NAAM, HATA WABAYA KWA SIKU YA UBAYA. 

NAAM, HATA WABAYA KWA SIKU YA UBAYA. 

Sehemu ya 1

Mithali 16:4 “Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya”.

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tujifunze maneno ya uzima; Huu ni mfululizo wa makala, zinazochambua baadhi ya maneno au vifungu, ambavyo vimekuwa vigumu kwetu sisi kuvielewa kuhusiana na Mungu. Na hiyo imepelekea hadi baadhi ya watu wasimwamini kabisa Mungu na wengine  kusema inakuwaje Mungu mwenye uwezo afanye vitendo kama hivi, au aruhusu mambo kama haya?

Hivyo katika makala hizi, tutaangazia uhalisia ya vifungu hivyo; Na tutapata amani katika hayo.

Kuna wakati Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake maneno haya;

Yohana 13:7  “Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye”.

Ikiwa na maana kuna mambo ambayo Mungu anayafanya , kamwe hatutakaa tuyaelewe kwa sasa, bali baadaye sana. Na “Baadaye”, inaweza kumaanisha kipindi kirefu kijacho, au wakati wa baada ya haya maisha.

Hivyo basi, hakuna mwanadamu anayeweza kutolea majibu kila jambo analolisoma kuhusu Mungu, isipokuwa tu tunapapasa-pasaka, na kuelewa yale tuliojaliwa kuelewa na Roho Mtakatifu kwa sasa (Matendo 17:27).

Leo kwa sehemu tutaona, kwanini Mungu alisema maneno haya.

Sehemu: Mithali 16:4 “Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya”.

Swali linaloulizwa hapo, Je! Ni kweli Mungu aliwaumba wabaya ili kutimiza kusudi la ubaya?

Jibu ni ndio kama ilivyoandikwa.

Utauliza, ni kwanini sasa aseme yeye ni Mungu wa upendo, apendezwaye na haki? . Jibu ni lile lile, afanyalo leo hatutalijua, sasa lakini tutalijua vizuri baadaye. Na mawazo yake si mawazo yetu.

Ni vichache tu tunaweza kujua kwanini amewaumba watu wabaya kama ibilisi na mapepo yake, na waovu kama akina Kaini, kora, Belshaza? Ili wafanye mabaya duniani?

Majibu tuliyopewa kuyaelewa, ni ili kutimiza makusudi yake matatu makuu;

  1. kufundisha
  2. kuadhibu
  3.  kuonyesha uwezo wake.

Kwamfano tunapoona hatma ya ibilisi na matendo yake maovu, hakuna hata mmoja anapendezwa na tabia kama zile, hivyo na sisi tutajilinda na dhambi ya uasi, kwa gharama zote, kwasababu tunajua mwisho wake utakuwa wapi. Hivyo yeye na watu wabaya wamekuwa funzo kubwa kwetu sisi, juu ya madhara ya dhambi.

Kama wasingekuwepo, tusingejua uzuri wa haki. Huwezi kujua sukari ni tamu kama hujawahi kuonja kitu kichungu, huwezi kujua hili ni joto kama hujawahi kuhisi baridi kabisa.  Vilevile hatuwezi kujua Mungu ni wa upendo kama hatujakaa na watu wabaya, kama vile wauaji, wabinafsi n.k

Vilevile ameruhusu kwa lengo la kuadhibu, pale tumkoseapo Mungu. Anaruhusu watu kama akina Nebukadreza wa Babeli, kutuadhibu, kama wafilisti kwa Israeli walipomkosea Mungu. Hivyo wanasimama pia kama fimbo ya Mungu kwa watu wake kuwafunza.

Na vilevile kuwapa sababu zote hao watu wabaya kwanini wanastahili hukumu siku ile ya mwisho kwa matendo yao.

 Pia sababu ya tatu ni  ili kudhihirisha uweza wake mwingi. Mungu huwa anaruhusu wachawi kama Yane na Yambre washindane naye ili atoe maajabu yake yote, anaruhusu watu kama Farao wawe na mioyo migumu ili aonyeshe uweza wake mkuu wa uokozi, aliruhusu taifa lake Israeli lizungukwe na maadui zake aonyeshe jinsi anavyoweza kuokoa.

Soma hapa;

Warumi 9:17  “Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.

18  Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu.

19  Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake? 20  La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?

21  Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?

22  Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu;”

Hivyo basi, hizi ni baadhi ya sababu, lakini zipo nyingine zaidi ya hizo ambazo tutakuja kuzifahamu baadaye.

Hii ni kutufundisha nini?

Ni kutufundisha unyenyekevu, tukubali kufanyika watu wema, ili tusiwe vyombo vya ubaya, Kwasababu kila jambo unaloliona duniani, liwe baya liwe jema, lipo chini ya makusudi ya Mungu, hakuna linalotokea kwa bahati mbaya, na ndio maana mengi ya hayo bado hayajaondolewa yote. Lakini utafika wakati yataisha.

Kumbuka  hatuna miaka 100 tu ya kumjua Mungu, bali tuna umilele mbeleni, Hivyo kwa kipindi hichi kifupi hatuweza kutoa habari zote za Mungu, na kumuuliza kwanini umeruhusu haya, au yale..tuwe watulivu.

Tupende mema tuwe salama, tumpe Kristo maisha yetu ili tusiwe vyombo vya ghadhabu kama Farao, bali vya heshima.

Bwana akubariki.

Mwendelezo unakuja..

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JE! UMECHAGULIWA TANGU ASILI?

KITABU CHA UZIMA

NGUVU YA UPOTEVU.

YESU NI NANI?

TOFAUTI YA MITUME, MANABII, WAINJILISTI, WACHUNGAJI NA WAALIMU NI IPI?

HATARI! HATARI! HATARI!

JINSI YA KUMSIKIA MUNGU, NA KUPOKEA MAFUNUO AU JUMBE KUTOKA KWAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments