Category Archive Wahubiri (Watumishi)

WEKA ANWANI HII KATIKA MAHUBIRI YAKO!

(Masomo maamulu kwa watumishi wa Mungu).

Je wewe ni mtumishi wa MUNGU?..Basi fuatilia mfululizo wa masomo haya katika tovuti yetu hii (www.wingulamashahidi.org).

Kama mtumishi wa Mungu kuna  Anwani au nembo au Lebo ambayo inapaswa iambatane na kila fundisho unalolitoa kwa wahusika. Na Anwani/lebo hiyo/nembo hiyo si nyingine Zaidi ya “TOBA”. Hakikisha mahubiri yako yanalenga Toba, au kuwakumbusha watu umuhimu wa kujitakasa.

Kwanini iko hivyo?

Hebu tujifunze kwa mmoja ambaye ni mjumbe wa Agano, tena ndiye Mwalimu wetu MKUU na Mwinjilisti MKUU YESU KRISTO.

Yeye katika mahubiri yake yote alihubiri “Toba”.. Huenda unaweza kusoma mahali akiwa anafundisha na  usione likitajwa neno Toba, lakini fahamu kuwa alikuwa anahubiri Toba kila siku katika mafundisho yake yote… Kwani biblia inasema kama yote aliyoyafanya BWANA YESU kama yangeandikwa basi dunia isingetosha kwa wingi wa vitabu.

Yohana 21:25 “Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa”

Kwahiyo Mahubiri ya BWANA WETU YESU yote Yalikuwa yamejaa toba.. sasa tunazidi kulithibitishaje hilo?.. hebu tusome maandiko yafuatayo..

Mathayo 4:17 “Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”

Nataka tuutafakari kwa undani huu mstari… anasema “Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”…. Zingatia hilo neno “TOKEA WAKATI HUO….TOKEA WAKATI HUO…TOKEA WAKATI HUO”.. Maana yake “kilikuwa ni kitu endelevu”, sio kitu cha kusema mara moja na kuacha, (hiyo ndiyo ilikuwa lebo ya mafundisho yake daima).. Kila alipohubiri lazima aliwahubiria pia watu watubu.

Umeona?. Je na wewe Mchungaji, na wewe Mwalimu wa injili, na Wewe nabii, na wewe Mtume, na wewe Mwimbaji wa injili.. LEBO YA MAHUBIRI YAKO NI IPI????.

Je! injili yako unayohubiri ni ya TOBA, au ya kuwafariji watu katika dhambi zao??.. Je unazunguka huku na kule kuhubiri injili ya namna gani?..Je ni injili ya Toba au ya Mali tu!.

Luka 24:45  “Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko.

46  Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu;

47  na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.

48  Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya”

Hakuna furaha, hakuna mafanikio, hakuna Amani ikiwa mtu yupo katika maisha ya dhambi.. utamhubiria afanikiwe lakini hata akiyapata hayo mafanikio basi dhambi itamuua tu na kumkosesha raha.. Raha pekee na Amani mtu ataipata baada ya kutubu, ndivyo maandiko yasemavyo..

Matendo 3:19 “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Toba ni nini?

VYA MUNGU MPENI MUNGU.

NAYAJUA MATENDO YAKO.

Ni lazima mtu aongozwe sala ya toba ili awe ameokoka?

WEKA KUMBUKUMBU YA MAMBO BWANA ANAYOKUFANYIA KWASABABU YATAKUFAA MBELENI.

Rudi nyumbani

Print this post

Tofauti kati ya makuhani na walawi ni ipi?

SWALI: Na je! Walawi na makuhani katika kanisa la sasa ni watu wa namna gani?

JIBU: Mungu alilichagua kabila moja kati ya kumi na mbili liwe kabila lake takatifu litakalosimama katika kazi na shughuli zote za kidini na ibada Israeli.

Sasa katikati ya hawa walawi ndipo walipotolewa makuhani ndani yake. Hivyo makuhani wote walikuwa ni walawi lakini walawi wote si makuhani.

Hizi ndizo kazi za walawi.

  1. Walawi wanasimama kama wasaidizi wa makuhani katika shughuli zote za kiibada mbele za Mungu. Hesabu 1:50
  2. Walisimama pia kama waandishi wa torati,  kufundisha na kutafsiri maandiko kum 33:10,
  3. Walisimama kama walinzi wa mazingira yote ya hema/ hekalu hesabu 3:21-26
  4. Walisimama kama wajenzi wa hema, na kulihamisha na kulijenga tena pale walipobadili makazi, Hesabu 1:48-54
  5. Walisimama pia kama waaamuzi, walitoa hukumu ya mambo ya sheria. kumb 17:8-13
  6. Vilevile walisimama kama waimbaji mbele ya hekalu la Mungu daima, 1Nyakati 9:33

Na hizi ndizo kazi za makuhani.

  1. Walifanya kazi za upatanisho wa dhambi na makosa ya watu, kwa sadaka za kuteketezwa na damu ipelekwayo ndani ya hema mbele ya madhabahu.(Waebrania 10:11-18)
  2. Waliwajibika kuwabariki watu. Kumb 10:8
  3. Pia walifanya kazi ya kulibeba sanduku la agano, popote pale walipokwenda. kumb 31:9

Kwasasa, kila mkristo, ni Mlawi. Kwasababu tayari ameshapewa uwezo ndani yake na karama, ya kuifanya kazi ya Mungu pale tu anapookoka. Kila mmoja ni kiungo kwa mwenzake ndani ya kanisa. Lakini mkristo anabadilika kutoka kuwa mlawi mpaka kuwa kuhani pale anaposimama hasaa kwa ajili ya huduma/kazi  ya Mungu kwa watu wake.

Anapobeba maono Fulani, labda  tuseme kulichunga kanisa, huyo ni kuhani wa Mungu, na hivyo anaposimama na kuwabariki watu basi Baraka hizo huwafikia watu moja kwa moja kutoka kwa Mungu, mfano tu wa makuhani wa agano la kale. Au anapotumika katika kuwafundisha, kuwaombea wengine, kuwasimamia wengine, haijalishi ngazi aliyopo, au mahali au jinsia, huyo rohoni ni kuhani wa Mungu.

Hivyo kila mkristo anaouwezo wa kuwa kuhani wa Mungu, kwasababu lengo la Mungu ni sote tuwe makuhani wake, sio tu walawi, Na Yesu Kristo Bwana wetu akiwa ni kuhani Mkuu.

1Petro 2:9  Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;

Bwana akubariki.

Je! Kristo yupo moyoni mwako?

Kama ni hapana, basi wakati ndio huu, mgeukie, akusamehe dhambi zako, kwa kutubu na kumaanisha kabisa kuziacha, naye atakukomboa. Ikiwa upo tayari kwa ajili ya mwongozo huo, basi waweza fungua hapa kwa mwongozo >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)

WALAWI WALIKUWA WENYE MIOYO YA ADILI KWA KUJITAKASA KULIKO MAKUHANI.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Kwanini Yesu aliwaambia wale wakoma wakajionyeshe kwa makuhani?

Sadaka ya Moyo ipoje? (Walawi 22:21).

Rudi nyumbani

Print this post

WALAWI WALIKUWA WENYE MIOYO YA ADILI KWA KUJITAKASA KULIKO MAKUHANI.

2Nyakati 29:34 Lakini makuhani walikuwa wachache, wasiweze kuchuna sadaka zote za kuteketezwa; basi ndugu zao Walawi wakawasaidia, hata ilipokwisha kazi, na hata makuhani walipojitakasa; kwa kuwa Walawi walikuwa wenye mioyo ya adili kwa kujitakasa kuliko makuhani.

Nakusalimu katika jina la Bwana Yesu.

Fundisho hili linawahusu sana sana viongozi wa kiroho / Watumishi wa Mungu wanaohudumia kundi la Mungu. Mfano wachungaji au maaskofu.

Kuna wakati wale walioteuliwa kuwa viongozi wa juu kabisa wanaweza wasiwajibike ipasavyo katika nafasi zao, je! Wewe kama mwangalizi wao ufanye nini?

Mfano tukirejea habari hiyo tunaona Mfalme Hezekia alipokusudia kulitakasa hekalu la Mungu, ambalo lilikuwa limefungwa na kusahauliwa, na baba yake.

Alitafuta makuhani wa kuhudumu upya katika nyumba ya Mungu. Ikumbukwe kuwa makuhani tu ndio walioruhusiwa kufanya shughuli zote za madhahabuni, ikiwemo kuvukiza uvumba na kuandaa zile sadaka zilizoletwa mbele ya nyumba ya Bwana.

Lakini hapo biblia inatuambia, Makuhani walikuwa wachache!. Utajiuliza ni kwanini? Sio kwamba hawakuwepo kabisa, walikuwepo, lakini biblia inatuambia waliokuwa na mioyo ya adili ya kuipenda kazi ya Mungu ndio walikuwa wachache.

Pengine, wengine walikuwa na udhuru zao, wakiona kuahirisha shughuli zao, na kwenda kuhudumu madhabahuni  ni kuvugiwa ratiba ni kazi ya kuchosha, haina faida, wengine hawakuwa tayari kujitakasa, kwa kuacha mambo mabovu yasiyowapasa makuhani, wengine wakawa wazito, wanavutwa vutwa sana, kazi ambayo inapaswa ifanyike haraka n.k..

Hivyo hiyo ikapelekea kundi la viongozi wa juu kabisa likawa chache sana. Na kimsingi ni lazima wawepo wahudumu wa kutosha katika kazi hiyo ya madhabahuni. Sasa wafanyaje. Ndipo hapo utaona Walawi ambao kazi zao ni za nje, ya hema kama vile usimamizi wa malango, kulinda hekalu, na kuimba. Ikabidi sasa waingizwe ndani kwa ajili ya kusaidia kazi za kikuhani.

Na sababu ya kufanya hivyo biblia inasema, wenyewe walikuwa ni “wenye mioyo ya adili kwa kujitakasa kuliko makuhani”.

Walikuwa na moyo wa kumtumikia Mungu zaidi hata ya wale wanaostahili. Hivyo wakapewa kazi za juu zisizowastahili na wakafanya vizuri na Mungu akawabariki, ijapokuwa ilikuwa ni kinyume na taratibu.

Hata sasa katika kanisa, ni rahisi kuona wenye ngazi za chini, ni wepesi na wenye mioyo ya uaminifu katika nyumba ya Bwana kuliko wale viongozi wa juu. Utaona ni kiongozi wa wakina mama, lakini kwenye maombi haudhurii, kuwafuatilia wanawake wenzake haangahiki. Lakini hapo hapo utaona kabinti kadogo, kanajibidiisha, haachi maombi yapite, anawapigia simu yeye kuwakumbusha kana kwamba ndio kiongozi mkuu, anatoa taarifa za maboresho na changamoto kwa kiongozi wake, mambo  ambayo hata huyo kiongozi hajui.

Sasa katika mazingira kama haya? Unadhani kiongozi ni nani? …Uongozi sio cheo, uongozi ni MOYO, uaminifu na kujitoa. Ikiwa wewe ni mwangalizi, hakikisha huyu aliye na MOYO ndio unampa wajibu na majukumu yote ya uongozi katika nafasi hiyo. Hata kama hajawekewa mikono, au hana uzoefu wowote, au hajatambulika rasmi.

Huyo huyo ndiye Mungu aliyemchagua, hao wengine ni makapi.

Kwani Bwana Yesu alishatangulia kusema maneno haya.

Mathayo 19:30  “Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza”.

Sio kwamba Mungu anao upendeleo.. Lakini alisema.. “ walioalikwa hawakustahili”(Mathayo 22:8).

Halidhalika hata katika ngazi nyingine zote, ikiwa mchungaji msaidizi haipendi kazi yake, usione vibaya, kumpa kazi hiyo shemasi mwenye MOYO wa kuwahudumia watu. Mungu atamtengeneza mwenyewe. Lakini ikiwa wewe ni kiongozi-mlegevu, tubu geuka, ipende nafasi yako, hudumu hapo kwa uaminifu kwasababu umepewa dhamana ambayo utakuja kuitolea hesabu yake siku ile ya hukumu.

Bwana awe nawe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Uadilifu ni nini kibiblia?

Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)

Kwanini Yesu aliwaambia wale wakoma wakajionyeshe kwa makuhani?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zilikuwaje?

Rudi nyumbani

Print this post

UTAJUAJE KAMA WEWE NI MTUMISHI WA MUNGU NA KRISTO YU PAMOJA NAWE?.

(Masomo maalumu kwa watumishi).

Jina la Mwokozi YESU KRISTO Lihimidiwe daima.

Je unajua namna yakujipima kama kweli wewe ni mtumishi wa Mungu na Kristo yu pamoja nawe?

Je unadhani ni ishara na miujiza ndio utambulisho pekee ya kwamba Kristo yu pamoja nawe?

Nataka nikuambie La!..Ishara na mijuiza si uthibitisho wa kwanza wa Kristo kuwa pamoja nawe, kwasababu biblia inasema Yohana Mbatizaji hakufanya ishara hata moja lakini bado alikuwa mkuu kuliko manabii wote waliotangulia.

Yohana 10:41 “Na watu wengi wakamwendea, wakasema, Yohana kweli hakufanya ishara yo yote, lakini yote aliyoyasema Yohana katika habari zake huyu yalikuwa kweli”.

Na pia wapo watakaofanya ishara lakoini atawakana kuwa hawajui…

Mathayo 7:22 “Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”.

Umeona kumbe kufanya ishara au kutofanya si tija!..Si uthibitisho wa kwanza kuwa Kristo yu nawe!.

Sasa ni kipi kinachotupa uthibitsho kuwa tunatembea na YESU katika utumishi tunaoufanya?.

Jibu tutalipata katika maandiko yafuatayo..

Yohana 12:26 “Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu”.

Hapo Bwana mtu akitaka kumtumikia, yani kuwa mtumishi wake BASI AMFUATE!!… Na yeye alipo ndipo na mtumishi wake alipo, au kwa lugha nyepesi “Yeye yupo pamoja na wale waliomfuata”.

Sasa tunamfuata vipi YESU?.

Tusome tena maandiko yafuatayo..

Luka 9:23 “Akawaambia wote, Mtu ye yote AKITAKA KUNIFUATA, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.

24 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha”.

Kumbe ili tuwe watumishi wa kweli wa Mungu, ambao Kristo atakuwa nasi muda wote ni lazima TUJIKANE NAFSI KILA SIKU??.

Sasa swali ni je tumejikana nafsi zetu?au tunazipenda nafsi zetu na kuzishibisha kwa kila tunachokitaka.

Huwezi kumtumikia Mungu na huku hutaki kuacha mila, huwezi kumtumiia Mungu na huku unaupenda ulimwengu.
Huwezi kuwa mtumishi wa Mungu na huku hutaki kuacha mizaha, na wala dhambi.

Huwezi kumtumikia Mungu na bado unaishi na mke/mume asiye wako. Fahamu kuwa Kristo hayupo na wewe hata kama unaona ishara na miujiza katika maisha yako..hiyo ni kilingana na maneno ya Kristo mwenyewe.

Kanuni ya kutembea na Kristo, itabaki kuwa ile ile MILELE! Nayo ni KUJIKANA NAFSI, KUBEBA MSALABA NA KUMFUATA YEYE!. Kwasababu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele (Waebrania 13:8).

Na hiyo ni kwa faida yetu na si yake! (Ayubu 35:7).

Huenda umeshamwamini Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako!.. Hiyo ni nzuri sana, lakini bado haitoshi, ni lazima uongezee hapo “KUJIKANA NAFSI!”. Na baada ya kufanya hivyo pia ujiandae kwa dhiki kwaajili yake.

Jiandae kuchekwa, kudharaulika, kuonekana mshamba, mjinga na usiyejielewa. Usiogope maana hizo ndizo chapa zake Yesu, (Wagalatia 6:17), na wewe sio wa kwanza, zilianza kwa Kristo BWANA WETU NA AKAZISHINDA.

Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

KAMA MTUMISHI WA MUNGU, TAFUTA MAARIFA KWA BIDII.

“Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia;Achukiaye mambo ya dhamana yu salama

Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?

MAHANAIMU (Jeshi la Mungu)!.

Rudi nyumbani

Print this post

JE UNAMHUBIRI KRISTO KATIKA KWELI YOTE?.

(Masomo maalumu kwa watumishi wa Mungu).

Kama Mtumishi wa Mungu je unamhubiri Kristo katika Kweli yote?.

Ni rahisi kutamani na kutafuta Ishara kama njia ya KUU ya Kumhubiri Kristo, lakini nataka nikuambie kama utatafuta ishara halafu umeacha kumhubiri Yesu Kristo katika kweli yote, hiyo kwako ni hasara kubwa sana?

Hebu tumtazame mtu mmoja ambaye hakufanya ishara hata moja lakini alimzungumzia Kristo katika kweli yote na hiyo ikafanya kazi yake kuwa kubwa sana mbele za Mungu,…na mtu huyo si mwingine Zaidi ya Yohana Mbatizaji.

Yohana 10:40  “Akaenda zake tena ng’ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohana akibatiza hapo kwanza, akakaa huko.

41  Na watu wengi wakamwendea, wakasema, YOHANA KWELI HAKUFANYA ISHARA YO YOTE, LAKINI YOTE ALIYOYASEMA YOHANA KATIKA HABARI ZAKE HUYU YALIKUWA KWELI.

42  Nao wengi wakamwamini huko”

Umeona? Yohana hakufanya ishara hata moja, hakutoa pepo, hakuponya mtu kwa jina la Bwana, hakushusha moto kama Eliya ingawa roho ya Eliya ilikuwa juu yake,  wala hakutembea juu ya maji ili watu waone waamini…. lakini Yote aliyoyasema kumhusu Yesu na ujio wake yalikuwa kweli, wala hakudanganya!..  Hivyo hiyo ikamfanya awe Nabii mkuu Zaidi hata ya Musa na Eliya na manabii wengine wote waliotangulia.

Luka 7:26  “Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? NAAM, NAWAAMBIA, NA ALIYE ZAIDI YA NABII.

27  Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako.

28  Nami nawaambia, KATIKA WALE WALIOZALIWA NA WANAWAKE HAKUNA ALIYE MKUU KULIKO YOHANA; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye”.

Huyo ni mtu ambaye hakufanya ishara yoyote! Lakini aliizungumzia Kristo katika KWELI YOTE!.. Kwahiyo kumbe kinachojalisha ni KWELI YOTE na si Miujiza wala ishara, wala umaridadi wala utashi!, bali KWELI YOTE!.

Je wewe kama Mtumishi wa Mungu, unahubiri madhara ya dhambi na hukumu ijayo?, au unahubiri tu mafanikio na kutoa pepo?.. Je unahubiri pia Ubatizo wa maji na wa Roho Mtakatifu au unahubiri tu upendo na faraja?.. Je unahubiri juu ya unyakuo na ziwa la moto, au unahubiri tu Amani?.. Ni Vyema kuhubiri yote pasipo kuacha hata moja, na hapo tutakuwa tumemhubiri Yesu katika kweli yote.

Epuka injili za kubembeleza na kuwastarehesha watu katika dhambi, Yohana Mbatizaji alihubiri na kusema…

Luka 3:7 “Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?

8  BASI, TOENI MATUNDA YAPATANAYO NA TOBA; WALA MSIANZE KUSEMA MIOYONI MWENU, TUNAYE BABA, NDIYE IBRAHIMU; KWA MAANA NAWAAMBIA YA KWAMBA KATIKA MAWE HAYA MUNGU AWEZA KUMWINULIA IBRAHIMU WATOTO.

9  NA SASA HIVI SHOKA LIMEKWISHA KUWEKWA PENYE MASHINA YA MITI; BASI KILA MTI USIOZAA MATUNDA MAZURI HUKATWA NA KUTUPWA MOTONI”.

Bwana Yesu atusaidie.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

NI INJILI GANI UNAHUBIRI?

MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA.

TOFAUTI YA UBATIZO WA YOHANA NA UBATIZO WA BWANA YESU

SAUTI NYUMA YA ISHARA.

NI NINI BWANA ANATAKA KUTOKA KATIKA MUUJIZA ALIOKUFANYIA?

Rudi nyumbani

Print this post

Jinsi ya kuandaa Somo la kufundisha

Jinsi ya kuandaa mahubiri ya kufundisha kanisani au kwenye semina.

Jinsi ya kuandaa mahubiri ya kufundisha kanisani au katika ibada. Zifuatazo ni dondoo chache zitakazoweza kukusaidia katika kuandaa Somo ambalo litakuwa na uvuvio wa Roho Mtakatifu.

1. Tafuta sehemu ya utulivu.

Hii ni hatua ya kwanza kabisa: Tafuta eneo lisilo na kelele, wala usumbufu, hakikisha husumbuliwi na mtu au simu. Hiyo inaweza kuwa katika chumba cha utulivu au mahali ambao hauwezi kusumbuliwa, Huo ni mlango wa kwanza unaouvuta uwepo wa Mungu karibu nawe, kwasababu maandiko yanasema Mungu wetu si Mungu wa machafuko (1Wakorintho 14:33) na pia ni Mungu anayezungumza katika mazingira tulivu.

1Wafalme 19:12 “na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu”.

Hivyo kabla ya kuanza kufikiri kuandaa somo au hubiri, jitenge na mazingira yote yatakayokuondolea utulivu, kwasababu ukikaa katika hayo mazingira hutamsikia Mungu, Hivyo zima simu kwa muda na pia kaa peke yako kwenye utulivu.

2. Kuwa na Kalamu na Karatasi.

Hii ni hatua ya pili: Andaa kalamu na karatasi kwasababu kabla ya kwenda kuwafundisha wengine, Roho Mtakatifu atakufundisha wewe kwanza.

Warumi 2:21  “basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe”

Kwahiyo wewe ni mwanafunzi wa kwanza wa Roho Mtakatifu kabla ya kwenda kuwafundisha wengine, na Mwanafunzi bora ni sharti awe na kalamu na karatasi kwa lengo la kuyarekodi yale anayojifunza. 

Usipokuwa na sehemu ya kurekodi yale utakayoenda kujifunza itakuwa ni ngumu hata kuyashika..

3. Fungua kwa Maombi.

Omba utakaso kwaajili ya nafsi yako, Omba uwepo wa Mungu ushuke mahali hapo, omba utakaso wa eneo ulilopo, omba roho ya ufunuo ishuke juu yako, kemea nguvu za giza na  zinazoshindana na azimio lako hilo (Tumia muda kidogo kuomba kwa kumaanisha).

4. Anza kusoma biblia na kutafakari

Baada ya maombi, anza kusoma biblia huku ukiruhusu akili yako itafakari. Wengi wakifika hii hatua wanafungua tu biblia na kutafuta mistari wanayoifahamu au watakayokutana nayo kwanza, pasipo kuruhusu tafakari katika fahamu zao.

Siri moja ya Roho Mtakatifu ni kwamba anazungumza na sisi pale tunapotafakari na si pale tunapoziba tafakari zetu. Unapokuwa katika kutafakari ndipo Roho Mtakatifu naye anaungana na tafakari zako pasipo kujua na ghafla unajikuta unafunguka akili na kujikuta unapokea vitu vipya, ambavyo ulikuwa huvijui, vitu hivyo vipya ambavyo ulikuwa huvijui vinavyokubaliana na Neno la Mungu ndio sauti ya Roho Mtakatifu, hivyo andiko hivyo ulivyovipokea kwasababu ndio vitakuwa sehemu ya somo lako ambalo Roho Mtakatifu anataka ujifunze wewe kwanza kisha ukawafundishe na wengine.

5. Omba tena

Hii ni hatua ya mwisho, baada ya kusoma na kutafakari kwa muda mrefu, na kupokea Funuo nyingi. Omba maombi ya mwisho ya kushukuru, kisha funga daftari lako.

Darasa lijalo tutajifunza jinsi ya kusimama na kufundisha kile ulichofundishwa na Roho Mtakatifu. Kwani ni muhimu pia kujua jinsi ya kufundisha ili usije ukajikuta unamzimisha Roho. (Kanuni ya kufundisha kwa matokeo yaliyokusudiwa ni rahisi sana, usikose darasa lijalo).

Maran atha

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JE! UPO KATIKA MAJI YA UTULIVU?

NIFANYE NINI ILI MUNGU AYAJIBU MAOMBI YANGU?

Wanikolai ni watu gani? Katika biblia?

JINSI YA KUSOMA BIBLIA.

Guruguru na Goromoe ni wanyama gani? (Walawi 11:30)

Rudi nyumbani

Print this post

Fahamu maana ya Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.

Mafundisho maalumu kwa watumishi wa Mungu (Wachungaji, Mitume, manabii, wainjilisti n.k.)

Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua”

Uongozi wa kidunia mara nyingi hutoa picha ya uongozi wa rohoni.

Kama andiko hilo linavyosema, “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua” maana yake ni kuwa kiongozi anayetawala nchi na huku moyo wake ni wa rushwa, kamwe hilo taifa halitakaa liendelee vile ipasavyo.

Kwamfano, mtu anataka kupitisha bidhaa zisizo na ubora bandarini ili ziuzwe ndani ya nchi. Lakini taarifa zinamfikia kiongozi, badala Yule kiongozi azipige marufuku, anapokea pesa kutoka kwa wale wanaotaka kuingiza, hivyo athari inakwenda kwenye jamii kwa tamaa zake za mali.

Au anaingia mikataba ambayo haina manufaa kwa watu wake, kisa tu kaahidiwa atalipwa pesa nyingi kutoka kwao. Hivyo rushwa zipo nyingi sio tu za kipesa, lakini pia za kiuongozi, kisa Yule ni rafiki, au ndugu, anampa nafasi ya utawala, lakini Yule mwenye ujuzi na ueledi ananyimwa. Sasa taifa lake kiongozi huyu, haliwezi kusimama kwa namna yoyote.

Lakini akiwa ni wa haki (Mtoa hukumu za haki), ni lazima tu nchi hiyo itastawi, Kwasababu maandiko yanasema haki huinua taifa.

Mithali 14:34 ‘Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote’.

Uongozi wa Rohoni.

Vivyo hivyo pia na viongozi wanaongoza kanisa la Kristo ambao kuna watu chini yao wanaowaangalia, katika ngazi yoyote iwe ni Maaskofu, Wachungaji, waalimu, wainjilisti, mitume na manabii. Wakiwa na mioyo ya rushwa ndani yao, kamwe kundi hilo halitathibitika.

Kwamfano, mchungaji anapendelea watu Fulani, anawapa nafasi ya uongozi au anawapa viti vya mbele, kisa tu wanachangia huduma kwa sehemu kubwa, hata kama haiwakidhi wanapewa kisa tu wana fedha nyingi, wanaachwa wale wenye uwezo wa Roho nyuma. Sasa Hiyo rohoni ni rushwa na ni mbaya sana kwa maendeleo ya kanisa.

Yakobo 2:1  Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.2  Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; 3  nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, 4  je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?

Mwingine atauza mafuta, au maji, au chumvi, kisha atasema ni lazima uvinunue ili upokee Baraka zako. Mwingine atasema ili unione mimi nikufanyie maombezi, toa kiwango Fulani, au nikutane na wewe kimwili. Hizo zote ni rushwa za kiroho na zinakuja kwa maumbile mengi sana.

Kunaweza kubuniwa michango ya aina mbalimbali katika kanisa, afadhali lengo lingekuwa ni kwa ajili ya maendeleo ya kazi ya Mungu, lakini unakuta lengo ni ili kiongozi apate fedha ajinufaishe maisha yake.

Mwingine anawachagua viongozi wa kanisani, kindugu, kisa Yule ni mjomba wake, au shemeji yake na kuacha wale walioteuliwa na Mungu.

Yote haya yakiwa ndani ya kiongozi yoyote, ambaye anasimama sio kwa ajili ya kundi bali kwa ajili ya nafsi yake. Kamwe mkusanyiko huo hauwezi kuendelea kiroho. Utazidi kudhoofika, kwasababu umekosa uongozi bora.

Ni vema kujihakiki wewe ambaye umeitwa kulichunga kundi, Maono yako ni nini kwa watu wa Mungu? Je! Ni Uwe tajiri na maarufu kupitia wao? Au ulijenge kanisa la Bwana? Kumbuka utatoa hesabu kwa utumishi wako siku ile ya mwisho, Na kama ukionekana uliwatesa na kuwanyanyasa utakatwa vipande viwili, kisha kutupwa katika ziwa la moto (Mathayo 24:48-51). Na adhabu yako inakuwa kubwa kushinda ya wengine kwasababu ulijua mapenzi ya Bwana wako lakini kwa makusudi hukuyafanya, Hivyo utaadhibiwa sana. Ogopa hukumu ya Mungu. Acha kuiga-iga mifumo ya makristo wa uongo. Tembea katika Neno, kielelezo chako akiwa Kristo ambaye hakuwa na upendeleo wala tamaa ya vitu.

Siku hizi ni siku za mwisho, tubu dhambi zako mgeukie Bwana kwa kumaanisha badili namna ya uongozi wako, simamia haki ya Mungu, uthibitike katika utumishi huo.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Vifungu vya biblia kuhusu Uongozi.

Nini maana ya Mhubiri 10:16, inaposema Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana?

Rushwa inapofushaje macho?

Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako (Mithali 27:23)

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

Bwana alimaanisha nini kusema “Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake”?

Rudi nyumbani

Print this post

Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako (Mithali 27:23)

Haya ni Mafundisho maalumu Kwa ajili ya watumishi, ikiwa wewe ni kiongozi, askofu, mwalimu, mchungaji, mtume, mwinjilisti, unayesimama mahali fulani katika kulitazama kundi la Bwana, au jamii ya watu waliookoka, basi mafundisho haya ni maalumu kwako.

Biblia inasema;

Mithali 27:23

[23]Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako;  Na kuwaangalia sana ng’ombe zako.

Mchungaji Bora sikuzote anatambua ni wajibu wake kuwa karibu na mifugo yake wakati mwingi. Ili Kuhakikisha Mahali wanapolala ni salama, wanaogeshwa Kila wakati, wanapata chakula Bora, afya zao pia ni njema na wanachungwa Mahali salama.

 Kwamfano kama mchungaji akiwa Hana desturi ya kwenda zizini. Tunajua mifugo Kwa kawaida Huwa Haijui kujisafisha yenyewe, matokeo yake ni kwamba lile zizi litajaa vinyesi na mwisho wa siku watapata magonjwa na kufa, na hasara inaangukia kwa mchungaji?

Vilevile akiiachia mifugo yake ianze kujichunga yenyewe, inaenda popote iwezavyo kujitafutia chakula, bila shaka itapotea, kama sio kuibiwa, au kuliwa na wanyama wakali, au kula vitu visivyostahili.

Hivyo utaona ni sharti Mahali palipo na mifugo, hapapaswi kukosekana mchungaji hata kidogo. Hii inatufundisha sisi tulio watumishi, kuhakikisha tunafahamu Hali mbalimbali za watu wale tunaowaongoza.

Tunawajibu wa kuwapa chakula kizuri kitakachowakuza (yaani Neno la Mungu lisiloghoshiwa), tuna wajibu wa kuwalinda kiroho, dhidi ya mafundisho potofu na mitego ya ibilisi, Kwa kuwaonya na kuwakemea pale inapobidi wavukapo mipaka.

Tuna wajibu wa kuwaombea, tunawajibu wa kuwafariji na kuzijali Hali zao za mwilini katika maisha Yao ya kawaida.

Hivyo wewe kama kiongozi ikitokea upo mbali na kundi lako, usikawie sana, ukaliacha kundi lako ma-miezi na ma-miaka,bila kujua maendeleo yao, ukadhani kwamba litaweza kujichunga lenyewe, hiyo ni hatari..ni heri uwe mtu wa kwenda na kurudi, kwenda na kurudi… lakini pia ukiwa karibu nalo usiwe mlegevu kupeleka jicho lako Kila eneo la maisha Yao ya kiroho na ya kimwili, kuangalia ni wapi Pana mapungufu au  shida..ili kuondoa kasoro hizo, Ili kundi la Bwana listawi kama vile yeye atakavyo.

Ndio maana ya hili andiko Mithali 27:23 “Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako;  Na kuwaangalia sana ng’ombe zako”.

Ni wajibu wako kufanya hivyo, kwa hiari yako mwenyewe na sio kama unalazimishwa;

1 Petro 5:2

[2]lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

LISHA KONDOO WANGU, LISHA WANA-KONDOO WANGU.

USINIPE UMASKINI WALA UTAJIRI. (Mithali 30)

Kwanini Nuhu alimlaani Kaanani badala ya mtoto wake Hamu,

EPUKA MAKUNDI ILI UTAKATIFU WAKO UDUMU!.

FANYA KAMA UONAVYO VEMA.

ZIJUE TABIA ZA AHADI ZA MUNGU KWA MWAMINIO.

Rudi nyumbani

Print this post

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

Mafundisho maalumu Kwa ajili ya watumishi wa Mungu.

Huu ni mwendelezo wa mafundisho maalumu Kwa ajili watumishi wa Mungu, ikiwa wewe ni Mchungaji, mwalimu, mtume, askofu,Nabii, au mtu yoyote unayemtumikia Mungu katika nafasi yoyote kanisani au kwenye huduma basi mafundisho haya yatakufaa sana.

Wakati ule Yakobo alipodhamiria kwenda kukutana na ndugu yake Esau baada ya kutengana naye Kwa muda mrefu..maandiko yanasema walifurahi sana walipoonana kule nyikani. Na baada ya mazungumzo Yale kuisha,  sasa ikiwa ni wakati wao wa kuondoka pale nyikani walipokutana waelekee Kaanani.

Na kama tunavyosoma habari tunaona ndugu yake Esau alimshurutisha wasafiri pamoja naye. Ndipo Yakobo akamwambia Esau kuwa jambo hilo ni gumu kwake..kwasababu ya Hali ya makundi mbalimbali na watu na mifugo aliyokuwa nayo..Tusome..

Mwanzo 33:12-17

[12]Kisha Esau akamwambia, Twende zetu, tusafiri, nami nitakutangulia.

[13]Akamjibu, Bwana wangu anajua ya kuwa watoto ni wachanga, tena kondoo na ng’ombe nilio nao wanyonyesha. Hao wanyama wakiharakishwa siku moja, watakufa wote.

[14]Tafadhali bwana wangu na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole kwa kadiri ya mwendo wa wanyama walio mbele yangu, na kwa kadiri ya mwendo wa watoto, hata nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri.

[15]Esau akasema, Nikuachie, basi, baadhi ya watu walio pamoja nami. Akasema, Pana haja gani? Na nione kibali tu machoni pa bwana wangu.

[16]Basi Esau akarudi siku ile ile akishika njia yake mpaka Seiri.

[17]Yakobo akaendelea mpaka Sukothi. Akajijengea nyumba, akawafanyia makundi yake vibanda. Kwa hiyo jina la mahali pale pakaitwa Sukothi.

Ni nini cha kujifunza hapo?

Yakobo alilitambua kundi analolichunga, alijua kuwa wapo watoto wachanga ndani yake, na mifugo pia michanga, Ambayo haijazoezwa kupelekwa mkiki mkiki, kwani ikilazimishwa kufanywa hivyo itakufa yote njiani. Hivyo akaomba muda wa kusafiri wake uongezwe, kusudi kwamba ayakokote taratibu taratibu mpaka yatakapofika kule Shekemu alipokuwa anapakusudia. Pengine mwendo wa siku moja tu ikamgharimu mwezi.

Tofauti na Esau yeye alikuwa na watu wa vita tu,watu walio hodari, Lakini Yakobo alikuwa na makundi yote. Na hivyo kwenda nayo taratibu taratibu ilimgharimu .

Hii ni kutufundisha asili ya msimamizi wa kweli, kwanza hulijali kundi lake, pia anakuwa tayari kuchukuliana na vile vyombo dhaifu. Kwasababu sio wote katika kanisa watakuwa na mwendo kama wa kwao, SI wote watakuwa wepesi kustahimili vishindo kama baadhi yao. Hivyo wewe kama kiongozi ni lazima ujifunze kuendana na makundi yote kama Musa kule jangwani, ili kisipotee chochote. Maana yake ni kuwa usiwe na haraka ya kufikisha kundi Mahali Fulani Kwa jinsi utakavyo, vinginevyo utawaua wengine.

Yakobo alipaita mahali pale Sukothi, kwasababu ndipo alipowajengea makundi yake vibanda. Na wewe pia jenga Sukothi yako.

Bwana akubariki.

Shalom

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

LISHA KONDOO WANGU, LISHA WANA-KONDOO WANGU.

TOFAUTI YA MITUME, MANABII, WAINJILISTI, WACHUNGAJI NA WAALIMU NI IPI?

Mtu asiye na akili ni nani kibiblia?

MAFUNDISHO YA NDOA.

MIGAWANYO MINNE (4), YA HUDUMA YA YESU.

Je! Mwendo wa Sabato ulikuwaje kibiblia?(Matendo 1:12)

Rudi nyumbani

Print this post

NI INJILI GANI UNAHUBIRI?

Masomo maalumu kwa watumishi wa Mungu (Wahubiri).

Je umebeba ushuhuda gani katika injili yako?.

Tujifunze jambo kwa Yohana Mbatizaji..

Yohana 10:40 “Akaenda zake tena ng’ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohana akibatiza hapo kwanza, akakaa huko.

41  Na watu wengi wakamwendea, wakasema, yohana kweli hakufanya ishara yo yote, LAKINI YOTE ALIYOYASEMA YOHANA KATIKA HABARI ZAKE HUYU YALIKUWA KWELI.

42  Nao wengi wakamwamini huko”.

Hapo maandiko yanasema Yohana hakufanya ishara yoyote kama alivyofanya Musa katika hatua ya kuwahubiria ukombozi wana wa Israeli, au kama alivyofanya Eliya aliposhusha moto, au kama alivyofanya Eliya na manabii wengine..

Lakini Yohana yeye tunasona alibeba kitu kingine cha ziada.. Na kitu hicho ni “USHUHUDA WA KWELI WA YESU”. Na ndicho kilichomfanya aonekane mbele za Mungu kuwa mkuu kuliko manabii wote waliotangulia..

Mathayo 11:9  “Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na ALIYE MKUU ZAIDI YA NABII.……

11  Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa WANAWAKE ALIYE MKUU KULIKO YOHANA MBATIZAJI; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye”.

Kwahiyo kumbe kinachojalisha si miujiza?, si ishara, si maajabu tunayoyatenda.. bali ni kile tunachokihubiri kumhusu Yesu?.. Je kina ukweli?.. na kama kina ukweli, je ni katika kiwango gani?

Yohana alianza kuhubiri habari za Toba na ondoleo la dhambi na kusema Ufalme wa Mungu umekaribia wamwamini yeye ajaye.

Mathayo 3:1 “Siku zile aliondokea Yohana Mbatizaji akihubiri katika nyika ya Uyahudi, na kusema,

Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”.

Injili ya namna hii ndiyo Bwana Yesu aliyoanza kuihubiri pia…

Mathayo 4:17 “Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”.

Umeona injili ya Yohana iliyovyofanana na ya Bwana?..Yohana aliuona ushuhuda wa Yesu na akauhubiri kabla hajaja, aliona hizi ni nyakati za kutubu na kumrudia Mungu, kwasababu ufalme wa Mungu umekaribia!!.. .

Vile vile hakuanza kuwaambia watu watubu halafu baadaye waendelee na dhambi zao, bali aliwaambia watubu na baada ya hapo wazae matunda yapatanayo  na toba zao, wala wasijisifie dini, wala madhehebu.. Maana yake baada ya kutubia uzinzi ni lazima waishi maisha ya usafi baada ya hapo, kama umetubia ulevi ni lazima wauache ulevi, kama wametubia ukahaba ni lazima wauache ukahaba na vifaa vyote vya ukahaba, ikiwemo mavazi!..(hiyo ndio maana ya kuzaa matunda yapatanayo na toba).

Luka 3:7 “Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?

8  Basi, TOENI MATUNDA YAPATANAYO NA TOBA; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto.

9  Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; BASI KILA MTI USIOZAA MATUNDA MAZURI HUKATWA NA KUTUPWA MOTONI”.

Injili ya namna hii ndiyo iliyobarikiwa na Bwana Yesu, na ndiyo iliyochaguliwa kuwa NJIA KWAAJILI YA BWANA!, Na ndiyo  iliyomfanya Yohana awe mkuu kuliko manabii wote ingawa hakufanya muujiza wowote.

Je! Na wewe kama mtumishi wa Mungu unahubiri nini? Je unahubiri mambo ya ulimwengu huu au injili ya ufalme wa Mbinguni??..  Injili yako ni ya magari na majumba na pesa?..

Kumbuka Injili ya ufalme wa mbinguni ni ile ile haijabadilika ambayo ni “kutubu na kuzaa matunda yapatanayo na toba kwamaana ufalme wa mbinguni umekaribia” Huo ndio ushuhuda wa Yesu na ndio roho ya unabii.

Ufunuo 19:10b “….. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii”.

Vile vile usikimbilia kutafuta au kutengeneza miujiza, usitumie nguvu nyingi kutafuta maajabu… bali tafuta kwanza Ushuhuda wa Yesu, ukiupata huo utakuwa umepata muujiza mkubwa sana katika utumishi wako!.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

TOFAUTI YA UBATIZO WA YOHANA NA UBATIZO WA BWANA YESU

WAKO WATATU WASHUHUDIAO MBINGUNI NA DUNIANI.

IJUE HEKIMA YA MUNGU KATIKA KUKUINUA KIMAISHA.

JE UMEKUFA PAMOJA NA NANI?

Rudi nyumbani

Print this post