DALILI NYINGINE INAYOUTAMBULISHA UZAO WA NYOKA

DALILI NYINGINE INAYOUTAMBULISHA UZAO WA NYOKA

Shalom mtu wa Mungu, karibu tena tuyatafakari maandiko, leo tutaona dalili nyingine kubwa inayoutambulisha UZAO WA NYOKA..kama biblia inavyosema ulimwenguni kuna watu ambao wanafanya dhambi kwa makusudi huku wakijua kabisa watu wanaofanya hivyo wanastahili hukumu ya mauti lakini wao wanaendelea kufanya hivyo kwasababu ile hali ya kujali au kuchukua tahadhari haipo ndani yao(ukisoma Warumi 1:32 utaona jambo hilo), hao watu sio wachache ni wengi sana..Embu tuitazame hii habari fupi itatukumbusha kitu  kingine cha msingi.

Mathayo 28:1 “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.

2 Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia.

3 Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji.

4 Na kwa kumwogopa, wale walinzi WAKATETEMEKA, WAKAWA KAMA WAFU.

5 Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa”………

11 Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka.

12 Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi,

13 wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. 14 Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi.

15 Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.”

Sasa kama tukiwatazama hawa askari ambao walikuwa wanalilinda kaburi la Bwana Yesu, pindi tu walipomwona Yule malaika kashuka pale, walitetemeka kwa hofu kubwa wakawa kama wafu, Na unajua mfu tabia yake ikoje?, Mfu huwa hawezi kufanya lolote anakuwa ameganda tu hapo chini, ndivyo ilivyowatokea hawa, ile hofu iliwafanya washindwe hata kukimbia au kufanya kitendo kingine chochote isipokuwa kungojea tu lolote litakalotokea, ni wazi maono yale ya wazi yaliwaingia sana moyoni, walitamani ingekuwa ni ndoto lakini haikuwa hivyo lilikuwa ni jambo la wazi kabisa mbele ya macho yao..

Waliona walichokiona, walisikia walichokisia, kulikuwa hakuna namna yoyote ungewashawishi kuwa Bwana Yesu hajafufuka kwa tukio lile, lakini kwa kuwa walipenda pesa kama Yuda, wakajiamulia tu kuudanganya uma kwamba hakuna kitu kama hicho, japo  ukweli wote ulikuwa ndani yao..Hiyo ni mbaya sana. Ndugu Uzao wa Nyoka sikuzote huwa na tabii hii, hata kama ukizungumza na Mungu uso kwa uso, hata kama ukaona uweza wake wote na ukuu wake wote ni rahisi kuchukuliwa na jambo dogo sana, na hata kukana alichokiona dakika chache tu hapo nyuma.

Walichokiona askari hawa hakina tofauti na alichokiona Sauli wakati anaelekea Dameski kuwaua watakatifu, tofauti yao ni kwamba Sauli alitubu na kugeuka kwa mono yale, kuonesha kuwa yeye ni uzao wa Mungu, lakini hawa wengine walikwenda kusambaza uzushi pamoja na kwamba wameona maono makubwa kama yale… kuonesha kuwa wao sio uzao wa Mungu, ni uzao mwingine wa nyoka.

Wapo watu wengi leo Mungu kajidhihirisha kwao kwa namna nyingi sana, wengine Mungu kasema nao kwenye ndoto wazi wazi, wengine wametokewa na malaika, wengine wameonyeshwa maono mengi,wengine wameuona mkono wa Mungu waziwazi katika mambo yao, wengine wameepushwa na hatari nyingi na kusema kabisa hakika huyu ni Mungu wala hakuna pingamizi, wengine hata walimwomba Mungu awafanikishe katika vitu vyao akawafanikisha sawasawa na walivyomwomba kwa wakati waliomwomba, wakatetemeka na kusema kweli Mungu yupo… wakaogopa kweli kweli wakalia, wakazimia, wakawa kama wafu wakasema Mungu wangu kuanzia leo nitakutumikia, wengine wakasema ukinipa nafasi ya pili basi mimi nitakutumikia milele, mimi sitatenda dhambi tena kuanzia leo, lakini cha kushangaza akitoka hapo siku chache baadaye, au miezi michache mbeleni, pengine kakutana tu na vitu vidogo vidogo visivyokuwa na maana vya ulimwengu huu vinavyopita, utamwona karudi nyuma kwa kasi kubwa kana kwamba  hajawahi kukutana na Mungu hapo nyuma hata siku moja…

Tena anaweza akawa ndio wa kwanza kuzungumza maneno ya mzaha kuhusu kazi ya Mungu au watumishi wake, lakini ndani ya moyo wake anajua kabisa Mungu alishawahi kumtembelea na kumwambia atubu. Watu kama hao wapo wengi sana inawezekana mmojawapo ni wewe unayesoma habari hii… Fanya utafiti uangalie utaona wale ambao hawajawahi kuuona uweza wa Mungu mwingi wale ambao Mungu anajihirisha kwao mara chache sana hao ndio wanaodumu na wanaomtumikia Mungu kwa moyo thabiti kuliko hawa wengine….na ndio maana Bwana Yesu alimwambia Tomaso heri wale ambao wameamini bila kuona..kwasababu alijua ugumu wa hawa wengine..

Ndugu unaendelea bado kumtumikia shetani na umesahau Mungu aliyokutendea hapo nyuma..Usidhani yataendelea kujirudia rudia hivyo kila siku, wakati utafika Roho wa Mungu ataondoka moja kwa moja ndani yako, utakachokuwa unangojea ni adhabu kubwa kuliko hata ile ya watu wa Sodoma na Gomora, Bwana Yesu ndio alisema  hivyo kama wale wangeona Ishara na maajabu Mungu anayowatendea watu leo hii, miji ile ingekuwepo hadi leo, hivyo basi akasema itakuwa rahisi kwa watu wale kustahimili adhabu kuliko sisi tuliyoyaona na kuyakataa.

Ndugu salimisha maisha yako kwa Bwana kithabiti..Anapokuita sio kana kwamba anataka kukunyima haki yako ya kuchagua unayoyataka hapana, lakini anakupenda UPEO hataki upotee hata unywele wako, hataki uende kuzimu hilo tu!…Tubu sasa ukabatizwe katika ubatizo sahihi, uanze kuuishia wokovu katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho duniani. Usikubali uwe sehemu ya UZAO wa nyoka ambao hata uhubiriweje injili na kuona maajabu yote hauwezi kugeuka..Naamini wewe sio mmojawapo na kwamba utapoisikia leo hii utageuka na kumwishia Kristo.

Ubarikiwe sana. Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki.


Mada zinazoendana:

UZAO WA NYOKA.

WATU WASIOJIZUIA.

UZAO WAKO UTAMILIKI MALANGO YA KUZIMU

MTI WA UZIMA NA MTI WA MAARIFA.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments