WAISRAELI WENGI SANA WANARUDI KWAO SASA.

WAISRAELI WENGI SANA WANARUDI KWAO SASA.

Shalom, Mtu wa Mungu, karibu tulitafakari kwa pamoja Neno la Mungu, biblia inasema Neno la Mungu ni Taa iongozayo miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Zab.119:105), hivyo ni vyema tukalitafakari hilo kila kukicha ili njia yetu iwe safi na salama..(Zab.119:9 “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako”).

Kama tunavyojua wengi wetu kwamba tunaishi katika siku za mwisho, na sio siku za mwisho tu! Bali ukingoni mwa siku za mwisho…Kwasababu siku za mwisho zilianza tangu zamani, sasa tupo ukingoni mwa hizo siku..Na kama tunavyojua ishara kubwa ya kututambulisha kuwa tupo ukingoni ni KUNYANYUKA KWA TAIFA LA ISRAELI. Ukienda kila mahali utasikia Israeli, Israeli..dunia ina mataifa mengi lakini ki-nchi kidogo kama kile kinavumisha upepo wa dunia na kuwa mada ya kuzungumziwa katika siasa yote ya dunia? Kuna nini pale?…Ni wazi kuwa kuna jambo la kiroho linaendelea kwenye Taifa hilo…Ndugu yangu hebu kama hujafuatilia ni nini kinaendelea kwenye Taifa hilo hebu tenga angalau wiki moja usiingie hata kwenye mitandao kuchat, tenga muda ulifuatilie kwa makini, soma historia ya Taifa hilo kwenye Biblia na kwenye historia…Ndio utajua tunaishi kipindi gani.

Wengi wetu tumezaliwa kipindi ambacho tunaambiwa kuna Taifa la Israeli, lakini wengi wetu hatujui kuwa Waisraeli wenyewe halisi, hawakukaa kwenye taifa lao, na kuwa na Mfalme wao wenyewe kwa takribani miaka 2,500 mpaka ilipofikia juzi tu mwaka 1948 ndipo wakarudi kuwa Taifa huru na kuwa na Raisi wao wenyewe…Kabla ya hapo walikuwa wametawanyishwa kwenye mataifa yote.

Sasa kama tunavyojua Kuwa Hawa Waisraeli tunaowaona, hawakua hivi, kwenye karne kadhaa huko nyuma… walikuwa wametawanyishwa katika Mataifa yote duniani, maandiko yanasema hivyo….Sasa kwanini Mungu aliwatawanyisha kwenye mataifa yote?..Jibu ni ili sisi watu wa mataifa tupate Neema, kwani Baada ya wayahudi (yaani waisraeli) kumkataa Masia wao Yesu Kristo, Bwana aliwaambia maneno haya…

Luka 21:20 “Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia.

21 Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.

22 Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.

23 Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.

24 Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara NA KUCHUKULIWA KATIKA MATAIFA YOTE; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia”

Sasa Swali lingine linakuja…Wayahudi/Waisraeli kutawanywa kwenye mataifa yote ina uhusiano gani na sisi watu wa mataifa kupata Neema?…Yaani wengine waumie ili sisi tupate Neema?..Wengine wachukuliwe mateka ndipo sisi tupate Neema?..Kwani Mungu hawezi kuwaacha tu wawe salama, na kutupa Neema wote sisi na wao?.

Ni swali zuri lakini ni vizuri pia kujua kuwa ili kimoja kipate uzima ni lazima kingine kife! Kwamfano ili ule tunda na kupata virutubisho vilivyomo ndani yake ni lazima ulichume kutoka kwenye mti, ulitafune na kulisagasaga…hapo ni sawa na umeliua…ili ule nyama ikusaidie kwa protini ni lazima mnyama Fulani auawe, huwezi kula kitu kizima…kadhalika ili upate kitu Fulani ni lazima hicho kitu kiwe kimepunguka kutoka sehemu Fulani, hata fedha mtu anazozotafuta ni kwamba zimepunguka sehemu Fulani zikaenda kwa huyo mtu, ikiwa na maana kuwa endapo ukifanikiwa kuzikusanya zote basi kwingine kutakuwa kumepunguka pia pakubwa, kwahiyo hakuna kuongezekewa kama hakuna kupunguka sehemu Fulani nyingine…wala hakuna kupata heshima Fulani kama mwingine hajapata dharau, hata cheo, au nafasi,ni lazima mmoja aondoke mwingine aingie…. Mambo ndivyo yanavyokwenda hivyo…Kwahiyo ili sisi watu wa Mataifa tupate heshima mbele za Mungu ni lazima wawepo wengine walioharibu mahali Fulani.

Kwahiyo Waisraeli walipomkataa Yesu na injili yake, wakawa wamejiharibia wenyewe hivyo hiyo ikawa faida kwetu sisi watu wa mataifa ndio maana Mtume Paulo aliwaambia..

Matendo 13:44 “Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu.

45 Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana.

46 Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa.

47 Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.

48 Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

49 Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote”.

Kwa dhambi hiyo walioifanya Mungu hakuishia tu kuwapokonya injili bali pia aliwatawanya kwenye mataifa yote, na hiyo pia ikawa ni faida ya PILI kwetu.

Kumbuka popote wayahudi wanapopelekwa, mahali pale lazima pabarikiwe hata kama wamepelekwa kwa makosa yao…mfano utaona Yusufu alipoingia Misri pamoja na wana wa Israeli wote, Taifa la Misri lilibarikiwa sana…Farao hakufa na njaa, na zaidi ya yote Farao aliyekuwa mtu wa Mataifa alipata nafasi hata ya kuoneshwa maono na Mungu mwenyewe, jambo ambalo si la kawaida Mungu kuzungumza na watu wamataifa.

Kadhalika utaona wakati Wana wa Israeli tena wamepelekwa Babeli utumwani, Mungu aliibariki Babeli kwa ajili ya wana wa Israeli waliomo mule, Babeli ilizidi kustawi, na pia Mfalme Nebukadneza alipata hadi Neema ya kuoneshwa maono na Mungu ya wakati ujao, jambo ambalo sio la kawaida Mungu kuzungumza na watu wa Mataifa, hiyo ni kutokana na waisraeli waliokuwepo kwenye hiyo nchi, ijapokuwa walipelekwa kule kwa dhambi zao lakini bado kulikuwa na Baraka Fulani za kimwili na kiroho zilizokuwa zinaambatana nao.

Kadhalika kipindi cha Esta, Mfalme Ahasuero alifanikiwa katika enzi yake kwasababu ya Esta, Mordekai pamoja na Wayahudi waliokuwepo kwenye ufalme wake..

Na sehemu zote ndio hivyo hivyo, popote Wayahudi walipokwenda kulibarikiwa mwilini na rohoni.

Vivyo hivyo katika siku zile baada ya kumkataa Yesu Kristo, walipotawanyishwa tena kwenye mataifa yote ulimwenguni, popote walipokaribishwa sehemu zile zilibarikiwa kimwili na kiroho, Ukiangalia mataifa mengi ya Ulaya, mafanikio yao yametokana na Wayahudi waliokuwemo kule kipindi kile, kadhalika na Marekani, na nchi nyingine zote…baraka zao ni kwasababu ya waisraeli waliowakaribisha kipindi wanatawanywa.. na Mungu kayabariki mataifa yote kwasababu ya Israeli na Baraka kubwa aliyowabaikia ya rohoni, ni KUWAPA MATAIFA ZAWADI YA YESU KRISTO. Hiyo ndio zawadi kubwa Mungu anayoweza kumpa mwanadamu…Kwahiyo sisi kuzawadiwa Yesu Kristo yaani kuzawadiwa hii Neema ya kumkubali Yesu Kristo ni kutokana na Wayahudi kuwemo humu mataifani, tulimo sisi.

Lakini cha kuogopesha ni kwamba wayahudi sasa wameshaanza kurudi nchini kwao, kidogo kidogo wameshaanza kuhisi makosa yao waliyoyafanya miaka 2000 iliyopia, mioyo ya kutubu kidogo kidogo imeanza kurudi ndani mwao, mamia kila siku wanamiminika kurudi kwao, hiyo ni ishara ya nini?..Ni ishara kuwa Neema inaondoka huku…Zile Baraka zinaondoka huku, baraka za rohoni na za mwilini…Kumbuka Baada ya majeshi ya Israeli kutoka Misri nini kilitokea huko nyuma?, jibu ni mapigo! ..hakuna Neema tena! Hujasikia tena tangu hapo na kuendelea Mfalme yeyote wa Misri anaota zile ndoto za kiMungu tena! Wala hujasikia chochote cha maana kilichokuwa kinaendelea Misri…Hiyo yote ni kwasababu Uzao wa Mungu umerudi kwao, na Bwana amewarudia watu wake.

Kadhalika wana wa Israeli waliporudi nchini kwao, baada ya kuchukuliwa Babeli, hutaona Mungu akishughulika tena na Babeli, au Umedi au Uajemi…Habari zao ndio zilikuwa zimeishia pale, sasa Mungu anarudi kushughulika na watu wake Israeli.

Ndugu, Hii Neema ipo ukingoni, hivi karibuni! Wayahudi wanakwenda kutubu kabisa kabisa! Na Bwana atawasamehe, na atawamwagia kipawa chake cha Roho, na wakati huo huo Roho Mtakatifu atakuwa ameshaondoka huku kwetu mataifani, yaani unyakuo utakuwa umeshapita! Kitakachokuwa kumesalia ni dhiki kuu na siku ya Bwana inayotisha!, Bwana akirudi leo hatutasema hatukusikia wala hatukuona, vyombo vya habari vinatuhubiria injili kila mahali, mtu asipotaka kuyatilia maanani basi ni kwa uzembe wake mwenyewe, mwenye macho haambiwi tazama, mwenye masikio haambiwi sikia

Ikiwa hii neema ambayo inafifia unaichezea, moja ya hizi siku itazima kabisa..Jitathimini wewe mwenyewe umesimama upande upi.

Maran Atha!

Tafadhali share na kwa wengine, Mungu akubariki.


Mada Zinazoendana:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Kwanini leo ndani ya Taifa la Israel lina watu wengi tena wakubwa halafu hao ndiyo mashoga na kwanini Taifa linaunga mkono swala la ushoga kiasi kikubwa vile

M
M
2 years ago

Ubarikiwe