JIHADHARI NA MKUTANO WA WATU WALIOCHANGANYIKANA.

JIHADHARI NA MKUTANO WA WATU WALIOCHANGANYIKANA.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu, lililo Taa ya miguu yetu na Mwanga wa njia yetu.

Kuna jambo la muhimu la kujifunza juu ya safari ya Wana wa Israeli kutoka Misri kuelekea Kaanani. Maandiko yanaonesha kuwa wana wa Israeli hawakutoka wenyewe Misri, bali walitoka na Kundi lingine lililochanganyikana.

Hebu tusome..

Kutoka 12:35 “Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi, walipata hesabu yao kama watu sita mia elfu watu waume waliokwenda kwa miguu, bila kuhesabu watoto. 

38 NA KUNDI KUBWA LA WATU WALIOCHANGAMANA MNO WAKAKWEA PAMOJA NAO; na kondoo na ng’ombe, wanyama wengi sana”

Umeona hapo?.. Kulikuwa na watu wengine tofauti na Waisraeli walioondoka Misri pamoja na wana wa Israeli.

Sasa swali ni je! kundi hilo lilikuwa ni kundi gani?.

Kundi hilo lilijumuisha baadhi ya Wamisri ambao huenda walikuwa hawataki kuendelea kuishi Misri, labda kutokana na aina ya Maisha ya Misri, pamoja na Wamisri ambao walioana na Waisraeli, maana yake huenda (mwanamke wa kimisri aliolewa na Mwisraeli) hivyo ni lazima aondoke na mumewe, au mwanamke wa kiisraeli aliolewa na Mmisri, na hivyo huyo Mmisri, hataki kumwacha mke wake huyo na akawa radhi kuondoka naye, na kwenda na wana wa Israeli.  Hivyo lilikuwa ni kundi kubwa sana!!..

Sehemu nyingine iliyotaja kundi hili lililochanganyikana ni mchanganyiko katika kile kitabu cha Mambo ya Walawi 24:10-16. (Kisa cha Yule mwana wa kiMisri, aliyechanganyikana).

Walawi 24:10 “Ikawa mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, ambaye babaye alikuwa Mmisri, akatokea kati ya wana wa Israeli; na huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, na Mwisraeli mmoja, wakapigana pamoja ndani ya marago; 

11 kisha huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli akalikufuru hilo Jina, na kuapiza; nao wakamleta kwa Musa. Na jina la mamaye alikuwa akiitwa Shelomithi, binti ya Dibri, wa kabila ya Dani. 

12 Nao wakamtia kifungoni, ili wapate kuambiwa neno litakalotoka kinywani pa Bwana.

13 Na Bwana akasema na Musa, na kumwambia,

14 Mtoe huyo aliyeapiza nje ya marago; na wale wote waliomsikia na waweke mikono yao kichwani mwake, kisha mkutano wote na wamwue kwa kumpiga kwa mawe.

15 Nawe nena na wana wa Israeli na kuwaambia, Mtu awaye yote atakayemlaani Mungu wake atachukua dhambi yake. 

16 Na yeye atakayelikufuru jina la Bwana hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzalia, hapo atakapolikufuru jina la Bwana atauawa”.

Sasa tukirudi katika habari ya Huu Mkutano uliochanganyika, huenda mkutano huu ukaonekana kama ulikuwa ni mwema, lakini kinyume chake ulikuja kuwa mwiba mkubwa kwa wana wa Israeli, kwani uliwakosesha sana mbele za Mungu wao.

Katika biblia tunasoma kwamba sio wana wa Israeli walioanza kumlalamikia Mungu kuhusu kutaka Nyama jangwani, bali tunasoma ni hili kundi lililochanganyikana ndilo lililoanza kunung’unika na hatimaye kushawishi mkutano mzima hadi wa wana wa Israeli kunung’unika, na kusababisha kuwa dhambi kubwa sana kwa wana wa Israeli.. Hebu tusome habari hiyo…

Hesabu 11:41 “Kisha MKUTANO WA WAFUASI WALIOKUWA KATI YAO, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?

 5 Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu”

Umeona tena hapo?.. maandiko yanasema “MKUTANO WA WAFUATI WALIOKUWA KATI YAO” ndio walioanza kushikwa na tamaa..wakata nyama..na ndipo Israeli wote nao wakaingiwa na tamaa.

Maandiko yanasema, agano la kale ni kivuli cha agano jipya..Safari ya wana wa Israeli kutoka Misri kuelekea Kaanani , inafananishwa na safari yetu ya kutoka katika utumwa wa dhambi, hapa duniani na kuelekea mbinguni.. Hivyo basi tunapokuwa katika safari hii, hatuna budi kujihadhari na watu waliochanganyikana, (yaani watu waliovuguvugu katika imani), kwasababu kwa nje wanaweza kuonekana hawana madhara yoyote, lakini tukijifunga Nira nao, na kutembea nao huko mbeleni watatukosesha na Mungu wetu na kuturudisha nyuma pakubwa sana, kama hawa walivyowakosesha wana wa Israeli.. Ndivyo maandiko yanavyosema..

2 Wakorintho 6:14  “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?

15  Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?

16  Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.

17  Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.

18  Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike”

Unapoanza safari ya Wokovu, ni Mungu kakuita wewe, na si wewe pamoja na rafiki yako au mfanyakazi mwenzako.. kama bado yeye hajaokoka hupaswi kujifunganisha naye Nira, maana yake ni kwamba kama mlikuwa mmezoea kwenda bar pamoja unaacha!, (wewe unapaswa umhubirie wokovu kuanzia huo wakati na kuendelea na si kujishikamanisha naye tena), kama mlikuwa mnaketi kuwasengenya watu, unaacha!, unajitenga naye katika hilo eneo.. Na mambo mengine yote mabaya hupaswi kuambatana naye, mpaka na yeye atakapobadilika na kuwa kama wewe.

Lakini usipoamua kujiachanisha naye katika utu wenu wa kale..basi tambua kuwa atakuja kuwa kikwazo kwako kumaliza safari yako salama ya Imani, (atakuwa ni lango la shetani kumtumia kukurudisha wewe nyuma) kama alivyolitumia lile kundi liliochanganyikana kuwarudisha Israeli nyuma kiimani.

Bwana atusaidie katika safari yetu ya Imani.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI.

Hema ya kukutania ni nini, na ilikuwaje?

JINSI MUNGU ANAVYOIPIGA NA KUIPONYA AFRIKA.

KUOTA UMECHOMWA KISU/KUOTA UMEPIGWA RISASI.

Kiti cha Rehema kilikuwaje? (Kutoka 40:20)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments