IMANI “MAMA” NI IPI?

IMANI “MAMA” NI IPI?

Moja ya somo pana sana katika biblia ni somo lihusulo IMANI. Imani ni kama Elimu, kama vile watu wasemavyo Elimu haina mwisho hali kadhalika Elimu ya IMANI nayo haina mwisho.

Watu wawili wanaweza wakasema ni wasomi, wamehitimu pamoja, wamepokea shahada kwa pamoja wakajulikana na serikali kama ni watu wasomi wazuri wenye manufaa makubwa katika nchi lakini unajua kuwa mmoja anaweza akawa ni mjinga kwa mwingine sawasawa tu na mtu Yule ambaye hajakwenda shule kabisa, Unauliza ni kivipi?.

Jaribu kufikiria mmoja alipomaliza elimu ya msingi alikwenda kusomea masomo ya urubani, na yule mwingine akaenda kusomea udaktari..sasa na elimu zao embu jaribu kumchukua Yule daktari umpe ndege aendeshe abiria, au umpeleke Yule rubani kwenye chumba cha upasuaji kwa vichwa vya wanadamu awatibu wagonjwa..wewe Unadhani ni jambo gani hapo litatokea?..Ni maafa makubwa sana..Sasa tukiwahukumu hawa wote kwa kutazama maafa yaliyotokea na kusema kuwa ni wajinga, tutakuwa hatujatathmini uhalisia wa mambo….Ukweli ni kwamba Yule daktari ni msomi lakini ni msomi aliyebobea katika mambo ya udaktari hivyo masuala ya Jeografia kwake ni kama maruweruwe, hali kadhalika na yule Rubani.

Na ndivyo ilivyo hata katika mambo ya Imani.. Imani haina mchipuko mmoja kama wengi wadhanivyo, Sio kila imani mtu aliyonayo ndani yake itatenda miujiza, sio kila imani mtu aliyonayo itamwokoa hali kadhalika si imani yoyote tu mtu aliyonayo ITAMPENDEZA MUNGU, vile vile sio kila imani itakuja kwa kulisikia Neno la Mungu, ukiyafahamu hayo vizuri itakujengea ufahamu mzuri wa kupima kiwango chako cha Imani kilipo…. Leo kwa neema za Bwana tutatazama kwa ufupi baadhi ya vipengele hivi vya imani, na kisha tutaangalia ni IMANI ya aina gani, ambayo Mungu anaiona kama ni kiini cha mkristo anapaswa awe nayo.

Embu tuchambue mojawapo ambayo tuliiona ikijitokeza kwa mtu fulani kipindi kile cha Bwana Yesu..Tunasoma:

Luka 7:1 Alipokwisha kuyamaliza maneno yake yote masikioni mwa watu, aliingia Kapernaumu.

2 Na mtumwa wake akida mmoja alikuwa hawezi, karibu na kufa; naye ni mtu aliyempenda sana.

3 Aliposikia habari za Yesu, alituma wazee wa Wayahudi kwake kumwomba aje amponye mtumwa wake.

4 Nao walipofika kwa Yesu, walimsihi sana wakisema, Amestahili huyu umtendee neno hili;

5 maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi.

6 Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu;

7 kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona.

8 Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.

9 Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii.

10 Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima”.

Sasa huyu Akida kumbuka hakuwa myahudi, wala hakuijua torati kama wayahudi wenyewe walivyokuwa, kwanza kwa wakati ule ilikuwa ni mwiko wayahudi kuchangamana na watu wa mataifa. Mtu huyu alikuwa ni akida wa kirumi, aliye chini ya utawala wa Kaisari, lakini alikuwa ni mkarimu sana tofauti na maakida wengine waliowekwa kuilinda Israeli,, aliwapenda wayahudi na kuwatendea mema, mpaka kufikia hatua ya kuwajengea Sinagogi, Lakini ikatokea siku moja mtumwa wake aliyempenda sana akaugua karibu na kufa, hivyo akahitaji uponyaji kutoka kwa Yesu, na wayahudi waposikia wakaenda kumwombea kwa Yesu ili aende kumponya. kama tunavyosoma habari ile Bwana akiwa njiani tu yule akida alipata taarifa kuwa YESU anakuja kwake, hivyo akatuma haraka haraka watu kwake na kumwambia atamke Neno tu, na mtumwa wake naye atapona…

Sasa jambo la kutazama hapo, si kawaida mtu kuwa na imani kubwa kiasi kile kama hajaipata kutoka mahali fulani..Imani haiwezi kuja kama haina chanzo..Lakini kumbuka biblia inatuambia Imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa Neno la Kristo.. Lakini huyu mtu hakuwa mkristo, wala hakuwa myahudi, bali mrumi..basi imani kubwa kama ile mpaka YESU kusema hajaiona hata kwa wayahudi, hata kwa kwa makuhani, hata kwa mitume, hata kwa marabi, yeye aliitolea wapi?.

Siri ipo pale pale kwenye maandiko tukisoma mbele kidogo utaona anamwambia Bwana “Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.”

Unaona hapo?, Yeye alitumia experience (au Uzoefu) wa maisha yake kumwesabia Mungu kuwa ni muweza..Yeye mwenyewe alijiona katika hali aliyopo, anao wakuu wengi juu yake ambao wakati wowote wakimwambia fanya hivi hufanya, tenda hili hutenda, hali kadhalika anao watumwa wengi chini yake akiwaamrisha fanya hivi hufanya tenda lile hutenda pasipo hata yeye kuwepo mahali husika na jambo lile hutendeka vile vile kama alivyotoa yale maagizo pasipo kuongezwa wala kupunguza..

Kwahiyo akasema huyu ni YESU naye ni MKUU kuliko sisi wote, mambo yale yale niliyoonyesha kwa watumwa wangu, au niliyoonyeshwa kwa wakuu wangu waliyafanyika bila kasoro yoyote pasipo sisi kuwepo, atashindwaje huyu kutoa tu maagizo na uponyaji kutokea, Kuliko kuja kujitaabisha huku?..Na ndio hapo akawambia Bwana aseme Neno tu!…Hapo hapo Akapokea alichokuwa anakitafuta!!.Haleluya.

Ndugu Imani yoyote ya kupokea chochote kwa Mungu, iwe ni uponyaji, au mahitaji, au mafanikio, au kutendewa miujiza, au kutenda miujiza, hiyo haitegemei Ile IMANI inayozungumziwa katika Warumi 10:17 “(Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.”)..hapana hii Inategemea ni jinsi gani wewe unavyomwelewa Mungu na kumchukulia hata katika hatua ya maisha inayopitia sasa, kwa kutazama tu mazingira yanayokuzunguka, au unayoyaishi unaweza ukaumba mambo makubwa mpaka dunia ikashangaa.

Itafakari tena ile habari ya Yule mwanamke aliyemwendea Yesu ambaye hakuwa myahudi kabisa, alitokea huko Tiro ambapo kwa sasa ni Nchi ya Lebanoni, lakini alipomwendea Yesu ili amponywe binti yake, Bwana alimwambia si vema kutwaa chakula cha watoto na kuwapa mbwa, lakini Yule mwanamke akamwambia Bwana hata mbwa hula makombo yanayondoka mezani pa watoto,.Ndipo Bwana akamwambia mama imani yako ni kubwa na iwe kwako kama utakavyo..(Marko 7:27)

Unaona huyu naye hakusoma mahali popote kwenye maandiko mpaka, awe na imani kubwa kama ile, kiasi cha Bwana kumwambia, Wote hawa wanatumia (uzoefu wao) wa maisha na kumuhesabia Mungu kuwa anaweza pia , na hivyo wanapata majibu ya maombi yao kwa Mungu.

Hata na wewe unaweza kupata lolote kwa Imani ya namna hiyo, uponyaji, kutoa pepo, na vitu vingine kama, gari, nyumba, mafanikio, kuamrisha vitu navyo vikatokea, n.k. na kwa jinsi utakavyoamini sana kwa kumchukulia Mungu kuwa anaweza ndivyo utakavyopokea zaidi. lakini fahamu kuwa Imani ya dizaini hiyo hata kama itafikia hatua ya kuweza kuhamisha milima bado uwezekano wa kwenda Jehanum ya moto ukawa ni mkubwa kwako kama hutafahamu shabaha ya Imani ambayo Mungu anataka kuiona kwa mtu.

Imani hii haiwezi ikakupa faraja, imani hii haiwezi ikakupa tumaini, imani hii haiwezi ikakupa uzima wa milele imani hii haiwezi ikakupa tumaini, Imani hii haiwezi ikakupa MAFUNUO kutoka kwa Mungu…Wengi leo wanaikimbilia hii ambayo kimsingi ni nzuri lakini wanasahau kiini cha imani mama impasayo kila mtu awe nayo kwa mambo yote.

IMANI MAMA NI IPI?

Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa NENO LA KRISTO”.

Sasa nataka ufahamu kuwa ipo imani inajengeka ndani ya mtu si kwa uzoefu fulani hapana, kama alioupata yule akida aliyeponyewa mtumwa wake au aliyoipata yule mama wa Tiro aliyeponyewa binti wake, bali ni kwa kulisikia Neno la Kristo tu, Kumfahamu Kristo tu kwa mapana yake na marefu yake basi, hii ni Imani timilifu katika Neno la Kristo. Si wengi wanayo, na hii haifikiwi hivi hivi labda kwa kusali sana, au kwa kufunga sana, hapana bali inafikiwa kwa kumjua sana Kristo tu katika Neno lake..Tunaposema kufahamu Neno la Mungu hatumaanishi kukariri vifungu vya biblia tu hapana, bali ni kupata ufunuo wa Yesu Kristo ni nani katika maisha yako, na hiyo inakuja kwa kumtafakari sana Bwana Yesu, na kumjua yeye kwa upana wake na urefu wake kwa maana biblia inasema katika “Wakolosai 1:19.. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza UTIMILIFU wote ukae;

Sehemu nyingine biblia inasema katika Waefeso 4:13 “hata na sisi sote tutakapoufikia UMOJA WA “IMANI” NA KUMFAHAMU SANA MWANA WA MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu”.

Shetani hapendi kabisa watu watafute IMANI ya NAMNA HII,..Hapendi kabisa watu wapoteze muda mwingi kufundishwa habari za YESU, bali za mafanikio na uponyaji tu kila wakati..Kwani anajua watu imani yako ikishajengwa katika ufunuo wa kumjua YESU KRISTO ni nani kwao? Basi watamsumbua sana yeye na kuleta madhara makubwa katika ulimwengu kwa roho. Kwahiyo hapendi watu wamjue sana Yesu Kristo, hababaiki watu wawe hata na imani ya kuhamisha mlima, hiyo haimbabaishi inaogopa sana mtu mwenye Imani iliyojengwa katika kumjua Yesu Kristo, nguvu za kufufuka kwake.

Jiulize ni kwanini utakuta mtu ameshakuwa ni mkristo kwa muda mrefu lakini leo hii hana hata Amani katika maisha yake, jiulize ni kwanini hana furaha, ni kwanini anaona kama vile Mungu hamsikii, ni kwanini anayo hofu ya kufa, kwanini anayumbishwa na mafundisho ya uongo, kwanini kila siku ni mchanga kiroho, kwanini hapokei mafunuo yoyote kutoka kwa Mungu, kwanini anawaogopa wachawi? Ni kwanini hata ujasiri kwa Mungu wake hana, na bado ni mkristo wa muda mrefu…

Hajui kuwa tatizo lipo hapo, Imani yake haijajengwa katika misingi ya kumjua YESU KRISTO bali katika misingi mingine..Amekuwa hataki kufundishwa habari za msalaba, yeye anataka tu, atabiriwe ndoa yake, atakata tu aombewe juu ya uponyaji wake, anataka tu aombewe biashara yake, anataka tu afundishe mafundisho laini laini, ya kubembeleza, ya faraja, mafupi, na ya kuchekesha,..Sasa ile Imani inayozungumziwa na Mungu mtu wa dizaini hii asitazamie kama ataipata.

Ndugu tafuta kumjua Yesu na uweza wake, weka uhusiano wako sawa na YESU maishani mwako, jishughulishe sana kumtafuta kwa kumchunguza, na kwa kusoma habari zake zote, na kwa kumtafiti sana, huko huko ndiko utakapopata ufunuo wa kumjua YEYE ni nani kwako. Zipo faida nyingi, na mojawapo ni kuwa wewe utayapata yote utakayotaka, ya mwilini na ya rohoni, ukimwomba Baba vya mwilini atakupa kwasababu tayari utakuwa ameshakuonyesha njia ya kuvipata, halikadhalika rohoni utakuwa ni amani, furaha, utulivu, tumaini, ujasiri,faraja na maji ya mito ya uzima kuyatakuwa yanatiririka moyoni mwako. Kwasababu Imani yako imejengwa katika misingi ya kumjua YESU KRISTO. Umeshapata ufunuo wa Yesu Kristo ni nani kwako, Hivyo shetani hawezi kukusumbua tena. Yesu Kristo ndio siri ya Mungu iliyotabiriwa itafunuliwa katika siku za mwisho, Unabii wote wa biblia unamuhusu yeye, na ushuhuda wake ndio roho ya Unabii (Ufunuo 19:10).

Ndugu ikiwa bado unasua sua katika imani, huu ni wakati wa kuweka mambo yako sawa, Tubu, anza mwanzo mpya na Bwana, badili mfumo wako wa maisha kwa ujumla na wa kumwendea Mungu, angalia Imani yako unaijenga katika Nyanja ipi? Kumbuka hilo eneo la IMANI ni pana kama ilivyo Elimu…Hivyo chaguo ni lako Ni matumaini yangu kuwa sote tutachagua kujenga katika misingi ya Neno lake ili tupate vyote.

Ubarikiwe sana. Tafadhali “Share” ujumbe huu na wengine, na Bwana atakubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

IMANI NI KAMA MOTO.

JE! NI SAHIHI KWA MKRISTO KUOA/KUOLEWA NA MTU WA IMANI NYINGINE?

JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?

IMANI YENYE MATENDO;

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments