FAHAMU MAISHA YA YESU KABLA YA HUDUMA.

FAHAMU MAISHA YA YESU KABLA YA HUDUMA.

Jina la mwokozi wetu Yesu Kristo litukuzwe milele na milele. Nakualika Tena wakati huu tujifunze maneno ya uzima wa Roho zetu.

Wengi wetu tunavutiwa na maisha ya Yesu alipoanza huduma, tunafurahishwa na jinsi alivyokuwa anafanya miujiza mikubwa, alivyokuwa anahubiri kwenye miji na vijiji, alivyokuwa anaponya wagonjwa,kutoa Pepo na kufufua wafu n.k.

Lakini ni Wachache sana wanaweza kuyatafakari maisha ya Yesu kabla ya huduma. Na hayo ndio Yana umuhimu sana kwetu kuliko Yale aliyoyadhihirisha baadaye.

Maandiko yanasema Yesu alimpendeza Mungu kabla hata hajaanza huduma yoyote ya kuhubiri, kutoa Pepo, na kuokoa watu…alishampendeza Mungu kabla ya hayo yote, tunalithibitisha hilo katika kitabu Cha Mathayo 3 siku Ile anabatizwa na Yohana, 

Mathayo 3:16-17

[16]Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake;

[17]na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.

Umeona alishampendeza Mungu kabla hata ya utumishi wowote, kuanza..tofauti na Leo tunavyodhani kwamba ili tumpendeze Mungu, ni sharti tuwe wahubiri wakubwa, au tuwe na upako, au tuwe wachungaji..hiyo sio kanuni ya Mungu.

Hivyo ni lazima tujue Mungu alipendezwa na Yesu kwa kipi? Ni kitu gani alikuwa anafanya mpaka kimfanye akubaliwe na Mungu namna Ile?

JIBU lipo katika Maisha aliyokuwa anaishi Kwa ile miaka 30 kabla ya huduma. Na hapa ndipo tunapaswa tupaangalie sana. Na tujifunze ili na sisi tufanane naye.

Watu wengi wanaona kama maisha yake ya awali yalifichwa sana, zaidi ya Yale aliyoyatenda katika huduma. Ni kweli ukitazama Kwa jicho la nje sehemu kubwa ya injili imeandika juu ya huduma ya Yesu, yaani ile miaka mitatu na nusu ya mwisho ya maisha yake. Lakini ukweli ni kwamba maisha ya Yesu kabla ya huduma ndio yameandikwa kwa wingi zaidi kuliko Yale aliyoyafanya katika huduma.

Hivyo Kwa neema za Bwana tutaona  juu ya maisha yake yalikuwaje, tangu utotoni mpaka anakaribia kuanza huduma.

Sehemu ya kwanza tutaona Mahali ambapo maandiko yameeleza moja Kwa moja maisha yake yalivyokuwa. Na sehemu ya pili tutaona maandiko ambayo sio ya moja Kwa moja, lakini yalimwelezea Yesu maisha yake.

Tukianza na maandiko yanayoeleza moja Kwa moja juu ya maisha yake. Kama yafuatavyo;

1) YESU ALIISHI MAISHA YA KUMPENDEZA MUNGU PAMOJA NA WANADAMU.

Luka 2:52

[52]Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Maisha yake yote alikuwa ni mtu mwenye bidii sana kuhakikisha hafanyi jambo lolote ambalo ni kinyume na mapenzi ya Mungu. Alikuwa yupo makini sana na hilo, lakini zaidi sana alihakikisha katika jamii hawi na harufu mbaya. Alizingatia kuwa na adabu na heshima Kwa Kila mtu aliyekutana naye.

Si ajabu watu walipomuona walimsifia sana, na kusema yule kijana anaheshima, yule kijana ni mtaratibu, natamani watoto wangu wangekuwa kama yule, hatumuoni kwenye kampani za wahuni, hatumuoni akiruka ruka na mabinti barabarani, hatumuoni akitembea Kwa majigambo barabarani, muda wote anatabasamu, hakasiriki haraka, anahekima kama za mtu mzima wakati bado ni kijana..

Yesu alipata sifa isiyo ya kawaida katika jamii, alipoishi duniani, hakuna mtu alimchukia Kwa Tabia zake, alijitoa kwelikweli kuishi kikamilifu katika jamii yake.

Na sisi pia hichi ndio kitu Mungu anataka kukiona katika maisha yetu tunapookoka kabla hata ya kufikiria kuwa wahubiri ,je  mtaani kwako unaonekanaje, shuleni kwako Tabia zako zikoje? Mwonekano wako unawavutiaje watu, ofisini kwako kauli zako na wanyakazi wenzako Zina mvuto gani mpaka watu wakuone wewe ni mtu Bora kuliko wengine wote?

2) YESU ALIKUWA MTIIFU

Luka 2:51

[51]Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.

Aliwatii wazazi wake, hakukuwa na kiburi ndani yake, Neno utiifu kwa Yesu lilikuwa ni kama pumzi kwenye mapafu. Alipoagizwa alifanya, alipotumwa alikwenda, maisha yake yalikuwa ni ya namna hiyo, ili kutunza hadhi yake aliyokuwa nayo ya kuwapendeza watu wote..

Na sisi je tunaweza tukawa watiifu Kwa wazazi wetu wa kimwili na wa kiroho? Tuwatii viongozi wetu wa kiroho hata kama tutakuwa tunafahamu jambo Fulani zaidi ya wao, maadamu Bwana katuweka chini Yao.Hatuna budi kufanana na Yesu. Bwana atusaidie juu ya hilo.

3) ALIPENDA KUKAA NYUMBANI MWA BABA YAKE

Hii ni sifa nyingine inayomwelezea Yesu Tabia yake.

Luka 2:41-49

[41]Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka.

[42]Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu;

[43]na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari.

[44]Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao;

[45]na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta.

[46]Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.

[47]Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake.

[48]Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.

[49]Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?

Akiwa kijana mdogo wa miaka 12, hakujali atakula nini, atalala wapi, ataoga wapi..alinogewa na ibada na mafundisho hekaluni akaona hata ule muda wa sikukuu hautoshi yeye kukata kiu yake Kwa Mungu, akaendelea kubaki palepale siku tatu, akiwa amefunga, yeye ni kujifunza tu, na kuyatafakari maneno ya Baba yake..

Wazazi wake hawakujua kuwa angekuwa na kiu Kali namna ile, lakini baada ya pale walimzoea, ikawa ndiyo desturi ya maisha yake yote.

Yesu alikuwa ni mtu asiye mtoro wa ibada, alikuwa anatumia majira yake mengi, kwenda kwenye masinagogi na kutafakari Neno la Mungu pamoja na viongozi wake wa kidini. Hakuwa mtu wa kujitenga Tenga, kama watu wanavyodhani.

Lakini pia alikuwa ni jemedari wa maombi kweli kweli na Dua.

Alikuwa anaomba sana Kwa bidii, Kwa kulia na machozi sana, na kwa kujimimina sana. Maandiko yanasema hivyo;

Waebrania 5:7

[7]Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;

Na sisi je tunaweza tukaiga Tabia hii ya Bwana. Je! Furaha yetu ni kuwepo uweponi MWA Bwana muda mwingi au kuwepo katika anasa za Dunia? Au katika biashara zetu? Ni lazima Bwana apewe kipaumbele Cha kwanza.

4) YESU ALIISHI MAZINGIRA YA KUFANYA KAZI

Pamoja na kuwa alikuwa ni mtiwa mafuta wa Bwana ameandaliwa Kwa kusudi moja tu la kuwaokoa watu. Lakini kipindi anasubiri wakati wa Bwana, hakukaa hivi hivi tu, Mungu aliruhusu afanye kazi.

Marko 6:3

[3]Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake.

Yesu hakuwa kama Yohana mbatizaji, Kukaa majangwani mbali na watu muda wote, lakini alikuwa ni mtu ambaye yupo katikati ya jamii, anayejulikana, anafahamika, alifanya kazi pamoja na baba yake ya useremala. 

Kwasasa tunaweza kusema alikuwa kariakoo akiuza vifaa vya majumbani na baba yake.

Lakini katika hayo yote aliishi maisha makamilifu ya kujichunga na kuwa na kiasi. 

Hii ni kutuonyesha kuwa unapookoka, uwapo popote pale iwe ni kazini, au kwenye biashara Yako, bado unaweza kumpendeza tu Mungu. Hivyo tusiruhusu kazi ziwe kisingizio cha sisi kutoishi maisha makamilifu. Yesu alikuwa ni mtu wa kujichanganya, lakini hakuruhusu dhambi iwe juu yake. Alipouza kabati hakukwepa kulipa Kodi, hakumuuzia mtu meza Kwa bei isiyoendana na thamani yake.  Hivyo ikampelekea Mungu ampende sana

Hayo ni maandiko ya moja Kwa moja yanayoeleza maisha ya Yesu yalivyokuwa.

Lakini maandiko mengine tunayapata wapi?

JIBU ni kuwa tunayapata katika kinywa Cha Yesu mwenyewe. Kwa kawaida mtu hawezi kusema maneno ambayo yeye hayaishi. Vinginevyo atakuwa ni mnafki, na Yesu yupo mbali sana na unafki, aliukemea sana, hata alipouona ndani ya mafarisayo na waandishi,walipowafundisha watu mambo ambayo wao hawayaishi.(Mathayo 23:1-5)

Hivyo ukitaka kufahamu Kwa kina maisha ya Yesu yalikuwaje sikikiza maagizo yote aliyokuwa anayatoa katika vitabu vyote vya injili.

Kwamfano. Mathayo soma sura yote ya 5-7 utaona maneno kadha wa kadha aliyokuwa anawafundisha makutano.

Anasema wapendeni adui zenu na kuwaombea(Mathayo 5:43-44): Yesu alikuwa anawaombea watu wote waliokuwa wanamchukia Kwa kumwonea wivu. Badala ya kuwatakia mapigo anawatakia maisha marefi, kuwaombea toba wageuzwe.

Anasema mtu akupigaye shavu la kuume mgeuzie la kushoto(Mathayo 5:38-40). Kuonyesha kuwa hakuwa mtu wa Shari, sikuzote alipotukanwa, au alipoaibishwa hakurudisha majibu, Bali alikubali kuaibishwa zaidi, ili aipushe malumbano zaidi.

Anasema amtazamaye mwanamke Kwa kumtamani amekwisha kuzini naye(Mathayo 5:28). Hakuwa na uvumilivu na macho yake, hakuwahi kuruhusu tamaa itawale maisha yake. Alijitenga na vichocheo vyote vya uzinzi, na mazungumzo yote yasiyofaa.

Alikuwa ni mtu wa kusamehe mara Saba sabini, hakuwa anawahukumu watu, au kuwalaumu(Mathayo 7:1-4)

Alikuwa si mtu wa kuruhusu hasira, aliona ukiwa hivyo adhabu Yako inakupasa ziwa la moto (Mathayo 5:21).

Bado alijishuhudia kuwa yeye ni mpole na mnyenyekevu (Mathayo 11:29), aliishi Kwa kujishusha, bila kumdharau yoyote, watu wote walikuwa na nafasi sawa kwake..

Na maandiko mengine mengi, aliyotuelekeza. Hivyo itoshe kusema maisha ya Yesu yaliyomfanya Mungu ampende kabla hata ya huduma ndiyo haya tunayoyasoma katika vitabu vya injili…

Hivyo ndugu Mimi na wewe yatupasa,. Tufikie hapo, acha kumuomba Mungu upako. Utakuja wenyewe tu endapo utampendeza Mungu kwanza kama Bwana Yesu, ukiwa unauhitaji. Penda mema chukia maasi..ndivyo Yesu alivyokuwa hapa duniani, hakuivumilia dhambi kwa namna yoyote, na matokeo yake Bwana akamtia nguvu kuliko mwanadamu yoyote aliyewahi kutokea hapa duniani.

Waebrania 1:9

[9]Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio.

Bwana atusaidie sasa tuishi kama Kristo, ili baadaye tutende kama Kristo.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa >> WHATSAPP-GROUP

Mada Nyinginezo:

Ni kweli hakuna mtu aliyewahi kuuona uso wa Mungu Zaidi ya Bwana Yesu?

Kibiriti ni kitu gani? kama kinavyozungumziwa kwenye maandiko?

Nini maana ya Ukuta uliopakwa chokaa (Matendo23:3)?

FANYA MAAMUZI KABLA HAZIJAKARIBIA SIKU ZA HATARI.

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

MAUMIVU  NYUMA-YA-HUDUMA.

WITO WA MUNGU

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments