Title February 2023

LIONDOE JIWE.

Ulishawahi kujiuliza ni kwanini siku ile Bwana Yesu alipofufuka kutoka katika wafu, hakupotea na kutokea nje ya kaburi kisha kuendelea na safari yake ya kuwatokea mitume, na watu wengine lakini kinyume chake ilimpasa kwanza jiwe la kaburini liondolewe, ndipo atoke?

Kimsingi Bwana Yesu alipofufuka alikuwa na uwezo huo wa kupotea na kutokea, utakumbuka alifanya hivyo kwa watu zaidi ya 500, Tukiachia mbali siku ile mitume walipokuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya wayahudi, Yesu aliwatokea na kuanza kuzungumza nao, wala hakuhitaji kuingia kwa kupitia mlangoni.

Lakini tukirudi kwenye kaburi, ilikuwa ni lazima apitie kwenye malango yake, na kama ni hivyo basi ni sharti pia jiwe liviringishwe ili atoke, na ndio maana malaika walitokea juu na kuifanya kazi hiyo (Mathayo 28:2).

Lakini sio wakati huo tu, utakumbuka pia kifo cha Lazaro, Bwana Yesu hakumfufua Lazaro hivi hivi tu, bali aliwaambia kwanza wale watu waliokuwa  pale waliondoe jiwe kwanza ndipo shughuli za kufufua ziendelee. Hii ni kanuni ya kiroho ya Mungu, hakifufuliwi chochote bila kwanza kuondoa jiwe.

Yohana 11:39  “Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne….

43  Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. 44  Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, Mfungueni, mkamwache aende zake.”

Na sisi pia, ili tumwone Yesu aliyefufuka na nguvu zake, ni lazima tuyaondoe mawe mioyoni mwetu. Tusitazamie Yesu atafanya lolote, au atatenda muujiza Fulani, hiyo haipo, atafufuka kweli lakini hatoweza kutoka mpaka tutakapoyaondoa mawe hayo makubwa mioyoni mwetu.

Mawe hayo ni yapi?

Ni ule ugumu wa mioyo yetu.

Kama tunavyofahamu sikuzote jiwe ni gumu, tofauti na nyama..si rahisi kuathiriwa na chochote, ukilipitisha kwenye moto litakuwa vilevile, ukilipitisha kwenye upepo haliwezi kukakamaa, ukilipitisha kwenye maji haliwezi kulowa, ukilipiga upanga, ndio kwanza upanga unaumia.

Wapo watu ambao wanasema wamemwamini Kristo, lakini hawapo tayari Kristo ayatengeneze maisha yao, bado mawe yamefunika mioyo yao, wanataka maisha yao ya sasa, na yale ya kale yasiwe na utofauti, lakini wakati huo huo wanasema wameokoka. Hawajui kuwa ukristo ni badiliko la maisha moja kwa moja.

Wakiambiwa, wasivae mavazi yampasayo mwanamume, wanaona ni unyanyasaji wa kijinsia, wakiambiwa, biblia inasema tusiipende dunia, kwasababu tukiipenda dunia, tunafanyika maadui wa Mungu( 1Yohana 2:15)…watakuambia hizo ni zama za kale, wakiambiwa kubeti ni dhambi, wanajifanya kama hawaoni, wao kila jambo linalogusa maisha yao ya dhambi, hupinga tu..

Hata waonyweje, hawataki kubadilika, Sasa, haya ndio mawe yanayomzonga Yesu asifufuke katika maisha ya watu wengi wanaosema wamempokea Yesu. Kamwe hawawezi kuona nguvu ya kufufuka kwa Yesu katika maisha yao, Watausikia tu upendo wa Yesu, lakini moyoni mwao kutakuwa kukame daima, wataisikia amani ya Kristo, lakini kiuhalisia wao hawajawahi kuionja mioyoni mwao. Yesu atabakia kuwa kama mtu Fulani mashuhuri aliyewahi kutokea zamani, kama tu wengine, lakini sio mwokozi, anayebadilisha maisha ya watu.

Ndugu yangu, jiachie kwa Bwana akuongoze kwa  jinsi apendavyo yeye na sio kama upendavyo wewe, ndivyo utakavyouona wema wake, na nguvu zake maisha mwako. Ondoa jiwe hilo, mbele yako, liviringishe mbali, moyo wako uwe wazi ili Yesu atoke afanye kazi yake, na Bwana atayamalizia yaliyosalia sawasawa na ahadi yake katika;

Ezekieli 36:26 “Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama”

Dunia ya sasa ni kujihadhari nayo sana, kwasababu, hata mpagani asiyemjua Mungu kabisa, ukimuuliza Je! Umempa Yesu maisha yako? Atasema ndio. Wokovu umepunguzwa na kufanywa kama staili tu, lakini sio geuko la maisha, Na ndicho shetani anachotaka kitokee kwako pia, ili kwamba usikae  uone nguvu za Yesu aliyefufuka katika maisha yako.

Hivyo ikiwa wewe ni mkristo vuguvugu, embu kuanzia sasa, amua kujitwika msalaba wako na kumfuata Yesu, usiogope kuonekana mshamba, usiogope kuonekana umerukwa na akili, hata Bwana mwenyewe, alionekana hivyo, sasa kwanini wewe uogope, usiogope kutengwa na ndugu kisa umeamua kubadili mfumo wa maisha.. Ondoa jiwe hilo linalouzinga moyo wako.

Bwana akutie nguvu.

Ikiwa hujaokoka na upo tayari kuanza maisha mapya ndani ya Kristo kwa kumaanisha kabisa, kuukataa ulimwengu na mambo yake yote, Basi, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithibitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuwa na uhalali kwa kuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako.

Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ikiwa utahitaji msaada wa hayo yote, basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

JIWE LILILO HAI.

Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika.

Biblia inapotumia neno “Bila kazi ya mikono”, ina maana gani?

CHAGUA NI JIWE LIPI LITAKALO KUFAA KWA UJENZI.

YESU MPONYAJI.

Ni kwa namna gani, upendo husitiri wingi wa dhambi? (1Petro 4:8).

URIMU NA THUMIMU NI NINI KATIKA BIBLIA?

Rudi nyumbani

Print this post

Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako.

SWALI: Mstari huu una maana gani?

Mithali 27:10 “Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako, Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali”


JIBU: Ni mstari unaolenga umuhimu wa marafiki wema katika maisha yetu. Hapo anaanza kwa kusema usimwache rafiki yako mwenyewe, lakini haishii tu kwa rafiki yako, anaendelea kusema pia hata rafiki wa baba yako. Kwasababu wanaweza wakawa msaada kwako wa karibu kuliko ndugu wakati mwingine.

Kauli hiyo haimaanishi kuwa ndugu hawana msaada, hapana, lakini kutegemea tu ndugu peke yake, na kuwapuuzia marafiki wema kwaweza kukukwamisha, kwamfano umezidiwa na ugonjwa chumbani kwako, na unahitaji huduma ya kwanza, hapo huwezi kumpigia simu ndugu yako aliye mkoa mwingine, au wilaya nyingine aje kukusaidia, ni wazi kuwa msaada wa kwanza utauhitaji kutoka kwa jirani yako.

Ndio maana ya huo mstari, usimwache rafiki yako mwenyewe, yaani usimpuuzie, wala usimpuuzie rafiki wa Baba yako hata kama sio rafiki yako. Marafiki wa ndugu zetu, mara nyingi hufanyika msaada mkubwa kwetu wakati mwingine, Hili ni jambo la kawaida katika jamii, mara nyingi tumeona marafiki wa wazazi, au wa ndugu zetu wakitumika kutusaidia kwa sehemu moja au nyingine.

Lakini tukiwa ndani ya Kristo, tunapata marafiki ambao ni zaidi hata ya ndugu, kwasababu wao, husukumwa na upendo wa Kristo ambao umezidi wote. Bwana ameahidi hivyo kwamba tukiacha vyote kwa ajili ya jina lake, basi hayo yote atatujalia (Marko 10:30).

Je! Umeokoka? Je! Unatambua kuwa hizi ni nyakati za mwisho, na Yesu yupo mlangoni kurudi? Maisha yako yapo kwa nani. Kama upo nje ya Kristo ni heri ukatubu sasa, kwasababu mlango wa neema unakaribia kufungwa, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kama hukubatizwa, ili upate ondoleo la dhambi na upokee kipawa cha Roho Mtakatifu, ikiwa utahitaji msaada huo basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi +255693036618 / +255789001312.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

USIWE ADUI WA BWANA

Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.

Usimwache mwanamke mchawi kuishi! Biblia ilimaanisha nini?

BASI, IWENI NA HURUMA, KAMA BABA YENU ALIVYO NA HURUMA

Je ni kweli Musa alikuwa mtu mpole kuliko wote duniani?

KWA HIYO NDUGU, VUMILIENI, HATA KUJA KWAKE BWANA.

NDUGU,TUOMBEENI.

Rudi nyumbani

Print this post

Je! Umeona asali? Kula kadiri ya kukutosha;

SWALI: Kwanini Biblia inakataza kula asali nyingi, nini maana ya mstari huu kiroho?

Mithali 25:16 “Je! Umeona asali? Kula kadiri ya kukutosha; Usije ukashiba na kuitapika”.

Pia sehemu nyingine inasema..

Mithali 25:27 Haifai kula asali nyingi mno; Vile vile mtu kutafuta utukufu wake mwenyewe si utukufu.


JIBU: Asali hufananishwa na Neno la Mungu,

Ezekieli 3:1 Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli.  2 Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo.  3 Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.

Soma pia Ufunuo 10:10. Utalithibitisha hilo.

Na kila mmoja wetu anashauriwa alisome Neno la Mungu (alile) sana kwasababu ndio uzima wetu (Mathayo 4:4).

Mithali 24:13 Mwanangu, ule asali, kwa maana ni njema, Na sega la asali lililo tamu ulionjapo

 Lakini katika maandiko hayo tunaona tena biblia inatuasa tusile nyingi mno kupita kiasi, ikaja kutuletea madhara..Sasa maana yake ni nini? Je! Tulipende Neno la Mungu kwa kiasi au la?

Jibu ni kwamba hapo haimaanishi tulisome/ tujifunze neno la Mungu kwa kiasi hapana.. Bali analenga katika Suala la NIA zetu.. Ni kawaida yetu sisi watoto wa Mungu, kuwa na NIA inayopitiliza hususani pale tunapolifahamu sana Neno la Mungu.

Kwamfano, tunaposoma juu ya neema ya Mungu iliyokuwa inatembea  juu ya Eliya, Kisha tunaposoma kitabu cha Malaki4:4-5, kwamba ahadi imetolewa kuwa Roho ya Elia itarudi tena katika siku za mwisho. Baadhi ya watu wanajiweka katika nafasi hizo, na wanaamini kuwa Mungu anakwenda kuwaandaa kwa roho hiyo ili waje kuionya dunia kwa mapigo na ishara kama za kwake.

Au Musa kafunga siku 40 bila kunywa wala kula, akaongeza na nyingine 40 na yeye bila uongozi wa Roho Mtakatifu anasema na mimi lazima nifunge hivyo.

Wapo wengine wanasema na mimi nisipotokewa na Yesu kama Paulo alivyotokewa kule Dameski, bado sitakwenda kuhubiri injili, hivyo wanasubiriwa kwa miaka watokewe wapewe maagizo, kwa kufunga na kuomba.  Sasa Hali kama hizi zina hatari kwasababu mwisho wa siku zinamfanya asiwe mtu wa matunda kwa kungojea jambo ambalo huwenda Mungu hajalikusudia katika maisha yao, kwasababu   amenia makuu kuliko kipimo kile alichopimiwa na Mungu.

Mtume Paulo aliyasisitiza sana makanisa juu ya jambo hilo akasema..

Warumi 12:16b  “.. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili

Na hapa pia anasema..

1Wakorintho 7:17  “Lakini kama Bwana alivyomgawia kila mtu, kama Mungu alivyomwita kila mtu, na aenende vivyo hivyo. Ndivyo ninavyoagiza katika makanisa yote. 18  Je! Mtu fulani ameitwa hali amekwisha kutahiriwa? Asijifanye kana kwamba hakutahiriwa. Mtu fulani ameitwa hali hajatahiriwa bado? Basi asitahiriwe. 19  Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu. 20  Kila mtu na akae katika hali ile ile ambayo alikuwa nayo alipoitwa. 21  Je! Uliitwa u mtumwa? Usione ni vibaya lakini kama ukiweza kuwa na uhuru, afadhali kuutumia. 22  Kwa maana yeye aliyeitwa katika Bwana hali ya utumwa, ni huru wa Bwana. Vivyo hivyo yeye naye aliyeitwa hali ya uhuru, ni mtumwa wa Kristo.

Ikiwa Bwana kakupa kipimo cha ushemasi, tembea katika hicho kwa uaminifu usilazimishe uwe nabii wa mataifa yote kama Yeremia. Bwana amekuokoa, tumika katika kipimo hicho hicho, ikiwa itampendeza kukunyanyua juu zaidi, basi atafanya kwa wakati wake, lakini kwasasa tujishughulishe na mambo manyonge,

Lakini si hayo tu, wakati mwingine katika kufahamu sana maandiko, hupelekea tabia za majivuno, kujiona unafahamu, kukataa kushauriwa kunazalika ndani ya mtu. Hivyo hupelekea kujifungia mwenyewe milango ya Mungu kuendelea kusema naye. Hivyo ili kuepuka kuitapika asali iliyo nzuri na njema, ni vizuri haya yote tukajiepusha nayo, tunapojifunza kwa bidii Neno la Mungu kila siku.

Tule asali kwa kadiri ya kututosha tusije tukashiba tukaitapika, kwa kukosa shabaha ya maandiko.

Maran Atha.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NJAA IPO?, USIACHE KULA ASALI.

Kwanini iwe ni nchi ibubujikayo maziwa na asali?

Je! Ni sawa kuingia katika shamba la mtu mwingine na kula jinsi utakavyo?

Kula uzao wa tumbo lako maana yake nini? (Kumbukumbu 28:53)

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

Aibusu midomo atoaye jawabu la haki (Mithali 24:26)

Rudi nyumbani

Print this post

MAJARIBU 10 WANA WA ISRAELI WALIYOMJARIBU MUNGU.

Hesabu 14:22 “kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya WAMENIJARIBU MARA HIZI KUMI, wala hawakuisikiza sauti yangu; 

23 hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;

24 lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki”

Maandiko yanaonyesha kuwa wana wa Israeli walimjaribu Mungu MARA KUMI, je ni wapi katika maandiko panaonyesha hayo?

1. JARIBU LA KWANZA: (Mkabala na bahari ya Shamu)

Kutoka 14:9 “Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. 

10 Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana. 

11 Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri?

12 Neno hili silo tulilokuambia huko Misri”

Hili ndio jaribu la Kwanza wana wa Israeli walilomjaribu nalo Mungu, ijapokuwa walishaona matendo yake makuu kwa Farao na Misri yote kwa ujumla jinsi alivyoipiga Misri na kuiharibu kwa ishara kubwa na maajabu mengi, lakini hapa wanamjaribu Mungu kuangalia kama atawapigania tena kinyume na Farao au la!.. jambo ambalo ni dhambi kwao kwani tayari wanaujua uweza wa Mungu na hivyo hakuna haja ya kumjaribu ili kuona atakachokifanya.

2. JARIBU LA PILI: (Maji ya Mara)

Kutoka 15:22 “Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

 23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara. 

24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko”

Hili ni jaribu la pili, baada ya kuona uweza wa Mungu wa kupasua bahari, lakini bado wakamjaribu Mungu kuangalia kama atawafanyia muujiza wa Maji au la.. Na Bwana akawapa maji kama walivyotaka lakini bado hawakuridhika…

3. JARIBU LA TATU: (Katika bara ya Sini, kutaka Nyama)

Kutoka 16:1 “Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri

2 Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; 

3 wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.”

Hili ni jaribu la tatu baada ya kumjaribu Bwana kwa maji ya Mara na sasa wanataka kumwangalia Bwana kama anaweza kuwafanyia muujiza wa Nyama katikati ya jangwa, na Bwana akawapa nyama, kama walivyotaka lakini bado hawakuchoka kumjaribu..

4. JARIBU LA NNE: (Kusaza kwa Mana).

Kutoka 16:19 “Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi.

 20 Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana”

Walipewa maagizo wasikisaze (yaani wasibakishe chochote mpaka asubuhi) lakini wao wakafanya kinyume chake kwa kusudi la kuchunguza ni nini kitatokea.

5. JARIBU LA TANO: (Ukusanyaji wa Mana siku ya Sabato)

Kutoka 16:26 “Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana. 

27 Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione. 

28 Bwana akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini? “

Mungu aliwaambia wasitoke kwenda kuokota Mana siku ya Sabato, bali wapumzike, kwasababu hiyo mana haitapatikana siku hiyo, lakini wenyewe wakatoka kwenda kuhakiki kama kweli haitapatikana?.. hivyo ikawa ni dhambi kwao.

6. JARIBU LA SITA: (Maji ya Refidimu).

Kutoka 17:1 “Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama Bwana alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe.

2 Kwa hiyo hao watu wakateta na Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwani kuteta na mimi? Mbona mnamjaribu Bwana?

3 Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?”

Baada ya kumjaribu Bwana kule Mara, kwa kutaka maji, sasa wanarudia tena yale yale makosa.. ya kutaka watokezewe maji ya kimiujiza..Kulikuwa hakuna haja ya kumjaribu Mungu mara ya pili, kwani tayari walishaona uweza wake mara ya kwanza, lakini wao walitaka kuona tena na tena..

7. JARIBU LA SABA: (Sanamu ya Ndama).

Kutoka 32:7 “Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao,

8 wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri”

Wametoka kunywa maji kimiujiza katika Mwamba, na kuhakiki kwamba Bwana yupo katikati yao, lakini hapa wanafanya makusudi kutengeneza sanamu ya Ndama, kama ishara ya kumsusia Mungu, ambaye wanajua kabisa yupo..

8. JARIBU LA NANE: (Moto wa Tabera)

Hesabu 11:1 “Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. 

2 Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma.

3 Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa Bwana ukawaka kati yao’

Manung’uniko haya ni yale ya kutafuta kuona kitu cha kimwujiza kutoka kwa Mungu, kwasababu walikuwa wameshajua kuwa Mungu anaweza kufanya lolote..

9. JARIBU LA TISA: (Tamaa ya Nyama)

 Hesabu 11:4 “Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?

 5 Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;

 6 lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu”

Wana wa Israeli wanataka nyama, si kwasababu walikuwa na njaa sana, bali kwasababu walikuwa wanataka kuona jambo jipya kutoka kwa Bwana..

10. JARIBU LA KUMI: (Wapelelezi wa Kaanani)

Hesabu 14:1 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.

 2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. 

3 Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?

4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri”.

Hili ndilo jaribu la mwisho, wana wa Israeli walilomjaribu nalo Mungu, nalo ndilo likawa Muhuri wa wao kuipoteza ahadi ya kuiona ile nchi, isipokuwa watu wa wawili tu, ambao ni Yoshua na Kalebu.

Nasi pia tunachoweza kujifunza katika habari hiyo kuwa “KUMJARIBU MUNGU NI DHAMBI KUBWA SANA”.

Kama tumeshaujua uweza wake kwanini tumjaribu?.. kama tumeshajua kuwa Mungu anaweza kutuokoa na hatari kwanini tujiweke katika hatari??.. Kama tumeshajua kuwa Mungu anaweza kutuokoa na yule mwovu kwanini basi tujisogeze karibu na yule Mwovu??.. Kama tumeshajua kuwa “tutakapokula vitu vya kufisha, havitatudhuru, kwanini basi tuvile makusudi”, kama umeshajua kuwa Mungu ni mponyaji kwanini basi tunywe sumu makusudi?..

Kama umeshajua kuwa Bwana anakupenda kwanini ujiuze kwenye dhambi ili uujaribu upendo wake???.. unadhani utabaki salama?

Ndicho wana wa Israeli walichokuwa wanakifanya, pasipo kujua kuwa wanafanya dhambi kubwa sana, ambayo itawagharimu kukosa kuingia Kaanani.

Kumbuka Hili ndilo jaribu ambalo shetani anawaangusha nalo watu wengi hata siku hizi za mwisho, na ndilo hata alilolichagua kama moja kati ya majaribu yake matatu yenye nguvu kubwa, ili aweze kumwangusha Bwana Yesu lakini alishindwa!,

Mathayo 4:5 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,

6  akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe

7  Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.”

Na wewe usimjaribu Bwana, usiujaribu Msalaba.

Bwana akubariki.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI.

JIHADHARI NA MKUTANO WA WATU WALIOCHANGANYIKANA.

MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.

Je Ni kweli haturuhusiwi kula nyama kulingana na Isaya 66:3?

UPEPO WA KUSI HULETA MVUA;

Rudi nyumbani

Print this post

Wapelelezi wa uhuru wa wakristo ni watu gani (Wagalatia 2:4)?

Jibu: Tuanzie kusoma ule mstari wa 3

Wagalatia 2:3 “Lakini Tito aliyekuwa pamoja nami, naye ni Myunani, hakulazimishwa kutahiriwa.

4  BALI KWA AJILI YA NDUGU ZA UONGO WALIOINGIZWA KWA SIRI; AMBAO WALIINGIA KWA SIRI ILI KUUPELELEZA UHURU WETU TULIO NAO KATIKA KRISTO YESU, ILI WATUTIE UTUMWANI;

5  ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi.”

Hapo kuna mambo matatu (3).. NDUGU WA UONGO, 2) WALIINGIA KWA SIRI, na 3) KUUPELELEZA UHURU.

1.NDUGU WA UONGO.

Watu waliookoka waliitwa NDUGU, na hata leo wanaitwa hivyo hivyo “Ndugu”, lakini wapo Ndugu wa Kweli na pia wapo wa “Uongo”. Ndugu wa kweli ni wale waliookoka kikweli kweli, ambao wapo katika kundi au kusanyiko katika Nia ya KRISTO na si kwaajili ya kutafuta mambo yao wenyewe (1Wakorintho 16:20 na Wagalatia 1:2).

Lakini “Ndugu wa Uongo” Hao ni watu ambao wanajiingiza katika kanisa, ikiwa Nia yao si kumtafuta Kristo wala kumtumikia bali kutafuta mambo yao mengine kama Fedha, au Fursa Fulani, na wengine kuupeleleza uhuru wa wakristo na wengine ni mawakala kabisa wa Ibilisi, wanajiunga kwa lengo la kuliharibu kundi na kulisambaratisha. Mfano wa hao ndio wale Paulo aliwaozungumzia katika waraka kwa Wafilipi..

Wafilipi 3:17 “Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi.

18  Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo;

19  mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani.

20  Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo”.

Makundi haya ya Ndugu wa Uongo, yamesambaa katika nafasi zote, kuanzia Wachungaji, Mitume, manabii, waimbaji, mpaka washirika/waumini.

2. WANAJIINGIZA KWA SIRI

Kundi hili la Ndugu wa Uongo, huwa hawajiingizi kwa wazi bali kwa siri, maana yake ni kwamba wanajigeuza na kufanana na Ndugu wa kweli.. lakini ndani yao wanajua ni nini wanatafuta sawasawa na maandiko yanavyosema..

2Wakorintho 11:13  “Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.

14  Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.

15  Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao”

3. KUUPELELEZA UHURU.

Sasa ni Uhuru gani ambao Wakristo wanao?.. Jibu: Ni uhuru unaotuweka mbali na utumwa wa Sheria… Katika Ukristo hatuna sheria za kutahiriwa, kwamba ni lazima mtu atahiriwe au asitahiriwe ndipo akubaliwe na Mungu, vile vile na sheria nyingine zote kama kushika sabato na kushika miezi na sikukuu, kuna aina fulani tu ya chakula n.k hizo zote maandiko yanasema tumewekwa huru nazo..

Wakolosai 2:16 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;

17  mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo……………………..

20 Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani,

21  Msishike, msionje, msiguse;

22  (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata maagizo na mafundisho ya wanadamu?

23  Mambo hayo yanaonekana kana kwamba yana hekima, katika namna ya ibada mliyojitungia wenyewe, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini hayafai kitu kwa kuzizuia tamaa za mwili”.

Sasa walikuwepo wayahudi ambao wanajiingiza katika kanisa la Kweli la Kristo, si kwa lengo la kumtumikia Bwana, bali kwa lengo la kuwatwika watu mzigo wa kushika sabato, na mwandamo wa mwezi na sikukuu za kiyahudi.

Hata sasa wapo watu baadhi ambao wengine wanatenda mfano wa hayo kwa kujua au kwa kutokujua, mfano mapokeo ya kushika sabato yanauua uhuru wetu katika Kristo, mapokeo ya kutahiriwa yanaua uhuru wetu katika Kristo n.k

Hivyo hatuna budi kuzipima roho, si kila pokeo ni la kupokea.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru

MWENGE WAKO WA UHURU UPO WAPI?

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

Kutekewa maana yake nini?(Mathayo 22:12)

“Si watu wa kutumia mvinyo sana”, je tunaruhusiwa kutumia mvingo kidogo?(1Timotheo 3:8).

Rudi nyumbani

Print this post

Kama Kristo alizichukua dhambi zetu na kutusamehe kwanini kila siku tunatubu?.

Jibu: Ni kweli Kristo alizichukua dhambi zetu kama biblia inavyosema katika kitabu cha Petro..

1Petro 2:24 “Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa”.

Lakini hiyo haimaanishi kuwa tumeshakamilika asilimia mia kwamba hatutakuwa na kasoro zozote kuanzia hapo na kuendelea…Kasoro chache chache na madhaifu machache chache bado tutaendelea kuwa nayo mpaka siku tutakapopata ukombozi wa miili yetu (Waefeso 4:30).

Wakati parapanda ya mwisho itakapolia hapo ndipo tutapata ukombozi wa miili yetu, na tutakuwa wakamilifu asilimia zote kwasababu tutapewa miili mingine isiyo na kasoro wala madhaifu.. lakini sasa ulimwenguni bado tupo katika mapambano, bado tupo vitani, bado ibilisi yupo, bado tutapitia vipindi vya kukosea vidogo vidogo, lakini si vya kutuangusha kabisa!!.. Kama kile Petro alichopitia wakati anakutana na Paulo kule Antiokia (Soma Wagalatia 2:11-14).

Vile vile tutapitia vipindi vya kuudhiwa, na kupata hasira, tutapitia vipindi vya kukosea kuongea, kukosea kutenda, tutapitia vipindi pia vya kuwakosa wengine pasipo kujua au kwa kujua, tutapitia vipindi vya kumkosa Mungu kwa kujua au kwa kutokujua n.k.. sasa kwa kasoro hizo zote tunazozibeba ni lazima tuwe watu wa kuomba rehema na toba mara kwa mara ili muda wote tudumu katika usafi na pia Bwana anyooshe mapito yetu..

Hiyo ndiyo sababu pia Bwana Yesu akatufundisha kuomba toba na rehema kila mara..

Luka 11:1 “Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake.

2  Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.]……………….

4 UTUSAMEHE DHAMBI ZETU, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu]”.

Kwahiyo ni lazima kuomba rehema na toba kila siku, kwasababu bado tupo katika mwili, na pia ni ishara ya unyenyekevu kwa Mungu.

Bwana atubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Fahamu Namna ya Kuomba.

JIRANI YANGU NI NANI?

Ni kwa namna gani, upendo husitiri wingi wa dhambi? (1Petro 4:8).

SALA YA BWANA. (Namna ya kuiomba)

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

KAMA MKRISTO EPUKE KUENDEKEZA BAADHI YA DHAMBI

Wewe umemwaga damu nyingi,

Kuna wakati Daudi aliingiwa na wazo la kumjengea Mungu nyumba, hivyo wazo hilo likawa jema sana machoni pa Mungu, likamfurahisha sana Bwana mpaka akamwahidia Baraka tele katika ufalme wake..Lakini tunasoma Mungu alimzuia Daudi asiijenge hiyo nyumba, bali mwana wake Sulemani ndiye aje kuijenga, sio kwamba Mungu alikuwa hatamani Daudi aijenge, hapana Mungu alimpenda sana, na alikuwa kipenzi chake, lakini kulikuwa na kikwazo kilichomkwamisha..

Embu tusome…

1 Nyakati 22:7-8

[7]Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wangu. 

[8]Lakini neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu; 

Sababu yenyewe Mungu ameitoa hapo kwamba Daudi “amemwaga Damu za watu wengi”..Daudi hakujua kuuwa kwakwe watu sio jambo ambalo lilikuwa linavutia machoni pa Bwana,japokuwa Mungu alikuwa pamoja naye wakati wote, hakujua kuwa kuua kule kulikuwa kunapeleka harufu mbaya mbele za Mungu aliye mtakatifu na msafi.

Hivyo wakati anapeleka ombi lake la kumjengea hekalu, Mungu akamkataza kwasababu alimuona ananuka damu za watu wengi, Na sikuzote Mungu hawezi kuruhusu mikono yenye damu, kushiriki katika kujenga vitu vitakatifu.

Ni nini  Bwana anataka tujifunze.

Sisi kama wakristo, zipo dhambi au makosa ambayo tunayazoelea kuyafanya mara kwa mara, lakini hatujui kuwa tunamkosea Mungu, wakati mwingine tunapumbazika, kuona rehema na fadhili zake zinatufuata kila mahali, lakini ndani ya mioyo yetu tunamwaga damu kila kukicha kama Daudi.

Kwamfano, katika agano jipya, hatuui kwa Upanga au kwa mkuki, maandiko yanasema..

1Yohana 3:15  “Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake.

Kitendo tu cha kuwa na chuki, na jirani yako, au ndugu yako, kumbe rohoni unatafsirika kama mwuaji, hivyo chuki hizo zinavyoendelea na kuzidi wakati baada ya wakati, zinavyozidishwa kwa watu wengine kadha wa kadha, ndivyo mtu huyo anavyoonekana anamwaga damu nyingi.

Na madhara yake utakuja kuyaona mbeleni, wakati ambapo unamwomba Mungu kibali cha kutenda jambo Fulani jema kwa ajili yake, anakuzuia, unataka Mungu atembee na wewe katika viwango Fulani vya juu, anakuzuia, kwasababu umeendekeza makosa au dhambi hizo kwa muda mrefu.

Hivyo, tunapaswa, kila inapoitwa leo, tuangalie ni wapi tumezoelea kupafanya ambapo hapampendezi Mungu, kisha tuache mara moja, ili isije kutuletea madhara mbeleni, Kama ni katika usengenyaji, tuache mara moja, kama ni katika uongo, rushwa, udhuru,wivu, manung’uniko tuache mara moja.

Bwana atusaidie

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

KWANINI DAUDI ALIKUWA NI MTU ALIYEUPENDEZA MOYO WA MUNGU?

EPUKA KUCHELEWA IBADA.

NAAM, HATA WABAYA KWA SIKU YA UBAYA. 

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?

KIFAHAMU KIGEZO  CHA KUSAMEHEWA NA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

Je Ni kweli haturuhusiwi kula nyama kulingana na Isaya 66:3?


Jibu: Tusome,


Isaya 66:3 “Yeye achinjaye ng’ombe ni kama yeye amwuaye mtu; na yeye atoaye dhabihu ya mwana-kondoo ni kama yeye avunjaye shingo ya mbwa; na yeye atoaye matoleo ni kama yeye atoaye damu ya nguruwe; na yeye afukizaye uvumba ni kama yeye abarikiye sanamu; naam, wamezichagua njia zao wenyewe, na nafsi zao zafurahia machukizo yao”.


Mstari huo tukiusoma kama ulivyo ni rahisi kutafsiri kuwa “Biblia imekataza kuchinja wanyama na kula nyama”…lakini kiuhalisia hiyo sio maana yake kabisa…kwasababu kama hiyo ingekuwa ndio maana yake basi pia hapo imekataza matoleo… na tunajua matoleo ni jambo linalokubalika mbele za Mungu (Warumi 25:26).


Sasa tukisoma kuanzia ule mstari wa kwanza utaona Mungu anawakemea au kuwaonya wale watu ambao wanakusanya vingi na vikubwa na kwenda kumtolea Mungu, wakidhani kuwa Mungu anapendezwa na sadaka zao hizo kubwa na nyingi na huku mioyoni wapo mbali na Mungu.


Na utaona Bwana anazidi kusema.. “Mbingu na dunia ni mali yake, hakuna chochote tutakachoweza kumpa yeye ambacho kitakuwa cha kipekee”…ikifunua kuwa Mungu hana haja na vitu bali mioyo yetu, kwasababu kila kitu ni chake.


Isaya 66:1 “BWANA asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani?


2 Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema BWANA; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu”.


Umeona?..Mtu mnyonge ndiye atakayemwangalia Bwana, mtu mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno lake…Maana yake mtu wa namna hii atakapoleta sadaka yake ndio Mungu atakayoikubali, lakini mtu mwovu na mwenye kiburi Mungu haitaki sadaka yake.


Sasa endapo mtu mwovu anayemkataa Mungu analeta sadaka yake mbele za Mungu, sadaka yake hiyo inaonekana kama ni sadaka ya hatia.


Kama akileta Ng’ombe na kumpeleka kwa Kuhani kama sadaka ya kuteketezwa, Bwana ataiona sadaka hiyo kama ni kafara ya Mtu sio ya ng’ombe, hivyo atajitafutia laana badala ya baraka.


Utaona maandiko yanazidi kulisisitiza hilo katika Mithali 15:8

.
Mithali 15:8 “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA…”

Ndio maana katika Isaya 66, Bwana anasema..


Isaya 66:3 “Yeye achinjaye ng’ombe ni kama yeye amwuaye mtu; na yeye atoaye dhabihu ya mwana-kondoo ni kama yeye avunjaye shingo ya mbwa; na yeye atoaye matoleo ni kama yeye atoaye damu ya nguruwe; na yeye afukizaye uvumba ni kama yeye abarikiye sanamu; naam, wamezichagua njia zao wenyewe, na nafsi zao zafurahia machukizo yao”.


Kwahiyo tunachoweza kujifunza ni kuwa, Bwana hapendezwi na matoleo mabaya, yeye alisema kulitii Neno lake ni bora kuliko dhabihu Soma (1Samweli 15:22).


Hivyo usipeleke madhabahuni fedha haramu, fedha iliyopatikana kwa rushwa, kwa wizi, kwa uuuzaji wa vitu haramu kama bangi, pombe, sigara au hata kwa uuzaji wa mwili.


Kumbukumbu 23:18 “Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya BWANA, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako, yote mawili”


Vile vile hatupaswi kumtolea Mungu dhabihu huku hatuna mapatano sisi kwa sisi..


Mathayo 5:23 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,
24 iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako”


Bwana Yesu atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Nyama zilizosongolewa ni zipi?Je kunywa damu ni dhambi?

HAPAKUWA NA NAFASI YA KUPITA KWA YULE MNYAMA ALIYEKUWA CHINI YANGU.

Kwanini Bwana aliwalenga mbwa na nguruwe tu katika Mathayo 7:6?

UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

MASWALI NA MAJIBU: YAHUSUYO NDOA- Sehemu ya 2.

Rudi nyumbani

Print this post

UPEPO WA KUSI HULETA MVUA;

SWALI: Nini maana ya huu mstari?

Mithali 25:23 Upepo wa kusi huleta mvua; Vile vile asingiziaye huleta uso wa ghadhabu.


JIBU: Maandiko yanasema Upepo wa kusi huleta mvua, hapo hasemi ‘upepo’ huleta mvua hapana bali anasema ‘Upepo wa kusi’, Maana yake ni kuwa kila aina ya upepo hubeba tabia yake, kwa mfano upepo wa Kaskazi, hauleti mvua, bali unaleta joto. Vivyo hivyo na pepo nyingine zote, hubeba tabia zao.

Hii ni kufunua nini?

Na sisi wanadamu huwa tunavumisha pepo zetu..Na ndio maana utasikia Neno “UVUMI” wa jambo Fulani, na taarifa hizo husambazwa kwa maneno ya vinywa vyetu, Hivyo kila jambo unalolitoa na kulipeleka kwa mtu mwingine au kwa jamii, huo ni upepo, na ni lazima uwe makini nao sana, kwasababu mwisho wa siku ni lazima ulete faida au madhara.

Na ndio maana hapo katika sehemu ya pili ya mstari huo anasema.. “Vile vile asingiziaye huleta uso wa ghadhabu”. Kusingizia ni neno linalojumuisha usengenyaji, au mtu anayechukua taarifa siziso za kweli na kuzipeleka kwa mwingine, Watu kama hawa, mwisho wa siku watavuna  ghadhabu tu, au kuchukiwa, au kusababishiwa madhara na wale waliotolewa taarifa zao. Kwasababu kila uvumi unamatokeo yake.

Lakini tukiwa watu wa kupeleka habari njema, watu wa kuhubiri habari za Kristo, Maana yake ni kuwa Upepo tunaovumisha ni wa heri sikuzote, hivyo tufahamu kuwa mwisho wake utakuwa ni mzuri, utatuletea neema badala ya ghadhabu, kupendwa badala ya kuchukiwa, kusaidiwa badala ya kufukuzwa.

Hivyo tuwe makini na taarifa, au maneno yanayotoka katika vinywa vyetu, biblia inasema..

1 Petro 2:1  Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. 2  Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;

Epuka masengenyo, na kuwazungumzia wengine vibaya.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kuwaogopa wanadamu huleta mtego,(Mithali 29:25)

NA UPEPO WA KUSI ULIPOANZA KUVUMA KIDOGO,

JIPE NAFASI KATI YA TAARIFA UNAYOIPOKEA NA MAAMUZI UNAYOYATOA.

IEPUKE GHADHABU YA MUNGU.

Dunia inalewa-lewa kama mlevi, nayo inawaya-waya kama machela.

Kwanini mtu afanye miujiza na bado asiende mbinguni?

Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.

Rudi nyumbani

Print this post

Mithali 24:17 inamaana gani kusema Tengeneza kazi yako huko nje?

SWALI: Naomba nieleweshwe maana ya huu mstari

Mithali 24:27

[27]Tengeneza kazi yako huko nje, Jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako.


JIBU: Zamani enzi za biblia, kilimo kilikuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa watu wengi kama ilivyo sasa katika  baadhi ya jamii.

Hivyo ilikuwa ni ajabu mtu kutumia rasilimali zake katika kununua au kujenga vitu visivyo na umuhimu sana, kama vile nyumba, nguo za kifahari, magari ya farasi n.k.angali shambani kwake hajajiwekeza vya kutosha.

Watu walikuwa wanakusanya kwanza chakula cha kutosha kujihakikishia shibe kwa miezi au miaka kadhaa, ndipo baada ya hapo hufikiria kutumia hazina zao katika kujenga, au kujiendeleza..lakini hawakujiendeleza kabla ya kuhakikisha mashamba yao yamewanufaisha..

Na ndio hapo Sulemani utaona anatoa ushauri ule ule..

Mithali 24:27

[27]Tengeneza kazi yako huko nje, Jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako.

Yaani kwa lugha rahisi ni kwamba tengeneza kwanza mambo yako uwe imara ndipo yale mengine ya ziada yafuate baadaye.

Ni kawaida ya mwanadamu kupenda, vitu vizuri kwanza kabla hajavitaabikia..

Alikuwepo Gehazi, mtumwa wa Elisha, yeye aliona kusubiri wakati wa Mungu ni kujichelewesha, kutumika kama mtumwa asiye na faida ni kupoteza muda, hivyo, zile zawadi zenye thamani nyingi zilizoletwa na Naamani, na Elisha kuzikataa, yeye akamwona kama alikuwa hapendi mema..lakini Elisha alimwambia maneno haya..

2 Wafalme 5:26

[26]Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng’ombe, na watumwa, na wajakazi?

Alimuuliza Je huu ndio wakati? ..kumbe kulikuwa na wakati lakini haukuwa ule..

Watu wanataka kula vitu vya Bwana lakini hawataki kutengeneza kwanza kazi zao huko mashambani, hawana muda wa kuifikiria kazi ya Mungu, hawana muda na kuhubiri injili ya kweli,wanachokifiria ni matumbo,  na kwamba watapata faida gani..

1 Timotheo 6:5-6

[5]… huku wakidhani ya kuwa utauwa ni njia ya kupata faida.

[6]Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa.

.Vilevile hata katika maisha ya kawaida, hekima hizi zinamafunzo, mtu atataka anunue simu ya milioni 2, lakini hana shughuli yoyote ya kumwingizia kipato, badala aitumie kama mtaji, kisha kile akipatacho kama faida ndio atumie kununua hayo mengine..

Bwana atusaidie, katika kuyapangalia maisha yetu ya rohoni na mwilini

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

TENGENEZA  NYAVU ZAKO, OSHA NYAVU ZAKO.

Nini maana ya vifungeni viuno vya Nia zenu? (1Petro 1:13).

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

USIWE ADUI WA BWANA

Nini maana ya Ukuta uliopakwa chokaa (Matendo23:3)?

Uchaga ni nini? (Luka 12:24)

NAAM, HATA WABAYA KWA SIKU YA UBAYA. 

Rudi nyumbani

Print this post