UMUHIMU WA KUZALIWA MARA YA PILI.

UMUHIMU WA KUZALIWA MARA YA PILI.

Ili kuelewa uzito wa Neno hili “KUZALIWA MARA YA PILI”, Ni vizuri tukarejea katika maisha ya kawaida kujifunza vitu gani vinaambatana na kuzaliwa kwa mtu. Mtu kabla hajazaliwa sehemu kubwa ya maisha yake yanakuwa yameshaandaliwa na vizazi vilivyomtangulia ni machache sana ambayo atakuja kuyaongeza yeye mwenyewe atakapozidi kukua, lakini asilimia kubwa mambo yake yanakuwa yameshakamilika.Na ndio maana inakuwa rahisi kumtabiri mtu atakuja kuwa wa namna gani kabla hata hajazaliwa.

Kwamfano wewe kabla  hujazaliwa ndugu zako walishajua kabisa utakuja kuwa mwafrika mwenye rangi nyeusi, na nywele za katani, na sio mchina au mzungu! na ndivyo ilivyokuja kuwa baada ya kuzaliwa kwako, hivyo hawakushangaa kukuona wewe uko jinsi ulivyo leo. Lakini Kwanini hawakustaajabia kukuona hivyo, ni kwasababu mababa zako na wenyewe wako hivyo hivyo kama wewe,

Kadhalika kama jamii yenu ni watu warefu au wafupi, ni rahisi watu kutabiri kimo chako kabla hata hujazaliwa. Pia Kama familia yenu ni ya kifalme, ni rahisi watu kutabiri kuwa utakuwa mfalme kabla hata hujazaliwa..na siku utakapokuwa mtu mzima na kuwa mfalme hawatastaajabia kukuona wewe hivyo. 

Ni kwasababu gani?. Jibu ni kwamba wameweza kusoma ukoo wako, na kuangalia tabia za mababa zako na mwenendo wao, na vyeo vyao wakaweza kuhitimisha maisha yako yatakavyo kuja kuwa. kadhalika na vitu kama majina,mtu kabla hajazaliwa watu wataishiakumuita majina ya ukoo kama Massawe, Wambura, Lema, Laiza,  n.k. ni kwasababu gani?. Jibu ni kwasababu ni lazima aje kuyarithi kutoka kwa mababa zake, Vivyo hivyo kama mababa wana magonjwa fulani ya kurithi, au tabia au laana fulani ni rahisi kutabiri hali ya mtoto atakayezaliwa itakuwaje mbeleni.

Tukirudi katika mambo ya rohoni kuna kuzaliwa pia mara ya pili. Na ukishazaliwa mara ya pili moja kwa moja unaingizwa katika ukoo husika ambao utakufanya urithi kila kitu kinachohusiana na ukoo huo. Kuanzia jina, tabia, cheo, mwenendo n.k.

Ukiamua leo hii kwa moyo wako wote kujiunga na Dini ya UBUDHA, kwa kufata taratibu zao walizokuwekea moja kwa moja utakuwa umezaliwa na kujiingiza katika Ukoo wa Budha, hivyo mambo yote yamuhusuyo Bhuda utabeba na ndio maana huwezi kushangaa kwanini wale mabudha wote wanafanana,. kimavazi, kimienendo na kitabia ni kwasababu wamezaliwa humo katika roho..Kadhalika na dini nyingine zote na vikundi vyote viwe vya kishirikina n.k..

Lakini pia kuna kuzaliwa mara ya pili  katika ukoo unaoitwa UKOO wa YESU KRISTO. Huu ni ukoo ulio juu sana kuliko koo zote, ni uzao mteule, wa kifalme wa Mungu mwenyewe,   Huku nako watu wanazaliwa. Lakini kabla mtu hajaamua kuzaliwa katika huu ufalme ni lazima ajue ni nani anayemzaa, pili jina la ukoo wake ni lipi, tatu tabia za huo ukoo ni zipi, nne, je! ataweza kuendana nazo?.  Kumbuka jina la ukoo huo Ni YESU KRISTO huo ndio msingi kukutambulisha kwamba wewe ni unamilikiwa na mwenye huo ukoo. kwasababu biblia inasema.

Matendo 4: 12 “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. “

Hivyo hatua ya kwanza ya kuzaliwa kama tunavyojua wakati wa utungu kwa mwanamke huwa yanaanza kutoka kwanza maji, kisha damu baadaye kiumbe, kadhalika katika roho mtu anapodhamiria kuzaliwa mara ya pili kwa KUTUBU kabisa kwa kumaanisha kuziacha dhambi, anapaswa akabatizwe kwanza katika ubatizo sahihi wa MAJI MENGI.. Na ni lazima abatizwe kwa JINA LA YESU KRISTO..Zingatia hilo JINA YESU huo ndio msingi wa kukutambulisha wewe kuwa umezaliwa katika ukoo wa Yesu. Kumbuka wengi wanabatizwa kwa jina la Baba, mwana na Roho Mtakatifu kimakosa. Mitume hawakufanya hivyo soma

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja KWA JINA LAKE YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”.

Soma pia (Matendo 8:16, 10:48, na 19:5) utathibitisha jambo hilo. Hivyo unapobatizwa kifasaha baada ya kutubu dhambi zako, zinakuwa zinaondolewa na unakuwa umeingizwa katika Ukoo wa kifalme, Sasa  hatua ya mwisho ni kupokea Roho Mtakatifu mpaka hapo utakuwa una uhakika kuwa wewe ni mwana wa YESU KRISTO.

Kuanzia hapo unakuwa umepanda daraja una haki zote za kukanyaga nguvu zote za yule adui, kwa Jina la YESU na hakuna lolote litakalokusumbua kwasababu umepewa mamlaka yote ya kifalme. Lakini haishii hapo, baada ya kuzaliwa unaanza kurithi zile tabia za ukoo huo uliouingia. Mfano BABA yako YESU KRISTO alipenda kuishi maisha matakatifu, wewe nawe  utaanza kujiona mwenyewe unachukia maisha ya uovu, utaanza kuona hamu ya pombe, sigara, uasherati, rushwa, wizi, utukanaji, tamaa vinaanza kuisha, ndani yako pasipo hata kujilazimisha au kutumia nguvu,..

Ni kwasababu gani? jibu ni kwamba zile tabia za Baba yako YESU zinaanza kujidhihirisha ndani yako pasipo hata wewe mwenyewe kuamua hivyo. Huu ndio uwezo wa kufanyika mwana unaotoka kwa Mungu aliouzungumzia katika

Yohana  1: 12 ” Bali wote waliompokea ALIWAPA UWEZO wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;

13 waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu”.

Kadhalika kama Baba yako(YESU), na mababa (mitume na manabii) walikuwa wanatabia za unyenyekevu, tabia za kusali, kufunga, kuwapelekea wengine habari njema, n.k. vivyo hivyo na mtoto naye atarithi tabia hizo, na zitatoka zenyewe ndani pasipo kulazimishwa kwasababu hizi unazaliwa nazo, haujifunzi..na ndio maana ya Neno hatuishi chini ya sheria, kwasababu sheria ya Mungu imefungwa ndani ya mioyo yetu haitutawali inatoka yenyewe.

Kadhalika pia kama baba yetu YESU alichukiwa na ulimwengu, vivyo hivyo na watoto pia watarithi na hayo..kwasababu yeye mwenyewe alitangulia kuwaonya akisema “mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu”..

Lakini huu UWEZO hauji hivi hivi na ndio maana tunasema kuna watu WALIOJIUNGA na watu WALIOZALIWA.  Wengi wanasema wamezaliwa mara ya pili, lakini hawajazingatia hatua za kuzaliwa mara ya pili, ikiwa na maana kuwa hawajatubu  dhambi zao kwa kumaanisha kuziacha, na hawajabatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa, na kwa jina la YESU KRISTO. 

Hivyo zile tabia za kurithi maisha ya YESU KRISTO haziwezi kuonekana ndani yao, hawa ndio waliojiunga badala ya kuzaliwa. Watajilazimisha kuwa kama wakristo, watajilazimisha waache uasherati watashindwa, watajilazimsha waache sigara,  pombe, watashindwa kwasababu wao wamejiunga na sio kuzaliwa.

Biblia inasema

1Yohana 3:9 “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, KWA SABABU UZAO WAKE WAKAA NDANI YAKE; wala hawezi kutenda dhambi KWA SABABU AMEZALIWA KUTOKANA NA MUNGU ”.

Unaona hapo? Ule UZAO WA MUNGU unakaa ndani yako. Lakini kama haupo ndani yako kamwe hutakaa uweze kuishinda dhambi au kumshinda shetani.

Hivyo ndugu, kumbuka dunia nzima na vizazi vyote vinajua, kuwa hakuna UFALME mwingine zaidi ya Ufalme wa YESU KRISTO. Huo ndio unaomiliki sasa dunia, na ndio utakaokuja kumiliki baadaye. Ndugu BWANA YESU sio mtu wa kawaida kabisa, sasahivi tunavyoongea anamiliki Mbingu zote, malaika wote, na sayari zote, na dunia yote, na kuzimu yote, na tunavyovijua na tusivyovijua,.amekaa katika mbingu za mbingu asikoweza kufika mtu yeyote huko sio malaika yoyote au mwanadamu. Na atakuja tena kuwachukua walio wake ikiwa na maana ule UZAO WAKE. kwenda kumiliki vyote naye, watu wa milki yake milele na milele..

Kwanini ukose baraka zote hizo, kwa mambo yasiyokuwa na maana ya kitambo tu?. Siku  ile wenzako wanaenda kung’aa kama Jua kama yeye alivyo wewe utakuwa wapi ndugu?. Bwana Yesu alisema dhahiri kabisa, katika..

Yohana 3: 5 ” Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.
6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili”.

Hivyo ndugu fanya juu chini uzaliwe mara ya pili kabla mlango wa neema haujafungwa.

 Ubarikiwe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

MIHURI SABA

JE! MKRISTO ANARUHUSIWA KULA NGURUWE, NA KUVUTA SIGARA NA KUNYWA POMBE?

JE! NI SAHIHI KWENDA KUMFUATA KIONGOZI WA DINI KWA MFANO PADRE NA KUMPIGIA MAGOTI KUMWELEZA DHAMBI ZAKO AKUSAMEHE?.

Unyenyekevu ni nini?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments