Category Archive INJILI

NI LAZIMA NIWE MBWEHA WA KRISTO!

Kama mwamini hizi si nyakati za kuishi kilegevu, unapoona, watu wanakufa katika dhambi na kwenda jehanamu bila kumjua Kristo, unajisikiaje, unapoona kazi za shetani zinasitawi, na kuwaharibu watu unawezaje kutujulia moyoni mwako?

Ni Funzo gani unalipata nyuma ya hasira ya Samsoni? Alipoona mke wake ameuzwa kwa wageni na baba-mkwe wake, je alitulia, na  kusema basi tu hii siyo bahati yangu? Kinyume chake Alinyanyuka kwa hasira akasema ninakwenda kulipiza kisasi, kwa hawa wafilisti.

Unajua alifanya nini?

Alikwenda kuwachukua mbweha mia tatu (300), Akawafunga wawili wawili mikia yao, kisha, akawafungia mienge ya moto, na kuwaachia waingie kwenye mashamba ya ngano ya wafilisti. Baada ya hapo ni jambo gani akawa analifanya? Ni kuwaangalia tu wale mbweha walivyokuwa wanayateketeza mashamba ya ngano hekari kwa mahekari. Jambo lililowafanya wafilisti waamke wote kwenye majumba yao wamtafute huyu Samsoni ni nani?

Waamuzi 15:3 “Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru.  4 Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili.  5 Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni”

Akimfunua nani?

Ni Yesu Kristo,

Bwana alipoona kazi za adui zinapaswa ziharibiwe pale Israeli. Alichofanya ni kuwachukua wanafunzi wake pia, akawatuma wawili-wawili akawaambia waende mahali alipotaka yeye kwenda, akawapa amri ya kutoa pepo, kupooza magonjwa na kuhubiri habari njema. Na unajua ni nini kilitokea baada ya pale, ndani ya kipindi kifupi, waliporudi?

Yesu alikuwa akiwaangalia “MBWEHA WAKE” katika roho wakiziharibu kazi za shetani, akasema, nalimwona shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme.. Ha! ha! ha! ha! Mbweha wamfanya kazi.

Luka 10:17  “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. 18  Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. 19  Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru”.

Na sisi (yaani mimi na wewe), tuliookoka, Ikiwa umeshajazwa “Roho Mtakatifu” wewe tayari ni mbweha, Sijui unasubiri nini kwenda kuziharibu kazi za shetani, kwa kumuhubiri Kristo, na wokovu wake? Unasubiri nini mpendwa?

Angalia Yesu alichokisema..

Luka 12:49  “Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi?

Moto umekwisha kuwekwa kwenye mkia wako, angalia usije ukazima kabla haujafanya kazi yake. Ndio huo moto wa Roho Mtakatifu unaochoma ndani yako, kukuagiza uhihubiri neema ya Kristo kwa ndugu zako na watu wengine ili waokoke.

Kwa pamoja tunaweza upindua ulimwengu. Tumuhubiri Kristo, hilo ndilo agizo kuu kwa wanadamu wote. Kila mmoja wetu ni mbweha wa Kristo. Simama sasa, pokea ujasiri, kamuhubiri Kristo, watu waokoke.

Bwana akubariki

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

KWANINI KILA MWAMINI ANAPASWA AWE MHUBIRI WA INJILI

JE! NYWELE ZAKO ZINAOTA AU ZIMESIMAMA?

KITENDAWILI CHA SAMSONI

HUDUMA YA MALAIKA WAWILI.

Rudi nyumbani

Print this post