Je! Ni sahihi kwa mkristo kuoa/kuolewa na mtu wa imani nyingine?

Je! Ni sahihi kwa mkristo kuoa/kuolewa na mtu wa imani nyingine?

JIBU: Kwanza sio sahihi kwa mtu aliyeamini kwenda kutwaa mke au mume asiye wa imani yake ya kikristo, kwasababu moja tu! nayo ni KUEPUKA KUGEUZWA MIOYO!..   Kumbuka jambo mojawapo ambalo Mungu aliwakanya sana wana wa Israeli hata kabla ya kufika nchi ya Ahadi ni suala la kuoa/kuolewa na watu wa jamii nyingine tofauti na wayahudi, na sio kwasababu labda ni wabaya, au hawavutii hapana, ni kwasababu moja tu! Watageuzwa mioyo yao wasiambatane na Mungu wa Israeli kinyume chake wataambata na miungu migeni. Na Mungu siku zote ni Mungu mwenye wivu!.   Tukisoma;

Nehemia 13:25 “………… nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.

26 Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini WANAWAKE WAGENI WALIMKOSESHA HATA YEYE.

27 Basi, na sisi, je! Tuwasikilize ninyi kutenda neno hili baya, hata kumhalifu Mungu wetu kwa kuwaoa wanawake wageni?”  

Unaona hapo?. Mfalme Sulemani pamoja na hekima zake zote nyingi za kuweza kupambanua mambo lakini aligeuzwa moyo, na wale wanawake wa mataifa mpaka kufikia hatua ya kuivukizia uvumba miungu migeni, Unadhani itashindanaje kwa mkristo mwingine yeyote wa kawaida?. Unaweza ukasema aa! Mimi nitaweza kumtawala, lakini hilo haliwezekani Mungu sio mwongo, akisema atakugeuza, ni kweli atakugeuza,.Mwanzoni utaona kama inawezekana lakini mwisho wa siku utajikuta unaangukia katika shimo kama Sulemani.   Vivyo hivyo ukimsoma Mfalme Ahabu alikoseshwa na Yezebeli mchawi, Samsoni naye alikoseshwa na Delila. Wote hawa wake zao walikuwa ni wanawake wa kimataifa n.k.  

Kwahiyo unapokuwa mkristo unapaswa umtafute mtu mwenye imani moja na yako ya kikristo, au kama sio basi umgeuze kwanza amgeukie Kristo ndipo umuoe au uolewe naye, vinginevyo utakuwa unajiweka mwenyewe katika hali ya hatari kubwa ya kumkosea Mungu, na kuishia katika majuto…   Lakini kama ikitokea mlishaoana tayari huko nyuma na mtu mwingine kabla wewe hujawa mkristo, na wewe baadaye ukaja kuamini na Yule mpenzi wako hajaamini lakini bado anaona vema kuishi na wewe hapo biblia inasema haupaswi kumuacha, unatakiwa ukae naye katika hali yake hiyo hiyo pengine wakati ukifika kwa matendo yako mema ya kikristo yatambadilisha na yeye naye aamini…

Lakini kama akichukizwa na uamuzi wako wa wewe kuwa mkristo na anataka kuondoka…Hapo haufungiki, anaweza kwenda, na biblia inaruhusu kutwaa mke/mume mwingine ila katika Bwana tu ambaye ni mkristo mwenye imani moja na wewe.   Soma.

1Wakoritho 7: 12 “Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache.

13 Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe.

14 Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe; na yule mke asiyeamini hutakaswa katika mumewe; kama isingekuwa hivyo, watoto wenu wangekuwa si safi; bali sasa ni watakatifu.

15 Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani.

16 Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo?”  

Kwahiyo hairuhusiwi kuoa mtu ambaye sio wa IMANI moja nawe kulingana na maandiko.  

Ubarikiwe sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada zinazoendana:

NDOA NA HARUSI TAKATIFU.

NDOA NA TALAKA:

JE! NI HALALI KUTOA CHETI KWA WAKRISTO WANAOOA?

NINI TOFAUTI KATI YA UZINZI NA UASHERATI ?

JE! KUFANYA MASTURBATION (PUNYETO) NI DHAMBI?

NAPENDA KUJUA MAANA NA TOFAUTI KATI YA MYUNANI, MFARISAYO NA MSADUKAYO.

UKWELI UNAOPOTOSHA.

DUNIANI MNAYO DHIKI.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments