Category Archive Mafundisho ya msingi

Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru.

Huwenda ukawa unajiuliza, Bwana Yesu alikuwa na maana gani kusema, Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru? . Je huko gizani ni wapi, na sirini ni wapi? Je yeye huwa anazungumza gizani.

Mathayo 10:26  “Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana.

27  Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba”

JIBU: Ni vema tukaifahamu tabia ya Bwana wetu Yesu Kristo, katika kufundisha jinsi ilivyokuwa alipokuwa anazungumza na watu mbalimbali. Yapo maneno au mafundisho au mafunuo aliyoyaweka wazi kwa watu wote, lakini yapo ambayo hakuyaweka wazi kwa kila mtu.

Mahubiri yake mengi aliyazungumza hadharani, lakini mengine haikuwa hivyo, kwamfano upo wakati alijitenga akapanda milimani, na wale waliomfuata ndio aliowafundisha (Mathayo 5:1), wakati mwingine aliingia nyumbani, hakutana kujulikana kwasababu alikuwa akitaka kuwafundisha wanafunzi wake tu, peke yao (Marko 9:29-31), wakati mwingine aliwaponya watu akawataka wasimdhihirishe, (Marko 1:44), wakati mwingine alijifunua utukufu  wake, kwa wale tu waliokwenda naye kuomba mlimani, uso wake ukawa unameta meta, kama jua, alipomaliza  akawakataza wasimwambie mtu, mpaka atakapofufuka (Mathayo 16).

Hayo ni mazingira mbalimbali, ambayo Yesu alisema nao bila kujulikana na kila mtu, Sasa mazingira hayo ndio aliyaita  “Gizani, au sirini”

Hii ni kufunua kuwa hata sasa Yesu anazungumza hadharani, lakini pia anazungumza sirini. Na yale ya sirini huwa ni makubwa zaidi na ndio maana haitaji yajulikane na kila mtu.

Watu wengi wanamsikia Yesu hadharani, lakini hawamsikii sirini. Hadharani, ni pale unaposikia mafundisho kanisani, mahubiri, semina, mkutano  n.k. Ni kweli Yesu atakufundisha mengi kupitia matumishi wake mbalimbali, na yatakujenga na ni muhimu ufanye hivyo.

Lakini lazima pia sirini pa Yesu uwe napo.

Je hapo ni wapi?

Ni eneo lako la utulivu la kimaombi na kutafakari”.

Ni muhimu sana kila mkristo, awe na wakati wake maalumu kila siku alioutenga wa kuzama uweponi, katika maombi, kusoma Neno na kutafakari shuhuda za Mungu maishani mwake. Ni muhimu sana.

Zaburi 91:1 AKETIYE MAHALI PA SIRI PAKE Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.

Mathayo 6:6  Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.

Hapa Yesu anataka uingie gharama, kidogo ili umsikie, au akuhudumie, au akufundishe. Ndio mfano wa wale waliomfata milimani. Vivyo hivyo na wewe, ingia gharama ya kudumu uweponi mwa Mungu. Ukiona mchana pana usumbufu, usiku ni muda mzuri sana, kuamka, tena masaa yako kadhaa kila siku,. Kumpa Bwana nafasi ya kukufundisha.

Ukiwa wa namna hii, hutamkosa Bwana popote pale. Kaa mahali pake pa siri. Kwasababu yupo pia sirini, akupe mambo mambo utayasema hadharani wakati fulani.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Kujazi ni nini? (Mathayo 6:4)

UMEFUNGWA KATIKA GIZA NA UVULI WA MAUTI?

AGIZO LA UTUME.

MKUU WA GIZA.

Rudi Nyumbani

Print this post

MSALABA NI ZANA YA UJENZI WA MAISHA YAKO.

Mwimbaji mmoja wa tenzi za rohoni aliandika hivi “Kama alivyoonyeshwa Yakobo zamani, msalaba umekuwa ngazi ya mbinguni (Tenzi no. 81, ubeti wa 2)”.. akirejea wakati ule  Yakobo alipokuwa amelala pale Betheli na akaona maono, ngazi kubwa kutokea mbele yake, na malaika wakikwea na kushuka kutoka mbinguni.

Mwanzo 28:11 “Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale.

12 Akaota ndoto; na tazama, NGAZI IMESIMAMISHWA JUU YA NCHI, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake…..

16 Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua.  17 Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, NAPO NDIPO LANGO LA MBINGUNI”.

Na ufunuo wa ngazi hiyo ni MSALABA.. Hakika! Kupitia msalaba wa YESU tunafika mbinguni, kupitia ufunuo wa msalaba wa BWANA YESU maishani mwetu, na si shingoni mwetu, tutamwona MUNGU!..

Lakini nataka pia tuutafakari msalaba kwa jicho lingine, kama “ZANA YA KUJENGEA MAISHA”. Hebu turejee kisa kimoja katika biblia kilichomhusu Nabii Elisha pamoja na wana wa manabii na kisha tutauelewa Zaidi msalaba wa BWANA.

2Wafalme 6:1 “Kisha, wana wa manabii wakamwambia Elisha, Angalia basi, mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu.

2 Basi twende mpaka Yordani, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili tujifanyie huko mahali pa kukaa. Akajibu, Haya! Nendeni.

3 Mmoja wao akasema, Uwe radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako. Akajibu, Nitakwenda.

4 Basi, akaenda pamoja nao. Nao walipofika Yordani, wakakata miti.

5 Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile.

6 Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali. AKAKATA KIJITI, AKAKITUPA PALE PALE, CHUMA KIKAELEA.

7 Akasema, Kiokote. Basi akanyosha mkono, akakitwaa”

Nataka tuutafakari huo mstari wa sita..“AKAKATA KIJITI, AKAKITUPA PALE PALE, CHUMA KIKAELEA”.

Hiki kijiti ni NINI?, na Chuma ni nini?

Chuma ni zana ya ujenzi, kumbuka huyu mtu alikuwa anakata mti kwaajili ya ujenzi ya makazi, na kwa bahati mbaya kichwa cha shoka kikaangukia majini, na shoka halikuwa la kwake bali aliazima tu!. Hivyo kazi ya ujenzi wa makazi yake ikasimama, na vile vile akabaki na deni ya kulipia kile kifaa.

Huenda shoka lako likawa ni elimu uliyo nayo, ambayo pengine kupitia hiyo ndio umefikiri kujenga maisha yako, au kazi uliyo nayo ambayo kupitia hiyo ndio unafikiria kujenga maisha yako, na makazi yako..Huenda shoka lako ni kipawa au uwezo Fulani ulionao ambao kupitia huo unaamini kazi yako itaisha salama.

Nataka nikuambie wakati unafikiri Elimu yako ni chuma kigumu cha kujenga maisha, au kazi yako ndio chuma kigumu cha kujenga maisha yako, au utashi wako ndio chuma kigumu cha kuchonga maisha yako..usisahau kuwa yapo maji pembeni yako!!!, na hiko chuma saa yoyote kitazama..na kile ulichotazamia kukikamilisha kitasimama, na hata kupata hasara kubwa ya madeni.

Sasa kitu pekee kinachoweza kutoa chuma ndani ya maji, hata kielee, si winchi, au sumaku, au kifaa kingine chochote chenye uwezo…bali ni KIJITI KIDOGO TU!.. Na kijiti hiko si kingine Zaidi ya MSALABA BWANA YESU!!.

(Kumbuka msalaba wa Bwana YESU si Rozari shingoni, au sanamu madhahabuni, au mti wa msalaba juu ya kaburi, bali ni ufunuo wa Mauti ya YESU moyoni)…Maana yake wokovu unaopatikana kupitia uelewa wa mauti ya BWANA YESU…ambao huo unazaa mtu kujitwika msalaba wake na kumfuata yeye.

Marko 8:34  “Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate.

35  Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha”.

Je! msalaba wa KRISTO upo moyoni mwako??, Umeubeba msalaba wako na kumfuata yeye??.. Au unajitumainisha na chuma ulicho nacho!..ukiamini kuwa elimu yako itakuokoa, au kazi yako, au cheo chako.. Hivyo vyote ukiwa navyo na KRISTO HAYUPO MOYONI MWAKO, UNAFANYA KAZI BURE!!!.

Na tena ni heri ukose hivyo vyote, Ukose elimu, ukose kazi, ukose cheo, ukose kila kitu…lakini msalaba wa KRISTO upo moyoni mwako, kuliko kuwa na vyote hivyo halafu huna YESU moyoni!!…NI HASARA KUBWA!!!

Ni heri ukayasalimisha maisha yako kwa BWANA YESU leo, kama bado hujafanya hivyo, na BWANA ATAKUSAIDIA, Ikiwa utahitaji msaada huo wa kumpokea YESU, basi waweza wasiliana nasi na utapata msaada huo…

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

ONA FAHARI JUU YA BWANA.

Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?

NJIA YA MSALABA

Kama ulimwengu ujao utakuwa na watakatifu tu, sasa hao watakaotawaliwa watatoka wapi?

UTHAMINI WITO WA PILI WA YESU ZAIDI YA ULE WA KWANZA.

Rudi Nyumbani

Print this post

MSINGI WA NYUMBA YA MUNGU, NI JINA LA MUNGU.

Kamwe hatuwezi kuitenganisha nyumba ya MUNGU na JINA LAKE.. Vitu hivi viwili vinakwenda pamoja DAIMA!!!..

Lakini nyumba ya Mungu inapogeuzwa na kuwa  nyumba ya Jina la Mchungaji, au jina la Nabii, au inakuwa nyumba ya Maji ya Upako, au mafuta ya Upako, au chumvi ya Upako..nyumba  hiyo inakuwa si nyumba tena ya Mungu bali inakuwa ni pango la wanyang’anyi kulingana na biblia.

Yeremia 7:11 “Je! Nyumba hii, IITWAYO KWA JINA LANGU, imekuwa pango la wanyang’anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana”.

Tunapoacha kulinyanyua jina la BWANA YESU ndani ya nyumba yake, na badala yake tunalinyanyua jina la Nabii, au Mchungaji, au Mtume, au mtu Fulani ndani ya kanisa, hapo MUNGU tunayemtamani hayupo!.

Tunapoliondoa jina la BWANA YESU ndani ya Kanisa, na kuanza kutumia mafuta ya upako kila wakati kama njia mbadala!…hapo tumemwondoa MUNGU kabisa na tumemweka mungu mwingine ambaye ni shetani..tunapoliondoa jina la YESU na kutumia chumvi au udongo kama mbadala wake, kwa kila changamoto inayouja mbele yetu…hapo MUNGU hayupo, bali tupo wenyewe!!.

Tunapoacha kuomba kwa jina la BWANA YESU na kuanza kuziomba sanamu..hayo ni machukizo makubwa..

Yeremia 7:30 “Maana wana wa Yuda wametenda yaliyo maovu machoni pangu, asema Bwana; wameweka machukizo yao NDANI YA NYUMBA HIYO, IITWAYO KWA JINA LANGU, hata kuitia unajisi”.

Kama Mkristo au Mhubiri kamwe usilitenganishe jina la BWANA YESU na NYUMBA YAKE!.. Nyumba yake imekusudiwa kukaa jina lake humo MILELE.. Hakuna wakati ambapo JINA LA YESU, Litaisha muda wa matumizi yake ndani ya KANISA.. Hicho kipindi hakipo!.

Zama hizi za siku za mwisho shetani amenyanyua uongo mkubwa sana, kuwa ZAMA ZA JINA LA YESU ZIMEPITA! Hivyo sasa jina la YESU halina nguvu tena wala hatulitumii tena.. Ndugu fahamu kuwa huo ni uongo wa adui asilimia zote, jina la YESU limekusudiwa kutajwa na kutumika ndani ya NYUMBA YAKE DAIMA..

2Nyakati 7:16 “Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ILI KWAMBA JINA LANGU LIPATE KUWAKO HUKO MILELE; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima”

Na tena Macho ya Mungu na Moyo wake upo katika Nyumba ile ambayo ndani yake LINAKAA JINA LAKE na si jina la Mtu au kitu. Na tena maandiko yanasema hakuna jina lingine tulilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo isipokuwa hilo jina la YESU.

Matendo 4:12 “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo”.

Na zaidi sana yanasema,  lolote lile tufanyalo liwe kwa tendo au kwa Neno tufanye yote kwa jina la BWANA YESU.

Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”.

Hivyo kwa hitimisho ni kuwa JINA LA YESU ndio MSINGI WA KANISA la kweli la MUNGU.. Mahali pasipotajwa wala kutumika jina hilo, mahali hapo hapana MUNGU wa mbingu na nchi bali pana roho nyingine, ambayo ni ya Adui shetani.

Mistari mingine inayozidi kuthibitisha kuwa nyumba ya MUNGU imekusudiwa kuwekwa jina lake milele ni kama ifuatayo.. 2Samweli 7:13, 1Wafalme 5:5, 1Wafalme 8:18-19, 1Wafalme 9:7, Yeremia 7:10-14, Yeremia 32:34 na Yeremia 34:15.

Je! Umempokea YESU kama Bwana na Mwokozi wa maisha yako?..fahamu kuwa tunaishi siku za mwisho za kurudi kwake mwana wa Adamu, na hukumu ya mwisho ipo karibu.

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je huduma za mitume na manabii, zinaendelea kufanya kazi hadi sasa?

Je ni kweli Tumejengwa juu ya Mitume na Manabii? (Waefeso 2:20)

ORODHA YA MITUME.

Je Mungu anaketi katika giza? (1Wafalme 8:12)

Nitamjuaje nabii wa Uongo?

Rudi Nyumbani

Print this post

MIMI NIKO AMBAYE NIKO

Musa alipomwuliza Mungu kuhusu jina lake, alitarajia kuwa atapewa jina Fulani maalumu kama vile jina la miungu mingine yoyote ijulikanayo mfano wa Baali, au arishtoreth, n.k.

Lakini tunaona Mungu alimjibu kwa ujumla na kumwambia, wakikuuliza jina langu waambie kuwa MIMI NIKO AMBAYE NIKO

Kutoka 3:14 Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO;akasema,Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli;MIMI NIKO amenituma kwenu.

Sasa kama ukitazama biblia yako kwa chini utaona imeeleza kwa tafsiri nzuri zaidi hiyo sentensi. Akiwa na maana kuwa NITAKUWA KAMA NITAKAVYOKUWA.

Yaani mimi sina jina moja maalumu, lenye sifa Fulani. Bali nitatambulika pindi niwapo katika hilo tukio, au tatizo au haja hiyo jina langu. Na kweli ndivyo ilivyokuwa baada ya pale. Tunaona Farao alipogoma tu, kuwaruhusu wana Israeli kutoka Misri tena kwa adhabu ya kuwaongezea kazi, ndipo hapo Mungu akaanza kujifunua kwa majina yake. Akamwambia Musa, kwa jina langu Yehova nilikuwa sijajifunua, sasa nitakwenda kujifunua, kwa jina hilo,

Kutoka 6:1 Bwana akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake. 

2 Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA; 

3 nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao. 

4 Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni. 

5 Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu. 

6 Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; 

7 nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri. 

8 Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo naliinua mkono wangu, niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA

Umeona? Jina la Mungu lililowatoa wana wa Israeli Misri ni jina la Yehova. Na baada ya hapo tunaona sehemu mbalimbali akijifunua kwa majina mengine mengi, kama Yehova yire, Yehova Nisi, Yehova shama, Yehova shalom, Ebenezeri, n.k. nyakati za vita, za mahitaji, za huzuni n.k. Kulingana na jinsi alivyowasaidia watu wake, walipomlilia.

Na mwisho kabisa akajifunua kwa jina kuu la UKOMBOZI, ambalo ni YESU, lenye maana ya Yehova-mwokozi.  

Hii ni kufunua nini?

Yatupasa tumwelewe Mungu wetu sikuzote kama “NITAKUWA KAMA NITAKAVYOKUWA”. Hana mipaka ya kujifunua kwake kwetu, nyakati za mahitaji atajifunua, nyakati za raha atajifunua, nyakati za magumu atajifunua, mabondeni atajifunua tu kwako, milimani ataonekana tu, yeye ni vyote katika yote. Uwapo visiwani, uwapo jangwani, uendapo mbinguni, ushukapo mahali pa wafu utamwona tu Mungu wako. Hakuna mahali hatajidhihirisha kwako. Pindi tu umwaminipo. Huhitaji kuwa na hofu na wasiwasi na kumwekea mipaka kwamba kwenye jambo hili au hili hataweza kuwepo au kujidhihirisha.

Swali ni je! Umemwamini Mungu aliyejifunua kwako kama mwokozi? Yaani Kristo? Kumbuka, kabla hujasaidiwa kwingine kote na yeye , unahitaji kwanza uokolewe, kwasababu umepotea katika dhambi, na mshahara wa dhambi ni mauti. Leo hii ukimwamini Yesu atakupa ondoleo la dhambi zako, utakuwa na uzima wa milele. Na utaufurahia wokovu kwasababu utakuwa tayari umevukishwa kutoka mautini kwenda  uzimani. Kumbuka hizi ni siku za mwisho. Itakufaidia nini uachwe katika UNYAKUO, angali nafasi unayo leo.Geuka umfuate Kristo.

Ikiwa upo tayari kumpokea Yesu maishani mwako, basi wasiliana na namba zetu chini kwa msaada bure wa kuokoka.

Ubarikiwe.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

Majina mbalimbali ya Mungu na maana zake.

JE! MUNGU NI NANI?

IKO NJIA IONEKANAYO KUWA SAWA MACHONI PA MTU.

Rudi nyumbani

Print this post

MAANA HUFUMBA MACHO YAO WASIONE!

Karibu tunayatafakari maandiko…

2Petro 3:3 “Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,

4  na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.

MAANA HUFUMBA MACHO YAO WASIONE neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;

6  kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia

7  Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu”.

Maandiko yanatuambia watu wa siku za mwisho watafumba macho yao WASIKUMBUKE KILICHOTOKEA WAKATI WA NUHU. Kwamba Mbingu zilikuwepo na nchi pia ilikuwepo, na watu walikuwa wanaendelea na mambo yao, wakidhihaki mahubiri ya Henoko na Nuhu kuhusiana na hukumu ya Mungu, na wakati ulipotimia wa kikombe cha ghadhabu ya Mungu kujaa, hakuna hata mmoja aliyesalia Zaidi ya Nuhu na wanawe na wake zao, jumla watu 8 kati ya dunia iliyokuwa imejaa mabilioni ya watu.

Sasa mambo hayo yalishawahi kutokea katika rekodi za wanadamu.. lakini watu WANAFUMBA MACHO YAO!, Wasione hilo, wala kulitafakari.. na hatimaye wanadhihaki wakisema mbona Yesu harudi!.. mbona tumesubiri na kusubiri!..

Lakini hao hao wanaelewa kilichotokea wakati wa Nuhu kuwa dunia iligharikishwa yote..na wanajua kabisa kuwa walikuwepo watu wenye dhihaka kama za kwao, wakisema hakuna Mungu, na hakuna mtakatifu duniani.. Lakini siku ilipofika ya kuokoka Nuhu peke yake na familia yako, ndipo walipoelewa kuwa walikuwepo wacha Mungu duniani, na tena Mungu haangalii wingi.

Ndugu usidanganyike!. KRISTO ANARUDI! Na wala hatakawia..

Waebrania 10:37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia”.

Baada ya Kristo kuwachukua watu wake, kitakachofuata duniani ni gharika ya Moto wa ghadhabu ya MUNGU juu ya wote wasiomcha Mungu, kama tu ilivyokuwa nyakati za Nuhu.

2Petro 3:7 “Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.

Hivyo kamwe usifikiri wala kuwaza, wala kutia wasiwasi juu ya ujio wa BWANA YESU KRISTO.. Kama ulishawahi kudanganywa, au kulaghaiwa basi ni wanadamu ndio waliokudanganya na kukulaghai, lakini MUNGU muumba wa mbingu na nchi, kamwe hajawahi kusema uongo, na hatakaa aseme uwongo..

Kizazi chetu kitahukumiwa zaidi kuliko kile cha Nuhu kwasababu laiti watu wa kipindi cha Nuhu, wangepata mfano wa wengine waligharikishwa kabla yao, huenda wangeyatii mahubiri ya Nuhu lakini hawakuwa na mifano kabla yao, lakini sisi tunao mfano, wa watu hao.. ni kitu gani kinatutia kiburi!.

Ni nini kinachotufumba macho, na kinachowafumba watu macho????

Unadhani ni shetani????... nataka nikuambie shetani anahusika kwa sehemu ndogo sana, (Na adui anapenda kila kitu asingiziwe yeye ili watu waendelee kujifariji namna hiyo)…..kinachowafanya watu KUFUMBA MACHO YAO, wasitafakari yaliyotokea nyakati za Nuhu na Sodoma na Ghomora ni KIBURI CHA UZIMA, na watu kwa mioyo yao wenyewe KUCHAGUA GIZA na KUIKATAA NURU.

Yohana 3:19 “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu”.

Siku hizi za Mwisho watu wameyafumba macho yao, wasione na wanajiaminisha ni shetani, kumbe si shetani bali ni wao…tupo! kizazi cha hatari sana..

Mathayo 13:15 “Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya”

Kwa hitimisho usilisahau andiko lifuatalo…

2Petro 3:8 “Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.

9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba”.

Ikiwa bado hujampokea BWANA YESU, bali mlango wa wokovu sasa upo wazi, na tunaishi ukingoni kabisa mwa wakati. Hatuna muda mwingi KRISTO anarudi!. Ni wakati wa kutubu na kuishi maisha masafi yanayoendana na toba yetu.

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

13  Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.

14  Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NUHU WA SASA.

UMEFUNULIWA AKILI?

KWANINI NI NUHU, AYUBU NA DANIELI?

Kuna tofauti gani kati ya uso wa Bwana na macho ya Bwana?

NI WAKATI UPI UTAUONA USO WA KRISTO?

Rudi nyumbani

Print this post

YESU KATIKA KUCHOKA KWAKE.

Mahali pekee ambapo maandiko yanaeleza kuchoka kwa Yesu, ni siku ile alipokuwa anatoka Uyahudi anakwenda Galilaya. Kwasababu safari yake ilikuwa ndefu, ya saa nyingi, ilibidi waweke kituo kwanza kwenye mji wa mmoja wa wasamaria, wapumzike. Yeye na wanafunzi wake kwenye kile kisima cha Yakobo.

Yohana 4: 5  Basi akafika kunako mji wa Samaria, uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa Yusufu mwanawe. 6  Na hapo palikuwa na kisima cha Yakobo. Basi Yesu, kwa sababu AMECHOKA KWA SAFARI YAKE, akaketi vivi hivi kisimani. Nayo ilikuwa yapata saa sita.

Jua la mchana likiwa kali, anasikia mwili ni mchovu hautaki, kufanya kazi yoyote, njaa zinauma, mpaka mitume wakaondoka kwenda kutafuta chakula mjini. Lakini katika mazingira hayo hayo Analetewa na Mungu mtu mwenye dhambi amshuhudie habari za neema ya wokovu. Ndio Yule mwanamke msamaria.

Lakini Yesu hakuwa na udhuru kwa kusema, huu ni muda wangu wa kupumzika, ni muda wangu wa kulala, ni muda wangu wa lunch nile na wanafunzi wangu. Alitii vilevile katika uchovu wake, akaanza kuongea na Yule mwanamke habari za ukombozi, kwa kipindi kirefu kidogo.

Lakini mwisho wa mazungumzo yao haukuwa bure, Yule mwanamke aliondoka, lakini baada ya muda mfupi alirudi na jopo la watu, ili kuja kumsikiliza Bwana Yesu, maneno aliyoshuhudiwa na yeye (Yohana 4:1-42). Na baada ya hapo tena, Samaria yote ikamwamini, sehemu nyingine mpaka wakawa wanataka hata kumfanya mfalme.

Lakini ni nini tunapaswa tujifunze katika habari hiyo?  Wengi wetu hatujui kufanikiwa kwa huduma ile ya Yesu pale ndani ya mwanamke Yule zaidi ya wengine wengi, kulitokana na gharama ambazo Yesu aliingia. Yaani katika kipindi cha KUCHOKA kwake, alikuwa tayari kulitimiza kusudi la Mungu. Kitendo hicho rohoni huwa kinageuka na kuwa IMANI, kubwa sana mbele za Mungu.

Je! Na sisi, tunaweza kujifunza jambo hili kwa Bwana. Je! visingizio cha kuchoka, tumeshindwa kutimiza makusudi mangapi ya Mungu, yenye matokeo makubwa kama haya? Nimetoka kazini, nimefanya kazi wiki nzima, hivyo nimechoka siwezi kwenda kuomba. Weekend ni siku yangu ya kupumzika, siwezi kwenda  kwenye ushuhudiaji?

Hatujui kuwa hapo ndipo Mungu anapathamini, tunataka siku ambayo tupo “free” tu.

Ukweli ni kwamba tukiwa watu wa kungojea siku ambazo tuna nafasi ya kutosha, au tuna afya, au tuna  fursa, au tume-relax si rahisi kuzalisha vema kama wakati ambao tutajiona sisi ni dhaifu. Katika dunia hii ya masumbufu na mahangaiko ya maisha, utajikuta mpaka unamaliza maisha yako hujapata hata huo muda wa kupumzika vema. Hivyo tumia fursa hiyo sasa.

Isaya 40:29 Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.  30 Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;  31 bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Hubiri injili nyakati zote, omba nyakati zote, soma Neno nyakati zote. Kumbuka wakati wa kuchoka, ipo nguvu ya Mungu kukusaidia. Jenga ufalme wa Mungu. Na Bwana atakutia nguvu.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

WALIKUWA WAMECHOKA NA KUTAWANYIKA KAMA KONDOO WASIO NA MCHUNGAJI.

NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?.

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

YESU HAYUPO KATIKA MAZINGIRA YALEYALE TU SIKUZOTE, USIJISAHAU.

Rudi nyumbani

Print this post

UWEZA WA MUNGU NJE YA WAKATI.

Tunaposikia kuhusu uweza wa Mungu wa kufanya mambo “nje ya wakati” moja kwa moja tunafikiria, juu wa wakati ambao umepitiliza muda wake. Lakini hatufikirii juu ya wakati ambao “bado haujafikiwa” ambao nao pia huitwa “nje ya wakati”.

Kwamfano Elisabethi alipokea ujauzito nje ya wakati, (yaani katika wakati uliopitiliza), wakati ambapo viungo vya uzazi havipo tena, mfano tu wa Sara. Lakini wakati huo huo Mariamu (mamaye Yesu), alipokea pia ujauzito nje ya wakati(Lakini wakati ambao haujafikiwa).

Ikiwa na maana kabla hata hajamkaribia mwanamume, alionekana tayari mimba imeshatungishwa tumboni. Huo ni uweza wa Mungu wa ajabu.

Ni lazima ufahamu kuwa katika maisha yako ya wokovu wewe kama mwaminio, majira yote mawili Bwana atakupitisha kwa mpigo. Fahamu kuwa kuna mahali utacheleweshwa kidogo,lakini pia kuna mahali utawahishwa haraka kabla ya wakati wake. Vyote viwili vitakwenda sambamba, Hivyo hupaswi kuwa na mashaka naye, kwasababu matokeo aliyoyatazamia Mungu juu ya maisha yako ya wokovu yatatokea tu.

Umtazamapo Mungu, usimweke kwenye kipimo tu cha “ndani ya wakati” ulichokizoea. Jiandae kwa lolote. Lakini mpango wake ni lazima utimie.

Maandiko yanasema..

Ayubu 22:21 Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.

Na pia anasema..

Warumi 11:33  “Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani!”

Ubarikiwe.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

UWEZA WA MUNGU UNAONEKANA WAPI?

INJILI NI UWEZA WA MUNGU, UULETAO WOKOVU.

MAVAZI YA NDANI NA YA NJE.

KUMBE MUNGU ANAWEZA KUKULIPA KWA USICHOSTAHILI!

Rudi nyumbani

Print this post

Dhamiri ni nini kibiblia?

Dhamiri au Dhamira ni nini kibiblia?


“Dhamiri” au kwa lugha nyingine “Dhamira” ni hisia ya ndani ya mtu (ya asili) inayompa kupambanua lililo jema na lililo baya, lililo zuri na lisilo zuri, linalofaa na lisilofaa. Hisia hii kila mtu anayo na haitokani na mafundisho au maelekezo, bali mtu anakuwa anazaliwa nayo.

Dhamiri ni kama mtu mwingine wa pili, aliyeko ndani yako ambaye anasahihisha hisia zako au maamuzi yako, kabla hujayafanya au baada ya kuyafanya. Kama jambo halipo sawa basi dhamiri inakushuhudia aidha kwa kukosa Amani au raha au ujasiri..

Vile vile kama jambo lipo sawa basi dhamiri yako ya ndani inakushuhudia kwamba kile ufanyacho ni chema, aidha kwa kupata furaha Fulani au Amani au ujasiri.

Kwamfano mtu anapofikiri “kuua/ kumwaga damu” au “kuiba”.. kabla ya kufanya kile kitu “dhamiri” ya ndani itamshuhudia kuwa kile kitu si sawa! Pasipo hata kuambiwa na mtu au kuhubiriwa, kuna kitu tu ndani yake kinamwambia hicho si sawa!.. Na kama ni mtu wa kujali basi haraka sana atahairisha maamuzi yake hayo.

Katika biblia neno Dhamiri limeonekana mara kadhaa.

Sehemu ya kwanza maarufu ni ule wakati ambao baadhi ya Waandishi na Mafarisayo walimletea Bwana YESU mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, kwa lengo la kutaka kumwua lakini pia kumjaribu Bwana. Lakini maandiko yanasema walipopewa ruhusa ya kumtupia mawe, wote walichomwa dhamiri zao na hakuna aliyemhukumu.

Yohana 8:3  “Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati.

4  Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini.

5  Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?

6  Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

7  Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.

8  Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

9  Nao waliposikia, WAKASHITAKIWA NA DHAMIRI ZAO, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.

10  Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?

11  Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.]”

Vile vile biblia inatabiri kuwa katika siku za mwisho, watatokea watu ambao watasema uongo ijapokuwa dhamiri zao zinawashuhudia, lakini hawatazisikiliza, na watu hawa watawafundisha watu mafundisho ya mashetani.

1Timotheo 4:1  “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

2  kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

3  wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli”

Mistari mingine ihusuyo dhamiri ni pamoja na Matendo 23:1, Warumi 2:15, Warumi 9:1, Warumi 13:5, na 1Timotheo 1:9.

Ikiwa ndani yako unahisi “Dhamiri yako imekufa” au “imepungua nguvu”… maana yake husikii chochote kikikuzuia au kukuhukumu unapofanya jambo lisilo sawa, basi fahamu kuwa adui kaharibu utu wako wa ndani, na hivyo unamhitaji Bwana YESU akuhuishe utu wako wa ndani kwa damu yake.

Unapompokea BWANA YESU, na kubatizwa na kujazwa na Roho wake mtakatifu, ule utu wako wa ndani uliokufa au uliofifia yeye (Bwana YESU) anauhuisha upya…na hivyo Dhamiri yako inafufuka na inakuwa safi. Hivyo fanya maamuzi leo ya kumsogelea yeye karibu na imarisha mahusiano yako naye.

Waebrania 9:14  “basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.

Nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

IKO NJIA IONEKANAYO KUWA SAWA MACHONI PA MTU.

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

Manabii walisema “Neno la Mungu likanijia” ..Maana ya hili neno ni nini?.

Rudi nyumbani

Print this post

ZIFAHAMU KARAMA 9 ZA ROHO MTAKATIFU NA UTENDAJI KAZI WAKE.

Karama tisa (9) za Roho mtakatifu tunazisoma katika kitabu cha 1Wakorintho 12.

Tusome,

1Wakorintho 12:4  “Basi pana tofauti za KARAMA; bali Roho ni yeye yule.

5  Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.

6  Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.

7  Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.

8  Maana mtu mmoja kwa Roho apewa NENO LA HEKIMA; na mwingine NENO LA MAARIFA, apendavyo Roho yeye yule;

9  mwingine IMANI katika Roho yeye yule; na mwingine KARAMA ZA KUPONYA katika Roho yule mmoja;

10  na mwingine MATENDO YA MIUJIZA; na mwingine UNABII; na mwingine KUPAMBANUA ROHO; mwingine AINA ZA LUGHA; na mwingine TAFSIRI ZA LUGHA;

11  lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye”.

Tuangalie utendaji kazi wa moja baada ya nyingine.

      1. NENO LA HEKIMA.

Hii ni karama ya upambanuzi wa jambo lililo gumu kutatulika.. Kwamfano kunaweza kutokea jambo katika kanisa ambalo ni gumu sana kutatulika au kufahamika, (fumbo kubwa)..sasa mtu mwenye karama hii ya Neno la Hekima anaweza kulijua jambo hilo na kulitatua, au kutoa mapendekezo ya kulitatua kwa njia ya mafundisho au matendo..

Mfano wa mtu aliyekuwa na karama hii ni Sulemani..

Watu wenye karama hii wakiwemo ndani ya kanisa, basi ndoa nyingi zitasimama, na wizi na mambo ya kando kando hayataweza kupata nafasi kwasababu yatawekwa wazi.

     2. NENO LA MAARIFA.

Hii ni karama ya MAARIFA kama jina lake lilivyo.. Mtu mwenye karama hii anakuwa na uwezo mkubwa wa kujua mambo mengi..ya kidunia na kibiblia.. (Maarifa aliyonayo kuhusu biblia yanamtofautisha na mtu mwingine).. Vile vile maarifa anayokuwa nayo juu ya mambo mengine ya ulimwengu yanamtofuatisha na mkristo mwingine.

Watu wenye karama hii wakiwemo ndano ya kanisa, mafundisho ya manabii wa uongo ni ngumu kupata nafasi, (kwasababu manabii wa uongo wanawadanganya watu wasio na maarifa ya kutosha) sasa wakiwepo watu wenye karama hii ya maarifa, basi wanaweza kulifundisha kundi au kulielekeza mambo mengi kiusahihi kabisa.

Lakini wakikosekana ndio linatimia lile Neno “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa (Hosea 4:6)”

     3. IMANI

Hii ni karama ya kutenda matendo ya Imani.. Watu wenye karama hii katika kanisa ni wale wenye kutenda au kuhamasisha watu katika kanisa kufanya matendo ya Imani. Na maisha yao yote yakijaa matendo ya Imani.

Huwa hawaogopi magonjwa, changamoto, wala dhoruba yoyote.. Kukitokea hofu wamesimama imara!, kanisa likiishiwa nguvu, watu wenye hii karama wanalitia nguvu na kulihamasisha..

Watu kama hawa wakiwepo katika kanisa basi kanisa hilo haliwezi kupungua nguvu ya kuendelea mbele, wala watu wake hawawezi kukata tamaa daima.

     4. KARAMA ZA KUPONYA.

Zinaitwa “Karama za kuponya” na si “Karama ya kuponya”… Maana yake ni Karama hii inafanya kazi ya kuponya vitu vingi, ikiwemo magonjwa, maisha, roho, nafsi na vitu vingine vilivyoharibika.

Mtu mwenye karama hii anakuwa na uwezo wa kumwombea mtu na akapona kirahisi, au kumfundisha mtu na akapokea uponyaji kirahisi.. Vile vile ana uwezo wa kumwekea mtu mikono akapokea uponyaji kirahisi ikiwa ana ugonjwa au maisha yake yameharibika.

Vile vile anaweza kumfundisha mtu na mtu yule akaponyeka roho yake na majeraha ya adui.

Vile vile kama kazi ya mtu au maisha yake yameharibika mtu mwenye karama hii anaweza kumjenga upya kwa kumfundisha au kumwombea na mtu yule akaponyeka kabisa kabisa dhidi ya mapigo yote ya yule adui.

Watu kama wenye karama hii wakiwemo ndani ya kanisa, basi kanisa hilo litakuwa na watu wanaosimama kila siku na hakuna atakayekuwa anaanguka.

     5. MATENDO YA MIUJIZA.

Hii ni karama ya Ishara ndani ya kanisa. Watu wenye karama hii ni wale ambao maisha yao yamejaa miujiza na ishara.. Wakiwemo ndani ya kanisa basi ni lazima kuna miujiza itaonekana ambayo itawashangaza wengi na kuwafanya waaamini mahali pale kuna Mungu.

Kuna watu wakiingia mahali au wakienda mahali lazima kuna tukio la ajabu litatokea pasipo hata kupanga au kusema (ni ishara ambazo zinafuatana nao).

Kunatokea ajali ghafla anatoka mzima bila dhara lolote.. hajala wiki 2 lakini bado anaonekana ana nguvu zile zile.. Anafika mahali kivuli chake kinaponya watu.. anaimba tu au anaongea!, watu wanajazwa Roho Mtakatifu n.k

Watu wa namna hii kwa ufupi, wanakuwa wanafanya vitu vya ajabu, na kuwa na matukio mengi ya kushangaza shangaza na wengi wenye karama hii wanakuwa na vipindi vya kukutana/kutokewa na malaika. Yote ni kwa lengo la kuthibitisha uwepo wa Mungu katika kanisa.

     6. UNABII

Hii ni karama inayohusika na kutabiri mambo yajayo au yanayoendelea sasa, au kuelezea yaliyopita.

Watu wenye karama hii wanakuwa na uwezo wa kuona mambo yajayo ya Mtu, Watu, kanisa au Taifa. Na nabii zao zinaegemea biblia. Na Mungu anawafunulia kwa njia aidha ya Ndoto, Neno au Maono.

Pia wana uwezo wa kumfundisha na kumwombea mtu au kumshauri kuhusiana na kile walichooneshwa! (kilichopita, kinachooendelea au kijacho).

Watu wenye karama hii wakiwemo ndani ya kanisa basi kanisa litasimama na kuendelea.

    7. KUPAMBANUA ROHO.

Hii ni karama ya kupambanua au kuzijaribu roho. Mtu mwenye karama hii anakuwa mwepesi wa kuzitambua roho (kama ni roho wa Mungu au roho nyingine).

Kama kuna roho ya uchawi inaingia basi anakuwa na uwezo wa kupambanua, kama ni roho ya uzinzi, wizi, uadui, fitina, n.k anakuwa na uwezo wa kuiona kabla ya wengine na hivyo kutoa mashauri au kuomba iondoke.

Vile vile mtu mwenye karama hii anakuwa na uwezo wa kujua utendaji kazi wa Roho Mtakatifu, ni rahisi kujua karama za watu katika migawanyo yake..(kwamba huyu ana karama hii na yule ile).. Na pia anakuwa na uwezo mkubwa wa kufundisha juu ya karama za roho.

Watu wenye karama hii wakiwemo ndani ya kanisa.. ni ngumu sana kanisa hilo kushambuliwa na roho nyingine..

     8. AINA ZA LUGHA.

Hii ni karama ya ishara ndani ya kanisa, ambayo madhumuni yake ni kama yale ya karama ya MIUJIZA.

Mtu mwenye karama ya lugha, anakuwa na uwezo wa kuzungumza lugha nyingi kimiujiza, (lugha za rohoni na za mwilini).. Lugha za rohoni ambazo (maarufu kama kunena kwa lugha).. mtu anakuwa na uwezo wa kuzinena na wakati mwingine kutoa tafsiri zake.

Lakini Zaidi sana anakuwa na uwezo wa kunena lugha nyingine za jamii nyingine.. Pindi anapojaa Roho Mtakatifu anajikuta anauwezo wa kunena lugha ya taifa lingine au kabila lingine ambalo sio lake, tena anazungumza vizuri sana.

Na watu wa wanapoona huyu mtu hajasoma kabisa lakini anaongea kiingereza kizuri namna hiyo, basi wanamshangaa Mungu na kumtukuza na kumwamini, na baadaye yule mtu akimaliza kunena basi anarudi katika hali yake ya kawaida ya kuongea lugha yake ya asili.

Watu wenye karama hii wakiwepo ndani ya kanisa..basi hofu ya Mungu inaongezeka na kuthibitisha kuwa Mungu yupo katikati ya kanisa lake.

     9. TAFSIRI ZA LUGHA.

Hii ni karama ya 9 na ya mwisho iliyotajwa katika orodha hii..  Karama hii inahusiana pakubwa sana na ile ya “Aina za lugha”.. Kwani mwenye karama ya Aina za lugha, mara nyingine atamwitaji huyu mwenye Tafsiri za lugha ili aweze kutafsiri kinachozungumzwa.. ili kanisa lisiingie katika machafuko. (Soma 1Wakorintho 14:27).

Hizi ndizo karama 9 maarufu katika biblia. Zipo karama nyingine kama za kukirimu, au Uimbaji hizo zinaangukia katika kundi la huduma ya UINJILISTI, Mtu anayeimba anafanya uinjilisti, hivyo ni mwinjilisti!.

Na mtu anaweza kuwa na karama Zaidi ya moja, (Maana yake mtu anaweza kuwa na karama ya Imani na pia ya kinabii au ya Aina za Lugha, na Tafsiri za lugha hapo hapo) ingawa jambo hilo linakuwa ni nadra sana!…. Lakini Roho Mtakatifu ndiye anayemgawia mtu na si mtu anajipachikia!.

Na kumbuka!. Karama za Roho Mtakatifu ni kwa lengo la kufaidiana na si kuonyeshana au biashara.. Karama nyingi shetani kaziua kwa njia hiyo (anawapachikia watu kiburi, au kupenda sifa na utukufu na fedha).. mwisho wa siku kile kipawa kinazima!.

Ili kufufua karama iliyozima, njia ni kujishusha, kuwa mnyenyekevu, vile vile uwe na nia ya Kristo ya kulijenga kanisa, na pia ukubali na uheshimu kujengwa na karama nyingine, lakini ukijiona wewe ni wewe huhitaji wengine, fahamu kuwa hata cha kwako hakitaweza kufanya kazi.

Kanisa la siku za mwisho, tuna tatizo kubwa sana wa kuruhusu utendaji kazi wa Roho Mtakatifu kupitia karama zilizowekwa ndani yetu.. Na tatizo kubwa lipo kwa “viongozi” na “wasio viongozi (washirika)”.

Viongozi wengi hawaruhusu vipawa hivi vitende kazi aidha kutokana na wivu, au kutokuwa na maarifa ya kutosha kuhusiana na vipawa hivyo…

Lakini pia na watu wengine ndani ya kanisa (washirika) wanaoujenga mwili wa Kristo. Wanapokataa kujishughulisha vya kutosha na mwili wa Kristo, basi vile vipawa vilivyopo ndani yao vinazima, na hivyo kanisa linabaki na karama moja au mbili zinazofanya kazi.

Fahamu kuwa unapoenda kanisani, unacho kitu cha kiroho kwaajili ya ule mwili.. Ni wajibu wako kupambana mpaka kitokee, na kionekanane na kifanye kazi…usinyooshee tu kidole, wala usilaumu tu, na wakati huo wewe mwenyewe karama imekufa ndani yako (hujijui wewe ni nani/wala nafasi yako ni ipi), kanisani unaenda tu kama mtu anayeangalia Tv asiyehusika na mambo yanayoendelea kule (Hiyo haifai kabisa kwa mkristo aliyeokoka).

Ukiambiwa uombe huombi!! Karama yako itatendaje kazi ndani yako??,..ukiambiwa ufunge hufungi!! kuhudhuria tu kwenye ibada ni lazima ukumbushwe kumbushwe!..na bado unalaumu kanisani hakuna karama?..hiyo karama ipo kwa nani kama si ndani yako, na wewe umeiua kwa ukaidi wako???

Katika nyumba ya Mungu kila mtu lazima awe kiungo, ndipo udhihirisho mkamilifu wa Roho utaonekana.

Bwana akubariki na atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NITAIFAHAMU VIPI KARAMA YANGU?.

JE! KARAMA NI UTHIBITISHO WA KUWA NA MUNGU?

USIJISIFIE KARAMA KWA UONGO.

Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?

JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?

Rudi nyumbani

Print this post

JE! UNAWEZA KUWA NA GEUKO KAMA LA DAUDI?

Tunapokisoma kisa cha Daudi, cha kumwiba mke wa shujaa wake (Uria), na kumlazimisha kuzini naye kwa siri, na baadaye kumuua mumewe , (2Samweli 11) tunaishia kuona picha mbaya sana ya Daudi. Na kumshutumu, na wengi wetu kusema Daudi ni mzinzi sana, iweje apendwe na Mungu namna ile, tena awe kipenzi cha Mungu?

Ni kweli kabisa alichokifanya Daudi hakistahili kufanywa na mtu yeyote, ambaye anamjua Mungu, mfano wa Daudi. Lakini kuna funzo kubwa sana ambalo wengi wetu hatulioni nyuma ya maisha ya Daudi baada ya pale.

Daudi alipozama katika dhambi ile, na kugundua makosa yake. Alikuwa na badiliko lisilo kuwa la kawaida. Sio kule alikokuwa anaomboleza usiku kucha, Hapana, lile lingekuwa la “kufoji” tu, ambalo yoyote anaweza kulifanya hata leo. Kinyume chake Daudi alikuwa na badiliko la kimatendo. Na hilo ndilo lililomfanya apendwe sana na Mungu.

Kwa namna gani?

Sasa angalia Daudi Yule Yule ambaye alikuwa ni mzinzi, mwenye tamaa ya hali ya juu,akiona tu mwanamke mzuri hajali, huyu ni mke wa mtu au la yeye alimwiba na kuzini naye. Lakini Dakika zake za mwisho hazikuwa hivyo. Alibadilika kwelikweli baada ya dhambi ile.

Utakumbuka hata alipokuwa mzee, Wakuu wa Israeli walikwenda kumtafutia Binti mzuri bikira katika taifa lote la Israeli, ili amlalie Daudi ampe joto kwasababu nguo za joto hazikutosha. Lakini biblia inasema Daudi alipolala naye ‘hakumjua’.

Kwa jinsi ya kibinadamu, binti alale, na mtu mwenye sifa ya tamaa kama Daudi, halafu asimwingilie. Lazima kutakuwa kuna jambo lingine limetendeka ndani ya maisha ya huyo mtu.

Tusome;

1 Mfalme 1:1

 “Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate moto.

2 Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto.

3 Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme.

4 Naye kijana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua

Ni wazi kuwa habari hiyo ilijulikana Israeli nzima, Daudi amelala na binti bikira mrembo miaka kadhaa lakini hajamwingilia. Ni shujaa kiasi gani. Hawakujua kuwa anawathibitishia Israeli kuwa yeye sio Yule wa zamani, sio Yule mzinzi mliyemzoea, ameshabadilika. Si mtu wa kulipuka lipuka tamaa ovyo kama alivyokuwa hapo mwanzo.

Hiyo ndio sababu Mungu alimpenda Daudi. Kwasababu alikuwa na badiliko la dhati Kwa Mungu wake. Je! Na sisi, tunaweza kusema tumeuacha ulimwengu kweli kweli pale tunapomgeukia Mungu, au tutakuwa na vimelea vya kidunia ndani yetu, pale tunapokutana na majaribu kama yale yale ya mwanzo. Tulipokuwa wazinzi na sasa tumeokoka, Je! Tuna ujasiri wa kuishi  maisha ya mbali zinaa, au bado tupo nusu nusu.

Tuwe na badiliko la dhati, leo tumeanguka katika dhambi Fulani mbaya, sasa tumetubu, tusiwe tena walewale wa kuanza kuangalia angalia nyuma kama mke wa Lutu. Mungu atakuchukizwa na sisi na mwisho wa siku tutakuwa jiwe la chumvi kama sio kutapikwa mfano wa kanisa la Laodikia.

Tumaanishe kwelikweli kuacha mambo maovu tuliyoyazoelea. Jifunze kwa Daudi. Yule sio mzinzi kama wewe unayejitumaisha kwa visa vyake vya zamani, ukadhani kuwa utanusurika hukumu ikiendelea na tabia hiyo.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?(Opens in a new browser tab)

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 4

Kwanini Daudi achukue mawe matano, na malaini na sio vinginevyo?

(Opens in a new browser tab)(Opens in a new browser tab)MADHIHIRISHO MATATU YA MUNGU.(Opens in a new browser tab)

Rudi nyumbani

Print this post