FANYA MAAMUZI KABLA HAZIJAKARIBIA SIKU ZA HATARI.

FANYA MAAMUZI KABLA HAZIJAKARIBIA SIKU ZA HATARI.

Mhubiri 12: 1 “MKUMBUKE MUUMBA WAKO SIKU ZA UJANA WAKO, KABLA HAZIJAJA SIKU ZILIZO MBAYA, Wala HAIJAKARIBIA MIAKA utakaposema, MIMI SINA FURAHA KATIKA HIYO”.

Biblia inasema “Mkumbuke” ikiwa na maana kuwa ni wakati ambao kuna “kusahau” wakati wa kupumbazwa na mambo mengi, …Na huo wakati si mwingine zaidi ya wakati wa UJANA. Na biblia inasema pia zitakuja nyakati au siku zilizo mbaya, ambazo zitakuwa sio za furaha, nyakati zisizofaa tena kumgeukia yeye,..

Tafakari kwa makini hiyo sentesi “Mkumbuke muumba wako kabla hazijaja siku !!” Ina maana sio kila wakati unafaa katika kumgeukia Mungu..Ni rahisi kusema nitakapokuwa MZEE nitamgeukia Mungu, au nitakapofikia kipindi Fulani au nitakapokuwa nimezidiwa sana, au nitakapokuwa nimefilisika sana, au nitakapokuwa katika ugonjwa wa kufisha, au siku nitakayokaribia kufa ndiyo nitakuwa karibu na Mungu. Ndugu hiyo ni hatari sana neema ya Mungu haiotewi. yeye anasema “mkumbuke Muumba wako kabla hazijaja siku zilizo mbaya”..zingatia hilo neno kabla!! Kabla!!,.Kumbuka Wengi wanaopata Neema ya kuokolewa katika hizo nyakati zilizo mbaya ni wale tu ambao hawajawahi kabisa kuisikia injili hapo nyuma, mfano wa Yule muhalifu aliyesulibiwa na Kristo pale Msalabani. Hivyo usiliweke hilo akilini kwa sisi wa kizazi hiki ambacho injili ya Kristo inahubiriwa kila siku barabarani lakini hatutaki kusikia au tunapuuzia tukitumaini itafika siku tu tumtafuta Mungu..Hilo tuliondoe akilini.

SASA HIZO SIKU ZILIZO MBAYA(au siku za matatizo) NI ZIPI? AMBAZO TUMEONYWA TUMKUMBUKE MUUMBA WETU KABLA HAZIJAFIKA??

Ukizidi kusoma mistari inayofuata utaona hizo siku siku mbaya zinazozungumziwa hapo ni zipi. Ukiwa na nafasi binafsi utasoma, sura yote ya 12,lakini kwasasa tutaangalia vipengele hivyo vikuu.

1)KABLA JUA, NA NURU, NA MWEZI, NA NYOTA, HAVIJATIWA GIZA; (Mhubiri 12:1-14)

Hapo anazungumzia siku ya Bwana inayotisha, ambayo ipo mbioni kuijilia dunia nzima,.Biblia inasema tumkumbuke Bwana kabla hiyo siku haijafika, siku ambayo Jua litatiwa giza, na mwenzi hautatoa nuru yake, na nyota za mbinguni zitakapoanguka…Siku ya kutisha ya hasira ya Mungu mwenyezi.

Amosi 5: 18 “Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya Bwana; kwani kuitamani siku ya Bwana? NI GIZA, WALA SI NURU.

19 Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma.

20 Je! SIKU YA BWANA HAITAKUWA GIZA, WALA SI NURU? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga” 

Amosi 8: 9 “Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya JUA LITUE WAKATI WA ADHUHURI, NAMI NITAITIA NCHI GIZA WAKATI WA NURU YA MCHANA.

10 Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu.”

Unaona sisi watu wa kizazi hichi, tunaishi karibu na siku hizo, mambo yote yanathibitisha hilo, siku yoyote mwisho unafika, kwani katika kalenda ya kibiblia tunaishi katika kanisa la mwisho linalojulikana kama Laodikia (Ufunuo 3).Na ndio kanisa hilo litakaloshuhudia mambo yote. Unyakuo pamoja na dhiki kuu.

2) KABLA YA KURUDI MAWINGU BAADA YA MVUA; (Mhubiri 12:2)

Kabla ya kurudi mawingu baada ya Mvua, inafunua “kipindi cha njaa kuanza” Kama vile Farao alivyoambiwa na Bwana itakuja miaka 7 ya neema, ya mvua tele na kisha baada ya hiyo itaanza miaka mingine 7 ya njaa, isiyokuwa na Mvua, kupanda wala kuvuna. Ndio kitu kile kile Biblia inachokizungumzia hapa, kwamba baada ya mvua mawingu yatarudi na kuanza vipindi vya njaa, Biblia inatabiri pia siku za mwisho Bwana ataleta njaa juu ya nchi, si njaa ya chakula bali njaa ya KUKOSA KUYASIKIA MANENO YA MUNGU.

Amosi 8: 11 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.

12 Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.

13 Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu”.

Neno la Mungu linatuonya TUMKUMBUKE MUUMBA WETU KABLA HIZO SIKU HAZIJAFIKA, Na hizo siku zimeshaanza kujitokeza duniani…Tunaona sasa Njaa ya Neno la Mungu imeanza kuongezeka..

3) KABLA HAIJAKATIKA KAMBA YA FEDHA; (Mhubiri 12:6)

Kabla ya uchumi wako binafsi kuanguka, Unaona hapo?? usiseme siku nitakapoishiwa fedha au nitakapokuwa naumwa sana ndipo nitakapomgeukia Mungu, au siku nitakapokaribia kufa..Bwana hadhihakiwi, yeye anasema TUMKUMBUKE KABLA HIZO SIKU HAZIJAFIKA, ikiwa na maana kuwa kama tutamkataa leo kwa makusudi tukiwa katika hali nzuri, hatakuwa na sisi wakati wa matatizo. Tukimkana leo yeye wakati wa ujana wetu, na yeye atatukana sisi wakati wa matatizo yetu, kumbuka Watakaompata katika hali za matatizo ni wale tu ambao hawakuwahi kuisikia injili hapo kabla, lakini kama ulishawahi kuisikia na unaipuuzia hakutakuwa na nafasi ya pili wakati matatizo yatakapokukumba.

4) KABLA MAVUMBI KUIRUDIA NCHI KAMA YALIVYOKUWA, NAYO ROHO KUMRUDIA MUNGU ALIYEITOA. (Mhubiri 12:7)

Biblia inasema katika Waebrania 9:27 “MTU AMEANDIKIWA KUFA MARA MOJA NA BAADA YA KIFO HUKUMU”..Ndugu, hakuna maombi yoyote yanayoweza kumsaidia mtu baada ya kufa, Mafundisho ya Toharani hayapo katika biblia takatifu, ni mafundisho ya Yule mwovu, ili kuwafariji watu kuwa baada ya kufa unaweza ukaombewa na ukatolewa katika maumivu ya moto, hakuna kitu kama hicho, baada ya kifo ni hukumu ndivyo Neno linavyosema, ndio maana hapa Bwana anatuonya

“mkumbuke Muumba wako kabla roho yako haijamrudia yeye” ikiwa na maana kuwa baada ya kufa hakuna nafasi yoyote ya kumgeukia Mungu, au kuokoka na lile ziwa la Moto, kama ulimkataa yeye katika enzi za uhai wako.

Ujana wako unaweza usiwe tu ujana wa mwili wako, bali hata ujana wa akili yako, Na ujana wa akili yako ndio huu, ambao unaweza ukapata nafasi ya kusikiliza Neno la Mungu, Siku ile hutasema hukusikia, Leo hii mkumbuke Muumba wako, kabla ya siku za matatizo kufika, kabla ya vipindi vya njaa, shida, mauti, kabla ya kurudi kwa pili kwa Kristo, kabla ya Mpinga-Kristo kunyanyuka, kabla ya siku ya ghadhabu ya Mungu kumiminwa, uukumbuke msalaba, usiwe miongoni mwa hao wanaodhihaki ambao biblia inasema “Mungu amewaletea nguvu ya upotevu” wauamini uongo ili wapotee. Ujana wako unautumiaje?, nguvu zako unampa nani?.

Biblia inasema nimewaandikia ninyi vijana kwasababu mna nguvu ya kumshinda shetani, hii ikiwa na maana kuwa utafika wakati hizo nguvu hutakuwa nazo za kumpinga shetani maisha mwako kama hutakuwa ndani ya Kristo. Embu jaribu kifikiria unapata faida gani leo unavyoishi katika hayo maisha ya dhambi?. Huoni kama upo katika hatari kubwa sana. Tubu angali bado upo katika siku njema, siku za neema, siku ambazo bado hazijawa mbaya, tuipishe ghadhabu ya Mungu ambayo hivi karibuni inakwenda kumiminwa katika dunia nzima.

Ni maombi yangu kuwa Bwana atakujali kufanyika kiumbe kipya.

Tafadhali “share” kwa wengine, 

Ubarikiwe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

CHUKIZO LA UHARIBIFU

JE! WEWE NI MWANA WA IBRAHIMU?.

UMUHIMU WA KUZALIWA MARA YA PILI.

JIRANI YAKO NI NANI?

UMUHIMU WA KUISHI MAISHA YAMPENDEZAYO MUNGU SASA.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments