungu waliingiliana na wana duniani..,je hao wana wa dunia hawakufa kipindi cha gharika..maana biblia inaonesha hakikubaki kitu chochote kilicho hai juu ya uso wa nchi…ispokuwa nuhu na watoto wake na baadhi ya wanyama na ndege wa angani..je hao wana wa dunia walitokea wapi

BARIKI LUKUMAY
BARIKI LUKUMAY
2 years ago

Kwakweli MUNGU awabariki Sana mzidi kueneza injili yake BWANA ,, binafsi nafurahia mno!!!!