BASI NIKAOGOPA, NIKAENDA NIKAIFICHA TALANTA YAKO.

BASI NIKAOGOPA, NIKAENDA NIKAIFICHA TALANTA YAKO.

Shalom…Bwana wetu Yesu Kristo atukuzwe milele. Karibu tujifunze maneno yake ya uzima.

Lipo la kutafakarisha sana, katika ile habari ya yule mtu aliyesafiri, na kuwaita watumwa wake watatu na kumpa kila mmoja talanta ya Fedha wakafanyie biashara.

Kama tunavyoijua habari yule wa kwanza aliyepewa talanta tano, akaleta faida ya talanta nyingine tano, Vilevile yule aliyepewa talanta mbili akachuma nyingine mbili…lakini yule aliyepewa moja..maandiko yanatuambia hakuchuma chochote…

Na sababu iliyomfanya ashindwe kufanya vile si nyingine zaidi ya  “WOGA”…Tusome..

Mathayo 25:24-30

[24]Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;

[25]basi NIKAOGOPA, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.

[26]Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya;

[27]basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.

[28]Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi.

[29]Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

[30]Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Aliogopa nini?

Aliogopa atakapojaribu kuifanyia biashara ataipoteza…aliogopa kupata hasara..hivyo akaona ni heri aihifadhi tu..mahali fulani mpaka Bwana wake atakaporudi amrudishie kilicho chake wamalizane..

Aliogopa kuchekwa, na kudharauliwa, na kudhihakiwa, alijiona hawezi kuzalisha kile alichopewa, hana uzoefu na biashara..hakutaka kujitosa kama wale wenzake…ambao wao pia waliijua hatari ya biashara kwamba kuna kupata na kupoteza, lakini hawakutaka kuzipa kipaumbele… lakini yeye akasema sitaki kupata magonjwa ya moyo..wacha niihifadhi tu..kwani nini! , maadamu sijamtapeli..akirudi nitamrudishia kilicho chake.

Ndugu hii hali ipo kwa wakristo wengi hadi sasa..hawataki kupiga hatua moja mbele kuuzalia matunda wokovu wao kisa tu HOFU, ya kupata hasara..

Hasara ya nini?

Hasara ya ndugu kuwatenga, kama ndugu zao wakisikia kaokoka, wakiwatenga itakuwaje?

Hasara ya kuonekana wamerukwa na akili,..

Hasara ya marafiki kuwacheka, kuwaona ni washamba, wamepitwa na wakati..kwasababu wameacha mtindo fulani wa maisha.

Hasara ya kufukuzwa kazi, au kushushwa cheo kazini, kisa tu hawali rushwa tena.

Hasara ya kuachwa na mke/mume kisa tu wamejitwika msalaba wao na kuwafuata..

Hivyo hofu kama hizi na nyingine nyingi zimekuwa kigezo  cha wakristo wengi kufukia talanta zao chini..wanasubiria tu siku ya kufa, Kristo aje na kuwauliza mmezalisha Nini kwenye Wokovu niliowapa siku ya kwanza…wenyewe waseme hakuna zaidi tu ya kuokoka..

Hii ni hatari kubwa sana…na jambo la kuhuzunisha..Ni lazima tujue “hakuna hatua moja mbele kama hakuna kujikana” Yesu aliye Bwana wetu alikubali kuchukiwa, kutengwa, kuonekana karukwa na akili, hadi kuuliwa, ili tu amzalie Mungu matunda yaliyo bora..(Yohana 7:5)

Marko 3:21

[21]Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili.

Na yeye mwenyewe akatuambia tusipojitosa kama yeye hatuwezi kuwa wanafunzi wake…

Luka 14:26-27

[26]Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

[27]Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Akasema pia..ili mbegu ya ngano iweze kuzaa na kuleta matunda mengi haina budi kuoza kwanza chini ya ardhi, ndipo baadaye ichipuke na kukukua na kuzaa..(Yohana 12:24)

Ni lazima tuonekane tumekufa kwanza ndipo tuzalishe talanta zetu..tuonekane tumepotea kwa ajili ya Kristo ndipo tupate karama zake, tukilikimbia hili, tujue hatutazalisha chochote, ukristo wetu utakuwa ni ule ule wa miaka nenda, miaka rudi.

Ndugu/dada umedhamiria kumfuata Yesu, embu acha udunia kwa moyo wako wote..acha vimini, acha marafiki wasiofaa, acha miziki, na tamaa za ujanani, mtafute Mungu kwa moyo wote, elekeza nguvu zako zote huko..Epuka kuwa mkristo-jina…yule wa kusema nimeokoka-nampenda Yesu, halafu maisha yako hayana ushuhuda hata chembe..

Maanisha sasa..kwasababu siku zinavyozidi kwenda, siku moja utakufa na utatolea hesabu wokovu uliopewa, ukauchezea kwa hofu za wanadamu na ulimwengu.

Bwana atusaidie..

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 1)

Azidishaye mali yake kwa riba, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.

Talanta ni nini katika biblia (Mathayo 25:14-30)

Nini maana ya huu mstari? “Yeye mwenyewe ataokolewa lakini ni kama kwa moto”

ANGALIA JINSI USIKIAVYO:

Yesu alifundisha kwa mifano. Je hiyo mifano maana yake nini?

HUJAPEWA MBAWA ZA KUKIMBIA MATATIZO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments